KURASA

Thursday, January 26, 2017

DONDOO ZA ZIADA KATIKA UFUGAJI WA KUKU

VITU AMBAVYO HUTAKIWI KURUHUSU KUKU WAKO WALE.

*Kuna baadhi ya vitu uwa tunawapa kuku kwa mazoea au tunawaachia tu tunapoona wanakula lakini ukweli vinakuwa na madhara hebu tuviangalie;

*VITUNGUU
vitunguu vina sumu iitwayo thiosulphate ambayo huua seli hai nyekundu. Iwapo utalisha kwa kiwango kikubwa itasababisha upungufu wa damu(anaemia) au kifo.

*MAHARAGWE MABICHI AU YASIYOPIKWA.
Maharagwe mabichi au yasiyopikwa yana sumu iitwayo hemaglutin ambayo ni hatari kwa kuku kwahiyo unashauriwa kupika au kuchemsha kuondoa sumu hii.

*MCHELE MKAVU.
Kuku wanaolishwa Mchele mkavu kuna hatari mchele huo kujikusanya tumboni na kusababisha matatizo.

*MAGANDA YA PARACHICHI
Kuku wanapokula maganda ya parachichi itapelekea kuingiza sumu mwilini kwa hiyo epuka maganda ya parachichi yasije kujichanganya na chakula.

*MBEGU ZA APPLE
Mbegu za apple zina sumu iitwayo cyanide japokuwa kuku wanapenda apples hakikisha unatoa mbegu.

*VYAKULA VYENYE CHUMVI NYINGI.
Vyakula vyenye chumvi nyingi husababisha ugonjwa uitwao hypernatremia kwa hiyo mwili wa kuku hauhitaji kiasi kikubwa cha chumvi. Kuku wanaweza kuvumilia kiasi kidogo cha chumvi nacho ni 0.25% kwenye maji. Endapo kutakuwa na uhaba inaweza kupelekea ugonjwa huo.


WADUDU WASUMBUFU KATIKA UFUGAJI WA KUKU ( VIROBOTO, CHAWA NA UTITIRI)

Mara nyingi wafugaji wanakabiliwa na changamoto kadhaa katika ufugaji wao wa kuku. Changamoto hizo ni  pamoja na wadudu wasumbufu mbalimbali mfano,  Viroboto, Utitiri na chawa. wadudu hawa wamekuwa tishio kubwa katika kufanya ufugaji wa kuku uwe wenye tija kutokana na kusababisha vifo vingi.

Katika banda lako la kuku ukivamiwa na wadudu hawa kwa hakika afya ya kuku wako itaanza kuzorota kwa haraka na kuwafanya kuku wako waonekane kama wanaumwa vile. Ni wadudu wanaonyonya damu kwa kiasi kikubwa sana na hivyo kusababisha kuku kufa kwa ugonjwa wa kuishiwa damu mwilini. Lakini vilevile kwa kuku wanaotaga huwafanya washushe utagaji wao ghafla. Ukiwatazama unaweza kuona kama wanaumwa kwa maana wanakonda, kuzubaa na kupoteza hamu ya kula. Muda mwingi wanakuwa wanajichokonoa na kujikuna katika manyoya yao kwa kutumia midomo yao. Hii ni kutokana na adha wanayopata hasa kuwashwa na maumivu wanayosababishiwa.

Viroboto ni rahisi kuonekana kwa kuwa wanakaa sehemu za wazi za kuku mfano kuzunguka maeneo ya macho,  katika ndevu na mapanga yao nk. Tatizo ni kwa utitiri na chawa wenyewe si rahisi kuonekana kama mfugaji siyo mfuatiliaji wa karibu wa kuku wake.  Utitiri na chawa wenyewe wanakaa ndani ya manyoya ya kuku kwenye ngozi kabisa. Utitiri ni mdogo kuliko chawa. Chawa wanakuwa weupe hivi wanajishika katika ngozi. Utawaona endapo utapekenyua katika manyoya ya kuku. Wakati utitiri wenyewe unatakiwa uwe na macho mazuri kuweza kuwaona kwa kuwa ni wadudu wadogo zaidi lakini ukipekenyua kwenye  manyoya na kufika ndani kabisa kwenye ngozi utawaona wakitembeatembea. Wanapenda kukaa kwenye kwapa za kuku na kwenye ngozi ya mwili wake

Usipojua vizuri kuhusu wadudu hawa unaweza ukadhani kuwa kuku wako wanaumwa ugonjwa mwingine kabisa katika magonjwa ya kuku. Na kwamba utahangaika kutumia gharama nyingi za madawa huku kuku wako wakiendelea kuzorota bila kupata nafuu ya matibabu unayohatumia. 

Ni muhimu kabla ya kutibu kuku wako ukawasiliana na mtaalamu wa mifugo (Ofisa Ugani) aliye karibu yako ili aweze kukusaidia kukukagulia na kubaini tatizo halisi la kuku wako.  Kwa maana kuku hawahitaji mchezo wa kubahatisha. Unatakiwa ujue ni tatizo gani hasa linawakabili kuku wako ili waweze kupatiwa tiba ya uhakika.

Sasa nini kifanyike kama banda lako litakuwa limevamiwa na Visumbufu hivyo?


Kuna dawa nyingi za kutumia, unaweza kutumia Dawa za unga za kunyunyiza mfano Akheri powder au Sevin (Dudu) Dust. Dawa hizi utanyunyiza kuku wako wote mmoja baada ya mwengine kwenye manyoya yao na sehemu zile ambazo zimevamiwa na wadudu hao mfano machoni na kwenye mapanga yao na vilevile utapaswa dawa hizo kunyunyiza kwenye maranda au vumbivumbi la ndani ya banda la kuku kwa sababu vumbi ni makazi mazuri ya Viroboto na Utitiri.

Lakini wakati mwingine unaweza kujitahidi kutumia dawa hizo za kunyunyiza kwenye mabanda na kuku wenyewe lakini zisifue dafu. Mara nyingi nimeliona hili  kwenye mabanda mengi ya wafugaji. Sasa ukifikia katika hali hii ufumbuzi wa haraka ni kufanya usafi wa banda lako lote. Ondoa maranda na  vumbi lote la samadi kisha deki kwa kutumia dawa ya V- RID Disinfectant. 


Pia utapaswa kupuliza dawa hiyo katika kuta za banda lako. Ukiona tabu kufanya hivyo basi baada ya kuondolewa samadi yote katika banda lako la kuku na kufuta vumbi ukutani, deki kwa maji vizuri bila dawa kisha baada ya banda kukauka vyema paka chokaa kote sakafuni ukutani hadi darini kama banda lako lina dari na kama halina basi utaishia tu katika kuta za banda na sakafuni.

Baada ya kukamilisha zoezi hilo ogesha kuku wako wote kwa kutumia dawa ya Paranex, Tik Tik au dawa yoyote ya kuogeshea mifugoiliyochanganywa kwenye maji yaliyowekwa kwenye dishi kubwa la lita ishirini au arobaini au hata ndoo unaweza kitumia. Uogeshaji utafanyika kwa namna ya kumtumbukiza kuku mmoja mmoja  katika lile dishi au ndoo kisha utamtoa.

Ni tendo linalotumia chini ya nusu dakika. Unamtumbikiza unamtoa unamtumbikiza tena unamtoa ni kama mara mbili hivi lengo ni kuhakikisha kuwa dawa inapenya vizuri katika kila sehemu ya mwili wake.

Baada ya kukamilisha zoezi hilo basi kuku wako watarudi bandani wakiwa wako vizuri na visumbufu vyote vikiwa vimetokomezwa kabisa. Kutokea hapo utaanza kuona sasa afya ya kuku wako ikianza kuimarika na kama walikuwa walishaanza kutaga watarudi katika utagaji wao wa kawaida.


Angalizo. Unapotumia dawa ya kuogesha ni vizuri zoezi hili likafanyika mchana wakati jua linawaka ili kusudi kuku waweze kukingwa na athari ya baridi itakayowasababishia kupata nimonia. Vilevile ni vizuri ukawa na mtaalamu karibu atakayekusaidia kuchanganya dawa kwa uwiano sahihi na maji ili kuepusha madhara kama dawa haitachanganywa katika uwiano.