KURASA

Friday, July 3, 2009

MAJI MOTO-RAFIKI WA MKULIMA




1.0 Utangulizi
Majimoto (Oecophylla longinoda) ni wadudu maarufu sana katika Kanda ya Kusini mwa Tanzania. Wanaitwa Majimoto kwa sababu wanapouma,, huleta maumivu kama ya maji ya kukandia jeraha!. Kwa msingi huo huo, wayao huwaita “malumila” wasambaa huwaita “madadada” na Wamwera nao huwaita “ mangongongo”. Majimoto ni maarufu sana kwa uhodari wao wa kujenga viota kwa kufuma majani mabichi .
Ukubwa wa kiota hutegemea ukubwa wa ukoo, aina ya mti na majani yatumikayo na ulaini wa majani yenyewe. Kuna aina ya miti zaidi ya 75 ambayo Majimoto wameonekana kujenga viota vyao, ikiwa ni pamoja na mikorosho, michungwa, miembe na mengineyo.



Utafiti wa awali uliofanyika kwa mahojiano na wakulima mbalimbali, umeonyesha kwamba wengi hawajui faida yoyote toka kwa wadudu hawa, zaidi sana walisimulia athari zao kwamba ni wadudu wanaouma sana na kuleta maumivu makali. Nimeandaa makala hii ili kuhamasisha na kufundisha watu kwamba Majimoto ni rafiki wa mkulima.

2.0 Maisha ya Majimoto
Ukoo wa Majimoto una malkia mmoja tu ambaye analishwa na watenda kazi wakuu, ambapo yeye kazi yake ni kutaga mayai. Akitaga mayai watenda kazi wadogo (minor workers) ndio huchukua na kuatamia na hatimaye kuwatunza wachanga wanapototolewa.

Watenda kazi wakuu ndio hufanya mawindo na mashambulizi makali katika mti hadi ardhini, nao hukamata wadudu aina nyingi tu ambao wanakutana nao. Mmoja akimshika mdudu, hutoa harufu ya tahadhari na kufumba na kufumbua Majimoto wengi hujikusanya na kusaidia mashambulizi hadi kuua na hatimaye kupeleka chakula katika viota vyao.




Majimoto hupenda kuishi na kuwalinda wadudu wengine aina ya “Homoptera” katika namna ya ushirika. “Homoptera” hao, kama vile Hilda spp, Coccos spp n.k., hutoa aina ya majimaji mwilini mwao (honey dew) ambayo hutumika kama chakula kikuu kwa Majimoto; wakati huo huo, wadudu hao hunufaika kwa ulinzi toka kwa Majimoto dhidi ya adui wa kila namna. Uhusiano huu hauleti madhara yoyote kwa wakulima wa korosho.

3.0 Matumizi ya Majimoto katika kuthibiti wadudu waharibifu
Tangu miaka ya nyuma (AD 304), Majimoto walitumika huko China kuthibiti wadudu waharibifu katika mazao kama vile michungwa. Katika nchi ya Tanzania, matokeo ya majaribio yameonyesha kwamba Majimoto ni wadudu mashuhuri sana katika kuthibiti mbu wa mikorosho na minazi. Mikorosho yenye Majimoto wengi haishambuliwi na mbu kulinganisha na ile isiyo nao. Majimoto wakitanda kwenye machipukizi, maua au tegu, hufanya ulinzi mzuri sana dhidi ya mashambulizi ya mbu waharibifu. Asilimia 65 ya mashamba ya korosho Kusini mwa Tanzania, tayari kuna makoloni ya wadudu hawa, lakini siyo mikorosho yote katika shamba ina Majimoto na asilimia 85 ya michungwa yote Tanga ina makoloni ya majimoto Hivyo, kuna haja kubwa ya kuwaneemesha Majimoto

:
3.1 Jinsi ya kuwaneemesha Majimoto.
Majimoto kama rafiki wa mkulima wanahitajika waneemeshwe ili waongezeke na wawe wengi katika mikorosho ili kufanya ulinzi thabiti dhidi ya wadudu waharibifu. Mbinu ambazo hutumika kuwaneemesha Majimoto ni pamoja na:
• Kuhamisha na kupandikiza Majimoto

Majimoto wanaweza kuhamishwa toka mti mmoja na kupandikizwa katika mti mwingine. Viota vya Majimoto vinaweza kukatwa toka mti mwingine na kufungiwa katika matawi ya mti mwingine, hasa karibu na eneo lenye machipukizi mapya. Majimoto hawa wanaweza kujijenga, kuzaliana na kuanzisha makoloni mengine mapya katika miti waliohamishiwa. Hii inadhihirika kwa ongezeko la idadi ya viota vinavyojengwa wiki moja hadi nyingine.
Angalia: Majimoto wa koo/familia mbili tofauti wanaweza kudhuriana. Uangalifu ufanyike kiasi kwamba upandikizaji wa Majimoto ufanyike kwenye mti ambao hauna kundi lingine ili kuepuka ugomvi na mauaji baina yao.

• Kueneza kwa njia ya kamba


Majimoto wanaweza kuenezwa kwa kutumia kamba kutoka mti mmoja hadi mwingine, ili kuifanya kamba kama daraja la juu kwa juu. Kamba inapaswa kufungwa kwenye tawi karibu na kiota cha Majimoto nao wataweza kupita hadi mkorosho mwingine na kuanzisha makoloni mapya hatimae kuzidi kuongezeka.
Majimoto hupendelea kupita kwenye kamba za kienyeji na hasa kamba zitokanazo na ukindu au magome ya miti. Hawapendelei kupita kwenye kamba za viwandani, hivyo epuka kutumia kamba ya katani au nailoni kwa ajili ya kazi hii na pia usishike kamba ya kienyeji kama umeshika vitu vyenye harufu kali kama mafuta ya kujipaka.

• Kuthibiti adui wa Majimoto


Imefahamika kwamba jamii ya Sisimizi (Pheidole megacephala) pichani juu na Sangala ni maadui wa Majimoto. Miti ambayo imetawaliwa na wadudu hawa, ni vigumu kukuta Majimoto wakijitawala. Ili kuwaneemesha Majimoto, inatupasa kuwadhibiti wadudu hawa.
Dawa ya AMDRO ndiyo itumikayo kuangamiza sisimizi. Dawa hii iliyo kama sukari, hunyunyizwa kuzunguka shina la mti lenye sisimizi. Kiasi cha gramu 4 za dawa hii kwa mti, inatosha kuthibiti sisimizi. Dawa inarudiwa tena endapo dalili za sisimizi kujitokeza tena zitaonekana.

Jinsi ilivyotengenezwa dawa hii, sisimizi huonekana kuipenda sana; maana, mara tu baada ya kunyunyiza, huibeba na kumpelekea malkia wao, ambaye baada ya kula hufa akifuatiliwa na ukoo mzima wa sisimizi. Kwa hiyo baada ya siku mbili tatu hivi, sisimizi wote watakuwa wamekufa, hivyo kutoa nafasi kwa Majimoto kuweza kutawala eneo lote.



Sangala hawadhuriki na dawa hii ya Amdro, badala yake, utafiti unaendelea kufanyika ili kupata dawa ya kuwathibiti sangala. Hata hivyo, grisi ya miti na wakati mwingine oili chafu, hutumika kuzungushia kwenye mashina ya miti iliyoshambuliwa na sangala ili kuwadhibiti wasipande juu. Matumizi ya ile kamba ya kuhamishia Majimoto kama daraja la juu