KURASA

Friday, December 11, 2009

TANGAWIZI

1.0 UTANGULIZI:
Jina la kitaalamu ni Zingiber officinale
Tangawizi ni aina ya zao la kiungo ambalo sehemu inayotumika ni tunguu (rhizome) ambalo huonekana kama mizizi ya mmea. Asili ya zao hili ni maeneo ya kitropiki ya bara la Asia na hasa katika nchi za India na China. Zao hili linazalishwa kwa wingi kutoka katika nchi ya Jamaica. Hapa nchini zao hili hulimwa katika mikoa ya Kigoma, Tanga, Morogoro, Pwani, Mbeya na Kilimanjaro.



Tangawizi hutumika kama kiungo katika kuongeza ladha, harufu na kuchangamsha katika vinywaji (kama chai, soda, juisi, vilevi n.k) na vyakula mbalimbali kama mikate, biskuti, keki, nyama za kusaga, achari n.k. Hutumika pia katika viwanda vinavyotengeneza madawa ya tiba mbalimbali kama dawa za meno, kikohozi, tumbo na muwasho wa ngozi n.k. pia hutumika katika vipodozi kama poda n.k).

2.0 AINA ZA TANGAWIZI
Hakuna uthibitisho wa aina za tangawizi ambazo hulimwa hapa nchini ila kuna dalili ya kuwa na aina za White Africa (Jamaica) na Cochin (flint); hii huwa na tunguu ngumu zenye nyuzi.

3.0 TABIA YA MMEA
Tangawizi ni mmea unaotambaa chini ya ardhi, wakati wa masika hutoa majani juu ya ardhi. Jamaica ina rangi hafifu ya kahawia na tunguu fupi wakati Cochin ina tunguu fupi zaidi lenye ngozi ya rangi iliyo kati ya kijivu na nyekundu. Mmea una urefu wa futi mbili na majani yake ni membamba marefu ambayo hufa kila mwaka yakiacha tunguu ardhini likiwa hai. Maua ya mmea huu yana rangi nyeupe au manjano.

4.0 HALI YA HEWA NA UDONGO
Zao hili hustawi katika maeneo yenye hali ya kitropiki, kutoka usawa wa bahari hadi mwinuko wa mita 1,500 au zaidi. Huhitaji mvua kiasi cha mm.1,200-1,800 na joto la wastani wa nyuzi za sentigredi 20-25. Hustawi vema katika udongo tifutifu wenye rutuba na usiotuamisha maji.

MMEA WA TANGAWIZI


5.0 UPANDAJI
Zao la tangawizi hupandwa kwa kutumia vipande vya tunguu vyenye kichipukizi kizuri angalau kimoja na huweza kukatwa katika urefu wa sm.2.5-5. Wakati mwingine, vichipukizi vinavyopatikana katika kumenya tangawizi huweza kuhifadhiwa na kutumika kwa kupanda. Kiasi cha kilo 840-1700 cha vipande vya tunguu huweza kutumika kwa kupanda katika hekta moja. Nafasi inayotumika kupanda ni kati ya sentimita.23-30 kwa 15-23 na kina cha sentimita.5-10 na mara nyingi hupandwa katika matuta. Baadhi ya mazao huweza kupandwa katika shamba la tangawizi ili kuweka kivuli chepesi ingawa si lazima kivuli kiwepo. Inashauriwa kumwagilia maji endapo mvua inakosekana.

Wiki 1-2 kabla ya kupanda weka mbolea ya samadi au mboji kiasi cha tani 25-30 kwa hekta na kwa kukuzia weka kiasi cha NPK kwa uwiano wa kilo 36:36:80. Tandaza nyasi shambani kuhifadhi unyevunyevu hasa pale kivuli kinapokosekana. Palizi hufanywa mara magugu yanapoota, dawa ya kuua magugu, kama simazine au round up hutumika.

MKATE WA TANGAWIZI NA LIMAO


6.0 Magonjwa na wadudu:
• Madoa ya majani yanayosababishwa na viini vya magonjwa viitwavyo Colletotrichum zingiberis na Phyllosticta zingiberi.
• Kuoza kwa tunguu; kunasababishwa na viini viitwavyo Pithium spp
• Mizizi fundo; inasababishwa na Meloidegyne spp.

7.0 UVUNAJI
Tangawizi huweza kuwa tayari kwa kuvuna kati ya miezi 9-10 baada ya kupanda, wakati majani yake yanapogeuka rangi kuwa njano na mashina kusinyaa. Tangawizi inayohitajika kwa kuhifadhi kwenye kemikali (preserved ginger in brine) huvunwa kabla haijakomaa kabisa, wakati ile iliyokomaa kabisa huwa kali zaidi na huwa na nyuzi hivyo hufaa kwa kukausha na kusaga. Mavuno hutofautiana kulinganana na huduma ya zao, mavuno yanaweza kuwa kiasi cha tani 20-30 cha tangawizi mbichi huweza kupatikana.

8.0 USINDIKAJI
Tangawizi ikisindikwa utapata unga, mafuta maalum (essential oils) n.k. Tangawizi iliyovunwa huweza kumenywa, kukatwa na kukaushwa juani au mara nyingine huchovywa katika maji yaliyochemka kwanza na ndipo kukaushwa au hukamuliwa mafuta. Pia tangawizi husindikwa na kuhifadhiwa kwenye chupa zikiwa zimechanganywa na sukari na/au chumvi au bila kuweka kitu chochote. Hata hivyo tangawizi ina Kiasi cha mafuta cha 16.0-18.0%.



9.0 SOKO LA TANGAWIZI
Soko la tangawizi lipo ndani na nje ya nchi, kiasi kikubwa kinauzwa nchini. Bei yake ni kati sh. 300-1,500/- kutegemeana na msimu.

10.0 GHARAMA ZA UZALISHAJI NA MAPATO
GHARAMA YA HEKTA MOJA:
Mbegu Tshs. 240,000/-
Vibarua 250,000/-
Mbolea(mboji/samadi) 150,000/-
Jumla 640,000/-
MAPATO:
Kilo 20,000 X300 =6,000,000/-