KURASA

Thursday, May 14, 2009

UFUGAJI WA SAMAKI WA CHAKULA - SEHEMU YA PILI

TILAPIA



Katika sehemu ya pili tutaongelea ufugaji katika bwawa la wastani kwa ajili ya samaki wa kitoweo na kuuza. Baada ya kuchagua sehemu ya kuchimba bwawa lako na kuzingatia vigezo vyote, kinafuatia ni uchimbaji wa bwawa lenyewe, kwa bwawa dogo uchimbaji unafanyikwa kwa kutumia mikono na vifaa kama jembe, sururu na chepe, kwa mabwawa makubwa inabidi kutumia mashine za kuhimbulia. udongo unaotolewa uwekwe kwenye kingo za bwawa na kutumika kuongeza kina, bwawa linatakiwa kuwa na kina kirefu upande mmoja na kina kinapungua kuelekea upande mwingine wenye kina kifupi, mfano mzuri angalia mabwawa ya kuogelea. Kwenye kina kirefu unaweka bomba lenye chekeche la nyavu za mbu kwa upande wa ndani ya bwawa kwa ajili ya kutolea maji, na bomba hili huzibwa lisitoe maji ila pale inapohitajika kupunguza maji.

MDAU AKICHIMBA BWAWA LA SAMAKI



Baada ya bwawa kukamilika kuchimbwa jaza maji mpaka juu ili kuangalia kama yanatuama na kama kuna kingo zinavuja, kisha weka chakula cha samaki ambacho ni mbolea ya samadi mchanganyiko ya kuku na ng’ombe kwa kipimo cha sehemu tatu za ng’ombe kwa moja ya kuku. Kwa bwawa lenye ukubwa wa ekari moja (70m*70m) kilo 80 za mchanganyiko huu huitajika kila siku, acha chakula kikae kwa siku 3 ndio uweze kuingiza samaki wako. Unaweza pia kuwalisha mabaki ya vyakula, pumba na mboga mboga, Lisha samaki wako kwa siku 6 na siku ya 7 usiwalishe , punguza maji robo na kujaza mengine. Bwawa lenye ukubwa wa ekari moja linaweza kuchukua samaki aina ya tilapia 2800-3000 ambao watakuwa tayari kuvunwa baada ya siku 90 – 120. Nivizuri kutumia samaki waliokwisha zalishwa sehemu /pembeni kwa sababu, ukiwaweka ili wazaliane wenyewe itachukua muda mrefu kuvuna kwa sababu samaki wakubwa wanatabia ya kula mayai na samaki wadogo. Kwa maelezo jinsi ya kutagisha samaki nitaanda makala inayojitegemea.

UJENZI WA MABWAWA YA KUDUMU



Uvunaji wa samaki hufanywa kwa kutoa maji yote katika bwawa na kuvuna samaki kwa ajili ya kuuza au kitoweo, baada ya kuvuna samaki wote bwawa limwagiwe chokaa, hii husaidia kuua vijidudu na kuzuia magonjwa kabla hujaingiza samaki wapya.
Adui mkubwa wa samaki wako ni vyura na baadhi ya ndege ambao hula samaki, pia kuna wanyama kama fisi maji ambao nao pia hula samaki, jinsi ya kujikinga na vyura ni kwa kuwaua kwa mkono na kuharibu mayai yao, ndege na wanyama unaweza kuwazui kwa kuweka uzio wa nyavu pande zote na juu.

BAADHI YA NDEGE WALAO SAMAKI