KURASA

Tuesday, June 19, 2012

UTITIRI - WADUDU WASUMBUFU WA MIKOROSHO


Utitiri wa mikorosho  au kwa jina lingine thrips (Thrips rubrocinctus), ni wadudu wadogo sana wenye mwili laini na rangi  kati  ya njano, kahawia au nyeusi. Utitiri  wakubwa  (adults) hutambulika kwa kuwa na mabawa na mwili wa kahawia (dark brown) au  mweusi,  pamoja  na upito  (band) wa rangi nyekundu kifuani. Wanaonekana vizuri kwa kutumia kikuzia umbo (lens).
Katika kipindi kirefu, utitiri ulikuwa ukionekana katika  maeneo mengi yanayolimwa korosho, lakini athari zake zilikuwa ndogo. Katika miaka ya hivi karibuni wameonekana kwa uwingi na kuleta hasara kubwa hasa katika  tarafa  za Lisekese na Chikundi wilayani Masasi.  Pia mashambulizi  ya wadudu hawa yameonekana katika wilaya za Nachingwea na Newala  kwa kiwango kidogo. Inakisiwa kuwa uongezekaji wa  wadudu  hawa husababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

MZUNGUKO WA MAISHA
Utitiri wakubwa hutaga mayai katika sehemu yachini  ya majani. Mayai yanaanguliwa baada ya siku 3 hadi 4 na  kutoa  vijititiri  vidogo  sana (larva I) ambavyo huwa ni  vyepesi  sana. Huingia  hatua  ya pili (larva stage II) baada ya siku 7 hadi 8.  Hatua hizi ndizo  ziletazo uharibifu mkubwa maana ndizo hatua za ulaji na ulafi  wa  hali ya juu. Baada ya wiki moja tena, ndipo hutokeza hatua ya kwanza ya “ninfu” (Nymph stage I) na hatua yake ya pili baada ya siku 3 hadi 4. Katika hatua hizi mbili (nymph stages), vijidudu hivi havitembei  wala  kula chakula bali hukaa mahali pamoja, hasa kwenye ardhi. Hatua hii ya “ninfu” hudumu kwa siku 11 hadi 12 kabla ya kupevuka na kuwa utitiri wakubwa (adults). Hivyo Mzunguko wa maisha yao toka yai hadi kupevuka ni mwezi mmoja. Utitiri hushamiri sana wakati wa  kiangazi mara tu  baada  ya mvua,  hasa kati ya mwezi June na Oktoba. Utitiri hupungua kabisa wakati wa mvua, hata hivyo huvuka msimu hadi mwingine kama utitiri wakubwa.

MASHAMBULIZI
Utitili wachanga pamoja na  wakubwa, hushambulia upande wa chini wa majani hasa yaliyokomaa, machipukizi na mashada ya maua. Utitili wachanga hubeba tone la majimaji mkiani na kudondoshea juu ya majani,  ambapo likikauka huacha doa la kahawia  au  nyeusi, lakini hasa rangi ya kutu. Maeneo yaliyoshambuliwa na  utitili  hubadilika rangi na kuwa na weupe weupe wenye mng’aro wa rangi ya fedha (silvery).  Baadaye hubadilika na kuwa na rangi ya udongo (kahawia), hatimaye hukauka na majani hupukutika Eneo  linaloshambuliwa hudumaa na uzalishaji  kuathirika. Maeneo mengi ambayo hushambuliwa na utitili huwa  korosho  hazizai kabisa. Miti iliyopukutisha majani kwa sababu yamashambulizi  ya utitiri, huweza kuchipuza tena kwenye mwezi Novemba na Desemba.

MAZAO MENGINE YANAYOSHAMBULIWA NA UTITIRI
Wadudu hawa hushambulia majani na hata maua ya aina  mbalimbali ya mazao na mimea, kama vile  mazao ya bustani (vitunguu nk), michungwa, pamba, aina ya nafaka. Kwa sababu ya wingi wa aina ya mimea inayoshambuliwa na utitiri,  udhibiti  wa wadudu hao unaweza kuwa mgumu kwa kiasi fulani.

KUSHAMIRI KWA UTITIRI
Wadudu hawa hupendelea mikorosho iliyosongamana,  isiyopitisha hewa vizuri, mikorosho  isiyopogolewa na mashamba yasiyohudumiwa kwa ujumla.  Hupendelea hasa miti mikubwa. Utitiri hupendelea hali ya ukame au kiangazi cha muda mrefu.

KUSAMBAA
Utitiri husambazwa hasa kwa njia ya upepo  au kwa kupanda vipando  (propagation  materials) ambavyo vimeshambuliwa.

KUDHIBITI KWENYE MIKOROSHO

Njia  pekee  inayotumika kudhibiti utitiri ni matumizi ya madawa. Dawa ya BASUDIN au KARATE ndiyo iliyopendekezwa  na watafiti kudhibiti utitiri wa korosho. Mchanganyiko wa mililita  5  za KARATE na lita moja ya maji  unatosha kudhibiti  wadudu hawa katika mti mkubwa usiozidi kipenyo (diameter) cha mita 10. Ni jambo la muhimu kukagua mashambulizi kuanzia mwezi Mei. Upuliziaji unaanza mara tu baada ya kuona dalili za  mashambulizi  au kuwaona wadudu wenyewe na kurudia baada yawiki tatu (siku 21).  Upuliziaji  unafanyika kutumia mashine ya moto (Mist blower) au yakawaida (Knapsack sprayer)  kutegemeana  na ukubwa wa mti. Ni muhimu kuanza kupuliza dawa mapema, ili kuweza kuwathibiti wadudu hawa wakiwa katika hatua zao za mwanzo kabisa za ukuaji wao ( hatua za lava na ninfu). Hii ni  muhimu kwa sababu ni vigumu kuudhibiti utitiri  wakubwa. Awamu 2 hadi 3 zinatosha kuthibiti wadudu hawa katika msimu mmoja. Ikibidi,  matunda (mabibo) yaliyopuliziwa dawa yasitumike mpaka baada ya siku 21

No comments:

Post a Comment