Jana nilipata mgeni ambaye ameomba jina lake nilifiche, mgeni huyu aliomba tukatembelee shamba langu dogo la miti ya mitiki lililopo Kiluvya umbali wa kama km 30 kutoka jijini Dar es salaam. Shamba hili dogo (la mfano) lina ukubwa wa ekari mbili ambazo ziko bondeni, ni bonde lenye rutuba sana na sehemu ya bonde hili hutuamisha maji wakati wa mvua nyingi.
MGENI WANGU
CHINI YA MITIKI KUNA MPUNGA, HII NDIYO SEHEMU INAYOTUAMA MAJI NA HAINA MITI MINGI
Eneo la shamba hili kama likipandwa lote linauwezo wa kuchukua miti 1000 ila kwa sababu sehemu ya bonde hutuamisha maji basi kuna miti 800 tu, kwa sababu mitiki haiwezi kuota sehemu yenye kutuama maji (rejea makala zangu za mwanzo) Msimu huu wakati mvua zitakapokuwa zinaishia na bonde halituamishi maji, nitajaribu kurudishia hiyo miti 200 iliyobaki ili nione kama itashika, kwa sababu nina imani kama itashika mpaka mvua zijazo hata kama maji yatatuama haitakufa.
CHINI YA MITIKI KUMEPANDWA MIHOGO
Huyu mgeni wangu ni mkulima ambaye ana shamba lake kiasi cha ekari 50 sehemu za vigwaza unaingia ndani kulia kuufuata mto Ruvu. Hili shamba lake ni jipya na anategemea kuanza kupanda miti ya mitiki wakati wa mvua zamwezi wa 11, kwa sasa hivi anaanda shamba lake kwa kukata miti michache iliyopo pamoja na kulima vichaka na majani
CHINI YA MITIKI KUMEPANDWA MAHINDI
Ameniambia ataanza na ekari kumi kwa msimu wa kwanza kwa hiyo anahitaji kiasi cha miche 5000, kwa hiyo nina kibarua cha kuanza kuandaa kitalu cha kuoteshea mbegu hizo. Kitalu changu nitakiandaa kule kluvya kwa sababu ya urahisi wa kupitia miche wakati wa kupanda, yaani unangoa miche na kwenda kuipanda siku hiyo hiyo, nilimwomba tukatembelee shamba hilo ili niweze kujua vitu kama udongo unarutuba kiasi gani na je unatuamisha maji au la na kwa kaisi gani? Pili kujua kiasi cha mvua cha eneo husika kwa kuangalia uoto wa asili. Pia alikuwa anataka kujua kama anaweza kuchimba kisima cha asili na kukilinda kwa miti ya mikuyu.