KURASA

Saturday, December 26, 2009

MAGONJWA MAKUU YA KAHAWA

Magonjwa makuu ya kahawa ni haya yafuatayo
- Chule buni (CBD)
- Kutu ya majani (Coffee leaf rust)
- Mnyauko fuzari (Fusarium)
Leo nitaongelea ugonjwa wa chule buni

CHULE BUNI (CBD- Coffee Berry Disease)
Chule Buni (CBD) ni ugonjwa wa matunda ya kahawa ambao umeenea sehemu nyingi nchini hasa zile za miinuko ya juu. Ugonjwa huu husababishwa na fangas wajulikanao kama colletotrichum kahawae. Ushambuliaji huwa ni mkubwa zaidi wakati wa mvua za masika kwani wakati huu hali ya unyevu unyevu kwenye hewa ni mkubwa na hali ya hewa ni ya baridi.

MFANO WA TUNDA LILISHAMBULIWA


MADHARA
Ugonjwa huu ni mbaya sana na huenea kwa kasi. Mbuni ulioshambuliwa haufi bali mkulima anaweza kupoteza mpaka asilimia 90 ya mavuno kwa mwaka kama hatazingatia namna bora ya kuuzuia.

Ugonjwa huu hushambulia mibuni katika hatua tatu muhimu nazo ni:
• Maua yanapochanua.
• Punje zikiwa changa na laini.
• Punje zinazoiva.

Madhara makubwa hutokea wakati punje zikiwa changa na laini.
Mara nyingi mibuni iliyoshambuliwa na Chule Buni matunda yake huwa na vidonda vyeusi na vilivyobonyea na hudondoka na mengine hubakia kwenye mibuni. Yale matunda yanayobakia yanakauka na kuwa chanzo cha uambukizaji kwenye mavuno ya msimu unaofuata. Picha ya mbuni ulioshambuliwa na Chule Buni

JINSI YA KUZUIA
Ili mkulima aweze kudhibiti vizuri ugonjwa huu anashauriwa:
• Kupunguza matawi yasiyotakiwa ili sumu iweze kupenya vizuri
na kufikia matunda yote.
• Kutumia sumu sahihi zilizopendekezwa kutumika kwenye kahawa.
• Kutumia kiasi na kipimo sahihi kilichopendekezwa.
• Kunyunyizia sumu wakati sahihi yaani:

1. Kabla ya ugonjwa haujatokeza.
2. Unyunyuziaji dawa uanze wiki tatu kabla ya mvua za vuli kuanza (Oktoba - Novemba) na kurudiwa tena mwezi mmoja baadae (Disemba).
3. Unyunyiziaji unaofuata ufanyike tena wiki tatu kabla ya mvua za masika (Machi) na kurudiwa kila mwezi hadi matunda yakomae (Julai)
• Aelekeze dawa kwenye matunda.



Mkulima anashauriwa kunyunyizia sumu mojawapo ya hizi zifuatazo:
1. Jamii ya mrututu - hasa zile nyekundu na za bluu zilizopendekezwa kudhibiti Chule buni. Mfano: Nordox, Cobox, Funguran-OH.
2. Jamii isiyo ya mrututu - hizi mara nyingi ni zile za maji maji zilizopendekezwa kutumika kwenye kahawa mfano: Bravo, Daconil na Dyrene.

FAIDA YA KUDHIBITI
Mkulima akidhibiti vizuri Chule Buni anapata faida zifuatazo:
1. Atakuwa amepunguza uwezekano wa kuendelea kuongeza kasi ya huu ugonjwa mwaka hadi mwaka.
2. Atakuwa ameongeza wingi na ubora wa kahawa.
3. Atakuwa amejiongezea kipato chake na kuwa na maisha bora zaidi.
4. Atakuwa ameongeza pato la taifa kwa ujumla.

MAMBO YA KUZINGATIA
• Mwisho wa msimu hakikisha unaondoa matunda yote haswa yale yaliyoshambuliwa na chule buni.
• Tambua wakati sahihi wa kuzuia huu ugonjwa.
• Nunua sumu sahihi zilizopendekezwa.
• Hakikisha matunda yote yanapata sumu vizuri.
• Epuka ununuzi holela wa sumu kwani unaweza kununua hata zile zilizokwisha muda wake.
• Mara upatapo tatizo onana na mtaalamu wa kilimo/afisa ugani aliyekaribu nawe.