KURASA

Thursday, April 25, 2013

NAMNA YA KUPAMBANA NA HARUFU MBAYA YA MBWA NDANI YA NYUMBA YAKO

Je unafuga mbwa  wako ndani ya nyumba yako kwa usafi wa hali ya juu, lakini umegundua harufu mbaya ya mbwa wako bado ipo ndani ya nyumba yako?  inawezekana ni kwa kiasi kidogo sana lakini bado inakera maana harufu mbaya ni mbaya tuu. Ambacho hujagundua ni kwamba kuna sehemu kadhaa ambapo hii harufu imejificha, sasa hapa nitakupa siri ya kuondoa harufu hii

(a)Matandiko anayolalia mbwa wako hakikisha yanafuliwa kila wiki, na itapendeza kama utakuwa na seti mbili ili wakati moja imefuliwa na kusubiria ikauke na jua basi unamtandikia hii nyingine

(b)Kama tandiko la mbwa huwa lina kaa kwenye kreti maalum basi tumia brashi kulisafisha na sabuni kisha nalo lianikwe, hii iwe angalau mara 1 kwa wiki, pia katikati ya wiki unaweza kuwa unalisafisha mara kwa mara kwa kutumia masine ya vakyum ya kusafishia mazulia

(c)Kama mbwa wako huwa analalia mito ya makochi yako, basi hakikisha ni mito ambayo inaweza kufulika ili nayo iwe inafuliwa mara kwa mara

(d)Midoli ya kuchezea mbwa wako nayo pia iwe ni ile ambayo inaweza kufuliwa na ifuliwe mara kwa mara ili kuondoa harufu

(e)Angalia sehemu ambazo mbwa wako hupenda kujificha mara kwa mara maana wakati mwingine huwa wanasahau mabaki ya chakula  na kusababisha harufu mbaya

(F)Kabla ya kusafisha mazulia yako yanyunyuzie na baking soda (sina jina la kiswahili) kisha safisha kwa kutumia mashine ya vakyum

PAMBANA NA KUNGUNI KWA KUTUMIA MAJANI YA MAHARAGE

Majani ya maharage yameonesha uwezo mkubwa wa kuweza kuwanasa kunguni kama watapita juu yake, majani ya maharage yanaweza kufanikisha zoezi hilo kwa sababu yana vinyweleo ambayo huwanasa kunguni mara wapitapo juu yake. Pia yana uwezo wa kudhoofisha miguu yao na kuwafanya wasiweze kutembea.

Matumizi ya majani haya kwa kutegesha kwenya chago za vitanda na sehemu nyinginezo yana uwezo mkubwa wa kupunguza uwepo wa kunguni ingawa shaka bado ipo kama yana uwezo wa kuangamiza na kutokomeza kizazi chote.

Kama njia hii itafanikiwa kwa asilimia 100 inamaanisha kupunguza gharama za kutumia kemikali za viwandani ambazo ni aghali ukilinganisha na majani ya maharage ambayo yanapatikana shambani na kwenye bustani zetu

Tatizo pekee ninaloliona kwenye njia hii ni muda wa kutokomeza kunguni kama wamevamia nyumba yako, njia hii inahitaji muda kiasi tofauti na kemikali ambazo zingeweza kuwaua mara upuliziapo, tatizo la kemikali nalo ni gharama, uchafuzi wa mazingira na pia usugu wa wadudu kwenye kemikali hizi ambazo wakati mwingine hupoteza uwezo wa kuangamiza wadudu.

jambo lingine gumu kwenye njia hii ni namna ya kuwafanya kunguni wavutiwe na kupita kwenye majani haya, kwani wasipopita juu yake njia hii haitakuwa na faida yoyote

Friday, April 12, 2013

FLAMINGO WA ZIWA MANYARA HATARINI KUTOWEKA

Ndege aina ya flamingo waliopo katika hifadhi ya taifa ya ziwa manyara wapo hatarini kutoweka, hii ni kwasababu ya matumizi ya mbolea za viwandani na viuatilifu kwenye kilimo katika mazingira yanayozunguka mbuga hii.

Siku hizi kumekuwa na matumizi makubwa sana ya mbolea na madawa ya kilimo katika kuongeza uzalishaji mashambani, baada ya kupuliziwa na kuwekwa ardhini mvua zinaponyesha kemikali hizi husombwa na maji hasa kutoka sehemu za miinuko. Maji haya ambayo mwisho wake huishia kwenye ziwa Manyara na kuchafua maji ya ziwa hili.

Ndege kadhaa hutumia maji ya ziwa hili ambalo lina magadi, wakinywa maji haya yenye kemikali hizo husababisha mapungufu kwenye mfumo wa umeng'enyaji chakula na madini aina ya kalsiam na fosforasi ndio huathirika. matokeo yake ni kwamba ndege hawa hutaga mayai ambayo maganda yake huwa dhaifu na kuathiri utotoaji wa vifaranga vya flamingo hawa.

Kutokana na athari hizi za mabadiliko katika ubora wa maji ya ziwa hili ni kwamba viumbe wote wanaotegemea ziwa hili kwa njia moja au nyingine nao wataathirika hasa baada ya kutokea athari za kiekolojia, kwa kawaida viumbe duniani huishi kwa kutegemeana na kwenye mfumo huu kiumbe kimoja tu kikiathirika maana yake ni kwamba viumbe wengine tegemezi wote wataathirika.
Ushauri muhimu ni kuendeleza kilimo cha asili kwa kutumia mbegu za asili, mbolea vunde au samadi za wanyama na pia kutumia dawa za asili kama utupa, muarobaini na pilipili kwa ajili ya kuulia wadudu waharibifu au kutumia njia za kibailojia kama sukuma vuta ili kukabiliana na wadudu waharibifu mashambani



Thursday, April 11, 2013

JKT (842 KJ) MLALE SONGEA NA JUHUDI ZA KILIMO KWANZA

Katika jitihada za kukabiliana na tatizo la wakulima kuuziwa mbegu za mahindi zisizofaa, kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) 842 KJ Mlale cha Songea mkoani Ruvuma, kimeanza uzalishaji wa mbegu za zao hilo ambazo zitakuwa mkombozi kwa wakulima wa Nyanda za Juu Kusini.

Mradi huo utawasaidia wakulima kulima mazao yao kwa uhakika na kwa utaalamu zaidi na kupata mavuno mengi na kuongeza kipato. Bwanashamba wa kikosi hicho Luteni Jackson Otaite, anasema kikosi kinajihusisha na kilimo cha mbegu za mahindi, mahindi ya chakula na kulima bustani za mbogamboga. “Mahindi yameuzwa kwa mkopo kwa Kampuni ya Highland Seed Growers ambayo ndiyo tuliingia mkataba kwa sababu kampuni hiyo haina fedha kwa sasa na bado thamani haijulikani kwa kuwa bado yanaendelea kuchambuliwa Kiwandani,” anasema. Anafafanua zaidi kuwa wanatarajia kuvuna tani 400 za mahindi ya chakula, tani 200 za mahindi ya mbegu na tani 25 za alizeti na mazao yote yanakadiriwa kuwa na thamani ya Sh330 milioni. Luteni Otaite anaeleza zaidi kuwa kikosi kimelima ekari 2.5 za mazao ya bustani na walivuna mbogamboga walizouza Sh7 milioni.

Anasema aina ya mahindi inayozalishwa na Mlale JKT ni Hybrid (H614) ambayo kukomaa baada ya miezi mitano na punje zake ni ngumu na haziliwi kirahisi na wadudu waharibifu, zinavumilia ukame na huzaa mahindi mawili kwa kila mmea na hutoa mavuno kati ya tani 1.5 hadi 2 kwa ekari. “Naiomba Serikali iongeze jitihada zaidi ya kuangalia uwezekano wa kupunguza bei za pembejeo za kilimo zikiwemo mbolea ambazo kwa sasa bei zake ziko juu sana,” anasema Luteni Otaite.

Kamanda wa kikosi hicho Meja Thomas Mpuku ameiomba Serikali kuanzisha utaratibu wa kutoa mbolea za ruzuku kwa vikosi vya JKT ili vizalishe mazao ya chakula na biashara kwa wingi pamoja na mahindi ya mbegu. Meja Mpuku, ameitaka Serikali kuwapa ruzuku za pembejeo ili waongeze uzalishaji badala ya utaratibu wa sasa wa kutoa ruzuku kwa wakulima pekee bila kuangalia wadau wanaowazalisha mbegu. Anasema baadhi ya matatizo ni upungufu wa wataalamu wa kilimo, kupanda kwa gharama za uzalishaji, uchakavu wa maghala, mchwa wanaoshambulia mahindi na kucheleweshwa kwa malipo.

JKT kuongeza uzalishaji
Anabainisha kwamba mipango ya baadaye ya kikosi hicho ni kuongeza ukubwa wa shamba kutoka ekari 650 hadi 800. Pia kupanua eneo la kulima bustani kutoka ekari 2 .5 hadi ekari 5 na kujenga bwawa litakalotumika kwa umwagiliaji. Mkuu wa Wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti amekipongeza kikosi hicho kwa jitihada hizo ambazo zinaonekana kuwa mkombozi wa kilimo. “Nimevutiwa na miradi yote ya maendeleo niliyoiona, nawatia moyo mkazane na jitihada hizo mtafika mbali, kwani miradi yenu ni madhubuti na hii iwe chachu kwa wanaohitimu, mkirudi majumbani kwenu mkawe mfano wa kuigwa kwa kilimo bora,” anasema Mkirikiti.

Wednesday, April 10, 2013

KUMUANDAA MNYAMA KABLA YA KUCHINJWA - STUNNING






Hii ni njia inayotumika kumuandaa mnyama kabla ya kuchinjwa, nia kuu ya stuning ni kumpunguzia mnyama maumivu wakati wa kuchinjwa, pia huondoa uwezekano wa mnyama kumuumiza mchinjaji na mwisho ni kuongeza ubora wa nyama.

Zipo njia nyingi au vifaa vingi vya kumuandaa mnyama kabla ya kuchinjwa lakini leo nitaongelea kifaa kijulikana cho kitaalam kama CAPTIVE BOLT PISTOL/GUN. Hiki ni kifaa kama bunduki ndogo ambapo ndani huwekwa baruti maalum au hutumia nguvu ya upepo ambayo ukifyatua kuna chuma imara chenye ncha kali  mbele (bolt)kina toka mara moja na kurudi ndani.

Boriti hii inakazi moja tu ya kutoboa sehemu ya mbele ya ubongo wa mnyama na kumfanya abung'ae na kupoteza fahamu, hii hurahisisha zoezi la uchinjaji na kufanya mnyama achinjwe bila kusikia maumivu yoyote. Kila mnyama anasehemu maalum ya kufanya stunning kama inavyoonyeshwa hapo kwenye michoro ya makala hii
http://www.youtube.com/watch?v=nr00arV2XIw kwenye link hii ya you tube unaweza kuona jinsi zoezi hili linavyofanyika kwa kutumia mashine maalum ya upepo

Tuesday, April 9, 2013

KILIMO BORA CHA VIAZI VITAMU

Utangulizi
Viazi vitamu ni moja kati ya mazao makuu ya mizizi nchini Tanzania ambalo hulimwa kwa ajili ya chakula. Zao hili ni moja kati ya mazao ya kinga ya njaa kutokana na sifa yake ya kuvumilia ukame. Zao la viazi vitamu, asilia yake ni Amerika ya Kati na ya Kusini. Nchini Tanzania, zao hili hulimwa zaidi katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Dodoma, Morogoro,Kagera,Arusha na Ruvuma.

Matumizi
Viazi vitamu hutumika kama chakula kwa kutayarishwa katika njia mbalimbali kama vichembe, na Matobolwa. Pia Unga wa viazi vitamu hutumika kutengeneza vyakula kama keki, maandazi, kalimati na tambi. Majani ya viazi huliwa kama mboga pia hutumika katika kutayarisha mboji.

Aina za viazi vitamu
Kuna aina nyingi za viazi vitamu zinazolimwa ulimwenguni. Hapa nchini Tanzania aina zinazolimwa zaidi ni Ukerewe, Simama, Kakamega, Karoti C, Mwananjemu, Ali mtumwa mayai, Mavuno, Pananzala, Kibakuli, Sinia,Vumilia na Polista

Uzalishaji
Zao hili hustawi maeneo mengi Nchini Tanzania. Viazi hustawi vizuri katika maeneo ya tambarare yenye udongo tifutifu, unaoruhusu maji kupenya kwa urahisi. Udongo wa mfinyazi na wenye kokoto nyingi haufai kwani huzuia mizizi kupenya na kupanuka.

Shamba jipya litayarishwe vizuri kwa kufyeka vichaka na kung’oa visiki. Majani yafukiwe wakati wa kutengeneza matuta ili kuongeza rutuba ya udongo.

Viazi vipandwe kwa kutumia Marando yenye urefu wa sentimita 30 kwa mavuno bora. Inashauriwa kutumia sehemu ya juu ya shina kwa mavuno zaidi. Marando yapandwe katika umbali wa sentimita 25 hadi 30 kutoka mmea hadi mmea na sentimita 60 hadi 75 kutoka tuta hadi tuta. Viazi pia vyaweza kupandwa kwa kutumia viazi vyenye afya vyenye uzito wa kati ya gramu 20 hadi 30. Hata hivyo inashauriwa kutumia marando ili kupata mavuno zaidi na kuepuka kuenea kwa magonjwa.

Kutunza shamba
Ni muhimu kupalilia viazi vitamu katika miezi miwili ya mwanzo ili kuupa mmea nguvu ya kutambaa vizuri. Baada ya muda huo, viazi huweza kufunika ardhi na hivyo huzuia uotaji wa magugu.

Viazi hushambuliwa na wadudu mbalimbali wakiwemo kipepeo, mbawa kavu, fukusi na minyoo fundo.Pia hushambuliwa na magonjwa yakiwemo magonjwa yanayotokana na virusi kama Sweet Potato Chlorotic Stunt virus (SPCSV). Magonjwa na wadudu yaweza kudhibitiwa kwa kuzingatia usafi wa shamba, kubadilisha mazao, na kuzingatia udhibiti sango.

Uvunaji
Viazi vitamu huwa tayari kuvunwa miezi mitatu hadi minne tangu kupanda kutegemea hali ya hewa. Viazi vinaweza kuvunwa kidogo kidogo kwa kutumia mikono, vijiti, jembe, au rato kadri vinavyohitajika. Aidha inashauriwa viazi visiachwe ardhini muda mrefu bila kuvunwa kwani vitakomaa sana na kuwa na nyuzi, na hivyo kuharibu ubora wake. Pia kuacha viazi muda mrefu hukaribisha mashambulizi ya wadudu kama fukusi na kuoza. Kwa maeneo makubwa zaidi, inashauriwa kutumia mashine ya kukokotwa na ng’ombe. Uvunaji ufanywe kwa uangalifu ili kuhakikisha viazi visikatwekatwe wala kuchubuliwa wakati wa kuvuna.

Mavuno ya viazi hutofautiana kulingana na aina, hali ya hewa, na udongo. Mavuno ya viazi yanakadiriwa kufikia tani 20 kwa hekta