KURASA

Tuesday, September 22, 2009

KILIMO KWANZA

AZIMIO LA KILIMO KWANZA


KWA KUWA Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lilifanya mkutano tarehe 2 na 3 mwezi Juni 2009 jijini Dar es Salaam, kujadili sera na mikakati ya kuleta mapinduzi ya kilimo cha Tanzania pamoja na utekelezaji wake chini ya kaulimbiu ya “KILIMO KWANZA”;


NA KWA KUWA asilimia themanini ya Watanzania hutegemea kilimo kwa ajili ya kuendeleza maisha yao;


KWA KUTAMBUA KUWA changamoto kubwa kwa Tanzania ni kupambana na umaskini na kwamba hili litawezekana hasa kwa kuongeza tija katika kilimo;


KWA KUZINGATIA KUWA Tanzania imejaaliwa kuwa na rasilimali za kutosha kwa ajili mazao, mifugo na uvuvi, ambazo kwa sasa matumizi yake yapo chini;


KWA KUFAHAMU KUWA Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kuwa na kiasi kikubwa cha maji kinachoweza kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji pamoja na ufugaji;


NA KWA KUTAMBUA KUWA jitihada za makusudi zimekuwa zikichukuliwa ili kuboresha kilimo bila mafanikio yakuridhisha;



HIVYO IMEAZIMIWA KWAMBA:

1.KILIMO KWANZA iwe ndiyo dhana ya kuleta mapinduzi ya kijani kwa lengo la kukifanya kilimo cha Tanzania kuwa cha kisasa na cha kibiashara;

2.Dhana ya KILIMO KWANZA ijumuishwe kwenye mipango mbalimbali ya Serikali ili kuhakikisha mafanikio ya utekelezaji wake;

3.Jitihada zifanyike katika kuongeza rasilimali mbalimbali ili kufanikisha utekelezaji wa KILIMO KWANZA;

4.Sekta binafsi ihamasishwe ili iongeze uwekezaji kulingana na wajibu wake katika utekelezaji wa KILIMO KWANZA; na

5.Utekelezaji wa KILIMO KWANZA utaongozwa na nguzo kumi zifuatazo:

I. Utashi wa kisiasa kutoa msukumo wa mapinduzi ya Kilimo.
II. Kugharamia mapinduzi ya Kilimo
III. Uboreshaji wa mfumo wa utawala wa kilimo.
IV. Mabadiliko ya mfumo mkakati katika kilimo.
V. Upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya kilimo.
VI. Vivutio vya kuchochea uwekezaji katika kilimo.
VII. Uendelezaji wa viwanda katika kuleta mapinduzi ya kilimo.
VIII. Sayansi, Teknolojia na Rasilimali Watu katika kuwezesha mapinduzi ya kilimo.
IX. Uendelezaji wa Miundombinu ili kuwezesha mapinduzi ya kilimo.
X. Uhamasishaji na ushirikishwaji wa Watanzania kuunga mkono na kutekeleza KILIMO KWANZA.

5 comments:

  1. Kila kitu kilichoandikwa/semwa kinaonyesha /letesha mategemeo , tatizo waTanzania ni watu wazuri sana kwa kutoa ahadi lakini sio kutekeleza. Mungu ibariki Tanzania yetu.

    ReplyDelete
  2. Hii ndiyo kauli mbiu ya CCM katika uchaguzi mwaka kesho nini. Ni yale yale tu hakuna jipya. KILIMO NDIYO UTI WA MGONGO WA TAIFA imetufikisha wapi? Nashangaa nchi bado imesimama wakati UTI WA MGONGO wake uko nyang'anyang'a. Medical miracle au?

    ReplyDelete
  3. Kilimo chetu inabidi kibadilike kutoka kwa wakulima wadogo wadogo mpaka angalau wakulima wa kati na hata jembe la mkono inabidi tuachane nalo na kuhamia kwenye wanyama kazi na matreka
    Wakulima pia wanahitaji ujuzi wa kuanzia mbegu gani watumie kwa sababu kila mbegu inayozalishwa huwa inahitaji mazingira fulani kama hali ya joto, mvua na udongo wa aina fulani
    Pia matumizi halisi ya mbolea na dawa za kuuliwa wadudu waharibifu kutokana na mahitaji ya zao na sehemu husika
    Tunahitaji kilimo cha umwagiliaji ili kuweza kuzalisha chakula mwaka mzima na kuacha utegemezi mvua za msimu peke yake
    Kwenye mifugo tunahitaji mbegu bora na kinga za magonjwa mbali mbali na hii inatakiwa kuanzia kwa wanyama pori mbugani kwa sababu wao ndio wanaobeba magonjwa mengi ya mifugo (carriers) mashamba ya mifugo yasitegemee mvua peke yake bali yawe na kilimo cha umwagiliaji kwenye mashamba ya nyasi

    ReplyDelete
  4. Bennet pengine hii isihusiane moja kwa moja na post hii. namomba miongozo ya ufugaji bora wa nguruwe na kuku wa kisasa wa mayai. nataka kujua namna ya kuwalisha na kuwanenepesha, yaani michanganyiko ya vyakula na vyakula vyenyewe.

    ReplyDelete
  5. Asante sana Bennet, kwakweli blog yako inaelimisha, nami naunga mkono maoni yako ya kilimo kwanza. Inatupasa watanzania tujue kuwa kila kitu sasa hivi kinaenda kwa technologia, hivyo serikali inapotuhamasisha sio kuitoa kibanzi kuwa mkulima mdogo hataweza, wewe anza kama una nia na kwakushirikiana tutadai kusaidiwa kwa mafunzo, mikopo inapobidi, lakini anza wewe.

    ReplyDelete