KURASA

Tuesday, September 18, 2012

SABABU ZA KASUKU/CHIRIKU KUJINYOFOA MANYOYA

SABABU

1 - Lishe duni, upweke na kukosa matunzo ya jumla

2 - Kama atakuwa anatafuna kucha zako unapomshika

3 - Viroboto au utitiri

4- Maambukizi ya bakteria au fangasi

5 - Banda dogo sana

6 - Lishe yenye vitamini A kwa wingi zaidi

NINI KIFANYIKE
1 - Hakikisha ndege wako anapata mlo kamili, unaweza kununua chakula kwenye maduka au ukachanganya mwenyewe baada ya kupata utaalam, apate matunzo yote muhimu na pia asiwe mwenyewe ni vizuri ukafuga dume na jike.

2 - Kama unatabia ya kumshika ndege wako hakikisha unavaa kitu cha kukinga asiweze kula kucha zako kama vile gloves

3 - Viroboto na uttiiri vidhibitiwe kwa kutumia dawa maalum kama vile akheri powder

4 - Maambukizi ya bakteria na fangasi yadhibitiwe mara moja kwa kutumia dawa kama ancobal

5 - Hakikisha ndege wako anaishi kwenye banda lenye ukubwa wa kutosha

6 - Punguza vyakula vyenye vitamini A kwa wingi kama vile karoti na mapapai

Tuesday, September 11, 2012

KILIMO BORA CHA MIHOGO


Zao la muhogo ni  muhimu sana kwa Tanzania zaidi kwa wakulima wadogo wenye kipato cha chini. Wakulima wengi huchanganya zao la muhogo na mazao mengine kama vile kunde, mbaazi, njugumawe, n.k. Umuhimu wa zao hili ni kutupatia cahakula na wakati mwingine kwa biashara. Kwa kanda ya kusini muhogo ni chakula kikuu ambacho kinachukua asilimia 75 ya chakula kwa maeneo yote ya mikoa ya pwani

Muhogo hustawi vizuri katika maeneo yaliyopo kwenye maeneo ya mita 0 – 1500 kutoka usawa wa bahari. Vile vile muhogo hustawi vizuri kwenye maeneo yanayopata mvua ya wastani wa mm 750  - mm1200 kwa mwaka. Muhogo hustawi vizuri kwenye ardhi ya kichanga. Vili vile zao la muhogo ni maarufu sana kwa uvumilivu wa hali ya ukame.

TEKNOLOJIA ZILIZOPO
  1. Mbegu bora za muhogo
Mpaka sasa hivi kuna aina mbili za mbegu bora ambazo zimathibitishwa kwa wakulima. Mbegu hizi huvumilia magonjwa, (batobato na matekenya), pia huzaa sana ukilinganisha na mbegu za kienyeji.
    • Naliendele
                 Huzaa tani 19 kwa hekta moja, na inaweza kuvunwa kuanzia miezi 9 toka ipandwe.


    • Kiroba
Huzaa tani 25 – 30  kwa hekta moja, na inaweza kuvunwa kuanzia miezi 9 toka ipandwe.

  1. Mbinu bora za kilimo cha muhogo
    • Uandaaji wa shamba
Shamba liandaliwe kabla ya msimu wa kuanza. Uandaaji wa shamba bora hufuata hatua zifuatazo:
- Kufyeka shamba
- Kung’a na kuchoma visiki
- Kulima na kutengeneza matuta
·         Uchaguzi wa mbegu bora za kupanda
Mbegu zinatakiwa zisiwe na magojwa yeyote, pia chagua mashina ambayo yamelomaa vizuri.
·         Upanadaji
Kuna njia tatu za upandaji wa muhogo:
-          Kulaza ardhini (Horizontal)
-          Kusimamisha wima (Vertcal)
-          Kuinamisha ( Inclined/Slunted)

Urefu wa kipande cha shina cha kupanda:
 Inashauriwa urefu uwe sm 30; lakini urefu wa kipande cha kupanda unategemea sana idadi ya macho yaliyopo kwenye hicho kipande, inashauriwa kipande kiwe na macho (4 – 6).

Nafasi ya kupanda:
Kwa upandaji wa shamba muhogo tupu, shina hadi shina ni mita 1 na mstari hadi mstari ni mita 1.Kwa shamba la mchanganyiko na mazao mengine, inategemeana na zao linalochanganywa; mstari hadi mstari ni mita 2 – mita 4 na shina hadi shina ni mita 1.


·         Palizi:
-          Palizi ya kwanza ifanyike mapema (mwezi 1) baada ya kupanda ili kuepukana na magugu yanayochipua haraka baada ya mvua kunyesha. Ndani ya miezi mine ya mwanzo mihogo haitakiwi kuwa na magugu ili kuepuka ushindni wa mahitaji muhimu (mwanga, mbolea, maji, n.k) kati ya muhugo na magugu.
-          Palizi hufanyika kwa kutumi jebe la mkono au dawa ya kuuwa magugu.
-          Wakati mwingine udhibiti wa magugu kufanyika kwa kutumia majani kwa kutandazwa juu ya udongo.
-          Plaizi hufanyika mara 2 – 3 hadi muhugo kukomaa.

·         Uvunaji:
Mihogo inaweza kuanza kuvunwa baada ya miezi 9 – 12 tangu kupandwa. Inashauriwa kuvuna katika katika kipindi cha jua; kwani wakati wa mvua kiwango cha wanga kwenye muhogo hupungua.

·         Usindikaji bora
Usindikaji bora wa muhogo unafanyika kwa sababu kuu mbili:
-          Kurahisisha/kuharakisha ukaushaji
-          Kuondoa sumu (cyanide) ilyoko kwenye baadhi ya aina za mihogo
-          Kuongeza ubora wa unga utokanao muhogo wenyewe.

Njia bora za usindikaji
-          Kwa kutumia mashine aina ya Grater
Hii hutoa chembechembe laini za muhogo, ambazo baadae hukamuliwa kwa kutumia kifaa kingine kiitwacho “presser” ili kuondo sumu iliyoko kwenye muhogo. Mashine hii hutumika hususani kwa muhogo mchungu.
-          Kwa kutumia mashine aina ya chipper
-          Mashine hii hutoa vipande vidogo vidogo (chips). Mashine hii hutumika hasa hasa kwa ajili ya mihogo mitamu/baridi.

Matumizi ya Muhogo
-          Muhogo unaweza kupikwa wenyewe kama chakula au kutengeneza unga
-          Unga wa muhogo unaweza kutengeneza vitu vyotekama vinavyotengenezwa na unga wa ngano kama vile biskuti, chapatti, maandazi, chichili, keki n.k.
-          Pia muhogo huweza kutumika viwandani kutengeneza bidhaa nyingine kama vile wanga.

  
iii         MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU
·         Magonjwa
Kuna magonjwa mawili ambayo ni muhimu sana na yanapunguza uzalishaji wa zao la muhogo.
a) Ugonjwa wa Matekenya au Ugonjwa wa michirizi ya kahawia
      katika    muhogo
  Ugonjwa huu ni maarufu kwenye sehemu zenye miinuko iliyo na urefu  chini ya mita 300 na unapatikana kidogo sana kwenye miinuko ya mita 500 na kuendelea ambako uenezaji wake wa kawaida hautokei kabisa.

            Visababishi:
            Matokeo ya uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba ugonjwa huu ulienezwa na mdudu mweuupe au inzi mweupe (whitefly) mwenye mabawa madogo.

Dalili za Ugonjwa
Sehemui zote za muhogo zinaweza kuonyesha dalili za uambukizo wa ugonjwa huu lakini ni vipengele gani vya ugonjwa na ni kwa kiwango gani hutegemea hali ya mzingira, hatua ya kukua kwa mmea kwa kulinganisha.

-          Kwenye majani
Dalili ya kwanza: Chlorosis rangi ya njani hutokea kwanza pembezoni mwa vena ndogo baadae huathtiri vena ndogo zaidi na inaweza kuwa doa (chlorosis) la rangi ya njano.
Dalili ya pili: Rangi ya njano ambayo haihusishwi vizuri na vena isipokuwa katika mbaka ya mviringo kati ya vena kuu kwenye hatua za mwisho za ugonjwa sehemu kubwa ya lamin inaweza isiathirike, majni yenye ugonjwa hubaki yameshikilia kwenye mmea kwa muda wa wiki kadhaa.

-          Kwenye shina
Huonekana kwenye tisu ya shina changa la kijani, jeraha la zambarau au kahawia linweza kuoneakan nje na kuingia ndani hadi kwenye gamba baaada ya kubandua gome la nje. Pia jeraha la nekrotiki kwenye kovu la shina hutokea baada ya majni kudondoka kutokana na umri wa mmea. Tawi/shina hufa kuanzia kwenye nch kuelekea chini na kusababisha kufa kwa mmea wote.

-          Kwenye mizizi
Kwa kawaida hutokea baada ya dalili za majani na wakati wa kipindi kati ya uambukizo na kufa, amabpo kifo cha mizizi hutokea kuanzia miezi 5 toka kupandwa. Dalili za mizizi zinabadilika nje ya mizizi na zinaweza kuwa kama kizuizimwanga au shimo au kufa kwenye gome.

Tishu inayo zunguka mshins ina doa la rangi ya kahawia au nyeusi. Wakati mwingine mizizi huonekana kuwa yenye afya kwa nje bila kuwa na matatizo yaliyowazi au bila kupungua ukubwa, lakini ikikatwa huonekana kufainakufa au rangi ya njano.

Uambukizaji na ueneaji

Ugonjwa wa CBSD unaambukizwa kwa njia ya vipandikizi vinavyotokea kwenye mimea iliyoathiriwa vinavyosababisha mmea kuonesha kwenye majani dalili za ugonjwa.
Kwa kuwa muhogo kwa kawaida huzalishwa kwa njia ya vipandikizi ugonjwa huu huingizwa kwenye sehemu mpya zilizopandwa kwa kutumia vipandikizi vilivyoambukizwa.
Kwa aina zinazovumilia sana kwenye hali za mabondeni, dalili mbaya sana hutokea wakati ugonjwa ukigundulika  katika hatua za mwanzo.
Uchunguzi umeonesha kwamba Bemisia afer ni mdudu/kisababishi ambacho ndicho kinachohusiana na maendeleo ya hivi karibuni kuhusu uhamishaji wa visababishi kama “ipomovirus”. Mara nyingine inaonesha nzi weupe (White flies) na kutokana na hali hiyo bado uchunguzi unaendelea zaidi.

Udhibiti/Kuzuia
ü  Njia ya msingi ya kuzuia/kudhibiti ugonjwa wa CBSD ni kuchagua mbegu kutoka kwenye mimea isiyo na dalili ya ugonjwa.
ü  Ubora wa mashina unahitaji kutunzwa kwa kuendelea kuchagua na kuangamiza ile iliyoambukizwa ambayo inaonekana wakati wa kuchipua.
ü  Hakikisha kuwa unapanda mbegu bora za mhogo ambazo zinastahimili uambukizo wa magonjwa.
ü  Hakikisha kuwa wakati wa uvunaji uonapo hali ya kuoza kwa mizizi ya mhogo ichome moto ili kutokomeza ugonjwa huo.
ü  Kuelewa dalili za ugonjwa wa CBSD kwa ajili ya kuchukua tahadhari ya kutokomeza ugonjwa huu.
ü  Hakikisha kuwa unaendelea kutunza mbegu bora zinazoonekana kuvumilia magonjwa sana.
ü  Hakikisha kuwa shamba la mhogo linakuwa safi kwa ajili ya kupunguza visababishi vya ugonjwa wa CBSD
      


b) Ugonjwa wa batobato au ukoma wa majani
      Ni ugonjwa ambao ulienezwa kwamara ya kwanza hapa Tanzani mwaka 1894, na baadae uliripotiwa katika nchi nyingine nyingi za Afrika Mashriki, Afrika Magharibi na Afrika ya Kati na sasa unafahamika kuwa upo maeneo yote yanayolimwa muhogo Afrika.

Katika viwango vya kuwepo kwa ugonjwa wa CMD na katika uwingi wa hasara zinazopatikana kutokana na CMD ni kati ya 15% – 20%. Hii ni sawa na tani milioni 15 – 18 zikilinganishwa na makadirio ya shirika la kilimo na chakula  duniani ya tani milioni 85 ya mwaka 1997.

Visababishi
Tangu ugonjwa wa CMD ulipoenezwa kwa mara ya kwanza, visababishi vilichukuliwa  kuwa ni virusi kwa sababu ya kukosekana kisababishi kingine. Kwa hiyo kutokana na kuwa mtazamo huu unalingana na matokeo ya uchunguzi wa awali inaonesha kwamba ugonjwa huu huenezwa na nzi mweupe (white fly).
Pia uchunguzi wa mara kwa mara umesababisha utambuzi wa virusi vya aina mbalimbali na tofauti kama ifuatavyo:
·         Ugonjwa wa batobato unaosababishwa na virusi vya Africa cassava mosaic virus
·        Ugonjwa wa batobato unaosababishwa na virusi vya Afrika mashariki (East Africa cassava mosaic virus)
·         Ugonjwa wa batobato unaosababishwa na virusi vya India (Indian cassava mosaic virus)


                  Dalili za ugonjwa wa batobato (Cassava Mosaic Disease-CMD)
                  
                  Dalili hutokea kwenye jani lenye uwaraza wa michirizi ambazo huathiri         
                   Sehemu zisizokunjamana za kutolea hewa na hufahamika katika hatua za    
                  Awali za ukuaji wa jani.
                  Sehemu za kloritiki hushindwa kutanuka hadi mwisho, hivyo mvutano unaji-
                  tokeza kutokana na ukuaji usiolingana na jani au majani madogo yaliyoharibika.
                
                  Majani yaliyoathirika sana hupungua ukubwa wa umbo, na hujikunja na kujitenga kwa
                  Sehemu zenye rangi ya njano na zenye rangi ya kawaida ya kijani.
                  Mmea hudumaa na majani machanga hupatwa na uvimbe.
                  Kloritiki ya jani inaweza kuwa ya rangi ya manjano nyepesi au rangi inayokaribia nyeupe
                  yenye kijani kidogo au kupauka kuliko ilivyo kawaida.

                 Uambukizaji na uenezaji
                  Ukoma wa mhogo huambukizwa kwenye vipandikizi vya shina ambavyo kwa kawaida
                  hutumika kuzalishia mmea.
                  Pia huenezwa na inzi mweupe (white fly) aitwae Bemisia tabaci G. Aina mbili za inzi au
                  Mbu hao Bemisia (Preisner Hhosny na Aleorodius disperses R) pia huambukiza mihogo
                  katika nchi za Afrika na India
                  Usambazaji wa vipandikizi unaweza kusababisha kuenea kwa ugonjwa wa CMD katika
                  Maeneo mapya.



                
 UHIBITI NA KUZUIA
                  -Hatua ya msingi ya kuzuia ugonjwa wa CMD ni kwa kuchagua vipandikizi kutoka kwa
                   Mmea ambao hauna uambukizo wowote.
                  -Ubora wa mashina unahitajika kwa kuendelea kuchagua na kuangamiza kwa kung’oa ile
                   Mihogo iliyoambukizwa ambayo inaonekana wakati wa kuchipua
                  -Hakikisha kuwa wakati wa kuvuna mihogo kwa ile iliyoathirika na ugonjwa wa CMD
                   inaangamizwa kwa kuchomwa moto.
                  -Hakikisha kuwa unatunza shamba na kuwa safi ili kupunguza wadudu waenezao CMD.
                  -Hakikisha una elimu ya kutosha juu ya dalili za ugonjwa wa CMD>

·         WADUDU NA WANYAMA WAHARIBIFU
-          Cassava Mealy Bug (CMB)

Wadudu hawa hushambulia kwenye ncha za mashina/matawi kwenye majani machanga. Athari zake ni kwamba majani ynadumaa na kujikusanya pamoja, hivyo basi kupunguza ukuaji wa mmea kwa ujumla. Vile vile urefu kati ya pingili na pingili huwa fupi sana.

-          Cassava Green Mites (CGM)

Wadudu hawa hushambulia majani mapya sehemu za chini. Madhara yake sio makubwa.

-          White Scales


Hawa ni weupe na hujishika kwenye shina na kufyonza maji kutoka kwenye mti wa muhogo. Vili vile wadudu hawa madhara yake sio muhimu.

-          Mchwa
Hawa hutafuna/hula mashina ya muhogo hasa wakati wa jua kali/kiangazi.
-          Wanyama waharibifu
Hawa hushambulia muhogo ukiwa shambani kwa kuula, kama vile nguruwe, panya, wezi, n.k

Udhibiti/Kuzuia
Kwa upande wa wadudu wanweza kudhibitiwa kwa njia zifuatazo:
ü  Kutumia dawa za kuulia wadudu
ü  Kutumia wadudu marafiki wa wakulima
      Kwa upande wa wanyama ni kuweka walinzi.








Friday, September 7, 2012

KILIMO BORA CHA KARANGA

Karanga ni mojawapo ya mazao yanayotoa mafuta. Katika Tanzania zao hili hustawi zaid katika mikoa ya Kusini Mashariki, Dodoma na Morogoro. Pamoja na kutoa mafuta vile vile zao hutumika kwa njia nyingine mbali mbali, nazo ni pamoja na:

1. Chakula cha wanyama (Mashudu na majani)
2. Kurutubisha ardhi
3. Chakula cha binadamu (Confectionary)

Kwa ujumla zao hili hutumika na wakulima kama zao la biashara.



HALI YA HEWA
Karanga hustawi vizuri katika maeneo yaliyopo kwenye miinuko chini ya mita 1500, toka usawa wa bahari katika Tanzania, na hustawi zaidi katika maeneo ambayo yanapata mvua za wastani wa mm 750 hadi mm 1200 kwa mwaka.
Vile vile karanga hustawi vizuri kwenye udongo wa kichanga, inashauriwa kutopanda karanga kwenye udongo mzito (mfinyanzi) hii ni kutokana na sababu kwamba, karanga hazistawi kwenye sehemu zinazo simama maji, na udongo mzito huleta hasara wakati wa uvunaji.

AINA ZA KARANGA
Kuna aina kuu tano bora za karanga ambazo zimetolewa kwa wakulima hapa nchini.

a. Red Mwitunde
Ilitolewa kwa wakulima miaka ya 1950.
Mbegu za muda mrefu (Virginia Spreading bunches).
Huchukua muda wa siku 120 -140 toka kupanda hadi kukomaa. Ina uwezo wa kutoa kilo 1000 kwa hekta. Mbegu zake ni kubwa na zina rangi nyekundu.

b. Nyota
Ilitolewa mwaka 1983.
Mbegu ya muda mfupi ( Spanish Errect Banch).
Huchukua siku 90-100 tangu kupanda hadi kukomaa. Ina uwezo wa kuzaa wastani wa kilo 1500 kwa hekta. Mbegu zake ni ndogo, na zina rangi ya udongo (Tan).
Aina hii ya mbegu zina tabia ya kuanza kuota tena shambani mara tu zikiisha komaa, hivyo ni muhimu kuzivuna mapema zikisha komaa.

c. Johari:
Ilitolewa mwaka 1985.
Mbegu ya muda wa kati (Virginia Spreading Bunches).
Huchukua siku 110 - 120 toka kupanga kuvuna. Mbegu zake ni kubwa na zina rangi ya udongo (Tan). Ina uwezo wa kutoa wastani wa kilo 1000 kwa hekta moja.

d. Pendo: .
Ilitolewa mwaka 1998.
Mbegu ya muda mfupi ( Spanish Errect Banch). Huchukua siku 90-100 tangu kupanda hadi kukomaa. Ina uwezo wa kuzaa wastani wa kilo 1500 kwa hekta. Maganda yake ni laini na mbegu zake ni kubwa, na zina rangi ya udongo (Tan). Kama Nyota, aina hii ya mbegu ina tabia ya kuanza kuota tena shambani mara tu zikisha komaa, hivyo ni muhimu kuzivuna mapema zikisha komaa.

e. Sawia:
Ilitolewa mwaka 1998.
Mbegu ya muda wa kati (Virginia Spreading Bunches).
Huchukua siku 110 - 120 toka kupanga kuvuna. Mbegu zake ni kubwa na zina rangi ya udongo (Tan). Ina uwezo wa kutoa wastani wa kilo 1000 kwa hekta moja.

Pamoja na mbegu zilizotajwa, kuna aina nyingine nyingi za kienyeji (local varieties) zinazotumiwa na wakulima katika sehemu mbali mbali.

UTAYARISHAJI WA SHAMBA
Shamba litayarishwe vizuri kuwezesha udongo kupenyesha maji na mizizi kirahisi. Karanga hupandwa kwenye matuta au sensa (shamba tambarare).

UTAYARISHAJI WA MBEGU
Karanga ambazo zinakusudiwa kwa mbegu zitunzwe na maganda yake bila kubanguliwa. Zibanguliwe karibu na msimu wa kupanda na kuchaguliwa. Baada ya kuchaguliwa zitiwe dawa, aina ya Fernasan D, Katika uwiano wa gramu 28 za dawa kwa kila kilo 10 za mbegu safi.

WAKATI WA UPANDAJI
Uamuzi wa kuchagua wakati mzuri wa kupanda niule utakaoliwezesha zao hilo kukomaa wakati wa mvua za mwisho. Kuchelewa kupanda, hupunguza mavuno. Ni muhimu kuchagua aina ya mbegu ambazo uvunaji wake unafanana na mazingiza ya eneo hilo kihali ya hewa.
Kwa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, karanga za muda wa kati na mrefu (Johari, Red Mwitunde) zipandwe kuanzia katikati, hadi mwishoni mwa mwezi Desemba. Karanga za muda mfupi (Spanish na Valencia) zipandwe kuanzia mwishoni mwa mwezi Desemba hadi katikati ya mwezi Januari.
Kwa mikoa ya Tanga, Morogoro na sehemu za mkoa wa Dodoma, karanga zipandwe mapema mwanzo wa mvua ndefu. (Februari/March).

NAFASI KATI YA MIMEA
Inashauriwa kupanda karanga katika mistari. Nafasi kati ya mistari ni sentimita 50, na kati ya mimea ni sentimita 15, kwa karanga zinazotambaa (Virginia Spreading types). Kama karanga zinapandwa kwenye matuta ya sentimita 90, zipandwe mistari miwili, kila tuta. Kwa nafasi hii kiasi cha kil 60-75 za mbegu hutumika kwa hekta moja.

Kwa karanga zilizopo kwenye kundi la Spanish/Valencia (zisizotambaa), nafasi kati ya mistari ni sentimita 50, na kati ya mimea ni sentimita 10. Endapo karanga zimepandwa kwenye matuta ya sentimita 90, panda mistari miwili , inayofanya nafasi sawa na sentimita 50 kwa sentimita 10. Kiasi cha kilo 80-100 za mbegu hutumika kwa hekta moja kwa kutumia nafasi hii.Kwa ina zote za mbegu, panda mbegu moja safi, katika kila shimo.

MBOLEA
Kufuatana na majaribio yaliyofanyika imeonekana kuwa karanga hustawi vizuri chini ya viwango vidogo vya phosphorus (TSP, SSP). Vile vile katika sehemu nyingine, karanga zimefanya vizuri kwa kutumia samadi. Ubadilishaji wa mazao (Crop Rotation) husaidia kutunza rutuba, hivyo kupunguza kiasi cha mbolea kinachotumika.Karanga zinaweza kulimwa baada ya mahindi, ili kutumia masalia ya mbolea.

UPALILIAJI
Karanga zipaliliwe zikiwa changa. Shamba lililotayarishwa vizuri na kuondolewa magugu ya muda mrefu (Perrenial weeds) linaweza kupalliwa mara moja, kwa sababu karanga hukua haraka, na zinaweza kushindana na magugu. Baada ya kutoa maua, karanga zisipaliliwe, hii inaweza kuharibu 'pegs', hatimaye kupunguza mavuno.

MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU:
1. MAGONJWA

(i) Ugonjwa wa kuoza (Aflatoxin)
Katika hali ya unyevu mwingi vimelea viitwavyo Aspegilus flavus huota ndani ya maganda na kushambulia mbegu za karanga. Vimelea hivyo hutoa kemikali ambayo ni sumu.

KUZUIA
 Hakikisha kuwa karanga haziharibiwi wakati wa kuchimba.
 Hakikisha karanga zinakaushwa vizuri (Unyevu wa 10%) kabla ya kuzitunza zitumike kama mbegu
 Karanga za kupanda zitiwe dawa aina ya Fernasan-D.

(ii) Ugonjwa wa Madoa na Kutu: (Cercospora Leaf Spots and Rust)
Magonjwa haya husababisha madoa ya rangi ya kikahawia hadi meusi kwenye majani.
Vimelea vinavyosababisha magonjwa haya viko vya aina tatu:

(a) Cersospora arachidicola. Husababisha Early Leaf Spot.
(b) Phaeoisariopsis personata. Husababisha Late Leaf spot.

Ugonjwa wa Early Leaf Spot hutangulia kuonekana, lakini magonjwa yote mawili yanaweza kujitokeza shambani kuanzia wiki 3-5 baada ya karanga kupandwa.

(c) Puccinia arachidis. Husababisha ugonjwa wa Kutu.

Kuzuia:
 Kupanda mapema.
 Kuondoa maotea ya karanga wakati wa kiangazi.
 Tumia dawa aina ya Chlorothalonil (Daconil 2787)

Dawa huwekwa kiasi cha kilo l.6 katika lita 800 za maji kwa hekta moja, kila baada ya siku saba, kwa majuma machache kuanzaia maratu dalili za ugonjwa zinapoonekana.
Uchunguzi juu ya aina zinazostahimili magonjwa haya bado unaendele kufanywa kwenye kituo cha utafiti wa kilimo Naliendele.



(iii) Ugonjwa wa Rosette (Rosette virus disease)
Ugonjwa huu huambukizwa na wadudu waitwao "Mafuta" Aphids (Aphis craccivora). Mimea ambayo imeshambuliwa na ugonjwa huu hudumaa, na inakuwa na madoa ya njano.
Ugonjwa wa Rosette (Ukoma)

Kuzuia:
 Kupanda mapema
 Panda karanga zako shambani katika nafasi za karibu karibu.
 Palilia na toa maotea shambani mwako.

(iv) Ugonjwa wa maganda matupu (Empty pods or pops)
Karanga zilizoshambaliwa na ugonjwa huu, huwa lazina mbegu (maganda matupu). Ugonjwa huu husababishwa na ukosefu wa madini ya Calcium (chokaa) kwenye udongo.

Kuzuia:
Tumia Calcium katika hali ya Gypsum (Ca SO4) kwenye mimea au weka Chokaa (lime - CaO) kwenye udongo kabla ya kupanda. Ugonjwa huu uko kwenye mikoa ya kusini mwa Tanzania (Lindi, Mtwara na Ruvuma) na hushambulia sana karanga za muda mrefu kama vile Red Mwitunde.
Majaribio hapa Tanzaniia hayajathibitisha kuweka chokaa (Liming) kuwa ni jibu sahihi la kupambana na ugonjwa huu, lakini ili kupunguza, kupanda mapema ni muhimu.

2. WADUDU WAHARIBIFU

(i) Mafuta Aphids au "Mafuta" (Aphis cracivora)
Hushambulia karanga kila msimu, lakini athari yao kubwa ni kueneza ugonjwa wa Rosette. Wakati wa mvua nyingi huoshwa toka kwenye majani, hivyo hawaleti madhara.

Kuzuia:
• Kupanda mapema
• kupanda karanga karibu karibu

(ii) Groundnut hopper: Hilda patruelis
Hufyonza mizizi, "pegs", na karanga changa, hivyo husababisha majani kuwa manjano, kunyauka, na mmea kukauka ungali mchanga. Wadudu hawa hushambulia mazao mengine kama vile maharage, kunde. alizeti na korosho, hivyo kunahitajika mzunguko (rotation) mzuri wa mazao.

Kuzuia:
• Kwenye mashamba makubwa, inashauriwa kutumia dawa aina ya Aldrin au chloropyrifos, kuchanganya kwenye ardhi kabla ya kupanda.
• Kunyunyizia Dimethoate mara tu wadudu wanapoonekana.
• Kutochanganya na zao la korosho au mbaazi kwenye shamba moja na karanga.

(iii) Mchwa.
Kuna aina mbili za mchwa ambao hushambulia na kusababisha uharibifu kwenye zao la karanga.
Aina ya kwanza ni wale ambao hutoboa sehemu ya chini kwenye mzizi, au kutengeneza matundu, na hukaa kwenye mmea wa karanga wakati wote zikiwa shambani.
Aina ya pili ni wale ambao hukata matawi yanayokua au kutambaa. Uharibifu huu huonekana zaidi kwenye shamba jipya. Kuchelewa kuvuna kunaweza kusababisha kupotea kwa mazao mengi, kutokana na kuharibika kwa mizizi, na kusababisha karanga nyingi kubakia shambani wakati wa kuvuna.
Kuzuia:
Mchwa wanaweza kuzuiwa kwa kutumia dawa aina ya Alandrin 40% ya unga, kwa kiasi cha kilo 2.5 kwa hekta., Njia rahisi ni kuchanganya dawa na mbolea aina ya Phosphate (TSP au SSP) au mchanga na kumwaga shambani kabla ya kupanda karanga.

(iv) Panya:
Hushambulia sana karanga zinapoanza kuota, na wakati zinapokaribia kuvunwa.

Namna ya Kuzuia panya:
• Tumia dawa za kuua panya
• Mitego
• Kuwachimbua toka aridhini walikojificha.

(v) Ndege
Kama panya, ndege hasa kunguru hushambulia sana karanga kabla hazijaota (mara baada ya kupanda), zinapoanza kuota, zinapokaribia na wakati zimekwisha komaa.

Kuzuia
• Kutumia mitego
• Kuamia
• Kuweka (kutundika/kuning’iniza) mzoga au kunguru mzima shambani.

UBANGUAJI NA UTUNZAJI WA KARANGA
Kubangua karanga ni kazi ngumu. Mtu mmoja anaweza kubangua kiasi cha kilo 12-15 kwa siku. Karanga zilizopo kwenye kundi la Virginia hubangulika kirahisi, kuliko aina ya Spanish au Valencia. Mashine za kubangulia karanga hupatikana hapa nchini, zinarahisisha kazi, lakini tahadhari isipochukuliwa huharibu karanga.
Karanga zinazokusudiwa kutunzwa kwa muda mrefu, zitunzwe na maganda yake kwenye ghala. Ghala iwe kavu, yenye kupitisha hewa, na imara kuzuia wanyama waharibifu kama vile panya.Ubora na uwezo wa karanga kuota huanza kupotea mara baada ya kubanguliwa.

Wednesday, September 5, 2012

NAGANA - Trypanosiasis

Ugonjwa huu hushambulia karibia mifugo yote na pia binadamu, kwa binadamu ugonjwa huu hujulikana kama malale. ugonjwa huu husababishwa na vijidudu vya protozoa vijulikanavyo kana Trypanosoma evansi na kusambazwa na mbung'o au ndorobo (glossina spp) vijidudu hivi vikimuingia mnyama vinatumia kiasi kingi cha sukari kwenye mwili wa  mnyama na  kuharibu seli nyekundu za damu na kusababisha  upungufu mkubwa wa damu kwa mnyama wako.

DALILI
1-Ugonjwa huu kwa ng'ombe unaweza usiwe hatari, wakawaida au hata  kuwa sugu na kuleta madhara makubwa ikiwamo kifo
2-Joto la mnyama hupanda hadi kufikia sentigredi 39 - 41
3-Mnyama hupata tabu kuona huku akitoa machozi mengi kama anayelia
4-Uzalishaji wa maziwa hupungua ghafla kwa kiasi kikubwa
5-Mnyama hupumua kwa tabu kwa kutumia nguvu
6-Mnyama huonyesha kuchanganyikiwa akili, anaweza kutembea kwa mduara, kupiga pika kichwa kwenye mabanda au chochote na mnyama  huweza kupoteza fahamu
7-Baadhi ya wanyama wajawazito huweza kutoa mimba, hii ni kwenye ile hali ya ugonjwa sugu ambao hushambulia pole pole
8-Kuvimba kwa matezi
9-Manyoya ya ng'ombe mgongoni wakati wa asubuhi yana kuwa yanang'aa fulani jua likiwaka, ila inahitaji uonyeshwe na wataalam kwanza

NG'OMBE AINA YA N'DAMA


UCHUNGUZI
Maafisa ugani wa mifugo watachukua sampuli za damu kutoka kwenye mkia au sikio la mnyama na vijidudu kuonekana kwa darubini ya umeme mkali kabla ya damu kukauka, pia njia ya kimaabara ya GIEMSA itasaidia
kwa uchunguzi zaidi wa kimaabara wadudu wanaweza kupandikizwa kwenye sungura, panya na simbilisi/pimbi na baadae njia ya PCR, ELISA kutumika kuangalia vichochezi vya mwili

TIBA
Kwa mifugo kama ng'ombe, mbuzi, kondoo, jamii ya farasi, mbwa na paka dawa kama diminaphen, diminakel hutumika kutibu ugonjwa huu, kwa upande wa binadamu sifahamu dawa gani inatumika

KINGA
1- Kuna njia ya kitaalam ijulikanayo kama sterile male technique, ambapo madume ya mbung'o hupigwa na mionzi ya gama na kushindwa kuzalisha yanapo panda, hii husaidia sana kwa sababu majike ya mbung'o hupandwa mara moja tu katika maisha yao wakati madume haya tasa huendelea kupanda majike tofauti tofauti
2- Dawa zinazomika kutibu ugonjwa huu zinaweza kukinga wanyama kama watapigwa kila baada ya miezi mitatu na mara 4 kwa mwaka
3- Kuna jamii ya ng'ombe wanaojulikana kama N'DAMA ambao hupatikana Afrika ya magharibi, aina hii ya ng'ombe inastahimili sana ugonjwa huu

Tuesday, September 4, 2012

SOTOKA YA MBUZI - Peste des Petits Ruminants (PPR)

Ugonjwa huu husababishwa na virusi na hushambulia kondoo na mbuzi ukiwa na dalili zote kama sotoka (rinderpest) inayoshambulia wanyama kama ng'ombe, nyati, ngamia nk. kwa taarifa tu ni kwamba ugonjwa wa sotoka (rinderpest) ulitokomezwa duniani mwaka 2011 na shirika la afya duniani WHO kudhibitisha hilo. Ugonjwa wa PPR ulisambaa sana miaka ya 1980 na kuathiri sehemu kubwa ya Afrika na duniani kote na ugonjwa wa PPR huwashambulia zaidi mbuzi kuliko kondoo na kwenye ng'ombe unaweza kuukuta kwa kupima damu lakini ng'ombe hawataonyesha dalili wala kuweza kusambaza ugonjwa huu wa PPR.

Ugonjwa huu huweza kuua wanyama kwa kiwango cha mpaka asilimia 100% kutegemeana na umri wa wanyama, afya, lishe na kuchoka kutokana na kufuata malisho   umbali mrefu sana. kwa wanyama wenye umri kati ya miezi 4 - 8 hali huwa mbaya zaidi na pia wanyama wenye maradhi mengine ni rahisi kushambuliwa kutokana na kinga kuwa chini

KUSAMBAA
Ugonjwa PPR husambaa kwa njia ya kugusana na virusi vya ugonjwa huu huwa kwenye matongotongo, makamasi, mate na kinyesi cha wanyama, kwa hiyo mnyama mwingine akigusa kimoja kati ya hivi ataambukizwa ugonjwa huu

DALILI
Dalili kwa wanyama ni kama kuharisha, homa kati ya siku 5 - 8, mnyama hutoa makamasi ya kawaida na baadae kubadilika rangi na kuwa ya kahawia kuziba pua na kusababisha ugumu wakati wa kupumua, michubuko kwenye pua na midomo na pia kusababisha wanya kutoona vizuri na matongo tongo kwenye macho, mnyama kuishiwa maji mwilini na pia mimba kutoka

UCHUNGUZI
Uchunguzi wa kitaalamu kugundua ugonjwa huu utafanywa na maafisa ugani wa mifugo kwa kuukagua mwili kuona uwepo wa makamasi ya kahawia, mnyama kutoa kinyesi cha maji maji chenye harufu mbaya, pia watachunguza njia ya hewa, chakula na sehemu ya juu ya mdomo (hard palate) kwney utumbo wa mnyama huwa na mistari kama ya pundamilia, kuvimba kwa mitoki na usaha kwenye mapafu, baada ya hapo damu ya  mnyama itachukuli na kupelekwa kwenye maabara ikisafirisha kwenye hali ya ubaridi (refrigeration)

DAWA
Ugonjwa wa PPR hauna dawa ila kwa wanyama watakaoweza kuhimili dawa za kuua bakteria (antibiotics) zitasaidia kuzuia mashambulizi ya juu dhidi ya bakteria

KINGA
Chanjo ya ugonjwa huu ipo, wasiliana na maafisa ugani wa mifugo katika eneo lako chanjo ni muhimu mara moja kwa mwaka kabla ya kuanza kwa mvua za masika, tenga wanyama wapya wiki tatu kabla ya kuwachanganya na wengine, tenga wanyama wagonjwa na wazima mara ugonjwa unapoibuka, osha mabanda yako kwa dawa zakuulia virusi kama virukill au tumia dawa za madoa kama JIK kiasi cha lita kwa lita 30 za maji kisha pulizia