KURASA

Sunday, March 29, 2009

MKUYU

MTI WA MKUYU



Huu ni mti unaopatikana sehemu nyingi sana duniani kuanzia ukanda wa joto mpaka nyanda za juu zenye baridi, ni mti ambao unakuwa na majani kipindi chote cha mwaka (evergreen) sehemu unazopenda kuota ni mabondeni na hasa sehemu chepechepe ingawa mara nyingine hupatikana hata sehemu ambazo si za majimaji sana.


SHINA NA MAUA/MBEGU




Mti huu unasifika sana kwa sifa ya kuhifadhi vyanzo vya maji, kama una kisima cha msimu ambacho hukauka maji kipindi cha jua kali basi panda mti huu karibu na kisima. Mti utakapo kuwa na ukubwa wa wastani kisima chako kitakuwa na maji mwaka mzima, mizizi yake ambayo hutambaa sana huifadhi maji ardhini yasichukuliwe kama mvuke wakati wa jua kali na pia kivuli cha majani yake pia husaidia kutunza maji ardhini

Mti huu umetajwa sana kwenye Biblia, Adam na Eva baada ya kula tunda la kati na kujikuta watupu walijisitiri kwa kutumia majani ya mkuyu, Zakayo wakati anataka kumuona yesu alitangulia mbele na kupanda juu ya mkuyu


MBEGU/MAUA



UPANDAJI
Ingawa ni mti mzuri sana kwa wanamazingira lakini ni mti mgumu sana kuuotesha, kuotesha kwa njia ya MBEGU ni ngumu zaidi kwa sababu mbegu zake (ambazo pia ni maua) nyingi huwa tupu ndani bila ile mbegu yenyewe, pia iliziote vizuri ni lazima ziliwe na popo ambao hupenda sana kula matunda yake na kisha ikitolewa kwa njia ya kinyesi ndio inaota vizuri zaidi (seed scarification), mwisho ni lazima ioteshwe sehemu iliyo chepechepe au imwagiliziwe sana.

Njia nyingine ni yakuotesha kwa kutumia matawi yake ambapo unakata na kuyaotesha kama vipandikizi, hii kidogo ina mafanikio lakini ni vipandikizi vichahe tu ndio vyenye uwezo wa kuota na vingi zaidi ya asilimia 90% havioti

Friday, March 27, 2009

KOMA-MANGA



Huu ni mmea unaopatikana sana sehemu za pwani kama Zanzibar, DSm, Tanga, Mombasa,Mtwara na lindi, mmea huu huzaa matunda yake ambayo huanza na ua kama kawaida na kisha tunda lenyewe. Komamanga kama tunda huwa la kijani kwa nje iliyochanganyika na kahawia, na ukilipasua ndani utakutana na mbegu nyingi zenye rangi nyekundu ambayo hutofautiana kukolea rangi na ukubwa kutokana na aina mbalimbali (specie)



MATUMIZI
Tunda lenyewe linatumika kama dawa ya kuongeza nguvu za kiume kwa wanaume, na pia zinasaidia kukomaza mbegu za uzazi kwa wanawake na wanaume. jinsi ya kutumia ni kulikata kisha unatoa mbegu zake na kuzila kama chakula.




matumizi mengine ni kama dawa ya tumbo kuharisha, pia yanasaidia kupunguza sukari mwili kwa wale wagonjwa wa kisukari (kwa kiasi kidogo). maua yake yakipondwa na kuchanganywa namji yatoa dawa ya kuoshea vidonda na kupunguza uvimbe.

Thursday, March 26, 2009

MHALINTA - Mti unaotoa povu la sabuni

MTI WENYEWE



Huu mti niliukuta mkoani Tanga wilaya ya Mkinga tarafa ya Maramba kijiji cha Muhinduro mtaa wa Majengo, ni mti unaokuwa mkubwa kama miti mingi tuliyoizoea ukiwa na majani ya wastani na unakuwa na majani muda wote wa mwaka (ever green)



MBEGU ZAKE
Ndizo hutumika kufulia nguo mbadala wa sabuni, unachotakiwa kufanya ni kukusanya mbegu kama 5 kwa ajili ya kufulia nguo moja, weka nguo yako ndani ya maji kiasi kisha chukua mbegu zako na uzipasue. Toa ile mbegu ya ndani na ubakie na maganda yake kisha tumia haya maganda kutengeneza povu ndani ya maji yako kisha fua nguo yako kama kawaida.



Wenyeji waliniambia kuwa mti huu unazaa kwa misimu miwili kwa mwaka kutokana na majira ya mvua sehemu za pwani yaani masika na vuli, na kila msimu huwa miti inazaa mbegu nyingi na za kutosha

OMBI kwa wanaoujua mti huu kwa majina mengine, jina la kiingereza na jina la kisayansi ninaomba wanifahamishe kwa kupitia blogu hii