KURASA

Tuesday, May 4, 2010

JINSI YA KULIMA BUSTANI KWENYE ENEO LENYE MAJIMAJI

Kutokana na tatizo la bwana Chacha Wambura Ng'wanambiti katika post hii hapa http://mataranyirato.blogspot.com/2010/05/aisifuye-mvua-imemnyea.html nimeamua kutoa maelezo kwa ufupi jinsi ya kukabiliana na sehemu ambazo maji husimama wakati wa mvua



1- Lima na tifua udongo kwa kutumia trekta la mkono (power tiller) kiasi cha inchi 12 chini, udongo mwingine unaweza kuujaza kama matuta na kuweka mifereji pande zote la eneo lako. Kama huna trekta hili pia unaweza kutumia jembe la kukokotwa na ng’ombe (plau)

2- Jaza majani makavu, vijiti, maranda ya mbao n.k kiasi cha inchi 5 -6 halafu mbolea vunde au samadi kiasi cha inchi 4 halafu rudishia udongo wako juu yake na hapo utakuwa umeinyajua ardhi yako kiasi cha inchi 8 juu (kumbuka maranda na mbolea vitadidia kidogo) kisha pitisha harrow au jembe la kukokotwa na ng’ombe ili kuweza kuchanganya vitu hivi



3- Acha udongo wako ukauke kiasi cha siku 3 kisha pitisha harrow au jembe la kukokotwa na ng’ombe tena ili kuvunja vunja mabonge ya udongo yaliyotokea wakati wa udongo kukauka na pia kuchanganya mchanganyiko huu zaidi

4- Weka tena mbolea vunde au samadi kiasi cha nchi mbili juu ya mchanganyiko huu kisha panda mbegu au miche yako na uizungushie udongo kiasi

5- Mwagia maji kadri inavyo hitajika kama udongo utakuwa mkavu, na uendelee kufuata kanuni za kilimo bora kama inavyoshauriwa kitaalamu

Friday, April 30, 2010

MSEELE - delonix elata

Kutokana na maombi ya ndugu Godleader A Shoo alitaka kujua matumizi ya mti wa mdodoma, mti huu hujulikana kitaalam kama delonix elata na jina la kiswahili ni mseele lakini watu wengi wanauita mdodoma kwa sababu imepandwa sana Dodoma na hii inatokana na kuhimili kwake hali ya ukame



Miti hii inauwezo wa kuhimili joto kali na baridi ya wastani kwa hiyo inaweza kuota ukanda wa pwani hadi ukanda wa akti mikoa ya Dodoma, Singida, Shinyanga n.k

MATUMIZI
1- Wengi huipanda kwa ajili ya mapambo na hii hutokana na mwonekano wake mzuri na pia maua yake yanapochanua hupendeza pia
2- Kwenye miti hii tunapata pia kuni kwa ajili ya kupikia na ndio maana hupandwa sana maeneo makame kwa sababu pia inakuwa haraka kiasi
3-Nguzo za kujengea pia zinapatikana kama mti utaacha ukue, nguzo si kubwa sana lakini kwa nyumba za vijijini zinatosha kabisa, pia nguzo hizi huweza kutoa mbao
4- Dawa za magonjwa mbali mbali kama vile majani yakipondwa husaidia kupunguza uvimbe na pia kupunguza sumu ya wadudu kama nyuki, manyigu, na nge. Pia mizizi yake ikichemshwa na kunywewa husaidia matatizo ya tumbo
5- Majani yake huweza kutumika kama chakula cha mifugo, ukipanda miche hii hakikisha hamna wanyama kama mbuzi na Ng'ombe maana wataila ikiwa midogo

MAUA YA MSEELE

Friday, April 23, 2010

FUNGATE LA MKULIMA

Tukiwa na babu na bibi yangu mzee Msumari nyumbani kwake Makorora Tanga, huyu ni mdogo wa mwisho wa Bibi mzaa Baba na ndiye aliyebakia pekee



Tunapata msosi na my wife wangu tukiwa kijijini kwetu, hapa ni Ugali, kuku wa kienyeji na Mchunga bila kusahau ngogwe na chachandu la mbilimbi halafu tunashushia na mnazi au boha



Kaburi la Marehemu Baba yangu mzee Reginald Bennet huko Muhinduro Tarafa ya Maramba Wilaya ya Mkinga Mkoa wa Tanga




Hili ni kaburi la marehemu Bibi mzaa Baba aitwaye Perpetua Mohamed kijijini kwetu Muhinduro Tarafa ya Maramba Wilaya ya Mkinga Mkoa wa Tanga


Wife akishangaa machungwa, yakiwa madogo hivi tunaita mawashata taa



NB Picha za tukiwa Lushoto na Pangani sitaziweka humu kutokana na maombi ya mke wangu (privacy)

Friday, March 26, 2010

KONDOO AKISAIDIWA KUZAA WATOTO MAPACHA

JINSI YA KUKATA MICHE YA MISOJI (MITIKI)

Kwa kawaida miche ya misoji mara baada ya kutolewa kwenye kitalu huitaji kukatwa, mjasiliamali aliyeko jijini Mwanza aitwae NAYMA aliniomba nimwelekeze kwa picha na mimi bila hiyana nilikwenda shamba na kung,oa mche mmoja na kuukata na kuupiga picha kabla ya kuukata na baada ya kuukata ili kupata kipandikizi

MCHE KABLA YA KUKATWA (angalia mishale kujua sehemu za kukata)


Mche wangu niliukata na kuacha kiasi cha nchi mbili au pingili mbili za vidole kwa sehemu ya juu ya mzizi na kwenye mzizi niliondoa ile sehemu nyembamba ya chini, kwa kawaida hii sehemu ya chini hufa mara baada ya kupandwa kwa sababu sehemu nene/kubwa ya mzizi inayoachwa ndiyo huifadhi maji na chakula cha mmea, nadhani hapa nitakuwa nimemsaidia kama bado nipigie kwenye ile namba niliyokupa

KIPANDIKIZI TAYARI KWA KUPANDWA


Kumbuka wakati wa kupandwa lazima uweke kisahani ili kiweze kukusanya maji kwa ajili ya ukuaji mzuri, kama ni udongo unaotuamisha maji usiweke kisahani bali wekea kama tuta au mwinuko

WEKA KISAHANI KAMA UDONGO HAUTUAMISHI MAJI


WEKA TUTA KAMA UDONGO UNATUAMISHA MAJI

Friday, March 19, 2010

MBWA WAKIPANDANA KWA NINI HUNASIANA AU KUNATANA?



Nadhani karibia kila mtu ameshawahi kuona mbwa wakipandana, kama bado basi maelezo haya yatakusaidia siku ukiwaona, mara baada ya mbwa dume kumpanda jike utaona dume anageuka na kupeana mgongo na jike kila mmoja akiangalia upande wake wakati huo huo, uume ukiwa bado ndani ya uke, wanakuwa kama wanavutana na wakati mwingine wanaweza kutoa milio kama wanalalamika, unaweza kuhisi wanaumia na ukataka kuwatenganisha ACHA na wala usijaribu kufanya hivyo utawaumiza.

Kwa kawaida mbwa dume anapoanza kumpanda jike uume unakuwa haujasimama bali husaidiwa na kiuongo kijulikanacho kama baculum, hii ni tishu kama mfupa na iko ndani ya uume wa mbwa. Wakati mbwa dume anapotaka kumwaga manii ndani ya uke ndipo damu hujaa kwenye uume na hapo uume hutanuka (kudinda) kwa hiyo akimaliza kutoa manii uume hunasa ndani ya uke kwa sababu ya kule kutanuka.



Mbwa dume anapogeuka anazipa muda Mbegu za kiume ziweze kuingia vizuri kwenye uke na hivyo kusababisha ujauzito, ukitumia nguvu kuwaachanisha, mbali na kuumia pia jike hataweza kupata ujauzito. Hiki ni kitu cha asili kwa hiyo husaidia pia kuzuia madume mengine yasiingilie tendo hili na kulikatisha wakati Mbegu bado zinaogelea na kuyafuata mayai kwenye mji wa mimba, kwa kawaida hata kama mbwa madume walikuwa wanapigana kila mmoja akitaka kumpanda jike, mara baada ya Yule aliyefanikiwa kupanda na kugeuka wale wengine huacha vurugu zote.

MBWA WALIONASIANA BAADA YA KUPANDANA


Tendo hili huchukua kati ya dakika 20 – 30 na mbwa hufanikiwa kunasuka mara baada ya damu kupungua kwenye uume na uume kusinyaa na kupungua ukubwa. Kwa mbwa dume ambaye ni mara yake ya kwanza kupanda basin a hata yeye huchanganyikiwa atakapoona amenasa, anaweza hata kujaribu kujinasua au kupiga kelele, unachotakiwa ni kumshika shika shika mbwa wako kichani huku ukimuongelesha kwa upole, yaani jaribu kumpunguza presha ili atulie

Monday, March 8, 2010

KILIMO CHA UYOGA

Miaka ya karibuni, utaalamu wa kuotesha uyoga umeanza hapa Tanzania baada ya watu kutilia maanani lishe bora ya protini na manufaa mengine ya zao hilo. Kwa kuwa uyoga upo wa aina mbalimbali, usitawishaji wake hutofautiana katika mahitaji yake, ikiwa ni pamoja na hali ya hewa, malighafi za kuoteshea, urahisi wa teknologia ya kuotesha katika mazingira ya Tanzania na soko lake kwa wananchi na katika hotel. Hata hivyo ni wananchi wachache tu wanaojua kilimo cha uyoga.



Uyoga unaozalishwa unafahamika. Aina zinazofaa kwa Tanzania ni zile ambazo hustawi vizuri, kwenye maeneo ya joto la wastani wa nyuzi joto 20C hadi 33C. Kwa mfano uyoga aina ya mamama n.k. Aina hizi za uyoga pia uhitaji hali ya unyevu hewani (moisture) wa kiasi cha asilimia 75%.

UOTESHAJI WA UYOGA
Kabla ya kuanza kuzalisha uyoga inabidi kuwa na chumba chenye paa ambalo litazuia jua, mvua, na vumbi. Chumba hiki kinatakiwa kiwe na sakafu inayohifadhi unyevunyevu pamoja na sehemu ya giza ambayo ni muhimu kwa kuotesha utando wa uyoga. Mkulima
wa kawaida anaweza kutumia kasha kama sehemu ya giza.

Mbegu za uyoga huzalishwa kwenye maabara zenye vifaa vinavyowezesha kuotesha mbegu hizo bila kuchafuliwa au kuchanganyika na vimelea kama bakteria, ukungu au jamii
nyingine za uyoga ambazo haziliwi. Hapa Tanzania hivi sasa maabara hizo zipo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kituo cha utafiti wa kilimo-Uyole na taasisi ya utafiti wa kilimo cha bustani- Tengeru (HORTI
Tengeru, Arusha).


HATUA MUHIMU ZA KUOTESHA UYOGA
Hatua muhimu za kuotesha uyoga baada ya kupata mbegu ni kama ifuatavyo:
Kusanya masalia ya mazao kama vile mabua, majani ya mpunga, ngano, pumba za mpunga au mahindi, masalia ya miwa baada ya kukamua nk. Vitu hivi hutumika kama mali
ghafi kwa kuoteshea uyoga.
Mabua, majani ya mpunga au migomba yakatwe kwa urefu usiozidi sm 6, au urefu wa vidole kwa kutumia panga au kisu.
Loweka mali ghafi kwenye maji ya kawaida kwa muda wa siku nzima (masaa 24).
Kisha yachemshe kwa muda wa saa mbili ili kuua vijidudu pamoja na vimelea vilivyomo.
Ipua na umwage maji yote halafu tandaza kwenye kichanja kisafi ili yapoe bila kuchafuliwa na vumbi au vijidudu.
Kisha jaza mali ghafi hii katika mifuko ya nailoni tayari kwa
kupanda mbegu.

NAMNA YA KUPANDA
Kuna aina mbili za upandaji

AINA YA KWANZA


Chukua mfuko wa nailoni wenye upana wa cm 40 - 45 na kimo cm 75. Weka tabaka la mali ghafi ya kuoteshea yenye kina cha sm 10 katika mfuko halafu tawanya mbegu ya uyoga juu yake. Baada ya kuweka mbegu, weka tena tabaka nyingine ya vioteshea na kuweka
mbegu juu yake. Endelea kuongeza tabaka kwa namna hii mpaka ifike ujazo wa robo tatu ya mfuko.

AINA YA PILI

Changanya malighafi ya kuoteshea (baada ya kuchemshwa na kupoa) na mbegu ya uyoga katika uwiano wa 1: 25 (mbegu : malighafi ya kuoteshea) kwa uyoga aina ya mamama (Pleurotus spp.)Kisha mchanganyiko huo ujazwe katika mifuko ya nailoni mifuko hii
iwe na ukubwa wa cm 20 kwa cm 40 ambamo unaweza kujaza kilo 1 – 1.5 ya mali ghafi ya kuoteshea.

Funga mifuko na toboa matundu kwenye mifuko yenye kipenyo cha cm 1 kwa kila umbali wa cm 6 hadi 10 kwa kila mfuko.Matundu yawe mengi ili kuingiza hewa ya kutosha ndani ya mifuko. Kumbuka uyoga ni kiumbe hai hivyo unahitaji kupumua kama inavyoonekana kwenye picha hapo chini.



MATUNZO
Weka mifuko kwenye chumba cha giza. Kwa mkulima wa kawaida waweza kutumia kasha lisilopitisha mwanga kama chumba cha giza. Acha mifuko humo kwa muda wa siku 14 - 21 bila kufunua ili ukungu mweupe uweze kutanda vizuri.Utando wa uyoga ukishatanda vizuri kwenye mali ghafi ya kuoteshea, hamishia kwenye chumba chenye mwanga na hewa ya kutosha kisicho pigwa na jua. Katika chumba chenye mwanga, mifuko inaweza kuwekwa
kwenye, meza, chanja la waya au miti. Mifuko inaweza pia kuning’inizwa kwenye kamba toka kwenye boriti za paa la chumba hicho. Unatakiwa kudumisha hali ya unyevu kwenye chumba hicho cha mwanga kwa kumwaga maji sakafuni. Ukiona vipando vinakauka
unaweza kunyunyizia maji yaliyochemshwa na kupoa juu ya mifuko mara tatu au zaidi kwa siku. Tumia bomba la mkononi lenye ukubwa wa lita moja kunyunyizia maji.
Tafadhali: usizidishe maji kwani maji yakiwa mengi sana yaweza kuozesha uyoga uliyoanza kuota. Aina nyingi za uyoga huanza kutoa vichwa (pini) siku 2 - 3 baada
ya kuwekwa kwenye mwanga.

UVUNAJI
Uyoga huwa tayari kuchumwa siku tatu baada ya vichwa /pini kuonekana.
Uyoga uvunwe kwa mkono kwa kushika katikati ya shina la uyoga kisha zungusha hadi uyoga ung’oke. Usiondoe kichwa peke yake katika kuvuna uyoga kwani kubakiza shina huzuia uyoga mwingine kutokea. Mkulima anatakiwa ajue soko la uyoga kabla ya kuvuna ili kuepuka gharama za kuhifadhi. Kwani uyoga ukishavunwa unatakiwa uliwe
kabla haujaharibika.

JINSI YA KUHIFADHI
i) Unaweza ukauweka uyoga kwenye mifuko ya karatasi na kuhifadhi kwenye jokofu.
ii) Unaweza ukauanika juani hadi ukauke na kuweka kwenye mifuko ya nailoni liyofungwa vizuri ili isipitishe hewa na unyevu.

SOKO LA UYOGA
i) Watu wengi hupenda uyoga mbichi uliotoka shambani wakati huo huo kama kitoweo, kwa kutumia kama nyama, samaki, au kama kiungo.
ii) Unaweza kuuza uyoga mbichi kwa bei ya shilingi 3000/= hadi 5000/= kwa kilo kwa uyoga aina ya mamama.
Pia unaweza kuuza nje ya nchi ikiwa uyoga wako ni kiasi kikubwa na uko katika viwango vinavyo kubalika kimataifa.



MAMBO YA KUZINGATIA
Uzalishaji wa uyoga huzingatia sana hali ya hewa na vifaa ulivyonavyo, hivyo basi, kabla hujachagua aina ya uyoga unaotaka kupanda pata ushauri kwa wataalamu walio
karibu nawe.

Ukishanunua mbegu, kama hupandi kwa muda huo, hakikisha umehifadhi mbegu hiyo kwenye jokofu. Kama huna jokofu la kuhifadhia, nunua mbegu baada ya kuandaa kila kitu. Hata hivyo, uotaji wa mbegu huwa mzuri kama zitakaa nje ya jokofu kwa siku mbili.

Mbegu za uyoga huwekwa ndani ya chupa yenye ujazo wa mililita 300, waweza kutumia chupa moja katika kupanda kwenye kilo 15 ya mali ghafi ya kuoteshea. Hakikisha
unamaliza mbegu yote iliyo ndani ya chupa kwani ikibaki itapata maambukizo ya vimelea.
Hakikisha unaponunua mbegu iwe ni nyeupe. Mbegu ambayo siyo nyeupe ni dalili za maambukizo ya vimelea vingine na hivyo haifai kwa kupanda.

Hakikisha chumba cha kupandia ni kisafi na hakipati vumbi toka nje ili kuzuia maambukizo ya magonjwa ya uyoga.

Usimwagilie uyoga maji yasiyochemshwa kwani maji hayo mara nyingi si salama. Yaweza kusababisha vimelea vingine kuota, kwani uyoga ni dhaifu kuhimili ushindani wa
vimelea.

Pia waweza kusababisha magonjwa ya uyoga ambayo kutibu kwake kunahitaji kutumia dawa za viwandani ambazo ni sumu na hivyo kusababisha madhara kwa mlaji. Unaweza kupata faida nyingi kutokana na uzalishaji wa uyoga,

FAIDA ZA UYOGA:-
Lishe kama protini inayolingana na ile ipatikanayo kwenye maziwa, samaki na kunde. Pia utapata vitamini B, C, na D, na madini ya joto, phosphoras, chuma na potashi.

Uyoga husadikika kutibu maradhi kama kifua kikuu, kisukari, moyo, shinikizo la damu na figo.

Masalia ya mazao hutumika katika kuzalishia uyoga, na baada ya kilimo cha uyoga yanaweza kutumika kama mbolea asili kwa kilimo cha bustani. Masalia ya kilimo cha uyoga pia hutumika kama chakula cha mifugo kama ng’ombe.

Kilimo hiki huhitaji eneo dogo sana la ardhi na kiasi kidogo cha maji, hivyo hupunguza tatizo la ukosefu wa ardhi na ugomvi katika jamii ambao unatokana na tatizo hilo.

Kilimo hiki ni njia nyepesi ya kutoa ajira kwa familia kutokana na gharama ndogo, teknolojia rahisi inayotumika na pato lake kubwa.

Sunday, February 21, 2010

MAKAKARA - PASSION FRUITS

Ni mimea inyotambaa na kuhimili hali nyingi za hewa (sio ukame) mme huu hustawi zaidi ukanda usio na baridi wastani wa 20c – 30c na kiasi cha mvua 1500mm za ujazo kwa Mwaka, tunda huwa na ukubwa wa sentimeta 10 kwa kipenyo na uzito gramu 90, kuna aina kadhaa za matunda haya lakini yale ya kijani/manjano hustawi zaidi ukanda wa pwani na yale yenye wekundu Fulani hustawi zaidi maeneo ya misitu, hupendelea udongo wa kichanga wenye mbolea na usiotuamisha maji, pia udongo usiwe na chumvi nyingi na pia kusiwe na mwamba chini kasi cha mita moja tu.



UPANDAJI
Mbegu zipandwe kwanza kwenye mifuko ya plastiki yenye udongo wenye rutuba ya kutosha , kiasi cha Mbegu 3 kwa kila mfuko na mara zinapoota mimea ikingwe na jua kali na ikifikia urefu wa sentimeta 30, huweza kuhamishiwa shambani
Kwenye shamba lako hakikisha kuna nguzo zenye waya mmoja kwa ajili ya mimea kutambaa juu yake, sehemu ya juu baada ya nguzo kuzikwa chini ibakie kama mita mbili na kati ya msatari na mstari iwe ni mita 2 (ukanda wa pwani ) na mita 3 ukanda wa juu kiasi, na umbali kati ya nguzo na nguzo kwenye mstari ni mita 6, na mimea ipandwe umbali wa mita 3 kati ya nguzo na nguzo kufuata mstari.



UANGALIZI
MBOLEA

Mbolea za viwandani ziwekwe kutokana na hali ya udongo, muone afisa ugani kilimo ili afanye vipimo kujua mahitaji na upungufu wa udongo,

MAGONJWA WADUDU
Wadudu kama chawa wa mimea na mchwa wekundu ndio adui wa makakara, pia fangasi husshambulia sana maua ya makakara. Dawa za jamii ya kopa zitumike mara dalili za magonjwa au wadudu kuonekana, kiasi cha kilo 2.8 – 3 hutosha kwa hekta moja au gramu 225 kwa ajili ya dumu moja la lita 20

MAGUGU
Makakara yanatakiwa yawe kwenye shamba safi lisilo na majani na magugu, jembe la Mkono au madawa kama ROUND-UP na GRAMOXONE ynaweza kutumika mimea ikishaefuka na kuwa juu kwenye waya

KUFUNDISHA MIMEA
Ni lazima kuyafundisha matawi mawili ya kwanza kwa kuyaelekeza kutambaa kwenye waya kila moja likielekea upande wake na matawi yatakayoota kutokana na matawi makuu nayo yaelekezwe juu kwenye waya yakifikia ukubwa wa sentimeta 30 – 40



KUPUNGUZA MATAWI
Silazima kupunguza matawi kwa sababu mmea mkubwa zaidi ndio hutoa matunda mengi zaidi, labda kama kuna matatizo katika uchumaji ndio unaweza kupunguza baadhi ya matawi kiasi.

UVUNAJI

Uvunaji huanza baada ya miezi 8 – 9 baada yam mea kupandwa na matunda hukusanywa baada ya kudondoka yenyewe chini baada ya kuiva kila baada ya wiki moja, matunda yahifadhiwe sehemu kavu na isiyo na joto , kiasi cha tani 5 – 10 huweza kupatikana katika hakta moja kwa msimu

Monday, February 8, 2010

DARAJA LINALOISHI



Huko nchini INDIA sehemu za CHERAPUNJEE ambako ni eneo tengefu lenye majimaji ambako wanapatikana watu jamii ya KHASIS huwa wanatumia mizizi ya miti jamii ya mipira kutengeneza madaraja kwa ajili ya matumizi ya kila siku.



Wanachofanya ni kuielekeza mimizi ya mti husika kukua kuelekea upende wa pili wa mto, kwa kawaida miti hii huwa na mizizi ya chini ya udongo na ile ambayo hutokea kwenye matawi na kuelea elea hewani, kwa hiyo mizizi hii inayoelea hewani huongozwa kukua kufuatana na matakwa ya watu hao mpaka upande wa pili na hapo huachiwa ikue kwa kuingia ardhini ili kupata uimara unaohitajika.



Ili kupata daraja kamili na lenye uimara unaohitajika zoezi hili huchukua kati ya miaka 10 hadi 15, na yapo madaraja yenye hadi refu wa futi 100 na huwa na uwezo wa kuhimili jumla ya watu 50 kwa pamoja kama wote watakaa juu ya daraja husika. Kati ya madaraja hayo lililo maarufu zaidi hujulikana kama UMSHIANG DOUBLE DECKER ROOT BRIDGE ambalo kama jina lake lilivyo lina njia mbili ya juu na chini

DARAJA LA UMSHIANG


Sunday, February 7, 2010

MBUZI WA MOROCCO

Mbuzi unaowaona pichani hupatikana nchini MOROCCO, inasemekana ni kawaida kuwaona mbuzi wakiwa wamepanda juu ya hivyo vichaka ni kwa sababu wanafuata matunda yajulikanayo kama ARGO, kutokana na kuyapenda sana matunda hayo basi mbuzi hao hudandia juu ya matawi ya vichaka ili kupata matunda hayo



Tuesday, January 26, 2010

SIMBA MWENYE FADHILA



Mwaka 1969 John Rendall na Ace berg walimuona mtoto wa simba (dume) aliyekuwa anauzwa huko Harrods alionekana mpweke ndani ya kibanda chake kidogo na wakaamua kumnunua na kwenda naye nyumbani kwao ambako ni ghorofani na wakampa jina la Christian. Paroko wa kanisa moja aliwaruhusu kucheza naye katika viwanja vya kanisa lakini ndani ya muda mfupi simba alikuwa haraka na kuwa mkubwa ambako kwenye nyumba yao asingeweza kuendelea kuishi zaidi ya hapo.

Wakaamua kumrudisha kwenye mazingira yake ya asili kwenye mbuga za Afrika na baada ya Mwaka walipotaka kumtembelea waliambiwa ya kwamba amekuwa mkubwa na kuwa na milki yake na sasa amegeuka mnyama pori kamili kwa hiyo ni hatari kama simba wengine kwa maana hiyo wasingeweza kumsogelea karibu tena, pamoja na hayo bado waliamua kwenda kumuangalia hivyo hivyo, baada ya kumtafuta kwa masaa kadhaa walifanikiwa kumuona…….. ukiangalia kwenye video hii utaona jinsi alivyo warukia kwa furaha akiruka ruka, kucheza nao huku nao wakimkumbatia na wala hakuwa mkali au hatari kwao kama walivyoambiwa, na mwisho alikuja simba mwingine jike ambaye alikuwa ni mke wake kwenye hiyo milki yake na huyo simba jike naye akabaki akiwaangalia tu na wala hakuwashambulia ( ni kama naye alitambulishwa)

Saturday, January 23, 2010

VODACOM NA WAATHIRIKA WA MAFURIKO



Katika kuthamini waliopatwa na maafa ya mafuriko pote nchini kampuni ya simu ya VODACOM imeanzisha kampeni inayojulikana kama RED ALERT itakayowawezesha wateja wake kuchangia kadri wawezavyo ili kuwasaidia waathirika wa mvua na mafuriko pote nchini

Kwa ufupi ni kwamba ukitaka kuchangia waliopatwa na maafa pote hapa nchini kama Kilosa, Same, Tanga na Dodoma basi tuma neno MAAFA kwenda namba 15599 na hapo utakatwa shilingi 250/= (PAMOJA NA KODI) kama mchango wako kwa waathirika wa mvua na mafuriko.

Serekali imefanya tathmini na kutangaza kwamba kiasi cha shilingi billioni 10 zinahitajika ili kuweza kuwasaidia wale walioathirika mpaka hali itakapo tengemaa, na kampeni hii ni kuanzia tarehe 24th January 2010 paka 30th January 2010 (wiki moja tu)

MTI MZEE ZAIDI DUNIANI

Mti mzee kuliko yote duniani ulio hai ni bristlecone pine (Pinus longaeva) unaoitwa Methuselah mti huu unapatikana marekani California katika mlima mweupe, mti huu ambao uko futi 11,000 juu ya usawa wa bahari una miaka 4838 na sio tu ni mti mzee zaidi bali ni kiumbe kizee zaidi duniani cha asili (non-cloned) kilicho hai
Kabla ya Methuselah haujagunduliwa kwamba ni mti mzee zaidi duniani Mwaka 1957 na Edmund Schulman iliaminika kwamba mti mkubwa aina ya Sequoias ndio mti wenye umri mkuwa zaidi ukiwa na miaka 2000

MITI AINA YA METHUSELAH HUKO CALIFORNIA KATIKA MLIMA MWEUPE


Mti mwingine aina ya Prometheus uligunduliaka baada ya mwanafunzi wa Mwaka wa mwisho chuoni 1964 ajulikanaye kama , Donald R. Currey alipokuwa akifanya majaribio ya kisayansi na kifaa chake cha kuchimbia viini vya miti miti kuvunjika ndani ya mti, aliomba ruhusa ya kuukata mti huo (iliauchunguze zaidi) kutoka idara ya misitu na alistaajabu alipokubaliwa (wenzetu hawakati miti hovyo hovyo bila sababu maalum) na baada ya kuukata mti huo ndipo walipogundua kwamba ni mti wenye umri mkubwa zaidi duniani ukiwa na zaidi ya miaka 5000.

MITI AINA YA METHUSELAH WENYE MIAKA 4838



Kwa hiyo Prometheus ndio mti mzee zaidi kugunduliwa lakini umekufa baada ya kukatwa na Methuselah ndio mti mzee zaidi duniani ulio hai mpaka sasa. Miti ya Methuselah iko mingi na yote ikiwa na umri zaidi ya miaka 4000 na ipo California katika mlima mweupe lakini mahali ulipo kutwa mti wa Prometheus pamefanywa siri kwani bado wanaendelea kulichunguza eneo hili wakiamini wataukuta mti mwingine wenye umri unaofanana na ule walioukata

KISIKI CHA MTI WA PROMETHEUS BAADA YA KUKATWA

Tuesday, January 19, 2010

MTI MPWEKE ZAIDI DUNIANI

Mti aina ya acacia ulioota kwenye jangwa la sahana nchini Niger ndio mti ulio mpweke zaidi baada ya kuwa umbali wa zaidi ya maili 250 pande zote bila kukutana na mti mwingine. Mti huu uligunduliwa Mwaka 1970 lakini uliota mahala hapo wakati jangwa halijawa kavu kama lilivyo sasa, kwa miaka hiyo ambako mti huu uliota haukuwa peke yake bali kulikuwa na miti mingine ila yenyewe ilikufa baada ya jangwa hili kuendelea kuwa kavu zaidi na kupata kiasi kidogo cha mvua

MTI MPWEKE PICHANI



Mtii huu Ulikufa baada ya dreva wa lori kutoka Libya alipougonga, inasemekana dreva huyo alikuwa akiendesha lori hilo huku akiwa amelewa pombe. Baada ya mti huu kufa wana sayansi walichimba pembeni yake na kugundua mizizi ilikwenda chini kiasi cha futi 120 (mita 36) mpaka kufikia maji ya chini ya ardhi (water table) Sasa hivi sehemu ulipoota mti huo imejengwa nguzo ya chuma kama kumbukumbu ya mti mpweke zaidi duniani

NGUZO MAHALI ULIPOKUWA MTI MPWEKE

Sunday, January 17, 2010

UGONJWA WA MIGUU NA MIDOMO - FOOT AND MOUTH DISEASE

KWATO ZA MNYAMA MWENYE FMD


Ugonjwa huu husababishwa na virusi jamii ya Aphtovirus vinavyoambukiza binadamu pia (Aphtae epizooticae) ambavyo vipo kwenye Makundi ya A, O, C, SAT1, SAT2, SAT3, Asia1, vinauwezo wa kuishi kwenye matezi na ndani ya mifupa (bone marrow) madhali PH isiwe chini ya 6 na vinauwezo wa kuendelea kuishi kwenye mwili wa mnyama aliyekufa au kwenye udongo kwa mwezi mzima madhali PH isizidi 6. Kama lilivyo jina lake ugonjwa huu hushambulia kwato na midomo (fizi)
Ugonjwa huua zaidi ndama kuliko wanyama wakubwa, hushambulia wanyama wenye kwato kama ng’ombe, mbuzi, kondoo, punda, farasi, nguruwe, nyati maji, na wanyama wengine wenye kwato wanyama jamii ya ngamia, llama na nyati pori, huwa hawasumbuliwi sana na ugonjwa huu

MIKONO YA MTU ALIYEAMBUKIZWA UGONJWA


KUSAMBAA
Ugonjwa hussambazwa kwa njia ya mate, machozi, kinyesi, viatu, vifaa vya kuhudumia wanyama, nyama, maziwa, magari na hata hewa hasa kwa ukanda wa pwani usizidi futi 300 kutoka usawa wa bahari, wanyama ambao wana vijidudu na hawaumwi (carriers) kama nyati pori pia husambaza ugonjwa huu.

DALILI KUU
Toka mnyama aambukizwe huchukua siku 2 -14 na dalili kuu ni uzalishaji wa maziwa kushuka, kusaga meno, joto hupanda, mnyama huchechemea na kurusha mateke, ukiangalia fizi na kati kati ya kwato utaona kama vipele ambavyo baadae hupasuka na kuwa vidonda, wanyama hutoa mimba na wanyama wadogo (ndama )hufa

DAWA
Ugonjwa huu hauna dawa, bali unaweza kutibu vidonda kwa kutumia dawa (antibiotic) kama ulipo hakuna dawa unaweza kutumia chumvi au magadi ukiyeyusha kwenye maji na kuosha kwenye fizi na kwato za mnyama

KINGA
Kuna chanjo za ugonjwa huu ambazo hupigwa , sindano ya pili hupigwa baada ya siku 30 na baada ya hapo ni kila baada ya miezi 6 ( waone maafisa ugani wa mifugo) unaweza kuwakinga wanyama wako kwa kuzuia mwingiliano na wanyama wengine na kabla ya kuleta mnyama mpya hakkisha amepata chanjo zote (sijui wangapi wanafanya hii) pia karantini zitumike mara mlipuko wa ugonjwa huu unapotokea, wanyama wenye ugonjwa wauwawe na kuchomwa moto (incineration)

MFANO WA KIBAO CHA KARANTINI


WANYAMA WENYE UGONJWA WAKICHOMWA MOTO

Tuesday, January 12, 2010

KAMBALE ANAYETEMBEA

Hii ni aina ya kambale inayopatikana sana bara la Asia na Africa, amepewa jina la kambale anayetembea sababu ya uwezo wake wa kujikongoja na kuhama toka sehemo moja hadi nyingine kupitia nchi kavu kwa dhumuni la kutafuta chakula au mazingira mazuri, sio kwamba anatembea bali hujinyanyua juu kwa kutumia mapezi yake na kujinyonga nyonga kama nyoka na ii humuwezesha kusogea mbele, ana uwezo wa kuka muda mrefu nje ya maji madhali ardhi isiwe kavu bali iwe na unyevu

Hupendelea kwenye maji yenye kina kifupi au yasiyotembea, kama kwenye vijito na mito, mabwawa, majaluba ya mpunga na sehemu yoyote ambayo maji hujikusanya. Hukua hadi sentimeta 30 (urefu wa rula ya mwanafunzi) hana magamba kama kambale wengine bali ngozi yake huwa na ulenda ulenda unaomsaidia atembeapo nchi kavu, ana rangi ya kijivu mpaka kahawia iliyokolea kabisa. Tofauti na yake na kambale wengine yeye hana mapezi ya kwanza juu ya mgongo bali pezi lake la pili huwa refu mpaka karibu na mwisho wa mkia, unapomvua kambale huyu usimshike akiwa hai au hata kama kafa mshike kwa umakini sababu ana miiba iliyojificha kwenye mapezi ya chini karibu na mkia



Hupendela halijoto kati ya 10c mpaka 28c, chakula chao kikuu ni samaki wadogo, wadudu, konokono wasio na magamba na mimea ya kwenye maji, kambale hawa wanatabia ya ulafi inayowafanya wawe hatari kwa viumbe wengine wa kweye maji

Saturday, January 9, 2010

ADHA YA MVUA JIJINI DAR ES SALAAM


Kuwasha taa ni muhimu maana madereva hawaoni vizuri mbele kwa sababu ya ukungu kwenye vioo vya mbele





Hapo hata dala dala hazitanui maana inaweza kudumbukia kwenye mtaro, njia haionekani




Ukiwa na mwamvuli hautaloana labda miguuni ndio kasheshe


Magari (hasa ya petroli) nayo hupata hitilafu na kuzimika, hii husababisha adha kwa wenye kuyamiliki na gharama za ziada kama kusukumwa na kuyatengeneza tena


Limebuma


Jamaa anashuka......


Jamaa hana la kufanya anatafakari.... nyuma foleni kama treni


Jamaa anafurahia mvua kwa sababu lazima atauza makoti na mabuti ya mvua hahahahhe!!!!! kufa kufaana


Vituo vya kuwekea mafuta navyo vimefurika maji, je yakiingia kwenye matanki ya mafuta si tutauziwa maji-balaa hili........



Hata zoezi la kuzoa taka hufanyika kwa tabu na jamaa hawana vifaa vya kujikinga angalau gum boot