KURASA

Sunday, September 6, 2009

HOMA YA BONDE LA UFA- tishio kwa wanyama na binadamu

1.UTANGULIZI

Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever) kupitia vyombo vya habari na kupitia Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) umeripotiwa kulipuka mara kwa mara katika eneo letu la Afrika ya Mashariki hasa katika nchi jirani ya Kenya. Ugonjwa huu, kama jina lake linavyoonyesha hutokea kwenye nchi zenye bonde la ufa na Tanzania ni mojawapo ya nchi hizo. Ugonjwa hutokea baada ya mvua nyingi na mafuriko yanayofuatia kuwepo kwa ukame wa muda mrefu.

Uchunguzi wa “remote sensing” uliofanywa na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) unaonyesha kuwa maeneo yaliyo na hatari zaidi ya kuambukizwa na ugonjwa ni pamoja na Kenya, Kusini mwa Somalia, Kusini na Kusini Mashariki mwa Ethiopia, Kusini mwa Sudan na Kaskazini mwa Tanzania.



2.HISTORIA YA UGONJWA

Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever) katika nchi ya Kenya umefahamika kwa zaidi ya miaka 60 iliyopita. Ugonjwa unaofanana na Homa ya Bonde la Ufa ulionekana mara ya kwanza nchini Kenya mwaka 1913. Tangu wakati huo matukio makubwa ya ugonjwa yameonekana katika nchi nyingi za Bara la Afrika ikiwa ni pamoja na Misri, Sudan, Somalia, Kenya, Msumbiji, Nigeria, Senegal, Tanzania, Uganda, Zambia, Zimbabwe, Namibia na Afrika ya Kusini.
Nchi ya Misri ilikumbwa na ugonjwa huu mwaka 1977 na 1978 ambapo watu wapatao 18,000 waliugua na 598 walikufa. Nchi ambazo taarifa zilitolewa za matukio ya ugonjwa huu nje ya Bara la Afrika ni pamoja na Yemen na Saudi Arabia. Kwa hapa Tanzania ugonjwa huu ulionekana mwaka 1979 na 1998 katika mikoa ya Mara, Arusha na Kilimanjaro ambapo ng’ombe, Mbuzi, kondoo na ngamia waliathirika.

3.VISABABISHI VYA UGONJWA NA JINSI UNAVYOENEA


Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever) unasababishwa na virusi viitwavyo Phlebovirus na ambavyo kitaalam vimewekwa katika familia ya Bunyaviridae. Virusi hivi huweza kuishi kwenye mayai ya mbu aina ya aedes, ambayo yana tabia ya kuishi kwenye vumbi kwa muda mrefu na kuanguliwa wakati wa mafuriko. Baada ya kuanguliwa mbu hawa husambaza ugonjwa kwenye mifugo na kwa watu wakati wanapofyonza damu. Mbu aina nyingine kama vile Culex, Mansonia, Anopheles, na Eretmapodites wanaweza kusambaza virusi vya ugonjwa kati ya wanyama na wanyama na kati ya wanyama na binadamu.



Lakini zaidi ya kupata ugonjwa moja kwa moja toka kwenye mbu binadamu wanaweza kupata ugonjwa kupitia kugusa damu au majimaji ya aina nyingine ya wanyama wakati wa kuchinja, kuzalisha wanyama wagonjwa, kushika vitoto vya mbuzi au kondoo vilivyokufa.

Aidha binadamu wanaweza kupata ugonjwa kutokana na kula vyakula visivyopikwa vizuri vitokanavyo na wanyama wagonjwa au wenye virusi.


4.DALILI ZA UGONJWA

4.1.Dalili kwa mifugo
Ugonjwa huu huwapata ng’ombe, mbogo, kondoo, Mbuzi, ngamia na binadamu. Ugonjwa huonekana zaidi kwenye maeneo ya watu wenye mifugo mingi. Dalili za kwanza katika wanyama ni kutupa mimba kwa wingi hususan katika kondoo na ngamia na vifo vingi vya ghafla kwa karibu asilimia 90 ya mbuzi na kondoo wachanga. Kwenye mbuzi na kondoo wakubwa dalili za ugonjwa ni pamoja na kutapika, kutokwa makamasi yenye damu na kuharisha, rangi ya njano kwenye ngozi ya ndani inayofunika macho, midomo na sehemu za uzazi na vifo katika asilimia 10 hadi 20 ya wanyama hawa. Ng’ombe hawaugui sana kama ilivyo kwa mbuzi na kondoo.

4.2.Dalili kwa binadamu
Dalili za ugonjwa kwa binadamu ni pamoja na kuumwa kichwa, kuumia macho wakati yanapoangalia mwanga mkali, mafua, homa kali, tumbo kuuma, kutapika na wakati mwingine kutapika damu. Virusi huchukua muda wa siku mbili hadi sita tangu kuingia mwilini hadi kuanza kuonyesha dalili na ugonjwa unaweza kusumbua kwa muda wa siku tatu hadi saba au zaidi. Vifo kwa binadamu vinaweza kutokea baada ya virusi vya ugonjwa huu kushambulia ubongo na viungo vingine vya mwili ambapo husababisha kuvuja damu.




5.KINGA NA NAMNA YA KUUEPUKA

Kama ilivyokwishaelezwa Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa unasababishwa na virusi na unaenezwa na mbu. Kwa hiyo njia mojawapo ya kuzuia mifugo isipate ugonjwa ni kuiogesha au kuinyunyizia dawa aina ya pyrethroids ambazo ni pamoja na Flumethrin, Deltamethrin na Alphacypermethrin. Dawa hizi tayari ziko nchini na zinatumika kuogeshea mifugo ili kuikinga isishambuliwe na kupe au mbung’o na zinaweza kutumika pia ili mifugo isishambuliwe na mbu.

Njia ya kuzuia binadamu wasipate ugojwa huu ni kutumia vyandarua. Pia wananchi wanaweza kuepuka ugonjwa huu kwa kupika vizuri vyakula vitokanavyo na mifugo. Wizara inashauri wananchi wachukue tahadhari hizi hata kama ugonjwa haujaonekana popote nchini kwa sababu kinga ni bora kuliko tiba.

Sunday, August 30, 2009

MIKARATUSI NA UKWAJU - TIBA YA KIFUA

Mikaratusi na ukwaju ni tiba yenye nguvu dhidi ya kifua na kukohoa, tiba hii ni rahisi kuandaa na haina gharama.



UAANDAAJI
Chukua jani moja au zaidi ya mkaratusi lililokomaa kutoka katika matawi machanga/mapya ya mti, ponda ponda na uchuje kwenye maji kiasi cha mililita 100-200, unaweza kutumia blender pia kusagia dawa hii, kisha changanya na juisi ya ukwaju, pia unaweza kuongezea tangawizi kidogo ukipenda.


MATUMIZI
Kunywa mchanganyiko huu mara 3 kwa siku kwa siku 3-5
Ukitumia mchanganyiko huu mara moja kwa wiki ni kinga tosha kwa magonjwa ya njia ya hewa



MUHIMU Ukichemsha majani ya mkaratusi chumbani na kuacha mvuke usambae chumbani ni kinga tosha juu ya mafua, pia huleta harufu nzuri chumbani (air freshener)

Monday, August 17, 2009

MBAAZI- cajanus cajan

Pamoja na kuwa ni chakula tulichokizoea sana, lakini mmea huu pia ni dawa ya magonjwa mbali mbali

MAANDALIZI

Chukua majani, maua au mizizi kiasi cha nusu kilo (ni vizuri kama utachanganya vyote) pondaponda na uloweke kwenye maji safi kiasi cha lita 2 kwa muda wa masaa 24.


Chuja na uweke dawa hii mbali na jua/joto, ni vizuri kama ataweka kwenye friji, kunywa kikombe kimoja kutwa mara 3 kwa siku 3




TIBA

Dawa hii inaweza kutibu magonjwa yafuatayo

1-Inauwezo mkubwa wa kushusha homa

2-Husaidia kuponesha vidonda.

3-Husaidia kurekebisha mzunguko wa hedhi kwa wanawake.

4-Husaidia kupunguza uvimbe

5-Huponyesha kifua na kukohoa.

6-Husafisha kibofu/njia ya mkojo.

7- Huongeza kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbali mbali

Tuesday, August 11, 2009

TANZANIANS BLOGGERS SUMMIT



Je wewe ni mwanablogu (Blogger) au mdau wa habari na mawasiliano kwa umma kwa kutumia mtandao? Kama jibu ni ndio, tafadhali unaombwa kujiorodhesha kwa ajili ya maandalizi ya Kongamano Maalumu la Kitaifa kwa ajili Wanablogu (Bloggers) na wadau wa habari na mawasiliano wa Tanzania (Tanzanians Bloggers Summit) linalotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu jijini Dar-es-salaam,Tanzania.

Dhumuni la kongamano hili ni Kuelimishana, Kufahamiana, Kuamsha Utambuzi Rasmi Kuhusu Tekinolojia ya Blogu na Mawasiliano ya Umma kwa Kutumia Mitandao, Kusaidia Utambuzi Rasmi juu ya mchango wa blogu nchini Tanzania kama chombo muhimu cha habari na mawasiliano, Kuelimishana jinsi gani blogu zinaweza kutumika katika kuleta maendeleo katika nyanja za kijamii, kisiasa na kiuchumi, kuburudisha, kukuza utamaduni nk.

Wataalamu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wataalikwa kutoa mada na mafunzo mbalimbali kuhusiana na tekinolojia ya kublogu, zana nyinginezo za mawasiliano mtandaoni kama vile mitandao jamii(social networking), online forums nk.Kutakuwa na vipindi vya maswali na majibu.
Ili kufanikisha maandalizi ya Kongamano hili la kihistoria, kujiorodhesha kwako ni muhimu sana. Muda wa kujiodhoresha ni kuanzia tarehe 12/8/2009 (Jumatano) mpaka 12/9/2009 (Jumamosi) tu.

Kinachohitajika ili kujiandikisha ni :
Jina Lako, Anuani yako ya barua pepe (E-mail), Mahali Ulipo au unapoishi (Nchi,mji nk),Namba ya Simu (sio lazima) na Anuani au URL(Universal Resource Locator) ya blogu yako (mfano www.kongamano.blogspot.com/wordpress.com/.com/typepad nk). Vyeti vya Ushiriki vitatolewa kulingana na habari utakazoziorodhesha hapa.
Unaweza kujiorodhesha kwa kutuma ombi lako kwa barua pepe kwenda; summit@bongocelebrity.com.

Zingatia tarehe za kujiandikisha.
Ni mwezi mmoja tu! Asante kwa ushirikiano. UMOJA NI NGUVU!

TEAK FOR SALE - MITIKI INAUZWA

SPECIE - tectona grandis (seed planted not cloned)

AGE - 18 years old

QUANTITY - 50 standing trees

LOCATION - Mahenge, Morogoro

CONTACT - mitiki1000@gmail.com

For serious buyer send your price offer & further negotiation will be made at the site

Monday, August 10, 2009

KICHAA CHA MBWA

KUSAMBAA

Kichaa cha mbwa kinaweza kusambazwa na mate ya wanyama, wengi tumezoea kwamba mbwa ndiye anasambaza kichaa, lakini wanyama wengine kama paka, popo, ng'ombe, mbweha, fisi na wengine wanaweza kukisambaza




DALILI ZA MBWA MWENYE KICHAA

siku 1-3 mbwa hubadilika zile tabia ulizozizoea hapa ni ngumu kidogo kugundua

siku 3-4 mbwa huwa na aibu na pia huwa anakwepa mwanga (photophorbia), anajifichaficha na kung'ata kila kitu kinachopita karibu yake hata kama karatasi limepeperushwa na upepo

siku 5 mbwa huanza kulemaa akianzia miguu ya nyuma (hind quarter paralysis) kisha kufuatia miguu ya mbele, baada ya siku saba mbwa hufariki




CHANJO
Mbwa wachanjwe dhidi ya kichaa angalau mara moja kwa mwaka, watoto wanaozaliwa na mama aliyechanjwa wachanjwe baada ya miezi mitatu baada ya kuzaliwa, unaweza kuwachanja kabla kama kuna mlipuko wa kichaa cha mbwa

Sunday, July 19, 2009

MBEGU BORA ZA MAHARAGE

Aina mbili ya mbegu bora za maharage zimeendelezwa/zimezalishwa katika kituo cha utafiti wa kilimo kilichopo Uyole mkoani mbeya. Mbegu hizo ni BILFA 16 na UYOLE 04. Kuzalishwa kwa mbegu hizi bora ni juhudi za muda mrefu za mpango wa kuzalisha mbegu bora za maharage lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji na maharage yakiwa katika sifa na ubora unapendekezwa na wakulima pamoja na walaji, wakulima hupendelea mbegu zinazohimili magonjwa, zinazohimili ukame na zenye mazao mengi wakati walaji hupendelea maharage yenye ladha nzuri na yanayoiva kwa urahisi yakiwa katika bei yenye unafuu.

Mbegu ya UYOLE 04 hutambaa, huzaa maharage yenye ukubwa wa wastani mpaka kubwa kabisa zikiwa na rangi ya maziwa, zinahimili magonjwa sugu kama kutu ya maharage na anthracnose, huiva haraka yakipikwa na huwa na ladha nzuri sana

Wakati wa kupanda mbegu hii hutegemea msimu wa kuanza na kuisha kwa mvua, kwa mfano sehemu ambazo mvua huisha mwisho wa mwezi wa 4 au mwanzo wa mwezi wa 5 basi upandaji uanze mwezi wa 3 kwa sababu ukuaji wa mbegu hizi mpaka kukomaa huchukua wastani wa siku 105. Kiasi cha mbegu zinazohitajika kupanda ni kilo 70 – 80 kwa hekta ambapo miche 200,000 huota na huweza kuzalisha kiasi cha tani 1.5 – 1.8 kwa kila hecta, mbegu hii hufaa sana kupandwa nyanda za juu kaskazini (mikoa ya Mbeya, Iringa, Songea na Rukwa) ambako ardhi imeinuka wastani wa mita 800 – 2000 kutoka usawa wa bahari na kuna baridi.


BILFA 16


Mbegu ya BILFA 16 huwa na rangi nyekundu mchanganyiko na maziwa kama nguo ya jeshi, mbegu ni za ukubwa wa wastani, huweza kuhimili sana magonjwa, mimea ni ya kijani kibichi yenye majani madogo madogo huwa na matawi 4 – 5 maua huwa na rangi ya pinki na vishubaka vya maharage huwa vyeupe na vikikomaa huwa rangi ya maziwa

. Kiasi cha mbegu zinazohitajika kupanda ni kilo 70 – 80 kwa hekta ambapo miche 200,000 huota na huweza kuzalisha kiasi cha tani 1.2 – 1.5 kwa kila hecta, ambacho ni kidogo ukilinganisha na UYOLE 04, mbegu hii hufaa sana kupandwa nyanda za juu kaskazini (mikoa ya Mbeya, Iringa, Songea na Rukwa) ambako ardhi imeinuka wastani wa mita 800 – 2000 kutoka usawa wa bahari na kuna baridi. Na mbegu hii hukoma baada ya siku 80 – 84 tangu kupandwa kwa hiyo hufaa kwenye maeneo yenye mvua za muda mfupi.

Saturday, July 11, 2009

MIGOMBA - KANUNI ZA KILIMO BORA

Hapa Tanzania kilimo cha migomba kimekuwepo Kwa miaka mingi. Kilimo hiki ni maarufu sana kwa sababu zao la ndizi limekuwa likitumika kama chakula kikuu kwa baadhi ya mikoa kama vile Kagera, Kilimanjaro na Mbeya na hivyo kulifanya muhimu, kufuatia mazao ya mahindi, mpunga, mtama, muhogo,viazi na mazao ya jamii ya kunde kama vile maharage.
Zao la ndizi linaweza kuwa moja kati ya mazao ya biashara iwapo litazalishwa kwa kufuata kanuni bora za uzalishaji wa zao hilo, ikwa ni pamoja na kupanda aina bora ya migomba inayozaa ndizi zinazotambulika katika masoko ya kimataifa.

ASILI YA MIGOMBA
Asili ya migomba ni nchi za Malaysia na India ambazo ziko Kusini Mashariki mwa Asia. Migomba inayolimwa sasa imetokana na migomba ijulikanayo kama Musa balbisiana ambayo asili yake ni India, na Musa acuminata ambayo asili yake ni Malaysia. Kutoka Malaysia na India migomba ilifika Afrika Mashariki katika karne ya tano

MAENEO YANAYOLIMWA MIGOMBA NCHINI

Nchini Tanzania mikoa inayoshughulika na kilimo cha migomba na kuzalisha zao la ndizi kwa wingi ni pamoja na Kagera, Kilimanjaro, Mbeya, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Kigoma, na Pwani. Hata hivyo zao hili linaendelea kuenea katika mkoa mingine nchini ikiwa ni pamoja na Dar es salaam,, Mwanza, Ruvuma, Shinyanga na Lindi. Pia Dodoma na Singida.
Kilimo cha migomba kinaweza kufanyika katika kipindi chote cha mwaka kulingana na kiasi na mtawanyiko wa mvua hasa mabondeni au kwa umwagiliaji.



MATUMIZI
Kilimo cha migomba kina faida nyingi, baadhi ya faida za migomba na
zao la ndizi ni: -
1Zao la chakula
2Zao la Biashara
3Kutengenezea pombe
4Kulisha mifugo
5Kutengenezea mbolea (mboji)
6Matandazwa shambani (mulch)
7Kutoa kivuli
8Kutoa nyuzi
9Kutengenezea vitu vya sanaa
10Kamba
11Malighafi ya kutengeneza vyakula na vinywaji mbalimbali.
12Dawa
13Majani kama miamvuli, sahani, vikombe na kata
14Kuezekea.

Ndizi kwa ajili ya chakula hutumika kwa kutengeneza vitu mbalimbali-:
1Makangale (Banana figs)
2Poda (Powder)
3Chenge (chips)
4Jeya (flakes),
5Juisi,
6Lahamu (jam)
7Vinywaji baridi, kama soda
8Mvinyo (Wine)
9Pombe kali
10Hamira

UZALISHAJI
Zao la ndizi likizalishwa kwa utaalamu unaokubalika huweza kutoa mazao yenye ubora wa hali ya juu na kuongeza uzalishaji kwa eneo. Mambo yafuatayo yafaa kuzingatiwa katika uzalishaji wa zao hili.

(a) Hali ya hewa
Kiasi cha chini cha mvua kifaacho ni 100mm kwa mwezi au 1200mm kwa mwaka. Mwinuko ni kutoka usawa wa bahari hadi mita 1800 juu ya usawa wa bahari. Zaidi ya mwinuko huo migomba haikui vizuri. Kiasi cha joto kinachofaa ni nyuzi joto za sentigredi 25 hadi 30 chini ya nyuzi joto 16 migomba haikui vizuri. Migomba hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha, kina kirefu, usiotuamisha maji na pia usiwe na chumvi. Chachu ya udongo inafaa iwe kati ya pH 5 hadi 8.

(b) Aina za ndizi
Kuna aina nyigi sana za ndizi. Nchini Tanzania ndizi zinazozalishwa, zipo za aina nyingi ambazo hutofautiana kwa majina kutokana na eneo au mkoa unaozalisha. Hata hivyo zinaweza kugawanywa katika makundi mawili. Aina ambayo huliwa kwa kuzichoma, kukaanga au kupikwa zikichanganywa na vyakula vingine kama vile nyama. Aina za ndizi hizo ni pamoja na Mzuzu, Mshale, Matoke, Bokoboko na Mkono wa Tembo.
Aina nyingine ni zile ambazo huliwa kama matunda, aina hizo ni kama vile Kisukari, Kimalindi, Mzungu na Mtwike.

Kuna aina nyingine za ndizi ambazo kwa sasa huzalishwa hapa nchini ambazo zina fahamika kwa ubora wake katika masoko ya ndizi ya kimataifa. Aina hizi ni pamoja na Williams, Grand Naine, Pazz, Jamaica, Gold Finger, Nyingine ni Uganda green, Embwailuma Giant na Chinese Cavendish.



(c) Utayarishaji wa shamba
1Safisha sehemu inayohusika kwa kutumia zana ulizonazo.
2Ng’oa visiki vyote na mizizi yake yote
3Lima sehemu hiyo kwa kutumia jembe la mkono, rato, au trekta ili kuwezesha mizizi laini ya migomba kupenya ardhini kwa urahisi.
4Baada ya visiki na magugu yote kuondolewa na hivyo ardhi kuwa wazi, uchimbaji wa mashimo ya kupandikiza machipukizi au miche ya migomba unaweza kufanyika.

(d) Nafasi ya kuchimba mashimo
Mashimo yatachimbwa kwa nafasi inayokusudiwa kutumika kati ya
mashina ya migomba na kati ya mistari kama ifuatavyo:-
1Migomba inaweza kupandwa kwa nafasi ya Umbali wa meta
2.75 kwa 2.75 kwa migomba mifupi kama Kimalindi na
Kisukari. (Mashina 1,331 kwa hekta )
2Umbali wa meta 3 kwa meta 3 kwa migomba ya urefu wa kati
kama Jamaica na Mshale (Mashina 1,110 kwa hekta)
3Umbali wa meta 3.6 kwa meta 3.6 kwa migomba mirefu zaidi kama
Uganda green Mashina 760 kwa hekta).

(e) Uchimbaji mashimo.
Uchimbaji mashimo inafaa ufanywe mapema kiasi cha juma moja hadi mwezi kabla ya muda wa kupanda. Shimo lichimbwe kwa kutenganisha udongo wa juu na wa chini.

Vipimo vya shimo ni vyema vikazingatiwa. Iwapo utachimba shimo la mviringo litafaa liwe na kipenyo cha sentimeta 60 hadi 90 na kina cha sentimeta 60 hadi 90. Iwapo utachimba shimo la mstatili au mraba litakuwa na urefu, upana na kina cha sentimeta 60 hadi 90, kutegemea kiasi cha mbolea kilichopo na kiasi cha kvua kinachonyesha sehemu hiyo. Uwekaji wa mbolea hufuatia mara baada ya mashimo kuwa tayari. Kiasi cha madebe 5 ya mbolea ya samadi iliyooza vizuri au mboji iwekwe kwenye lundo la udongo wa juu kando ya kila shimo na ichanganywe kisha mchanganyiko wa mbolea na udongo urudishiwe katika shimo kisha kijiti kichomekwe katikati ya shimo hilo, ilikuonyesha sehemu ambapo mche au chipukizi litapandwa.

(f) Kuchagua machipukizi bora
Machipukizi mazuri yanayofaa kwa mbegu ni yale yenye sifa hizi hapa chini: -
Sifa za chipukizi bora
1Liwe chipukizi sime, yaani lenye majani membamba na siyo
chipukizi maji yaani lisiwe lenye majani mapana.
2Litoke kwenye mgomba (shina) wenye afya nzuri, usiokuwa na
magonjwa, minyoo ya mizizi, wala vifukusi vya migomba.
3Litoke kwenye mgomba wenye sifa ya kuzaa mikungu
mikubwa.
4Liwe na afya nzuri na lisiwe na dalili za ugonjwa, wadudu, au
mayai ya vifukusi.
5Urefu uwe kati ya meta 1 na meta 2
6Kipenyo cha sehemu ya chini ya shina la chipukizi (tunguu) kiwe ni kati ya sentimeta 15 hadi 25.

(g) Upandaji wa machipukizi
Wakati unaofaa kupanda machipukizi ni mwanzoni mwa msimu wa mvua. Chomoa kile kijiti na chimba shimo la kiasi cha sentimeta 30x30 katikati ya shimo lililojazwa mchanganyiko wa udongo na samadi kisha panda chipukizi hilo.

Rudishia udongo na hakikisha tunguu lote limefunikwa vizuri. Shindilia udongo ili chipukizi lisimame wima imara. Machipukizi yanayo tarajiwa kupandwa yanatakiwa kuondolewa mizizi yote ili kudhibiti minyoofundo na fukuzi wa migomba. Pia maji ya moto au dawa kama vile furadani inaweza kutumika kuulia wadudu kwenye mizizi ya migomba.

UTUNZAJI WA SHAMBA NA MIMEA.
(a) Uwekaji wa matandazwa (mulching
)
Kazi hii ni vyema ikafanywa mara baada ya kupanda kama inawezekana. Matandazo yawe ni makavu na unene wa sentimeta 15 ili kuhifadhi unyevu, kuzuia magugu na yakioza yataongeza mbolea.

(b) Uongezaji wa mbolea
Baada kupanda ni vyema kuongeza mbolea madebe 2 kuzunguuka shina la migomba kila baada ya miaka miwili au mitatu. Mbolea hii inatakiwa kuchanganywa na udongo na kufunikwa kwa matandazwa.

(c) Umwagiliaji maji shambani
Migomba huhitaji maji mengi. Wakati wa kiangazi. Inafaa kumwagilia ili kuto kupunguza sana ukubwa na wingi wa ndizi zinazotarajiwa kuvunwa kwa mwaka. Kiasi cha maji kinachotakiwa kwa wiki ni milimita 25, yaani eneo linalo zunguka shina la migomba lilowe kabisa.

(d) Kupunguzia machipukizi
Inatakiwa kupunguza mimea ya migomba kwa kila shina na kubaki mimea mitatu tu, yaani Mgomba wenye ndizi (Mama), Mgomba mkubwa ambao bado haujazaa lakini unakaribia kuchanua (Mtoto), Mgomba mchanga uliochipua hivi karibuni ( Mjukuu)

(e) Uondoaji wa Majani Makavu
Mimea ya migomba inafaa iondolewe majani yote makavu ili kuondoa uwezekano wa kuwepo mazalia ya wadudu na magonjwa, kuruhusu mionzi ya jua na kufanya urahisi wa kuhudumia shamba .Pia hufanya shamba kuonekana safi.

(f) Uondoaji wa ncha mwishoni mwa matunda
Baada ya mkungu kutoa ndizi, ua hunyauka na kubakiza ncha mwishoni mwa matunda. Ncha hizo hupaswa kuondolewa .Huduma hii husaidia kupunguza uwezekano wa kujeruhi matunda wakati wa kusafirisha jambo ambalo kupunguza ubora wa tunda.

(g) Kuweka Miega
Miega ni nguzo au kamba ambazo hutumika kuzuia migomba iliyobeba mikungu mikubwa isianguke kutokana na uzito mkubwa. Miega ni ya lazima katika sehemu zenye upepo mkali. Kazi hii inatakiwa kufanywa kwa uangalifu ili isijeruhi ndizi na mgomba wenyewe.




(h) Uondoaji wa kichombezo cha ua la kiume (Shumba)
Uondoaji wa shumba huwezesha matunda kukua vizuri, kuongezeka uzito wa mkungu pia huzuia magonjwa kama vile ugonjwa wa mnyauko wa migomba (Banana Baterial Wilt), ugonjwa wa Majivu nchani mwa matunda (Cigar end rot). Ukataji hufanyika juu ya kovu la pili baada ya kichana cha mwisho, kwa kutumia kisu kikali.

UVUNAJI
Zao la ndizi huweza kuanza kuvunwa katika kipindi cha miezi 9 hadi miezi 15 tangu kupandwa kwa chipukizi. Muda wa kuvunwa hutegemea hali ya hewa. Katika sehemu za joto ndizi huvunwa mapema zaidi kuliko sehemu za baridi. Pia migomba iliyopandwa kwa kutumia machipukizi huzaa mapema kuliko iliyopandwa miche iliyozalishwa kwa chupa (tissue culture)

MATUMIZI YA RIBONI

Riboni za rangi moja (au alama ya kamba) hufungwa kwenye migomba ya umri mmoja mara tu inapoanza kuchanua, na riboni ya rangi nyingine hufungwa kwenye migomba itakayoanza kuchanua wiki mbili hivi zinazofuata na kuendelea hivyo ili kurahisisha kuitambulisha mikungu ambayo itavunwa kwa wakati mmoja. Pia matumizi ya riboni hurahisiha utunzaji wa kumbukumbu ili kujua ni lini na ni mikungu mingapi itavunwa.

WAKATI UNAOFAA KUVUNA
Mkungu wa ndizi huweza kuvunwa katika hatua tofauti kulingana na matumizi, aina na mahitaji ya soko. Mkungu huachwa kwenye mgomba mpaka vidole (matunda ) vimejaa. Uzito wa mkungu hongezeka haraka katika wiki mbili za mwisho, ambapo migongo ya ndizi hutoweka.
Ndizi zinaweza kuvunwa zikiwa zimekomaa na zimeiva kwa kiasi cha asilimia 75 kwa ajili ya kusafirishwa mbali, pia zinaweza kuvunwa zikiwa kukomaa na zimeanza kuiva kwa ajili ya soko la karibu, au zikiwa zimekomaa na kuiva kabisa kwa ajili ya soko na matumizi ya nyumbani Njia bora ya kukata mkungu, ni ile inayohakikisha kuwa mkungu wa ndizi hauanguki chini na kuvunja, kuchubuan au kuharibu ndizi, jambo ambalo litapunguza ubora. Ukichelewa kuvuna ndizi zinaweza kuharibiwa na ndege, wanyama, wadudu au kuibiwa.

MKUNGU WA NDIZI AMBAO UMEONDOLEWA SHUMBA


UBORA WA NDIZI
Ndizi zenye sifa nzuri sokoni ni zile ambazo zimekomaa kwa kiasi kinachotakiwa na zenye vidole vyenye urefu mzuri na visivyo na michubuko. Pia ziwe hazijashambuliwa na magonjwa wala wadudu waharibifu.

KIASI CHA MAVUNO
Mavuno ya ndizi hutegemea zaidi aina ya migomba, hali ya hewa, utunzaji wa mimea shambani. Mavuno huweza kufikia hadi tani 60 au zaidi kwa hekta kwa mwaka. Hata hivyo mavuno mazuri kwa mkulima wa kawaida yasipungue kati ya tani 20 hadi 30 kwa hekta kwa mwaka.

MAGONJWA
Ugonjwa wa hatari sana ulioingia hivi karibuni katika wilaya ya Muleba na maeneo mengine mkoani Kagera kutoka nchi jirani ya Uganda ni wa Mnyauko wa migomba unaosababishwa na bakteria (Banana Bacterial Wilt). Magonjwa mengine yanayosumbua zao hili ni Kuoza tunguu, Ugonjwa wa panama, Ugonjwa wa majivu nchani mwa tunda, Sigatoka, na Moko.

WADUDU WAHARIBIFU
Wadudu wanaosumbua zaidi hili ni Minyoo fundo (Banana nematodes), na Vifukuzi (Banana weevils).

UDHIBITI WA MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU
Magonjwa na wadudu hawa huweza kuepukwa kwa kufuata kanuni bora za uzalishaji wa zao hili. kama usafi wa shamba na kuchagua chipukizi bora. Au kupanda miche iliyozalishwa kwa chupa (Tissue culture banana seedlings) Hata hivyo mara mataizo haya yakitokea muone mtaalam wa kilimo aliye karibu ili aweze kukupa ushauri wa dalili za ugonjwa wa mnyauko wa migomba unaosababishwa na bakteria

Friday, July 3, 2009

MAJI MOTO-RAFIKI WA MKULIMA




1.0 Utangulizi
Majimoto (Oecophylla longinoda) ni wadudu maarufu sana katika Kanda ya Kusini mwa Tanzania. Wanaitwa Majimoto kwa sababu wanapouma,, huleta maumivu kama ya maji ya kukandia jeraha!. Kwa msingi huo huo, wayao huwaita “malumila” wasambaa huwaita “madadada” na Wamwera nao huwaita “ mangongongo”. Majimoto ni maarufu sana kwa uhodari wao wa kujenga viota kwa kufuma majani mabichi .
Ukubwa wa kiota hutegemea ukubwa wa ukoo, aina ya mti na majani yatumikayo na ulaini wa majani yenyewe. Kuna aina ya miti zaidi ya 75 ambayo Majimoto wameonekana kujenga viota vyao, ikiwa ni pamoja na mikorosho, michungwa, miembe na mengineyo.



Utafiti wa awali uliofanyika kwa mahojiano na wakulima mbalimbali, umeonyesha kwamba wengi hawajui faida yoyote toka kwa wadudu hawa, zaidi sana walisimulia athari zao kwamba ni wadudu wanaouma sana na kuleta maumivu makali. Nimeandaa makala hii ili kuhamasisha na kufundisha watu kwamba Majimoto ni rafiki wa mkulima.

2.0 Maisha ya Majimoto
Ukoo wa Majimoto una malkia mmoja tu ambaye analishwa na watenda kazi wakuu, ambapo yeye kazi yake ni kutaga mayai. Akitaga mayai watenda kazi wadogo (minor workers) ndio huchukua na kuatamia na hatimaye kuwatunza wachanga wanapototolewa.

Watenda kazi wakuu ndio hufanya mawindo na mashambulizi makali katika mti hadi ardhini, nao hukamata wadudu aina nyingi tu ambao wanakutana nao. Mmoja akimshika mdudu, hutoa harufu ya tahadhari na kufumba na kufumbua Majimoto wengi hujikusanya na kusaidia mashambulizi hadi kuua na hatimaye kupeleka chakula katika viota vyao.




Majimoto hupenda kuishi na kuwalinda wadudu wengine aina ya “Homoptera” katika namna ya ushirika. “Homoptera” hao, kama vile Hilda spp, Coccos spp n.k., hutoa aina ya majimaji mwilini mwao (honey dew) ambayo hutumika kama chakula kikuu kwa Majimoto; wakati huo huo, wadudu hao hunufaika kwa ulinzi toka kwa Majimoto dhidi ya adui wa kila namna. Uhusiano huu hauleti madhara yoyote kwa wakulima wa korosho.

3.0 Matumizi ya Majimoto katika kuthibiti wadudu waharibifu
Tangu miaka ya nyuma (AD 304), Majimoto walitumika huko China kuthibiti wadudu waharibifu katika mazao kama vile michungwa. Katika nchi ya Tanzania, matokeo ya majaribio yameonyesha kwamba Majimoto ni wadudu mashuhuri sana katika kuthibiti mbu wa mikorosho na minazi. Mikorosho yenye Majimoto wengi haishambuliwi na mbu kulinganisha na ile isiyo nao. Majimoto wakitanda kwenye machipukizi, maua au tegu, hufanya ulinzi mzuri sana dhidi ya mashambulizi ya mbu waharibifu. Asilimia 65 ya mashamba ya korosho Kusini mwa Tanzania, tayari kuna makoloni ya wadudu hawa, lakini siyo mikorosho yote katika shamba ina Majimoto na asilimia 85 ya michungwa yote Tanga ina makoloni ya majimoto Hivyo, kuna haja kubwa ya kuwaneemesha Majimoto

:
3.1 Jinsi ya kuwaneemesha Majimoto.
Majimoto kama rafiki wa mkulima wanahitajika waneemeshwe ili waongezeke na wawe wengi katika mikorosho ili kufanya ulinzi thabiti dhidi ya wadudu waharibifu. Mbinu ambazo hutumika kuwaneemesha Majimoto ni pamoja na:
• Kuhamisha na kupandikiza Majimoto

Majimoto wanaweza kuhamishwa toka mti mmoja na kupandikizwa katika mti mwingine. Viota vya Majimoto vinaweza kukatwa toka mti mwingine na kufungiwa katika matawi ya mti mwingine, hasa karibu na eneo lenye machipukizi mapya. Majimoto hawa wanaweza kujijenga, kuzaliana na kuanzisha makoloni mengine mapya katika miti waliohamishiwa. Hii inadhihirika kwa ongezeko la idadi ya viota vinavyojengwa wiki moja hadi nyingine.
Angalia: Majimoto wa koo/familia mbili tofauti wanaweza kudhuriana. Uangalifu ufanyike kiasi kwamba upandikizaji wa Majimoto ufanyike kwenye mti ambao hauna kundi lingine ili kuepuka ugomvi na mauaji baina yao.

• Kueneza kwa njia ya kamba


Majimoto wanaweza kuenezwa kwa kutumia kamba kutoka mti mmoja hadi mwingine, ili kuifanya kamba kama daraja la juu kwa juu. Kamba inapaswa kufungwa kwenye tawi karibu na kiota cha Majimoto nao wataweza kupita hadi mkorosho mwingine na kuanzisha makoloni mapya hatimae kuzidi kuongezeka.
Majimoto hupendelea kupita kwenye kamba za kienyeji na hasa kamba zitokanazo na ukindu au magome ya miti. Hawapendelei kupita kwenye kamba za viwandani, hivyo epuka kutumia kamba ya katani au nailoni kwa ajili ya kazi hii na pia usishike kamba ya kienyeji kama umeshika vitu vyenye harufu kali kama mafuta ya kujipaka.

• Kuthibiti adui wa Majimoto


Imefahamika kwamba jamii ya Sisimizi (Pheidole megacephala) pichani juu na Sangala ni maadui wa Majimoto. Miti ambayo imetawaliwa na wadudu hawa, ni vigumu kukuta Majimoto wakijitawala. Ili kuwaneemesha Majimoto, inatupasa kuwadhibiti wadudu hawa.
Dawa ya AMDRO ndiyo itumikayo kuangamiza sisimizi. Dawa hii iliyo kama sukari, hunyunyizwa kuzunguka shina la mti lenye sisimizi. Kiasi cha gramu 4 za dawa hii kwa mti, inatosha kuthibiti sisimizi. Dawa inarudiwa tena endapo dalili za sisimizi kujitokeza tena zitaonekana.

Jinsi ilivyotengenezwa dawa hii, sisimizi huonekana kuipenda sana; maana, mara tu baada ya kunyunyiza, huibeba na kumpelekea malkia wao, ambaye baada ya kula hufa akifuatiliwa na ukoo mzima wa sisimizi. Kwa hiyo baada ya siku mbili tatu hivi, sisimizi wote watakuwa wamekufa, hivyo kutoa nafasi kwa Majimoto kuweza kutawala eneo lote.



Sangala hawadhuriki na dawa hii ya Amdro, badala yake, utafiti unaendelea kufanyika ili kupata dawa ya kuwathibiti sangala. Hata hivyo, grisi ya miti na wakati mwingine oili chafu, hutumika kuzungushia kwenye mashina ya miti iliyoshambuliwa na sangala ili kuwadhibiti wasipande juu. Matumizi ya ile kamba ya kuhamishia Majimoto kama daraja la juu

Friday, June 26, 2009

NAZI

MNAZI



Tumezoea kwamba siri ya umri mrefu ni maji, lakini si maji peke yake ila yaambatane na ulaji mzuri, leo nawaletea siri ya NAZI ambazo ni zao la mti wa mnazi (cocos nicifera) ambao uko katika jamii ya mipama (palms) inayojumuisha miti kama michikichi, mitende na mingineyo tuyoitumia kama mapambo

NAZI KABLA YA KUFULIWA MAGANDA


Mti wa mnazi au MTI WA UHAI kama ninavyouita ni mmea unaostawi na kupatikana kanda za pwani na sehemu zenye joto, mikoa kama Tanga, Dar, Pwani, Mtwara, Lindi, Mafia na Zanzibar hupatikana kwa wingi. Kila sehemu ya mti huu inatumika katika maisha ya kila siku ya mwanadamu, makuti kuezekea na kutengenezea mafagio, tunda lake ni chakula, maganda ya nazi kwa ajili ya kuzuia upotevu wa maji kwenye bustani/shambani (mulching) magogo hutoa mbao na hutumika kutengenezea mitumbwi, na sehemu yoyote ya mnazi huweza kutumika kwa ajili ya kupikia kuanzia makuti, mahanda, vifuuu n,k

NAZI BAADA YA KUFULIWA


Jamii za watu wanaotumia sana nazi huwa hazishambuliwi na magonjwa kama kisukari, presha ya kupanda na magonjwa mengine ya moyo na kiasi kikubwa cha lehemu (cholesterol) mwilini ukilinganisha na jamii zinazotumia vyakula vyenye kupikwa na mafuta yanayotokana na mimea mingine kama karanga, alizeti, ufuta, mahindi n.k. kwa mfano mikoa kama Tanga na Zanzibar ambako kwa wastani mtu hutumia kiasi cha nazi 120 kwa mwaka katika vifo 1000 vya watu wazima ni vifo 1 – 2 vinavyohusiana na magonjwa ya moyo wakati mikoa ambayo hawatumii nazi karibu robo ya vifo hutokana na magonjwa ya moyo.

MAHANDA YA NAZI



Kuna taarifa kwamba nazi huongeza kiasi cha lehemu mwilini je ni vipi? Ukweli ni kwamba nazi inayotumika moja kwa moja yaani inakunwa na kupikiwa hapo hapo haina madhara ya lehemu, ila nazi inayohifadhiwa ndio huwa na tatizo hili kwa sababu huchanganyika na hewa ya haidrojeni (hydrogenation) na kuwa sawa na yale mafuta mengine ya viwandani KWA HIYO nazi iliyohifadhiwa baada ya kukunwa au tui lililohifadhiwa huweza kusababisha kuongezeka lehemu mwilini

NAZI ILIYOVUNJWA


Moja kati ya vyakula vichache duniani ambavyo walaji hawana mzio (allergy) nacho ni nazi, pia inasifika kwa kupunguza kiasi cha sukari mwilini, maji ya dafu husafisha figo na kibofu

NAZI ILIYOKUNWA TAYARI KUTENGENEZEWA TUI


MAHANDA YA NAZI YAKIZUIA UPOTEVU WA MAJI KWENYE CHUNGU CHA MAUA

Saturday, June 20, 2009

MMBONO- JATROPHA (bio diesel)

1.0 UTANGULIZI
Mmbono kwa kitaalam Jatropha curcas ni mti jamii ya nyonyo wenye mbegu zitoazo mafuta yenye sifa kama nyonyo. Huota kwenye maeneo ya nyanda kame na yenye upungufu wa rutuba. Mmea hauliwi na mifugo wala wanyama pori na kufanya mmea ufae kulimwa kwenye maeneo ya wafugaji huria. Mmea hutoa mbegu zenye mafuta ambayo hayaliwi bali hutengenezea sabuni, kuendesha mitambo, gesi kama nishati. Kutokana na faida nyingi kwa binadamu kiafya, kiuchumi na mazingira, mmea unaweza kuzalishwa kama zao. Mmea huu umetokea Marekani ya Kati na kusambazwa hadi Afrika Mashariki na Wareno.

2.0 AINA
• Mmea ni wa jinsia moja (monoecious) na maua yake huwa ya jinsia moja.
• Mmea unaweza kudumu hata zaidi ya miaka 50.
• Kuna aina tatu za mmea ambapo aina moja iliyopo Mexico huliwa baada ya kukaangwa.
• Kwa sasa aina inayopo hapa Tanzania; Jatropha curcas haifai kuliwa bali kwa matumizi mengine.




3.0 MAZINGIRA:
Mmea huweza kustawi katika mvua za kuanzia 250mm hadi 2380, lakini uzalishaji mzuri huwa kwenye 625mm – 750mm. Kwenye sehemu zenye unyevu wa kutosha, mkulima atapata matunda wakati wote wa mwaka.Mmea hustawi kwenye nchi za Kitropiki na una tabia ya kustahimili ukame. Mmea hustawi kwenye udongo usiotuamisha maji, wenye tindikali kuanzia Ph 4.5. Mmea hupatikana kwenye mwinuko kuanzia mita 0 hadi mita 1600 juu ya usawa wa bahari ila hustawi vizuri kati ya mita 450-750 juu ya usawa wa bahari.

4.0 UTAYARISHAJI SHAMBA
Shamba litayarishwe mapema kwa kuchimba mashimo kabla ya mvua.

5.0 UTAYARISHAJI MBEGU/VIPANDIKIZI

Tumia mbegu zilizokomaa na kujaa vizuri. Mbegu zioteshwe katika vitalu ili kupata miche bora. Miche ikae kitaluni miezi 2 hadi 3. Kama utapanda moja kwa moja shambani, tumia kilo 5-6 kwa hekta. Au pandikiza vipandikizi vyenye urefu wa sm 45–100 katika shimo la sm 30. Mbegu huota kuanzia siku 9 na kutoa matunda baada ya miaka 3–4. Vipandikizi hutoa matunda kuanzia miezi 9 kutegemea na sehemu.

6.0 KUPANDA KWA NAFASI.

Panda mbegu 2 kwa shimo kwa kina cha sm 2 hadi sm3. Nafasi kati ya mche ni 2.5m x 2.5m.Nafasi kama hiyo hukupatia miti 1600 kwa hekta moja.Aidha nafasi ya 3mx3m itumiwe katika kilimo mchanganyiko wa mibono na mazao mengine.

7.0 PALIZI NA KUPUNGUZA MICHE
Punguzia miche baada ya wiki 4 na kubakiza mmoja, kutegemea na utayarishaji shamba. Palizi sio lazima ifanyike isipokuwa kama umefanya kilimo mchanganyiko palizi inaweza kufanyika kwa kuzunguka mmea au kufyeka magugu mara moja kwa mwaka. Kukata matawi kufanyike baada ya mwaka mmoja au miwili.

8.0 KUZUIA MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU
Hakikisha mimea haisongani na shamba ni safi. Mmea haushambuliwi na magonjwa ila wadudu jamii ya beetle, golden flea beetle wanashambulia majani. Athari ya mavuno hutokea endapo uharibifu katika majani utafikia zaidi ya asilimia 40. Mkulima afanye ukaguzi wa shamba lake mara kwa mara na kuwasiliana na wataalam wa kilimo kabla ya kupiga madawa.




9.0 UVUNAJI
Matunda yaliyokomaa tayari kwa kuvunwa huwa na rangi ya kahawia. Uvunaji hufanywa wa mikono au kwa kupiga kwa fimbo au kifaa maalum kilichotengenezwa kwa kutumia waya, mfuko wa pamba na fimbo ndefu, mbegu huguswa na kipande cha waya na kudondoka kwenye mfuko au kitambaa kilichowekwa chini ya mmea.Kiasi cha kuanzia gramu 300 hadi kilo 9 za mbegu zinaweza kuvunwa kwa mmea au tani 2 – 6 kwa mwaka kwa hekta. Mti unaweza kutoa mbegu mfululizo kwa mwaka kwa sehemu zenye unyevu au kuzaa mara mbili kwa msimu sehemu zenye ukame.

10.0 HIFADHI YA MAZAO
Baada ya kubangua mbegu kwenye matunda zikaushwe vizuri kabla ya kuhifadhiwa kwenye mifuko ya plastiki/magunia. Hifadhi mavuno kwenye sehemu kavu na dhibiti viumbe waharibifu kama panya.


11.0 MANUFAA YA MMEA

(1)Mbegu hutoa mafuta mengi yanayotengeneza sabuni na nishati ya kuwashia taa, jiko na gas, nchi nyingi hutumia mafuta haya kama diesel. Nishati hiyo mbadala hupunguza kasi ya matumizi ya kuni/mkaa na hivyo kuhifadhi mazingira.
• Zao linafaa katika maeneo ya nyanda kame yenye migogoro ya wafugaji na wakulima kwa vile mmea hauliwi na mifugo.
• Baada ya kusindika mbegu, mashudu hutoa mbolea ya komposti yenye ubora kama mbolea ya kuku.
• Uzalishaji wake una gharama ndogo ukilinganisha na mazao mengine
• Kama zao, wakulima wataongeza pato na kupunguza kasi ya magonjwa ya ngozi.
• Kuzuia mmomonyoko wa udongo kwa njia ya upepo na maji.





12.0 MASOKO
Mmea hutoa bidhaa kama mafuta, sabuni, gesis na mbolea zenye manufaa mengi kwa jamii. Hivyo wakulima wazalishe kwa wingi, wafanye mikataba na wasindikaji, wasafirishaji na wanunuzi wa mazao, kutumia mbinu za masoko na kupata mafunzo ya kutosha ili kutosheleza mahitaji ndani na nje ya maeneo ya uzalishaji

Kuna baadhi ya wanamapinduzi ya kilimo wanaupinga mmea huu, wakiamini kwamba kwa sababu mkulima anapata hela nyingi na kwa muda mfupi, basi wakulima wengi wataacha kupanda mazao ya chakula na badala yake watapanda mmea huu. matokeo yake ni kuwa uzalishaji wa chakula utapungua sana duniani na kusababisha njaa

Saturday, June 13, 2009

MAZIWA YA NGAMIA NA KISUKARI

AINA ZA KISUKARI
Aina ya kwanza ya kisukari ni pale mgonjwa anapohitaji kutumia insulin kila siku, aina hii huwa ni asilimia isiyozidi 10 ya wagonjwa wote wa kisukari, miili yao huzalisha insulin kidogo sana au haizalishi kabisa.Aina ya pili ni ile ambayo mwili mgonjwa wa mgonjwa huzalisha insulin lakini mwili unashindwa kuitumia na baada ya miaka kadhaa mwili hushindwa kuzalisha insulin na kusababisha aina ya kwanza ya kisukari


MDAU AKIMKAMUA NGAMIA


Maziwa ya ngamia yamekuwa yakisifika katika kuwasaidia wagonjwa wa kisukari aina ya kwanza kama watakunywa maziwa haya kiasi cha nusu lita kwa siku. Kwa kawaida mgonjwa wa kisukari aina ya kwanza huitaji kiasi cha ankara 20 za insulin kwa siku lakini akitumia maziwa haya huitaji kiasi cha ankara 6 – 7 za insulin kwa siku.



Huko india katika jimbo la Rajasthan kuna jamii/ kabila linayoitwa Raica ambalo husifika kwa ufugaji wa ngamia, jamii hii husifika kwa kutokuwa na wagonjwa wa kisukari isipokuwa kati ya wale wachache ambao huwa hawatumii kabisa maziwa ya ngamia




Maziwa ya ngamia pia husifika kwa kusaidia wagonjwa wa shinikizo la juu la moyo, pia husaidia katika kupambana na vimelea kama virusi na bakteria. Kwa mfano mgonjwa wa kifua kikuu anayaetumia dawa na maziwa ya ngamia hupata nafuu haraka zaidi ya yule asiyetumia maziwa ya ngamia

Sunday, June 7, 2009

UTUPA - DAWA YA KUULIA WADUDU

Huu ni mmea unaopatikana zaidi sehemu zenye baridi na nyanda za juu na unastawi sehemu zenye mvua za wastani na nyingi, huwa hauhimili ukame. Ni mmea unaokua haraka na kusambaa kama usipodhibitiwa, baadhi ya nchi umepigwa marufuku kupanda kwa sababu ya kutishia uoto wa asili



MATUMIZI
KUFUKUZA PANYA / MCHWA

Kama shamba lako limevamiwa na panya wanaochimba ardhini, panda huu mmea pamoja na mazao mengine kwa umbali wa mita 3 kila upande (3m * 3m) na mpakani mwa shamba lako, baada ya mwaka mmoja shaba halitakuwa na mashimo ya panya. kwa njia hii hii pia utafanikiwa kufukuza mchwa, kwenye majumba unaweza kuupanda kwenye kingo za nyumba na mpakani, kama kuna kichuguu cha mchwa panda miche hii na kichuguu kitakufa baada ya mchwa kuhama.

KUOGESHEA MIFUGO
Chukua kiasi cha kilo moja ya majani ya utupa na maji lita 25 loweka kwa masaa mawili (2) mpaka matatu (3) au chemsha kwa dakika 30 na lita 27 za maji, chuja kwa kitambaa kisha weka kwenye bomba lakuogeshea changanya na sabuni ya unga kidogo ili iweze kunata kwenye mwili wa mnyama wako na hapo inakuwa tayari kwa matumizi ONYO usitumie kuogeshea nguruwe hawana uwezo wa kuhimili dawa hii kwenye ngozi zao




KUNYUZIA SHAMBANI / BUSTANI
Chukua kiasi cha kilo moja ya majani ya utupa na maji lita 5 loweka kwa masaa mawili (2) mpaka matatu (3) au chemsha kwa dakika 30 na lita 6 za maji, chuja kwa kitambaa kisha weka kwenye bomba na uanze kunyunyuzia shambani au majumbani kwa minajili ya kuua wadudu kama mbu, mende, n.k

KUHIFADHI NAFAKA KWENYE GHALA
Chukua gram 100 za unga wa majani ya utupa changanya na mahindi au maharage kilo 100, funga vizuri gunia lako na hifadhi kwenye ghala. Dawa hii huwa na nguvu kwa muda wa mwaka mzima.

MBEGU ZA UTUPA



MATUMIZI MENGINE
Mmea huu ukipandwa mchanganyiko na mazao mengine huongeza rutuba ardhini kwa kuongeza kiasi na naitrojeni, mbegu zake hutumika kama chanzo cha protini kwenye ufugaji wa mbuzi ila zisiliwe nyingi kwani ni sumu, Unga wa mbegu zake unauwezo wa kusababisha samaki wapooze (paralyze)unga wa utupa gram 1 na maji lita 2.5 hutumika kama dawa ya minyoo kwenye ngombe na mbuzi kwa kiwango cha 1cc kwa kilo 10 za mnyama,

Wednesday, June 3, 2009

UJENZI WA BARABARA KISARAWE MPAKA KAZIMZUMBWI




Jumatatu nilikuwa nimeenda Kisarawe maeneo ya visegese (SHAMBA) ndio nikakutana na huu ujenzi wa barabara ambao uko katika hatua za matayarisho. Nilipoongea na wahusika wa kampuni ya ujenzi ya SKYLINK waliniambia barabara hiyo ya lami itakwenda mpaka maeneo ya kijiji cha Kazimzumbwi ambako kunatarajiwa kujengwa kiwanda kipya cha saruji.

UPIMAJI UNAENDELEA


Ujenzi huu utakuwa faraja kwa wakazi wa kazimzumbwi na sisi wakulima wenye mashamba maeneo karibu na hayo, kwa mfano mimi kutoka Kisarawe mjini ambapo lami ilikuwa ndio mwisho wake nilikuwa naendesha kilometa 8 kwenye barabara ya vumbi, kwa sasa nitabakiwa na kilometa zisizozidi 2 kutokea Mpuyani ambapo huwa nachepuka kwenda kwenye barabara inayoelekea Kilvya.


VIJIKO KAZINI






Kiwanda cha saruji pia ni faraja kwa taifa kwani bidhaa hiyo imekuwa ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi kwa ujumla, wananchi wataajiriwa kama wafanyakazi na vibarua na hivyo kuongeza ajira, serekali kwa upande wake itanufaika na kodi ya mapato kutoka katika kiwanda hicho

KAMBI YA UJENZI

Friday, May 29, 2009

UTALII WA NDANI

PUNDAMILIA - MIKUMI



Nchi yetu Tanzania imebahatika kuwa na vivutio vingi vya utalii zikiwemo mbuga za wanyama, sehemu za kihistoria na sehemu za kijografia kama milima na mapango. Mara nyingi tumezoea kuona wageni wakija nchini mwetu kutalii na kutembelea vivutio vyetu wakati sisi wenyewe tukiwa wavivu kutembelea sehemu hizi adimu.

TWIGA - MBUGA YA ARUSHA


Kwa bahati nzuri mimi ni mtembezi/msafiri sana na ninapenda sana safari, hii imenisababishia kuweza kutembelea baadhi ya sehemu za utalii kama mbuga za Serengeti, Ngoro ngoro, Saadani, Mikumi, Manyara, Katavi, Arusha, Selous, sehemu nyingine za kitalii ni kama Kitulo, Amboni, Bagamoyo, msitu wa kazimzumbwi ulioko kisarawe, Kimondo cha Mbozi, daraja la Mungu Kiwira, Ziwa ngosi katika kreta iliyoko karibu na isangati katika safu za milima ya Rungwe na mara kadhaa nimeshiriki uwindaji katika mapori ya akiba.

TANDALA - KATAVI



Mara nyingi wizara ya utalii imekuwa ikihamasisha utalii wa ndani kwa kuweka ada ndogo kwa waTanzania kwenye mbuga zake, na mara nyingine huandaa safari za kitalii kwa gharama nafuu. Kwa Mfano mwaka jana wakati wa saba saba kulikuwa na safari za kutembelea mikumi kwa siku moja kutokea dsm kwa gharama za shilingi 10,000 kwa kila mtu, hii ilijumuisha usafiri na ada ya kuingia mbugani, Ukiangalia gharama halisi hiki kiasi kilikuwa kinatosha nauli ya kwenda tu mikumi nahisi watu walikuwa wanachangia mafuta tu lakini basi lilikuwa halijai watu kila siku ya safari.

FLAMINGO - ZIWA MANYARA


Kumekuwa na uhamasishaji wa wanafunzi kwenda mbugani wakati wa likizo, ambapo huchangishwa kiasi Fulani cha fedha na kisha kusafirishwa kwa pamoja kwa kutumia mabasi kwenda mbugani. Mara nyingi shule binafsi ndio zimekuwa zikijihusisha na safari hizi za utalii wa ndani, wakati kumekuwa na msukumo mdogo kutoka shule za serekali.

KIFARU - NGORONGORO


Utalii pia umekuwa na mwamko mdogo kutokana na gharama za usafiri na malazi, kwa sababu sehemu za kitalii zina malazi aghali hata kama utalala nje ya mbuga, kwa mfano mji wa mto wa mbu ulioko nje ya mbuga ya Manyara gharama ya malazi iko juu. Pia kuingia mbugani kunahitaji gari la 4WD ambalo itabidi ukodi toka kwenye makampuni ya kitalii na pia utajitaji mtu wa kukuongoza (guide) kwa wale walio karibu na mbuga hizi wanaweza kutumia usafiri binafsi ili kupunguza gharama.

SIMBA - SERENGETI

Wednesday, May 27, 2009

VUNJA - JUNGU




Huu ni msimu ambao huku kwetu wanakuwa wengi sana, hiki ni kipindi ambacho mvua zinaishia na kuelekea kwenye majira ya baridi (joto kupungua) hawa wadudu huzaana sana kipindi hiki na hujazana kwenye taa za majumbani na wakati mwingine huingia ndani

DUME



Kuna baadhi ya jamii huwakamata na kuwala kama vile kumbi kumbi na senene, lakini si wengi waliozoea kuona wakiliwa, ukimshika vibaya na anakapata nafasi anaweza kuku ng'ata ingawa hana sumu yoyote na kidonda chake ni kidogo kinachoweza kupona chenyewe.

JIKE



Kama una bustani ya maua na mboga mboga na unasumbuliwa na wadudu kuvamia mara kwa mara, basi unaweza kuwapandikiza wadudu hawa na wakakusaidia katika kuondoa wadudu waharibifu kwa njia ya kibaiolojia, kwa sababu wana tabia ya kula wadudu wengine kama chakula chao. ili kuweza kujua madume na majike angalia rangi zao, madume huwa na rangi zilizokooza na kijivu wakati majike huwa na rangi ya kijani kibichi


WAKIPANDANA