1. Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Katika Utayarishaji Wa Mihogo
Mibichi Na Ukaushaji
1.1 UTAYARISHAJI
Mihogo mibichi iliyovunwa huoshwa mara mbili. Uoshaji wa kwanza ni ule wa kuondoa udongo baada ya kuvuna, na uoshaji wa pili ni baada ya kumenya mihogo kabla ya kukausha.Baada ya kuoshwa mihogo humenywa kwa kutumia kisu kikali, na kutumbukizwa ndani ya maji safi. Baada ya kumenya kiasi kinachotakiwa mihogo huoshwa na maji safi hadi kuwa myeupe.
1.2 UTENGENEZAJI WA CHIPSI
Mihogo iliyo safi huwekwa ndani ya mashine ya kuzungushwa kwa mikono au mashine ya kuzungushwa kwa mota ya umeme, kisha huparuliwa na kutoka vipande vidogo vidogo ambavyo huanikwa katika makaushio bora.
1.3 KWA MIHOGO MICHUNGU
Baada ya kuparuwa mihogo kuwa chipsi, huwekwa katika mifuko safi (viroba) na kuwekwa mahali penye kivuli kwa muda usiopungua saa sita ili kuacha sumu iliyoko kwenye mihogo kupotea kabla ya kukausha.
1.4 UKAUSHAJI
Mihogo safi ambayo imeparuliwa au kukatwa vipande vidogo vidogo hukaushwa katika makaushio bora kwenye jua kali. Makaushio bora huwa ni yale ambayo yamejengewa kichanja kilichoinuliwa mita mbili kutoka ardhini, na kutandazwa chekeche ya plastiki juu yake, yenye matundu madogo yasiyoweza kupitisha chembechembe za mihogo mikavu Kitambaa safi cha kaniki au mikeka safi huweza kutumika pia kama tandiko la juu ya kichanja ambapo chipsi za mihogo huweza kukaushwa kwa hali ya usafi.
VICHANJA BORA VYA KUKAUSHIA MIHOGO
Epuka kukaushia chipsi za mihogo katika majamvi mabovu juu ya ardhi kwani uchafu utakaoingia ndani ya mihogo hautakuwa rahisi kuondoa tena na husababishsa bidhaa ya unga kutokuwa na ubora.Ukaushaji duni wa mihogo Uharibifu au upotevu unaosababishwa na ukaushaji duni husababisha muhogo kubadilika rangi na kupata ukungu.
UKAUSHAJI DUNI WA MIHOGO
1.5 NJIA BORA ZA KUKAUSHA MIHOGO
Mihogo iliyoparuliwa (chipsi) hukaushwa na baadaye kusindikwa ilikupata unga.
VIFAA NA MALIGHAFI
• Mihogo safi
• Kisu kikali kisichoshika kutu.
• Mashine ya kuparua (grater)
• Kaushio bora
• Kitambaa cheusi kikubwa cha kutosha na kilicho safi au majamvi safi
• Vifungashio.
MASHINE YA KUPARUA MIHOGO(grater)
UTENGENEZAJI WA MAKOPA YA MIHOGO
• Menya mihogo safi kuondoa maganda
• Parua kwa kutumia mashine kupata chipsi.
• Anika kwenye kichanja au kaushio bora lilotandikwa kitambaa cheusi kilicho safi au jamvi safi ili kuzuia uchafu kuingia ndani ya chipsi.
• Sambaza na geuzageuza vipande hivyo ili kuharakisha ukaukaji.
• Muda wa kukausha hutegemea hali ya jua na ukubwa wa vipande. Vipande vidogo hukauka upesi na huwa bora kwa mlaji. Vipande vikubwa huchelewa kukauka na hupoteza ubora
• Fungasha vipande vilivyokaushwa kwenye magunia safi, kasha hifadhi kwenye maghala bora.
1.6 KUHIFADHI MIHOGO MIKAVU (Chipsi Au Makopa)
Njia pekee ya kuhifadhi mihogo kwa muda mrefu ni kwa kuhifadhi mihogo iliyokaushwa. Muhogo uliokaushwa huweza kuhifadhiwa kwa muda wa miezi 6 hadi 12 bila kuharibika. Makopa yanashambuliwa na dumuzi zaidi kuliko chipsi, hivyo inashauriwa kuhifadhi mihogo iliyoparuliwa na kukaushwa (chipsi) ambayo inakuwa katika hali ya unga unga na kufanya mashambulizi ya dumuzi yapungue kabisa.
Chipsi za mihogo zinaweza kuhifadhiwa katika magunia safi ya juti na kupangwa ndani ya ghala juu ya chaga. Pia chipsi zinaweza kuhifadhiwa katika hali ya kichele ndani ya sailo au kihenge bora. Mihogo haihifadhiwi kwa kutumia madawa ya viwandani. Hifadhi kwa hali ya ukavu, usafi na kagua ghala mara kwa mara kuona kama kuna mashambulizi ya panya na chukua tahadhari kuepuka upotevu wa chakula hicho. Aidha hifadhi kwa muda ulioshauriwa ili kudumisha ubora wa bidhaa.
2 KUSINDIKA MIHOGO ILIYOKAUSHWA
2.1 Kusindika muhogo uliokaushwa kupata unga
VIFAA
• Mashine ya kusaga
• Mifuko ya kufungasha
• Mashine ya kufungia mifuko
• Chekeche
• Mizani
• Muhogo safi uliokaushwa vizuri.
MASHINE YA KUSAGIA MIHOGO
JINSI YA KUSINDIKA
• Saga muhogo uliokaushwa kwenye mashine ili kupata unga.
• Chekecha kwa kutumia chekeche laini. Ukubwa wa matundu ya chekechekeche hutegemea kiwango cha ubora wa unga kinachotakiwa na soko.
• Weka unga kwenye mifuko kutegemea matakwa ya soko (kilo 1,2,5,10, au 50)
• Funga vyema kwenye mifuko ya kufungashia ili hewa isiingie
• Hifadhi kwenye chaga au fremu zilizowekwa mahali pakavu na pasipokuwa na mwanga mkali.
2.2 Viwango vya ubora wa unga wa muhogo uliokaushwa Unga laini
• Unga huu unapochekechwa kwa kutumia chekeche yenye matundu madogo
(milimita 0.60) hupenya karibu wote (asilimia 90)
Unga wenye ulaini kati
• Unga huu unapochekechwa kwa kutumia chekeche yenye matundu makubwa (milimita) 1.20) hupenya karibu wote (asilimia 90).
2.3 MATUMIZI YA UNGA WA MIHOGO
Hutumika kupika ugali, uji na katika kutengeneza maandazi, tambi, keki, biskuti,kababu, donati, mkate, chapati na chapati maji.
Virutubisho vinavyopatikana kwenye gramu 100 za unga wa muhogo ni kama ifuatavyo
Maji asilimia 13
Nguvu kilokalori 320
Protini gramu 1.7
Vitamini C miligramu 4
Kalsiamu miligramu 4
Fosiforasi miligramu 135
Potasiamu miligramu 885
W anga gramu 84
Madini ya chuma miligramu 2
Napenda sana zao la muhogo, ni zao zuri sana kwa chakula na biashara ukianzia majani, matawi na mizizi
ReplyDeleteDada ni kweli kabisa yaani hapo utapata kila kitu ugali, mboga(kisamvu) Somo zuri sana umenikumbusha mbali huu unga ndio niliokulia mimi. Ila nakumbuka mama alikuwa akiiloweka mihogo baada ya kumenye kwenye maji na inakaa siku kadhaa na baadaye anaishafisha na kuianika kwenye mpasa (wa matete) na unga wake ulikwa mweupe kabisa na mtamu. Na pia kuna sehemu nyingine wanapenda hiyo ya kuvunduka na mihogo inakuwa na ukungu mweusi wanasema ni lishe nzuri . Nimefurahi na nimelipenda sana somo la leo. Usengwili kaka.
ReplyDeleteBennet atanisaidia..., nafikiri kuvundika mpaka ikatoa ukungu huo mweusi au fungus ni katika sehemu ya uandaaji wa mihogo kusindikwa kabla ya kutwanga au kusagwa kutengeneza unga. Hao fungus huondolewa kabla mihogo haijaanikwa.Na hao fungus wana uwezo wa kukata makali ya sumu uliyopo kwenye jamii fulani za mihogo.... Au Bennet wasemaje, mie sijabobea kwenye utaalamu huo, lakini enzi hizo kijijini, nilikuwa naona wanafanya hivyo.
ReplyDeleteKwa mihogo michungu inapowekwa kwenye kivuli kwa masaa matano inatakiwa iwe imelowekwa kwenye maji, pia unaweza kukausha ukasaga kisha unga ndio ukauloweka kwenye maji kwa masaa matano, hii husaidia kuondoa sumu aina ya cyanogen/cyanide iliyopo kwenye mihogo
ReplyDeleteInapoweka ukungu mweusi wale ni fungus ambao pamoja na kupunguza sumu, pia hutumia sukari iliyopo kwenye mihogo na mwisho hutoa aina nyingine ya sumu na kuiacha kwenye mihogo, ndio maana kitaalam haishauriwi kuiacha mpaka ipate fungus/ukungu
Mada nyingine tunastahili kuwa tunazibandika kwenye "vibaraza" vyetu ili hata wale wavivu wa kutembelea hizi makala muhimu wasizikwepe.
ReplyDeletePia hizi ndizo tunazohitaji kwenye magazeti yetu na sio makala za mapenzi pekee.
Nakumbuka nikiwa sekondari Ndanda Masasi Mtwara tulikuwa tunapata MAKOPA (mihogo ya kukausha) kutoka Newala. Ilikuwa safi saaaana. Cha ajabu ni kuwa tulikuwa tukitumia mihogo kama kitafunio cha uji. Duh!!!
Asante kwa elimu na kumbukumbu Kaka
Pamoja
sikuwa nafahamu chochote kuhusu usindikaji wa mihogo.
ReplyDeleteNashukuru kwa habari hii
Asante kwa info. hii inaelimisha pamoja na posts zilizopita. pia nafurahia sana picha unazoweka ila kama inawezekana weka blog address chini kidogo kama ulivyofanya hiyo picha ya Mheshimiwa Rais, hizi nyingi ukiweka adress katikati unatupunguzia uhondo wa kuenjoy picha au wenzangu mnasemaje?ni wazo tu.
ReplyDeletemimi nina maswali machache
ReplyDelete1. je nikimaliza kuosha mihogo na kuikata na kuianika ikakauka nikipeleka kusaga moja kwa moja ina madhara??
2. je ivyo virutubisho ulivyoweka hapo juu nni viko automatically au vinaongezwe??
3. je nitajuaje mihogo michungu na amabyo sio michungu
4. unga wa mihogo unapendwa?? mtu anaweza kufanya kama biashara ya kudumu ambayo for future plan?
asante
Nina shamba la mihogo lilopamba kiasi cha ekari mbili...natafuta mteja
ReplyDelete