KURASA

Tuesday, October 7, 2008

UANDAAJI WA VIPANDIKIZI KABLA YA KUPANDA


Kabla ya kupanda mche wa mtiki inabidi uandaliwe kukabiliana na mazingira magumu hasa ukame, ili miche iweze kumea vizuri baada ya kupandwa inabdi ikatwe juu na kwenye mizizi na kubakia kama vipandikizi.


Mche unakatwa juu na chini na kubakia juu robo na robotatu kwenye mzizi, hii inasaidia kuanza kukua mara moja na hata kama mvua zitakuwa hafifu bado miche hii itahimili ukame kwa muda mrefu zaidi.


Vipandikizi pia vina sifa ya kuwa na uwezo wa kunyooka bila kupinda pinda wakati wa ukuaji, tofauti na miche ya kwenye vipakti.
Sehemu ya juu ya kipandikizi inaachwa na macho mawili tu kwa ajili ya kutoa matawi ambapo yatakapoanza kuchipua moja litakatwa na kubakia na moja ambalo litakuja kuwa mche na mti bora hapo baadae


Ukiangalia picha hapo juu, kulia kwako ni miche kabla haijakatwa kubakia vipandikizi na kushoto kwako ni fungu la vipandikizi kabla ya kukatwa. Na huyo jamaa hapo anaonekana akipanda kwenye shimo la wastani moja ya vipandikizi vyake

Tuesday, June 10, 2008

KUPUNGUZA MAJANI


Hii ni hatua muhimu sana kwa ukuaji wa miti ya mitiki, na mara nyingi hufanyika ili kupunguza upotevu wa maji toka kwenye mmea. Mara nyingi kipindi cha jua miche midogo huwa ipata tabu sana kupambana na hali ya ukame, na kama ilivyozoeleka ukanda wa pwani ambako ndio miti hii inastawi zaidi huwa na jua kali sana mpaka kufikia kiasi cha nyuzi joto za sentigredi 33 - 34.

Miti ya mitiki huwa inapoteza maji mengi sana kupitia majani yake kwa sababu ina majani mapana sana ambayo yanapoteza maji mengi sana kipindi cha jua (evaporation). Kipindi cha kupunguzia majani ni kipindi ambacho ardhi inakuwa wazi kwa sababu hatua hii hufanyika mara baada ya kupalilia miti yako

Wakati wa kupunguzia majani inabidi kuwe na umakini ili kuepuka kuvunja sehemu ya juu ya mti (kikonyo) na unapopunguzia majani ni lazima utoe jani moja kila upande. Unaweza kutumia mikono lakini ili kuepuka madhara nashauri visu vidogo vitumike kupunguza majani ya chini.



Monday, June 9, 2008

UPANDAJI

Upandaji wa mitiki huafanyika mara baada ya mvua za kwanza kuanza kwa sababu ukuaji wa miche midogo huitaji mvua za kuendelea kwa kipindi kirefu, pia mvua za kwanza huwa na nitrogen ya kutosha kusaidia ukuaji wa mimea.

Vipimo vya upandaji kati ya mche na mche ni mita 2.5 mpaka 3, kama utatumia kipimo cha mita 3 kwa 3 ekari moja (mita 70 kwa 70) itaingia miche kama 530 kwa wastani. miche ya mitiki hubananishwa wakati wa upandaji ili kuisaidia ikue kwa kunyooka kwenda juu ingawa mingine ya katikati itapunguzwa baada ya miaka 5 - 6 kuipa nafasi ile iliyobaki kama 260 iweze kunenepa zaidi.

Mashimo ya mitiki hayahitaji kuchimbwa kabla kwa sababu yanaweza kufukiwa na mvua, kwa kawaida mashimo haya yana kuwa na urefu usiozidi futi moja (urefu wa rula ya mwanafunzi) kwa hiyo siku ya upandaji wachimbaji wa mashimo ndio wawe wapimaji wa nafasi kati ya mti na mti. Wale wapandaji wahakikishe kwamba sehemu ya mzizi inakuwa chini ya ardhi na imefunikwa na udongo yote na sehemu ya shina inakuwa juu.

Miti ikishapandwa iachiwe sehemu kidogo ya kisahani kwa ajili ya kuhifadhia maji kidogo, nyasi kidogo zinaweza kuwekwa kuzunguka shina ili kuzuia unyevu kunyonywa na jua (evaporation) ingawa hii wakati mwingine inaweza kuwavutia mchwa wakashambulia mche wako.

Miche ikianza kuchipua baada ya siku chache vichipukizi zaidi ya kimoja vitachipua, hapa inatakiwa uvikate vyote na kubakiza chenya afya (viwili vitakuwa sawa)

UANDAAJI WA MICHE KABLA YA KUPANDWA

Upandaji wa mitiki hufanyika katika namna mbili, wa kwanza ni ule wa kupanda miche ikiwa mizima kutoka katika vifuko na ya pili ni kutumia miche toka kwenye kitalu ambako inashauriwa kuing'oa na kisha kukata sehemu ya mzizi na shina, ambako utabakiwa na mzizi 70% na shina 30%.

Kitaalamu miche iliyokatwa na kubaki kama vipandikizi ina sifa mbili kubwa
(a) Miche itakayoota katika vipandikizi hivi ina uwezo mkuwa wa kuhimili ukame iwapo kutakuwa na upungufu wa mvua za msimu wakati wa upandaji. Mara nyingi miche ikipandwa kwenye mvua pungufu, huua sehemu ya juu ya shina/mche na sehemu ya chini ya mzizi kama vile miti inavyopukutisha majani, na hii husaidia kuhifadhi maji ndani ya mmea. Sasa kabla hili halijatokea sisi tunakata kabisa hizo sehemu zitakazo kufa iwapo kutakuwa na mvua pungufu.

(b) Miti inayoota katika vipandikizi inaasilimia kubwa zaidi ya kukua kwa kunyooka kwenda juu, wakati miti iliyokulia kwenye vifuko ina uwezo zaidi ya kupinda kwa sababu wakati wa uotaji ikiwa midogo, miche hushindana kukua na kukimbilia mwanga wa jua. Wakati huu ndio mche huanza kupinda kufuata mwanga ili kushindana na ile iliyokua haraka. Ili kuepuka hili, kata miche yako na ianze kuchipua upya ikiwa shambani kwenye nafasi.

Vipandikizi vilivyokatwa vinauwezo wa kukaa mpaka siku 7 bila kufa hadi siku ya kupandwa shambani, kwa maana hiyo unaweza kuvisafirisha toka mkoa mmoja hadi mkoa mwingine kwenda kuvipanda. Kama utakuwa umeandaa vipandikizi vyako na mvua zikawa bado kuanza, weka udongo kwenye chombo chochote mwagia maji kidogo (yasituame) halafu chomeka vipandikizi vyako na usubiri siku ya mvua kuanza ili ukavipande

UANDAAJI WA SHAMBA

Kabla ya kupanda miche ya mitiki shamba ni lazima liwe limeandaliwa, uandaaji wa shamba ni lazima ufanyike mapema kabla ya mvua kuanza kunyesha kwa sababu upandaju huanza mara baada ya mvua za kwanza kunyesha.

Uandaaji wa shmba la mitiki ni wakawaida kama ule wa mashamba mengine, visiki vyote ni lazima ving'olewe kisha majani yote yalimwe na ikiwezekana yatiwe moto kwa umakini wa hali ya juu kuepusha madhara ya moto.

Kama ulimaji utakuwa ni wa trekta au kutumia jembe la kukokotwa na wanyama (plau) hii ni nzuri zadi kwa sababu majani yatafukiwa ardhini na kuongeza rutuba kwenye udongo. uuaji wa magugu kwa kutumia madawa kama round up wanamazingira huwa hatushauri, ingwa ni njia moja ya haraka na nafuu zaidi kuliko kulima kwa jembe lolote lile.

Kwa ukanda wa pwani mvua za masika huanza kati ya mwezi wa 3 - 4 kwa hiyo ni vizuri sana kama utaanza kuandaa shamba kwenye mwezi wa 2 (february) na mvua za vuli huanza kwenye mwezi wa 11 (November) kwa hiyo shamba liwe tayari kwenye mwezi wa 10 (October)

Ni vizuri pia ukaangalia na mwenendo wa mvua na lini zinategemewa kuanza kwa kupitia kwa wakala wa hali ya hewa hapa nchini (Tanzania Meteological Agency) kupitia tovuti yao ambayo ni
http://www.meteo.go.tz/wfo/seasonal.php

Saturday, May 24, 2008

MICHE BORA KWENYE KITALU




SPECIE tectona grandis (teak)
SEEDS SOURCE Bombani Muheza Tanga
DATE PLANTED January 2008
AGE 3 moths from germination
GERMINATION RATE 70%
USED SEEDS TREATMENT METHOD deep soaking & changing water after 12hrs for 4 days



Friday, May 23, 2008

KITALU CHA MITIKI














Ninashauri kitalu kiwe karibu na shamba na pia chanzo cha maji kiwe karibu. Kitalu cha mitiki kinaweza kuwa katika tuta lolote lile la juu au la chini, udongo unaofaa ni ule wenye rutuba na usiotuamisha maji. Tuta liwe kwenye sehemu yenye mwanga wa kutosha na kusiwe na kitu kitakachokinga mwanga wa jua, hii ni kwa sababu mbegu na miche ya mitiki inahitaji mwanga wa jua wa kutosha.




UOTESHAJI


Mbegu za mitiki zioteshwe kwa mistari zifukiwe kiasi cha kama sentimeta moja chini ya udongo, hakikisha kwamba mbegu haziwi chini sana ya udongo hii itasaidia katika uchipuaji wa mbegu zako. Nafasi kati ya msitari na msitari ni sentimeta kumi (10).




Uotaji wa mbegu huchukua muda kiasi cha siku 30 - 45, wakati wote huu kabla na baada ya kuota kitalu inabidi kimwagiwe maji ya kutosha angalau mara moja kila siku, maji yamwagiwe taratibu kwa kutumia vyombo vya kuwagilia (watering can) ili kuzuia kuzifukua mbegu zilizopo ardhini. Mara baada ya mbegu kuota ziendelee kumwagiwa maji ya kutosha.




Maara baada ya miche kufikia uefu wa sentimea 8- 10, mbolea za kukuzia zinaweza kuwekwa ili kuhahkikisha miti inakuwa na nguvu, wkati huu unaweza kupunguza kiasi cha maji ya kumwagilia ili kuzuia mbolea kuchkuliwa na maji.




UTUNZAJI


Muda wote hakikisha magugu yanang'olewa ili yasinyang'a nyane chakula na miche yako, hakikisha pia kingo za tuna zinanyanyuliwa muda wote kuzuia upotevu wa maji. Huna haja ya kutandaza nyasi juu ya tutalako kwa ajili ya kuzuia upotevu wa maji, kumbuka mbegu za mitiki zinahitaji mwanga wa kutosha na hewa ili ziweze kuchipua.






Kama utagundua kuna wadudu wanaoshambulia kitalu chako, omba ushauri kwa mabwana shamba dawa gani utumie ingawa ni nadra sana mitiki kushambuliwa na wadudu.




Kwa wale watakaouza miche hii au wanategemea kuisafirisha umbali mrefu, basi itawalazimu kuiweka kwenye vifuko, hii iatahisisha usafirishaji mpaka shambani, ingawa kitaalamu miche ya kwenye vifuko huwa inakufa mingi zaidi na huwa inapindapinda wakati wa ukuaji. Uhamishaji wa miche kwenye vifuko hufanyka wakati miche ina urefu wa sentimeta za wastani 2

Thursday, May 22, 2008

MBEGU

Mbegu za mitiki lazima zikusanywe kutoka katika miti iliyokomaa, hii itasaidia katika uotaji kwa sababu mbegu za miti hii ni ngumu kidogo kuota. Unaweza kupata mbegu kutoka kwenye mashmba makubwa ya miti au ukanunua kutoka kwa wakala wa mbegu za miti wa taifa (TTSA) ambao wana matawi yao katika kanda tofauti nchini (Morogoro, Lushoto na Iringa) http://www.ttsa.co.tz/

Mbegu zilizo bora ni zile zilizohifadhiwa mahali pakavu, kabla ya kupanda mbegu inabidi ziloekwe kwenye maji yanayo tembea kama mto kwa siku 3 (masaa 72) au unaweza kuzitia kwenye gunia na kuloweka kwenye chomba chenye maji kwa masaa 72, huku ukibadilisha maji kila baada ya masaa 8 -12. Hakikisha unapoloweka mbegu, lile gunia unalifunga na kitu kizito kama jiwe ili ziweze kuzama kabasa ndani ya maji.

Kila unapobadilisha maji utagundua kwamba maji unayomwaga yanakuwa na rangi nyekundu, hii ni kawaida kwa miti hii huwa inaacha alama ya rangi nyekundu (red dye) kama utakata matawi yake kwa mkono.

Ukisha maliza kuloweka mbegu kwa masaa yasiyopungua 72, mbegu zianikwe kwenye jua ili ziweze kukauka kabisa. Unaweza kuzianika juu ya bati ili kuharakisha ukaukaji, hakikisha unazi tandaza ili zikauke vizuri, hii inaweza kuchukua hata siku mbili kama hamna jua la kutosha. Mara baada ya kukauka mbegu zikusanywe na kuhifadhiwa mahali pakavu na pasipo na joto tayari kwenda kupandwa kwwenye kitalu.

UTANGULIZI

Watu wengi siku hizi wamekuwa wakijihusisha na upandaji miti katika mashamba binafsi, miti hii ina matumizi mbali mbali ikitumika kama mipaka, chanzo cha kuni, mbao, chakula cha mifugo, urembo n.k.

Miti ya mitiki ni moja ya miti inayotoa mbao ngumu na aghali zaidi duniani, vitu kama boti na mashua, vitako vya bunduki, fimbo za askari, milango na samani mbalimbali za majumbani hutengenezwa kutokana na miti hii.

Mti hii inasifika kwa uimara wa kutoliwa na wadudu kama mchwa na kuoza kutokana na maji kwa sababu ina hali ya mafuta mafuta. Mbao zake zina rangi nyekundu iliyokolea na kama mti litunzwa vituri kwa kupunguziwa matawi mapema, mbao zinakuwa hazina vidoda vidonda.

Kwa hapa nchni mashamba makubwa yanapatikana Kilombero, mtibwa na longuza (Lushoto) pia kuna wakulima wadogo wadogo katika mikoa ya Tanga, Morogoro na Pwani.

Kwa kawaida miti hii hustawi zaidi katika ukanda wa pwani wenye joto na mvua nyingi, hustawi katika udongo wa kitifu tifu wenye mbolea ya kutosha na usio tuamisha maji kabisa. Miti inayopandwa mabondeni inakuwa haaraka sana kuliko iliyopandwa sehemu za miinuko, ingawa miti ilipondwa kwenye miinuko inatoa mbao bora zaidi kutokana na kukua taratibu kidogo.

Uvunaji unaanza baada ya miaka 6-7 kwa kutoa miti ya kujengea ambayo hupatikana kwa kupunguza miti ya kati ili ile inayobaki iweze kukua zaidi. Mbao huanza kuvunwa baada ya miaka 12 - 15, ikifuatiwa na miaka 18. 20, 25, kumbuka uvunaji huu unafanywa kwa kupunguza nusu ya miti (kati ya mti na mti) na kuacha inayobaki iendelee kukua zaidi
.