Uandaaji wa mbegu za mipapai imekuwa ni changamoto kwa baadhi ya watu, leo nitaongelea uaandaaji wake mpaka kupanda na kupata miche yako
Mbegu tulizotumia leo ni LADY RED ambazo hufaahamika zaidi kama Malkia FI toka nchini Taiwan na huzalishwa na kampuni inayojulikana kama KNOWN-YOU kama zinavyoonekana hapo pichani
Fungua mbegu zako na uziweke kwenye chombo kisafi kisha jaza maji kiasi, ziloweke humo kwa siku 5 na kila siku badilisha maji
Siku ya 6 zitoe na uziweke kwenye kitambaa kisafi kukwepa mashambulizi ya fangas, Funga vizuri na lowesha maji kitambaa chako na ukihifadhi sehemu salama
Zoezi hili linatakiwa kufanyika ndani ya nyumba au banda ambalo litazikinga mbegu dhidi ya jua la moja kwa moja
Siku ya 7 ukifungua utaona baadhi ya mbegu zimeanza kupasuka na tayari kwa kuanza kuota, panda mbegu zako moja moja kwenye viriba ambavyo ulishaviaandaa kabla kwa kuvijaza udongo wenye rutuba, kama utaweka mbolea hakikisha ilishaoza kabla, viriba viwekwe kwenye kivuli hasa chini ya miti
Baada ya siku kadhaa mbegu zako zitaanza kuota kama inavyoonekana pichani
Udongo unatakiwa uwe wenye rutuba na usiotumisha maji
Hakikisha unamwagia maji kila siku angalau mara moja na hasa jioni wakati hali ya joto imepungua
Baada ya wiki 2 miche itakuwa imefikia kimo cha sentimeta tano, hapa unaweza kuongeza mbole ya kukuzia kama ya kuku na pia kuondoa miche yako kwenye kivuli na kuiweka juani kama njia ya kuandaa kukabiliana na hali ya shamba (hardening off)