KURASA

Thursday, May 6, 2010

KUPUNGUZIA MATAWI MITI JAMII YA MICHUNGWA

Bw Elyc ameniambia kwamba nimwelekeze jinsi ya kupunguzia matawi ya miche yake jamii ya michungwa nami namwomba azingatie haya

1- Kipindi kizuri cha kupunguzia matawi miti yako ni kipindi cha jua na wakati huu mimea isiwe na matunda wala maua

2- Matawi yanakatwa sehemu zile zenye magonjwa , zilizokufa, matawi yaliyofungamana au katikati ya mti ili kuufanya utawanyike vizuri

3- Pia punguza matawi yaliyopo kwenye njia pamoja na matawi yanayoelekea kuelemewa kutokana na kuwa na matawi madogo mengi zaidi

4- Tumia zana maalum za kupunguzia matawi kama mikasi na misumeno maalum inayopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo, uwe mwanagalifu vifaa hivi visikuumize maana vina ncha kali na tumia vifaa vya kujikinga kama mabuti maalum ya mashambani na glovu za mikononi

5- Milimao inabidi ipunguziwe matawi kila Mwaka au kila baada ya miaka miwili, kila tawi lipunguze kiasi cha robo au theluthi ya juu, kwa kufanya hivi mlimao hautakuwa mkubwa sana na kusababisha usumbufu wakati wa kuvuna

MCHUNGWA AINA YA JAFFER



6- ZINGATIA
(a)Panda miche yako kwa nafasi zinazokubalika kitaalam laa sivyo mime yako ikibanana itakuwa inakimbilia juu, kwa michungwa aina ya jaffer panda mita 8 kwa 8 (8m * 8m) na kwa aina ya Valencia panda (5m * 8m)

(b)kumbuka kupunguzia miche yako jamii ya michungwa kuna maanisha kupunguza mazao kwa sababu mti mkubwa ndio unazaa matunda mengi, usiupunguze matawi mti wako kama huna sababu ya kufanya hivyo

(c)Vifaa vinavyotumika kwa ajili ya kupunguzia matawi viwe na makali ya kutosha kuepusha kupasua na kuchana matawi, unaweza kuomba afisa ugani wa eneo lako ili akuonyeshe kwa vitendo

(d)Kama utachanganya michungwa ya jaffer na Valencia uipande kwa uwiano wa 2:5 yaani katika kila michungwa 7 miwili iwe jaffer na mitano iwe Valencia, hii ni kwa sababu michungwa aina ya jaffer ni mikubwa na inazaa sana na inawahi kuiva lakini haihimili sana ukame, michungwa ya Valencia ina uzazi wa wastani na inahimili ukame kwa hiyo ukiichanganya shambani utapata mavuno ya mwanzo kwenye jaffer na mavuno ya kati yatakuwa na mchanganyiko wa jaffer za mwisho na Valencia za mwanzo na kisha mwisho utapata mavuno ya Valencia tu. Kwa hiyo utakuwa na machungwa katika msimu wote wa mavuno na ii itazuia machungwa kuiva yote pamoja na kuharibikia shambani