Leo asubuhi nilikuwa na mgeni mwingine ambaye ni mfugaji wa samaki anayeanza/mwanafunzi , alikuwa amekuja nyumbani kwangu kunitembelea na kujifunza. Kwangu pia ilikuwa ni bahati kwa sababu ilikuwa ni siku ya kufanyia usafi wa jumla chombo cha kufugia samaki (aquarium), nilimwomba anisaidie kwa sababu ki ukweli chombo ni kikubwa kiasi maana inachukua lita za maji 220 sawa na ndoo 11 za lita 20 zilizojaa.
JIWE LENYEWE
Kazi ilianza kwa kupunguza maji kwa kutumia kinyonyeo (syphone) na kwenda kuyamwaga maji kwenye maua, ikifuatiwa na kutoa urembo wote wa ndani pamoja na majani, sasa kuna mawe matatu ambayo nilipoyatoa sikuyaweka mahali pakavu na kuyasafisha kama urembo mwingine bali nilichota kiasi cha maji tuliyoyatoa na kuyaweka kwenye chombo kingine na kuweka mawe haya. Mgeni wangu akaniuliza kwanini hayo mawe siyasafishi, nikamjibu haya mawe yanaishi jamaa akashangaa na mimi ikanibidi nianze kumfafanulia maana yake.
MAWE YANAYOISHI YAKIHIFADHIWA KWENYE MAJI(PEMBENI) USAFI UKIENDELEA KWENYE CHOMBO KIKUU
Kwa chombo ambacho ndio kwa mara ya kwanza kinatumika kufugia samaki, inashauriwa yale maji uliyochukulia samaki toka kule uliko wanunua yawe ni kutoka katika chombo chenye samaki na yasiwe yametoka bombani moja kwa moja. Katika kanuni za usafishaji chombo cha samaki, unatakiwa usisafishe filter zaidi ya cheke cheke lake ambalo ndilo huchuja uchafu, nia na madhumuni kwa yote mawili ni kuhakikisha kwamba ule mfumo wa bakteria muhimu ndani ya chombo chako unakuwepo na haufi kabisa hata baada ya kufanya usafi wa jumla na kuweka maji mapya.
CHOMBO MARA BAADA YA USAFI KABLA YA KURUDISHIWA MAWE, UREMBO MWINGINE NA MFUNIKO WA JUU WENYE TAA NA WATER PUMP
Kwa kuzingatia hayo mimi niliamua kutumia mawe haya ambayo yanapatika kwenye mito hapa nchini, kila ninaposafisha na kuondoa maji yote kwenye chombo cha samaki. Mawe haya yana nafasi za matundu mengi yanayoruhusu maji kujaa ndani ya jiwe hili, kwa hiyo mfumo wa bakteria muhimu nao huwa ndani na ndio maana nikaliita jiwe linaloishi . Faida ya mawe haya ni kwamba yakuwa na mazingira ya kujificha na giza ndani yake kwa hiyo kufaa zaidi kama makazi ya bakteria hawa muhimu na huwa nayaweka ule upande wa pili ambao hauna filter. Ikumbukwe kwamba upande wenye filter ndio upande unaowekwa chakula kwa hiyo kuwa na vinyesi vingi na mabaki mengi ya chakula na kuwa na mazingira mazuri zaidi ya bakteria kuishi, sasa ili kufanya mazingira yawe sawa basi mimi niliamua kuweka mawe haya upande wa pili.
JIWE NDANI YA CHOMBO KAMA LINAONEKANA CHINI YA SAMAKI MWEKUNDU
Kama unafuga samaki aina ya CAT FISH ambao hula utando na ukungu ndani ya chombo chako mara zote hupenda kukaa upande wa filter na wakati mwingine kunata kwenye filter yenyewe kwa sababu ndipo kwenye ukungu mwingi uletwao na bakteria, sasa ukiweka mawe haya upande wa pili utaona kwamba cat fish wako wanatembea pande zote za chombo chako na hapo utaona umuhimu wa jiwe linaloishi.
CHOMBO CHA SAMAKI BAADA YA USAFI KUKAMILIKA FILTER IKO PEMBENI KUSHOTO NA MAWE YAPO CHINI KULIA
Kazi kweli kweli! mimi nilijia haye mawe ni kwa ajili ya kujisafisha (kusugulia miguu) huwa nayanunua niwapo nyumbani sikujua kama yana uhai. Nimejifunza kitu leo tena Ahsante!!
ReplyDeleteKaribu sana Dada Yasinta, umekuwa mfuatiliaji wangu mzuri sana na kunitia moyo kwa maoni yako. Wengi wao huwa wananitumia email kila siku kuniuliza maswali nao pia nawashukuru
ReplyDeleteBwana Bennet. Ni mara yangu ya kwanza kutembelea hapa. Mimi pia ninavutiwa sana na udadisi wa miti. Jirani yetu wakati ule wa vijiji vya Ujamaa alikuwa mganga wa kienyeji na nyumba zake zote (zaidi ya nne) zilikuwa zimeenea mizizi na vikolombwezo vya kila aina karibu kila sehemu. Kwa vile alikuwa mzee, daima nilikuwa nashangazwa na jinsi alivyoweza kufahamu majina ya mizizi ile iliyotapakaa kila kona katika nyumba zake na matumizi yake - bila daftari wala prescription. Kila mara tulipoumwa na nge, buibui na wadudu wengine tulikimbilia kwake na alituelekeza vitu vya kufanya. Kutoka wakati ule udadisi wangu wa miti iliyotuzunguka ukawa umeasisiwa na mpaka leo hii ningali nao. Kwa kuwa nimekugundua basi nitakufuatilia kwa karibu ili nijifunze kutokana na ujuzi wako.
ReplyDeleteHao samaki unawafuga ni kwa ajili ya mapambo au hata siku umekosa mboga unaweza kudabua mmoja ukambanika na kujilia ugali wako? Mimi ninataka kufuga samaki wa kula kijijini (si mradi wa biashara). Una utaalamu wo wote kuhusu jambo hili?
Nashukuru sana masangu kwa kunitembelea humu kwenye kijiwe changu, kwanza nitapenda na mimi nijifunze pia hizi dawa toka kwako.
ReplyDeleteHawa samaki ninaofuga ni wa urembo siwezi kupata kitoweo humu, lakini nina ujuzi tosha kama unataka kufuga samaki wa kula, cha muhimu ni kuwasiliana ili uweze kuchota ujuzi huu