KURASA

Tuesday, June 19, 2012

UBWIRI UNGA - UGONJWA MKUU WA MIKOROSHO


Moja ya matatizo makubwa ya uzalishaji wa  zao  la korosho ni ugonjwa wa Ubwiri unga.Ugonjwa huu unasababishwa  na vimelea aina ya uyoga (fungus) viitwavyo Oidium anacardii. Ugonjwa huu ni muhimu sana, kiasi kwamba kama haukuthibitiwa,  unaweza kupunguza mavuno kwa zaidi ya asilimia 70.       Ugonjwa huu umeenea katika  mikoa  yote inayolima zao hili Tanzania.  Hapo awali ugonjwa huu ulikuwa unaitwa kwa jina la“ukungu” kutokana na uhusiano wake mkubwa na haliya hewa ya ukungu  (litabwe  kwa  Kimakonde) unaoonekana  alfajiri/asubuhi katika miezi ya Juni - Septemba.  Hivyo  basi,  jina la Ubwiri unga linatumika sasa ili kuwawezesha wakulima wasichanganye vitu hivyo viwili.

MASHAMBULIZI
Ugonjwa huu unashambulia maeneo yote machanga na teketeke  katika  mti wa mkorosho, hasa machipukizi, majani, maua, mabibo na korosho changa (tegu). Athari kubwa  ya ugonjwa  huu inatokana na mashambulizi ya maua, ambayo hushindwa kufunguka  na  kuwezesha chavua kufanya kazi yake,  hatimaye  hunyauka  na kukauka.

DALILI
Maeneo yaliyoshambuliwa na ugonjwa huu, hufunikwa na unga unga mweupe au wakijivujivu  ambao huonekana kama vumbi vumbi. Vimelea au chembe chembe zinazoshambulia ni ndogo ndogo sana na hazionekani dhahiri kwa macho, ila kwa darubini. Chembe chembe hizi zinapozaliana kwa wingi katika maeneo ya mshambulizi, ndipo huonekana kama unga unga mweupe/kijivu. 

KWENYE MAJANI
Pamoja na kufunikwa na unga unga,  majani yaliyoshambuliwa husinyaa, hubadilika rangi, wakati mwingine hukunjamana. Majani machanga zaidi yanaweza kupukutika, ambapo yale yaliyokomaa hayashambuliwi. Masalia ya mashambulizi  kwenye majani yaliyokomaa, huonekana kama mabaka ya kahawia, hata hivyo hayapukutiki.

KWENYE MAUA
Maua yanaweza kushambuliwa hata kabla ya kuchanua. Pamoja  na  kufunikwa na unga unga weupe/kijivu, maua yaliyoshambuliwa sana hushindwa  kuchanua  na hatimaye hukauka kabisa na kuwa kama “majani yachai”. Hili ndilo sababisho kubwa la upungufu wa zao la korosho.

KWENYE MABIBO

Mabibo yaliyoshambuliwa huonyesha  unyafuzi,hupasuka pasuka na ngozi yake huonekana kuwa chafu. Hatimaye,  mabibo  hayo huwa madogo kwa umbo, yenye  maji kidogo  sana, hivyo kuyafanya maji yake kuwa matamu sana.
KWENYE TEGU NA KOROSHO
Tegu  zilizoshambuliwa  huweza kubadilika rangi yake ya kijani/nyekundu na kuwa ya hudhurungi au bluu iliyo mzito. Tegu zikishambuliwa zingali changa sana, huweza kupukutika. Tegu zilizoshambuliwa zikifikia kukomaa, zinaonyesha uharibifu mkubwa wa ngozi yake na huonekana chafu, hatimaye, wakati wa mauzo hutengwa katika  daraja  lachini (grade II).

KUSTAWI KWA UBWIRI UNGA
Vimelea vya Ubwiri unga vinaishi kwenye mimea iliyo hai tu, haijawahi kuoteshwa katika  maabara.  Ugonjwa huu hushamiri na kustawi vizuri katika  majira  yenye ukungu, hasa  kuanzia mwezi Mei/Juni hadi Septemba karibu kila mwaka. Mazingira mwafaka kwa ugonjwa huu ni:
• Joto: 26 - 28 0C (bora 25 C)
• Unyevu (RH): 80-100% (bora 95%)

Ubwiri unga pia hupendelea  zaidi mikorosho iliyosongamana na isiyopitisha hewa vizuri. Ugonjwa huu hupendelea mazingira ya kiangazi, hasa  kuanzia mwezi Juni hadi Septemba, haupendelei hali ya mvua na  joto jingi.  Hivyo basi, katika miezi mingine (hasa wakati wa masika), vimelea hujificha na kuishi Kwenye maotea  au machipukizi uvunguni  mwa mikorosho au kwenye maua yasiyo ya msimu. Hivi ndivyo  vyanzo vya Ubwiri unga, vyenye uwezo wa kuhifadhi ugonjwa msimu hadi mwingine. Ugonjwa huu husambazwa kwa upepo ambao nao  pia hushamiri sana katika miezi ya Mei/Juni hadi Septemba.

KUDHIBITI
Zipo njia aina tatu zinazotumika kuthibiti Ubwiri unga, nazo ni mbinu za asili, mbegu bora na madawa.

MBINU ZA ASILI (Cultural control)

Kuondoa vyanzo vya Ubwiri unga (sanitation).
Hii ni kazi ya mikono ya kuondoa machipukizi na maotea yanayojificha kwenye uvungu  wa  mikorosho, kutumia vifaa kama vile upanga, mundu, shoka nk. Msingi wa kazi hii ni kupunguza kasi ya ugonjwa huu katika shamba kwa kuchelewesha mlipuko na  kasi ya mashambulizi. 

Kubadili mazingira ya ugonjwa katika miti.
Kupunguzia  matawi  (prunning) ya mikorosho ili kufanya  umbile  la  mwamvuli katika miti, ili kuruhusu joto na upepo kupenya kirahisi, inasaidia sana kuthibiti Ubwiri unga.
Kupunguza  miti (thinning) iliyosongamana na kuacha nafasi ya kutosha kati  ya miti, itasaidia kupunguza kuenea kwa ugonjwa.  Miti ikiwa  katikanafasi  ya kutosha, itawezesha hewa  kupenya  vizuri na kubadili mazingira ili yasiwe mazuri kwa kustawi kwa ugonjwa.

Kupanda mikorosho inayovumilia/kuhimili ugonjwa.
Ipo baadhi ya mikorosho  ambayo  inaweza  kuhimili mashambulizi ya ugonjwa hata kuweza  kutoa  Mazao bila ya kutumia kinga yoyote.  Aina zingine zinaweza kutoa maua na kuzaa kabla  ya  athari za ugonjwa hata kuweza kukwepa mashambulizi.  Hii  ni  baadhi  ya mikorosho  bora  ambayo hatimaye imepandwa katika eneo moja katika vituo  vyetu vyote vya kuendeleza korosho (Cashewnut Development Centre )kama NALIENDELE. Mbegu zinazopatikana toka mashamba hayo ni mbegu bora (polyclonal seed) ambazo zinaweza kuzaa bila madawa, lakini huzaa vizuri zaidi kama mtu atatumia dawa pia.


MATUMIZI YA MADAWA

Dawa ya Salfa (Sulphur)
Salfa ndiyo dawa inayotumika kwa wingi zaidi kukinga ugonjwa wa Ubwiri unga. Dawa hii ambayo ni ya unga, inapulizwa kwa kutumia mashine maalumu (motorised blower)  ya kupulizia dawa k.m. Maruyamana Solo. Kiwango cha  gramu  250 kwa mti, kwa mzunguko, ndicho kinapendekezwa.  Hivyo basi kwa mizunguko mitano kiasi cha kilo 1.25  cha  salfa kwa mti kwa mwaka kinahitajika.  Pia kuna salfa za maji kama Thiovit ambazo unaweza kupulizia kwa kutumia vinyunyuzia dawa vya kawaida (knapsack sprayer)

Wakati wa kuanza kupulizia sailfa
Mpulizo wa kwanza unaanza ambapo karibu asilimia 20za maua yamejitokeza na wakati sawa, zaidi ya asilimia 5 ya maua hayo tayari yawe  yanaonyesha dalili  za ugonjwa. Upimaji wa maua ili kujua  lini  upuliziaji  uanze, inasaidia kufanya matumizi sahihi  ya  dawa,  hatimaye faida/pato litakuwa kubwa kwa mkulima.
Inashauriwa kwamba upuliziaji ufanyike asubuhi na mapema, wakati ambapo kuna umande. Asubuhi, upepo nao  huwa  hauna nguvu sana na inashauriwa upuliziajiusizidi ya saa 3 asubuhi. Umande unasaidia salfa ya unga iweze kunata kwenye majani na maua. Ila kwa salfa ya maji kama thiovit unaweza kupulizia wakati wowote.vipindi vifuatavyo, vimependekezwa katika upuliziaji:Siku 14      14      14       21     21 

Dawa zingine badala ya salfa.
Madawa kadha wa kadha yamefanyiwa  utafiti sambamba na salfa. Aina tatu za dawa hizo   (waterbased  organics), zimependekezwa kwa matumizi ya wakulima, nazo ni Bayfidan, Anvil na Topas.  Kiwango cha upuliziaji ni ml 10 - 15 za dawa ndani ya0.75  -  1.25  za  maji kutegemeana na ukubwa wa mti. Vipindi kati ya mipulizo ni wiki tatu (siku  21)  na awamu (raundi) 3 zinatosha kwa msimu. Inashauriwa kwamba kutokana na gharama za dawa yamaji, zinafaa zitumike kwenye mikorosho ambayomkulima ana uhakika wa kutoa zaidi ya kilo 4 baada ya kupulizia.  Miti inayotoa chini ya kiasi hicho heri isipuliziwe, vinginevyo italeta hasara

2 comments:

  1. Nimefurahi sana kusoma utaalamu huu katika blogger. nataka kuuliza katika heka moja ni miche mingapi ya mahindi inastahili kuwepo ili kutoa matokeo mazuri kujua kila heka utapata gunia ngapi?. vivyo hivyo kwa ufuta na halizeti ukizingatia kupanda kwa mistari?. mlangwaa@yahoo.com

    ReplyDelete
  2. Nataka kujua kuhusu nikitaka kuanzisha ugugaji wa samaki vitu gani vya muhimu vya kuanza navyo

    ReplyDelete