KURASA

Saturday, July 11, 2009

MIGOMBA - KANUNI ZA KILIMO BORA

Hapa Tanzania kilimo cha migomba kimekuwepo Kwa miaka mingi. Kilimo hiki ni maarufu sana kwa sababu zao la ndizi limekuwa likitumika kama chakula kikuu kwa baadhi ya mikoa kama vile Kagera, Kilimanjaro na Mbeya na hivyo kulifanya muhimu, kufuatia mazao ya mahindi, mpunga, mtama, muhogo,viazi na mazao ya jamii ya kunde kama vile maharage.
Zao la ndizi linaweza kuwa moja kati ya mazao ya biashara iwapo litazalishwa kwa kufuata kanuni bora za uzalishaji wa zao hilo, ikwa ni pamoja na kupanda aina bora ya migomba inayozaa ndizi zinazotambulika katika masoko ya kimataifa.

ASILI YA MIGOMBA
Asili ya migomba ni nchi za Malaysia na India ambazo ziko Kusini Mashariki mwa Asia. Migomba inayolimwa sasa imetokana na migomba ijulikanayo kama Musa balbisiana ambayo asili yake ni India, na Musa acuminata ambayo asili yake ni Malaysia. Kutoka Malaysia na India migomba ilifika Afrika Mashariki katika karne ya tano

MAENEO YANAYOLIMWA MIGOMBA NCHINI

Nchini Tanzania mikoa inayoshughulika na kilimo cha migomba na kuzalisha zao la ndizi kwa wingi ni pamoja na Kagera, Kilimanjaro, Mbeya, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Kigoma, na Pwani. Hata hivyo zao hili linaendelea kuenea katika mkoa mingine nchini ikiwa ni pamoja na Dar es salaam,, Mwanza, Ruvuma, Shinyanga na Lindi. Pia Dodoma na Singida.
Kilimo cha migomba kinaweza kufanyika katika kipindi chote cha mwaka kulingana na kiasi na mtawanyiko wa mvua hasa mabondeni au kwa umwagiliaji.



MATUMIZI
Kilimo cha migomba kina faida nyingi, baadhi ya faida za migomba na
zao la ndizi ni: -
1Zao la chakula
2Zao la Biashara
3Kutengenezea pombe
4Kulisha mifugo
5Kutengenezea mbolea (mboji)
6Matandazwa shambani (mulch)
7Kutoa kivuli
8Kutoa nyuzi
9Kutengenezea vitu vya sanaa
10Kamba
11Malighafi ya kutengeneza vyakula na vinywaji mbalimbali.
12Dawa
13Majani kama miamvuli, sahani, vikombe na kata
14Kuezekea.

Ndizi kwa ajili ya chakula hutumika kwa kutengeneza vitu mbalimbali-:
1Makangale (Banana figs)
2Poda (Powder)
3Chenge (chips)
4Jeya (flakes),
5Juisi,
6Lahamu (jam)
7Vinywaji baridi, kama soda
8Mvinyo (Wine)
9Pombe kali
10Hamira

UZALISHAJI
Zao la ndizi likizalishwa kwa utaalamu unaokubalika huweza kutoa mazao yenye ubora wa hali ya juu na kuongeza uzalishaji kwa eneo. Mambo yafuatayo yafaa kuzingatiwa katika uzalishaji wa zao hili.

(a) Hali ya hewa
Kiasi cha chini cha mvua kifaacho ni 100mm kwa mwezi au 1200mm kwa mwaka. Mwinuko ni kutoka usawa wa bahari hadi mita 1800 juu ya usawa wa bahari. Zaidi ya mwinuko huo migomba haikui vizuri. Kiasi cha joto kinachofaa ni nyuzi joto za sentigredi 25 hadi 30 chini ya nyuzi joto 16 migomba haikui vizuri. Migomba hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha, kina kirefu, usiotuamisha maji na pia usiwe na chumvi. Chachu ya udongo inafaa iwe kati ya pH 5 hadi 8.

(b) Aina za ndizi
Kuna aina nyigi sana za ndizi. Nchini Tanzania ndizi zinazozalishwa, zipo za aina nyingi ambazo hutofautiana kwa majina kutokana na eneo au mkoa unaozalisha. Hata hivyo zinaweza kugawanywa katika makundi mawili. Aina ambayo huliwa kwa kuzichoma, kukaanga au kupikwa zikichanganywa na vyakula vingine kama vile nyama. Aina za ndizi hizo ni pamoja na Mzuzu, Mshale, Matoke, Bokoboko na Mkono wa Tembo.
Aina nyingine ni zile ambazo huliwa kama matunda, aina hizo ni kama vile Kisukari, Kimalindi, Mzungu na Mtwike.

Kuna aina nyingine za ndizi ambazo kwa sasa huzalishwa hapa nchini ambazo zina fahamika kwa ubora wake katika masoko ya ndizi ya kimataifa. Aina hizi ni pamoja na Williams, Grand Naine, Pazz, Jamaica, Gold Finger, Nyingine ni Uganda green, Embwailuma Giant na Chinese Cavendish.



(c) Utayarishaji wa shamba
1Safisha sehemu inayohusika kwa kutumia zana ulizonazo.
2Ng’oa visiki vyote na mizizi yake yote
3Lima sehemu hiyo kwa kutumia jembe la mkono, rato, au trekta ili kuwezesha mizizi laini ya migomba kupenya ardhini kwa urahisi.
4Baada ya visiki na magugu yote kuondolewa na hivyo ardhi kuwa wazi, uchimbaji wa mashimo ya kupandikiza machipukizi au miche ya migomba unaweza kufanyika.

(d) Nafasi ya kuchimba mashimo
Mashimo yatachimbwa kwa nafasi inayokusudiwa kutumika kati ya
mashina ya migomba na kati ya mistari kama ifuatavyo:-
1Migomba inaweza kupandwa kwa nafasi ya Umbali wa meta
2.75 kwa 2.75 kwa migomba mifupi kama Kimalindi na
Kisukari. (Mashina 1,331 kwa hekta )
2Umbali wa meta 3 kwa meta 3 kwa migomba ya urefu wa kati
kama Jamaica na Mshale (Mashina 1,110 kwa hekta)
3Umbali wa meta 3.6 kwa meta 3.6 kwa migomba mirefu zaidi kama
Uganda green Mashina 760 kwa hekta).

(e) Uchimbaji mashimo.
Uchimbaji mashimo inafaa ufanywe mapema kiasi cha juma moja hadi mwezi kabla ya muda wa kupanda. Shimo lichimbwe kwa kutenganisha udongo wa juu na wa chini.

Vipimo vya shimo ni vyema vikazingatiwa. Iwapo utachimba shimo la mviringo litafaa liwe na kipenyo cha sentimeta 60 hadi 90 na kina cha sentimeta 60 hadi 90. Iwapo utachimba shimo la mstatili au mraba litakuwa na urefu, upana na kina cha sentimeta 60 hadi 90, kutegemea kiasi cha mbolea kilichopo na kiasi cha kvua kinachonyesha sehemu hiyo. Uwekaji wa mbolea hufuatia mara baada ya mashimo kuwa tayari. Kiasi cha madebe 5 ya mbolea ya samadi iliyooza vizuri au mboji iwekwe kwenye lundo la udongo wa juu kando ya kila shimo na ichanganywe kisha mchanganyiko wa mbolea na udongo urudishiwe katika shimo kisha kijiti kichomekwe katikati ya shimo hilo, ilikuonyesha sehemu ambapo mche au chipukizi litapandwa.

(f) Kuchagua machipukizi bora
Machipukizi mazuri yanayofaa kwa mbegu ni yale yenye sifa hizi hapa chini: -
Sifa za chipukizi bora
1Liwe chipukizi sime, yaani lenye majani membamba na siyo
chipukizi maji yaani lisiwe lenye majani mapana.
2Litoke kwenye mgomba (shina) wenye afya nzuri, usiokuwa na
magonjwa, minyoo ya mizizi, wala vifukusi vya migomba.
3Litoke kwenye mgomba wenye sifa ya kuzaa mikungu
mikubwa.
4Liwe na afya nzuri na lisiwe na dalili za ugonjwa, wadudu, au
mayai ya vifukusi.
5Urefu uwe kati ya meta 1 na meta 2
6Kipenyo cha sehemu ya chini ya shina la chipukizi (tunguu) kiwe ni kati ya sentimeta 15 hadi 25.

(g) Upandaji wa machipukizi
Wakati unaofaa kupanda machipukizi ni mwanzoni mwa msimu wa mvua. Chomoa kile kijiti na chimba shimo la kiasi cha sentimeta 30x30 katikati ya shimo lililojazwa mchanganyiko wa udongo na samadi kisha panda chipukizi hilo.

Rudishia udongo na hakikisha tunguu lote limefunikwa vizuri. Shindilia udongo ili chipukizi lisimame wima imara. Machipukizi yanayo tarajiwa kupandwa yanatakiwa kuondolewa mizizi yote ili kudhibiti minyoofundo na fukuzi wa migomba. Pia maji ya moto au dawa kama vile furadani inaweza kutumika kuulia wadudu kwenye mizizi ya migomba.

UTUNZAJI WA SHAMBA NA MIMEA.
(a) Uwekaji wa matandazwa (mulching
)
Kazi hii ni vyema ikafanywa mara baada ya kupanda kama inawezekana. Matandazo yawe ni makavu na unene wa sentimeta 15 ili kuhifadhi unyevu, kuzuia magugu na yakioza yataongeza mbolea.

(b) Uongezaji wa mbolea
Baada kupanda ni vyema kuongeza mbolea madebe 2 kuzunguuka shina la migomba kila baada ya miaka miwili au mitatu. Mbolea hii inatakiwa kuchanganywa na udongo na kufunikwa kwa matandazwa.

(c) Umwagiliaji maji shambani
Migomba huhitaji maji mengi. Wakati wa kiangazi. Inafaa kumwagilia ili kuto kupunguza sana ukubwa na wingi wa ndizi zinazotarajiwa kuvunwa kwa mwaka. Kiasi cha maji kinachotakiwa kwa wiki ni milimita 25, yaani eneo linalo zunguka shina la migomba lilowe kabisa.

(d) Kupunguzia machipukizi
Inatakiwa kupunguza mimea ya migomba kwa kila shina na kubaki mimea mitatu tu, yaani Mgomba wenye ndizi (Mama), Mgomba mkubwa ambao bado haujazaa lakini unakaribia kuchanua (Mtoto), Mgomba mchanga uliochipua hivi karibuni ( Mjukuu)

(e) Uondoaji wa Majani Makavu
Mimea ya migomba inafaa iondolewe majani yote makavu ili kuondoa uwezekano wa kuwepo mazalia ya wadudu na magonjwa, kuruhusu mionzi ya jua na kufanya urahisi wa kuhudumia shamba .Pia hufanya shamba kuonekana safi.

(f) Uondoaji wa ncha mwishoni mwa matunda
Baada ya mkungu kutoa ndizi, ua hunyauka na kubakiza ncha mwishoni mwa matunda. Ncha hizo hupaswa kuondolewa .Huduma hii husaidia kupunguza uwezekano wa kujeruhi matunda wakati wa kusafirisha jambo ambalo kupunguza ubora wa tunda.

(g) Kuweka Miega
Miega ni nguzo au kamba ambazo hutumika kuzuia migomba iliyobeba mikungu mikubwa isianguke kutokana na uzito mkubwa. Miega ni ya lazima katika sehemu zenye upepo mkali. Kazi hii inatakiwa kufanywa kwa uangalifu ili isijeruhi ndizi na mgomba wenyewe.




(h) Uondoaji wa kichombezo cha ua la kiume (Shumba)
Uondoaji wa shumba huwezesha matunda kukua vizuri, kuongezeka uzito wa mkungu pia huzuia magonjwa kama vile ugonjwa wa mnyauko wa migomba (Banana Baterial Wilt), ugonjwa wa Majivu nchani mwa matunda (Cigar end rot). Ukataji hufanyika juu ya kovu la pili baada ya kichana cha mwisho, kwa kutumia kisu kikali.

UVUNAJI
Zao la ndizi huweza kuanza kuvunwa katika kipindi cha miezi 9 hadi miezi 15 tangu kupandwa kwa chipukizi. Muda wa kuvunwa hutegemea hali ya hewa. Katika sehemu za joto ndizi huvunwa mapema zaidi kuliko sehemu za baridi. Pia migomba iliyopandwa kwa kutumia machipukizi huzaa mapema kuliko iliyopandwa miche iliyozalishwa kwa chupa (tissue culture)

MATUMIZI YA RIBONI

Riboni za rangi moja (au alama ya kamba) hufungwa kwenye migomba ya umri mmoja mara tu inapoanza kuchanua, na riboni ya rangi nyingine hufungwa kwenye migomba itakayoanza kuchanua wiki mbili hivi zinazofuata na kuendelea hivyo ili kurahisisha kuitambulisha mikungu ambayo itavunwa kwa wakati mmoja. Pia matumizi ya riboni hurahisiha utunzaji wa kumbukumbu ili kujua ni lini na ni mikungu mingapi itavunwa.

WAKATI UNAOFAA KUVUNA
Mkungu wa ndizi huweza kuvunwa katika hatua tofauti kulingana na matumizi, aina na mahitaji ya soko. Mkungu huachwa kwenye mgomba mpaka vidole (matunda ) vimejaa. Uzito wa mkungu hongezeka haraka katika wiki mbili za mwisho, ambapo migongo ya ndizi hutoweka.
Ndizi zinaweza kuvunwa zikiwa zimekomaa na zimeiva kwa kiasi cha asilimia 75 kwa ajili ya kusafirishwa mbali, pia zinaweza kuvunwa zikiwa kukomaa na zimeanza kuiva kwa ajili ya soko la karibu, au zikiwa zimekomaa na kuiva kabisa kwa ajili ya soko na matumizi ya nyumbani Njia bora ya kukata mkungu, ni ile inayohakikisha kuwa mkungu wa ndizi hauanguki chini na kuvunja, kuchubuan au kuharibu ndizi, jambo ambalo litapunguza ubora. Ukichelewa kuvuna ndizi zinaweza kuharibiwa na ndege, wanyama, wadudu au kuibiwa.

MKUNGU WA NDIZI AMBAO UMEONDOLEWA SHUMBA


UBORA WA NDIZI
Ndizi zenye sifa nzuri sokoni ni zile ambazo zimekomaa kwa kiasi kinachotakiwa na zenye vidole vyenye urefu mzuri na visivyo na michubuko. Pia ziwe hazijashambuliwa na magonjwa wala wadudu waharibifu.

KIASI CHA MAVUNO
Mavuno ya ndizi hutegemea zaidi aina ya migomba, hali ya hewa, utunzaji wa mimea shambani. Mavuno huweza kufikia hadi tani 60 au zaidi kwa hekta kwa mwaka. Hata hivyo mavuno mazuri kwa mkulima wa kawaida yasipungue kati ya tani 20 hadi 30 kwa hekta kwa mwaka.

MAGONJWA
Ugonjwa wa hatari sana ulioingia hivi karibuni katika wilaya ya Muleba na maeneo mengine mkoani Kagera kutoka nchi jirani ya Uganda ni wa Mnyauko wa migomba unaosababishwa na bakteria (Banana Bacterial Wilt). Magonjwa mengine yanayosumbua zao hili ni Kuoza tunguu, Ugonjwa wa panama, Ugonjwa wa majivu nchani mwa tunda, Sigatoka, na Moko.

WADUDU WAHARIBIFU
Wadudu wanaosumbua zaidi hili ni Minyoo fundo (Banana nematodes), na Vifukuzi (Banana weevils).

UDHIBITI WA MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU
Magonjwa na wadudu hawa huweza kuepukwa kwa kufuata kanuni bora za uzalishaji wa zao hili. kama usafi wa shamba na kuchagua chipukizi bora. Au kupanda miche iliyozalishwa kwa chupa (Tissue culture banana seedlings) Hata hivyo mara mataizo haya yakitokea muone mtaalam wa kilimo aliye karibu ili aweze kukupa ushauri wa dalili za ugonjwa wa mnyauko wa migomba unaosababishwa na bakteria

9 comments:

  1. Asante sana kwa somo hili.Nina migomba yangu kule Ruhuwiko. Nitajitahidi kufuata maelezo yako Ahasante

    ReplyDelete
  2. Duh Bennet unanitamanisha kweli yaani ungejua nina order ya ndizi 50 kg, lakini mpaka niagize Equador, yaani
    Tanzania ingekuwa karibu!!! we acha tu

    ReplyDelete
  3. Kaka Ben mimi siku zote niko interested sana na dawa/herbs za kiasili,ila leo hujatuambia mgomba unaweza tibu magonjwa gani kwa binadamu au hujapata mahari panapoelezea utabibu wa mgomba? ni hayo tu mkuu!!!

    ReplyDelete
  4. Na mkaa je, nasikia kuna wagagnga wa kienyeji huagiza waletewe mkaa wa migomba kuweka mambo sawa!

    ReplyDelete
  5. Asante kaka, umenikumbusha sana nyumbani kwa kunionyesha migomba na kuniongezea elimu kuhusu migomba na ndizi. Hakika wewe ni mtaaluma.Hongera sana Mkuu

    ReplyDelete
  6. mkuu blog yako inapendeza sana hongera sana
    pia nawe nakukaribisha katika blog yangu japo utoe maoni kidogo karibu sana(www.biasharanikilimo.blogspot.com).
    MAONI WATU WAACHE KUWA WACHUUZI WAZALISHE. KI UKWELI DUNIANI KUNA UPUNGUFU MKUBWA SANA WA CHAKULA.

    ReplyDelete
  7. je migomba kama FIA inapandwa kwa umbali gani?kwa heka
    nijibu ndani ya sullyjdbilly@yahoo.com

    ReplyDelete
  8. Naomba kujua kuwa TANI moja ya ndizi n sawa na mikungu mingapi na bei ya tani moja ama mkungu mmoja ni kiasi gani?

    ReplyDelete
  9. Kaka umeeleza vizuri sana ila masoko yaani bei inakuaje?

    ReplyDelete