KURASA

Sunday, March 29, 2009

MKUYU

MTI WA MKUYU



Huu ni mti unaopatikana sehemu nyingi sana duniani kuanzia ukanda wa joto mpaka nyanda za juu zenye baridi, ni mti ambao unakuwa na majani kipindi chote cha mwaka (evergreen) sehemu unazopenda kuota ni mabondeni na hasa sehemu chepechepe ingawa mara nyingine hupatikana hata sehemu ambazo si za majimaji sana.


SHINA NA MAUA/MBEGU




Mti huu unasifika sana kwa sifa ya kuhifadhi vyanzo vya maji, kama una kisima cha msimu ambacho hukauka maji kipindi cha jua kali basi panda mti huu karibu na kisima. Mti utakapo kuwa na ukubwa wa wastani kisima chako kitakuwa na maji mwaka mzima, mizizi yake ambayo hutambaa sana huifadhi maji ardhini yasichukuliwe kama mvuke wakati wa jua kali na pia kivuli cha majani yake pia husaidia kutunza maji ardhini

Mti huu umetajwa sana kwenye Biblia, Adam na Eva baada ya kula tunda la kati na kujikuta watupu walijisitiri kwa kutumia majani ya mkuyu, Zakayo wakati anataka kumuona yesu alitangulia mbele na kupanda juu ya mkuyu


MBEGU/MAUA



UPANDAJI
Ingawa ni mti mzuri sana kwa wanamazingira lakini ni mti mgumu sana kuuotesha, kuotesha kwa njia ya MBEGU ni ngumu zaidi kwa sababu mbegu zake (ambazo pia ni maua) nyingi huwa tupu ndani bila ile mbegu yenyewe, pia iliziote vizuri ni lazima ziliwe na popo ambao hupenda sana kula matunda yake na kisha ikitolewa kwa njia ya kinyesi ndio inaota vizuri zaidi (seed scarification), mwisho ni lazima ioteshwe sehemu iliyo chepechepe au imwagiliziwe sana.

Njia nyingine ni yakuotesha kwa kutumia matawi yake ambapo unakata na kuyaotesha kama vipandikizi, hii kidogo ina mafanikio lakini ni vipandikizi vichahe tu ndio vyenye uwezo wa kuota na vingi zaidi ya asilimia 90% havioti

Friday, March 27, 2009

KOMA-MANGA



Huu ni mmea unaopatikana sana sehemu za pwani kama Zanzibar, DSm, Tanga, Mombasa,Mtwara na lindi, mmea huu huzaa matunda yake ambayo huanza na ua kama kawaida na kisha tunda lenyewe. Komamanga kama tunda huwa la kijani kwa nje iliyochanganyika na kahawia, na ukilipasua ndani utakutana na mbegu nyingi zenye rangi nyekundu ambayo hutofautiana kukolea rangi na ukubwa kutokana na aina mbalimbali (specie)



MATUMIZI
Tunda lenyewe linatumika kama dawa ya kuongeza nguvu za kiume kwa wanaume, na pia zinasaidia kukomaza mbegu za uzazi kwa wanawake na wanaume. jinsi ya kutumia ni kulikata kisha unatoa mbegu zake na kuzila kama chakula.




matumizi mengine ni kama dawa ya tumbo kuharisha, pia yanasaidia kupunguza sukari mwili kwa wale wagonjwa wa kisukari (kwa kiasi kidogo). maua yake yakipondwa na kuchanganywa namji yatoa dawa ya kuoshea vidonda na kupunguza uvimbe.

Thursday, March 26, 2009

MHALINTA - Mti unaotoa povu la sabuni

MTI WENYEWE



Huu mti niliukuta mkoani Tanga wilaya ya Mkinga tarafa ya Maramba kijiji cha Muhinduro mtaa wa Majengo, ni mti unaokuwa mkubwa kama miti mingi tuliyoizoea ukiwa na majani ya wastani na unakuwa na majani muda wote wa mwaka (ever green)



MBEGU ZAKE
Ndizo hutumika kufulia nguo mbadala wa sabuni, unachotakiwa kufanya ni kukusanya mbegu kama 5 kwa ajili ya kufulia nguo moja, weka nguo yako ndani ya maji kiasi kisha chukua mbegu zako na uzipasue. Toa ile mbegu ya ndani na ubakie na maganda yake kisha tumia haya maganda kutengeneza povu ndani ya maji yako kisha fua nguo yako kama kawaida.



Wenyeji waliniambia kuwa mti huu unazaa kwa misimu miwili kwa mwaka kutokana na majira ya mvua sehemu za pwani yaani masika na vuli, na kila msimu huwa miti inazaa mbegu nyingi na za kutosha

OMBI kwa wanaoujua mti huu kwa majina mengine, jina la kiingereza na jina la kisayansi ninaomba wanifahamishe kwa kupitia blogu hii

Wednesday, February 18, 2009

MBILIMBI

MTI WA MBILIMBI (M-MBILIMBI)




Huu ni mmea unaopatikana sana sehemu za pwani kama Zanzibar, Tanga, Dar es salaam, Kibaha n.k Ni mmea ambao hauwezi kuhimili ukame wala baridi kali na unastawi zaidi kwenye mvua za kutosha na udongo usiotuamisha maji kabisa.


MATUMIZI


Miaka mingi mbilimbi zimekuwa zikijulikana kwa matumizi ya achali ndio maana sehemu nyingine mbilimbi zilitungwa jina la PICKLE FRUIT. Utengenezaji wa achali uko wa kuchanganya vitu tofauti tofauti kama nyanya, vitunguu, pilipili, ndimu, malimao, chumvi, maembe n.k ambavyo vinankuwa katika vipande vidogo vidigo, unaweka kwenye chupa na kuanika juani kwa siku kadhaa (ingawa baadhi huupika mchanganyiko huu)

Mbilimbi pia hutumika kutengenezea siki (vinegar) na mvinyo, hii mara nyingi hufanyika viwandani na sio majumbani kama ilivyo achali.

Mbilimbi pia ni dawa kwa magonjwa kama chunusi, kifua na kukohoa na mengineyo mengi. Ili kutibu kukohoa unatakiwa utafune mbilimbi kama tunda mara mbili mpaka tatu kwa siku ukichanganya na chumvi kupunguza ukali wake au unaweza kula mbilimbi zilizoiva ambazo ndio zina vitamin C zaidi ya mbichi. Majani na maua yake ni dawa ya vidonda, unaponda ponda na kufunga kwenye kidonda kwa siku kadhaa, pia yanapunguza uvimbe.

MAUA YA MBILIMBI



Mbilimbi mbichi ambazo ni kali huwa na acid ijulikanayo kama OXALIC kwa kiasi kingi hivyo huweza kutumika kungarishia vitu vilivyotengenezwa na chuma, shaba na aluminium kwa kusugulia na kisha kusafisha na maji safi

Monday, February 16, 2009

ALOE VERA - KINGA YA MALARIA


Sina uhakika na jina halisi la mme huu wengi wanauita SHUBIRI au SHUBIRI MWITU wengine huiita LITEMBWE (nafikiri ni jina la kiluga) kuna makala kadhaa zinasema shubiri ni mti kamili na wala si mmea, kama yuko ambaye anajua kwa uhakika naomba atusaidie.

Naomba mkumbuke kwamba kila ninachoandika humu ni kwamba nimehakikisha ukweli wake labda kwa kuona au kutumia mimi mwenyewe na wala sijasoma sehemu na kisha kuandika humu.

Nitaongelea kuhusu Aloe vera kama kinga ya malaria, kwa sababu mimi mwenyewe nilisha wahi kuwaandalia watu hii dawa na ikawasaidia, kwa mfano kuna ndugu yangu mmoja alikuwa anaumwa na malaria kila baada ya miezi 2 - 3. nilimpa hii dawa dozi moja tu na aliweza kukaa miezi 14 (mpaka leo hii)bila kuumwa malaria

Inasemekena kwamba mmea huu unauwezo wa kutibu magonjwa mengi kama vidonda, muwasho wa ngozi na harara, husaidia kusaga chakula, hupunguza uvimbe, hupunguza kiasi cha lehemu (cholestrol) mwilini na mengineyo


Huu ni mmea maarufu sana duniani kutokana na kuwa na uwezo wa kutibu magonjwa mengi, na pia unapatikana sehemu nyingi za dunia hasa zile ambazo hazina baridi. Vipodozi vingi vya ngozi vinachanganywa na mmea huu ili kuvipa uwezo zaidi wa kutunza ngozi


Mmea huu unatumika zaidi kama majani ingawa shina na mizizi yake nayo ni dawa pia, mmea huu huwa na umbo la kama katani/mkonge au mmea wa nanasi ila wenyewe ni mdogo kidogo na huwa laini zaidi


Majani yake yana sehemu mbili, kuna ganda la nje na maji ya ndani (jelly) ganda la nje lina kemikali za kutibu zaidi na ule utando wa ndani una virutubusho vingi sana ambavyo ni kinga za mwili


KINGA YA MALARIA
Kama unasumbuliwa na homa ya malaria mara kwa mara, chukua majani mawili yaliyo komaa, yaoshe vizuri na kata kata katika vipande vidogo.


Changanya na maji vugu vugu kisha saga kwa kutumia kisagio (blender) au twanga kwenye kinu kidogo, chuja na kisha ongeza maji hadi upate bilauri (jug) nzima, unaweza kuhifadhi dawa hii kwenye friji MATUMIZI kunywa vikombe viwili mpaka vitatu kwa kila siku kwa siku 5 - 7. Hii itakusaidia kuongeza kinga ya mwili wako maradufu na unaweza kurudia dozi hii mara baadda ya miezi 3 - 4.

Monday, December 22, 2008

MILONGE (moringa oleifera)



Hii ni miti ambayo haiwi mikubwa sana, inakuwa na maua meupe na kisha hutoa mbegu ndogo zinazokuwa kwenye magamba marefu kama kisu. miti hii hustawi zaidi ukanda wa pwani wenye mvua kiasi na joto, hustawi zaidi kwenye udongo usiotuamisha maji na inaweza kustawi kwenye udongo usio na rutuba nyingi na inahimili ukame kwa kiasi kikubwa.

MATUMIZI
Majani yake huweza kupikwa kama mboga na kuliwa, pia yanaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu bila ya kuathiri ubora wake wa virutubisho (nutritional value) majani yake yanavirutubisho vingi kuliko vyakula vingi tulivyozoea mfano


Ina vitamin A nyingi zaidi ya karoti
Ina Calcium nyingi zaidi ya Maziwa
Ina madini ya chuma zaidi ya spinach
Ina vitamin C nyingi zaidi ya Machungwa
Ina madini na pottasium zaidi ya Ndizi
ina protein nyingi zaidi ya nyama na mayai



MATUMIZI MENGINE
Maganda ya mbegu zake yanaweza kutumika kutibu maji(water treatment)unachukua maji yako ambayo unahisi si salama, unachanganya na maganda ya mbegu zilizopondwa pondwa kiasi, unayaacha kwa muda yatuame kisha unayachuja na yanakuwa salama kwa matumizi


Mbegu za milonge zinaweza kutumika kama dawa ya kupunguza sukari mwilini kwa wagonjwa wa kisukari, unachukua mbegu mbili au tatu unazipasua na kuchukua kokwa ya ndani na kutafuna mara 3 kwa siku, matumizi yanaweza kuongezeka au kuzidi kutegemeana na hali ya mgonjwa

Picha hapo chini inaonyesha mbegu za mlonge juu na kulia kwake ni baada ya kupasuliwa na kupata kokwa ya ndani (ambayo ni dawa ya kupunguza sukari mwilini), funguo imewekwa ili kujua ukubwa halisi wa mbegu


Sehemu yoyote ya mmea kama majani, magamba, mizizi, au maua yakipondwa pondwa na kupakwa kwenye sehemu yenye uvimbe ni dawa tosha ya kupunguza hali hiyo, pia dawa hii inauwezo mkubwa wa kupunguza sumu kama umeng'atwa na wadudu kama nyuki, manyigu/dondola, siafu, tandu, nge nk

Mbegu zake zinatoa mafuta (40%) yanayojulikana kama BEN OIL, ambayo hutumika kulainishia mitambo maalum kama saa za ukutani, pia mafuta haya ni dawa ya upele na harara

Monday, December 15, 2008

MAGONJWA YA SAMAKI NA TIBA

Kuna magonjwa mengi ya samaki yanayosababishwa na fangasi, bacteria, protozoa, parasites, virus na mazingira yenyewe. Hapa nitajaribu kuongelea magonjwa machache ambayo mimi ninauzoefu nayo yaani yameshanitokea na nikapambana nayo

Ichthyosporidium (WHITE SPOTS)
Huu ugonjwa kwa kifupi hujulikana kama ICHI, husababishwa na fungus ambao huingia kwa kupitia ngozi na kisha kushambulia maini na figo.




Dalili zake ni samaki kuogelea kwa kupindapinda au kivivu, tumbo kuonekana kama halina kitu (hollow) na alama nyeupe nyeupe kwenye mwili wa samaki

Tiba yake ni pottasium per manganate kwenye maji, Phenoxethol 1% kwenye chakula na Chloromycetin kwenye chakula, dawa zote zinapatikana kwenye maduka (pet shops). kwa kawaida ICHI wana miznguko miwili ya maisha, akizaliwa anaogelea na kujishikiza kwenye mwili wa samaki, kisha anashuka chini kwenda kuzaana (replitications)na kurudi kwenye mwili wa samaki tena. Kwenye hatua hii pottasium per manganate ndio inafanya kazi ya kuzuia ICHI kurudi tena kwenye mwili wa samaki


LEECHES
Ugonjwa huu husababishwa wadudu wa nje (external parasites)ambao hujishikiza kwenye mapezi na mikia ya samaki. Dalili yao ni kuwaona wakiwa wamejishikiza kwenye sehemu zilizotajwa na ndani ya ngozi, huwa na umbo la kama moyo na rangi ya kijivu/nyeupe



Kwa sababu dalili zinaonekana wazi kwa macho, mara nyingi ugonjwa huu huingia kwenye tank lako kwa njia ya konokono na majani

Matibabu ni kuwaweka samaki ndani ya maji yenye chumvi kiasi cha asilimia 2.5, baada ya dakika 15 leeches wengi watakuwa wamedondoka chini na wale watakaobaki unaweza kuwatoa kwa kutumia kibanio (forceps)
Tiba nyingine ni kwa kutumia Trichlorofon kiasi cha 0.25m/l (robo miligram kwa lita moja ya maji) majani yanaweza kuondolewa ugonjwa kwa kutumia potassium permanganate kiasi cha 5mg/l (miligram 5 kwa lita moja ya maji)

KUOZA MKIA NA MAPEZI
Huu ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria, dalili zake kubwa ni kuwa na rangi nyekundu au rangi ya udongo (hudhurungi) kama damu imevilia kwenye kona za mapezi na mkia na kisha baadae sehemu hizi hunyofoka na kubakia kibubutu.




Sababu kubwa ni kuumia kunakosababishwa na kujigonga au madume kupigana, TB pia inaweza kusababisha hali hii

Tiba yake ni kwa kutumia antibiotics kama tetracycline au chloramphenicol kiasi cha 20-30mg/l (miligramu 20-30 za dawa kwa lita moja ya maji)au mili gramu 250 (1 capsule) kwa chakula cha gramu 25

ingawa magonjwa mengi yanasababishwa na vimelea lakini mazingira nayo pia yanachangi katika kuongeza kasi ya magonjwa, ukizingatia yafuatayo unaweza kuwakinga samaki wako.
(a)Nunua samaki wako toka kwa mtu mwenye uzoefu wa kufuga na ambaye unauhakika samaki wake hawana magonjwa

(b)Samaki wapya watengwe kwa muda kwenye chombo kingine (hospital tank0 kwa siku kadhaa kabla ya kuchanganywa na wengine

(c)hakikisha samaki wako hawali zaidi ya kiwango chao na kuvimbiwa, lisha kwa kipimo sahihi

(d)Epuka kuwaweka samaki kwenye mazingira mabaya kama maji machafu, kuweka samaki wasiopatana pamoja, kuwasumbua kwa kuwashikashika na kugonga gonga tanki

(e)Samaki wagonjwa watengwe kwenye tank lingine (hospital tank)

(F)Nyavu zilizotumika kutolea samaki wagonjwa ziwekwe dawa (disinfection) zikaushwe juani na zioshwe vizuri hii ni pamoja na tank na vitu vyake

(g)hakikisha tank halina kitu chochote cha chuma (metal) na maji ya hospital tank yasiingie kwenye tank kuu

Sunday, December 7, 2008

UPANGAJI (AQUARIUM ARRANGEMENTS)

Upangaji wa tank lako ni muhimu ili kuwapa samaki mazingira mazuri kwa matokeo bora, wakati wa kupanga kuna vitu vya msingi na muhimu vya kuzingatia, na kabla ya kununua au kujenga tank lako lazima ujue ni samaki gani unataka kuweka na idadi yao. Baadhi ya samaki kama Goldfish,, Shaks, Koi n.k huwa wakubwa mpaka kufikia futi moja, kwa hiyo wanahitaji chombo kikubwa zaidi.


WATER PUMP
Hii hukaa nje na kusukuma hewa ndani kwa kupitia mawe ya hewa (air stones) ambazo lazima zikae katikati ya tank, pia kuna aina mbali mbali za urembo ambazo nazo zinaingiza hewa, hizi zinaweza kuwekwa kokote ila ni muhimu zisambae ndani ya tank.

WATER FILTER
Ni vizuri kama itawekwa upande mmoja wa tank na kusukuma maji kwa urefu kuelekea upande mwingine, hii husaidia kuweka mzunguko wa maji ambapo chini maji yanavutwa na na juu yanatolewa na pump.

SAKAFU
Sakafu ya tank lako lazima iwe na mchanganyiko wa mchanga na changarawe, ambao hutumika kwa ajili ya mimea kujishikiza. Mchanga na changarawe pia zinatumika kama filter kwa sababu zinachuja uchafu na mabaki ya chakula

MAPAMBO
Hii inajumuisha mimea, urembo na sehemu za kujificha samaki, mapambo yawe ya kutosha ili samaki wajisikie huru kwa sababu inawafanya waone kama wako kwenye mazingira yao halisi



MAJI
Kama unatumia maji ya bomba ni vizuri yawe yamekaa angalau masaa 12 baada ya kukingwa toka bombani. Hii ni kwa sababu huwa yanatiwa chlorine ili kuuyafanya yawe salama kuyanywa, hii chlorine huua samaki. Ukiyaweka wazi kwa masaa zaidi ya 12 chlorine huondoka kwa njia ya mvuke (evaporation), maji wazuri zaidi kutumia ni ya visima vya kuchimba (drilled water wells)kwa sababu yana chumvi chumvi za asili zinazosaidia kuwakinga na magonjwa

baada ya kuweka maji ya bomba kwenye tank unaakiwa uweke chumvi ya mezani kijiko kidogo kwa lita kwa lita 25 za maji, ukianzia na kumuweka samaki mmoja na kumwacha kwa saa zima huku ukimchunguza, ukimwona yuko salama unaweza kuwaweka samaki wote waliobakia

MAJANI NA MIMEA (aquatic plants)

Majani ni kitu muhimu sana katika ufugaji wa samaki, kazi ya majani ni kusafisha maji na kuweka mazingira ya uhasilia kwa samaki, kuna majani ya bandia lakinioiyanabakia kama urembo tu kwa sababu hayawezi kusafisha maji. Ili majani yakue kwa kiwango kizuri ni lazima mahitaji yafuatayo yazingatiwe


MWANGAZA
Mwanga wa kutosha unahitajika kwa ajili ya ukuaji wa majani na mimea ya majini, hii husaidia katika tengenezaji wa chakula kwa kutumia majani yake, mwanga wa tube lights ni mzuri zaidi ila usiwe mwingi sana kwa sababu utachangia ukuaji wa algae kwenye maji. kiwango cha mwanga kinachoshauriwa ni 1.5 watts kwa kila galon ya maji (1.5wpg), mfano tank la galon 20 linahitaji taa ya watts 30




MIZIZI
Mizizi ya mimea na majani inahitaji kujishikiza kwenye sakafu yenye udongo, changarawe au mchanga ili iweze kufyonza virutubisho, inashauriwa usiweke changarawe tu bali uchanganye na mchanga


VIRUTUBISHO
Ili mimea iweze kukua vizuri inahitaji virutubisho kama nitrogen, potasium, phosphorus, chuma na kadhalika, nitogen ambacho ni kirutubisho kikuu kinapatikana kwenye vinyesi vya samaki amabvyo vinatoka kama ammonia. Pia maji yenyewe na chakula cha samakikina madini haya kwa kiasi kidogo



CARBON-DIOXIDE
Hii ndio hewa inayotumiwa na mimea na inapatikana kutokana na samaki wanavyo pumua (respiration). Kwa kawaida samaki wanavuta oxygen na kutoa CO2 ambayo ndio inatumiwa na mimea, wingi wa upatikanaji wa hewa hii ya co2 inategemeana na wingi wa samaki.

Saturday, December 6, 2008

WATER FILTER AND PUMP

WATER PUMP



Hiki ni chombo muhimu sana katika ufugaji wa samaki, kazi yake kubwa ni kuingiza hewa ndani ya chombo cha samaki. Kwa kawaida aquarium huwa inafunikwa sehemu kubwa ya juu na hivyo kupunguza kiwango cha hewa inayoingia. Water pump inaongezea hewa katika style tofauti, hewa inaingia kupitia mawe ya hewa(air stones) na pia kwa kupitia urembo mbali mbali ambao unakuwa ukicheza, kuzunguka au kufunuka na kuruhusu hewa kuingia

mirija ya pump


Kwa kawaida water pump inakuwa nje na inaingiza hewa kwa kutmia mirija inayoingia ndani ya maji mpaka kwenye sakafu ya chombo, ambako huunganishwa na vitu husika kama mawe ya hewa na urembo mbalimbali, pump pia husaidia kuleta mzunguko wa maji na kujenga hali ya mazingira ya uhalisia kwa samaki kama wako mtoni au bwawani/ziwani.

WATER FILTER
Hii hfanya kazi zote kama pump ila tofauti ni kwamba yenyewe ina kazi ya ziada ya kusafisha na kuchuja uchafu kwenye maji

Kwa filter ndogo huwa zinazama ndani ya maji (submeged) kwa sababu huwa zinapoozwa joto na maji hayo hayo,Sehemu ya chini ya filter huvuta maji na hewa huvutwa kutokea juu kwa kutumia mrija mdogo unaokuwa nje ya maji na sehemu ya kati huwa inatoa mchanganyiko wa maji na hewa.

Filter kubwa hukaa nje na mipira ya kutoa maji na kuingiza maji na hewa ndio huingia kwenye maji, hizi mara nyingi huwa zinatumiaka kwa ajili ya aquarium kubwa na mabwawa au vyombo vingi kwa mara moja kwa sababu vinaweza kusafisha vyombo zaidi ya kimoja kwa wakati

Ndani ya filter kuna chujio ambalo husafishwa kwa urahisi mara linapochafuka kwa wastani wa mara moja kwa wiki na likichoka huwa lina badilishwa

Friday, December 5, 2008

GOLD FISH

Hawa wapo aina nyingi sana duniani, lakini hapa kwetu Tanzania kuna aina ambazo ni maarufu zaidi aina hizo ni Gold, Black Moor, Bubbles eye,Oranda, Telescope eye Shibunkins, Red cap n.k


RED CAP




Ni samaki wagumu kiasi wanaoweza kuhimili mazingira ya wastani, wanahitaji joto la wastani mpaka baridi kiasi, kwa mazingira ya tanzania hawahitaji heater na wala wasiwekwe sehemu amabayo watapata mwanaga wa jua moja kwa moja (direct sunlight) labda kama uko sehemu zenye baridi sana

SHUBUNKINS


Hakikisha chombo cha kufugia kina nafasi ya kutosha, gold fish mkubwa nahitaji kiasi cha lita 25 za maji peke yake ili aweze kuishi maisha mazuri. kwa kaida samaki hawa huwa wanachafua sana maji kwa sababu ya tabia yao ya kula sana wakati wote (piggy), na inamchukua muda mfupi kukitoa chakula kwa njia ya kinyesi

BLACK MOOR


Chombo cha kufugia kinatakiwa kiwe na sehemu za kujificha samaki kiasi cha 50% - 70% ili samaki wajione wako salama. Hakikisha unapunguza maji 25% kila baada ya wiki na kuweka maji mapya, na kila baada ya wiki 4 unatoa maji yote, unasafisha chombo chako, mawe, filter pamoja na urembo uliopo ndani na kuweka maji mapya 100%

TELESCOPE EYES

Gold fish huwa wanakula mara mbili kwa siku, tumia chakula maalum ambacho kinauzwa madukani, vyakula kama uduvi, dagaa na ubongo vinaweza kulishwa kama wako kwenye bwawa tu kwa sababu huchafua sana vioo na maji. Gold fish huwa wanakula chochote kile (omnivorous)ila inabidi uwe makini usije ukawalisha zaidi (overfeeding) kwa sababu wanaweza kufa

GOLD



Hakikisha chombo kina mfumo wa kusafisha maji (filter) na mfumo wa uingizaji hewa (pump)ili kujua kipimo halisi cha ukubwa wa filter na pump itabidi usome mwongozo wa mtumiaji na mtengenezaji (user manual)

BUBBLES

Sunday, November 30, 2008

SAMAKI WA UREMBO (AQUARIUM FISH)

Baada ya kuongelea kilimo cha mitiki, sasa naomba nigeukie upande mwingine wa ufugaji wa samaki wa urembo majumbani au popote.

Samaki wa urembo wako aina nyingi, wanamahitaji na tabia tofauti, tumezoea kuona wengi wakifugwa kwenye vyombo vya kioo (aquarium) na mara chache kwenye mabwawa. Mara nyingi majumbani wanakuwa kwenye aquarium na kwa wale wazalishaji (breeders) wnazalisha na kukuza kwenye mabwawa, mara chache sana wanatumika kwa ajili ya urembo kwenye mabwawa


Samaki wako aina nyingi lakini kwa hapa Tanzania waliozoeleka sana ni goldfish, koi, angels, cichlids, barbs, sharks, parots, catfish, gupies, sotas, zebra na kadhalika, na mimi nitajaribu kuwachambua ufugaji na mazingira wanayohitaji kwa baadhi ya samaki ingawa mahitaji yao hayatofautiani sana

Tuesday, October 7, 2008

UANDAAJI WA VIPANDIKIZI KABLA YA KUPANDA


Kabla ya kupanda mche wa mtiki inabidi uandaliwe kukabiliana na mazingira magumu hasa ukame, ili miche iweze kumea vizuri baada ya kupandwa inabdi ikatwe juu na kwenye mizizi na kubakia kama vipandikizi.


Mche unakatwa juu na chini na kubakia juu robo na robotatu kwenye mzizi, hii inasaidia kuanza kukua mara moja na hata kama mvua zitakuwa hafifu bado miche hii itahimili ukame kwa muda mrefu zaidi.


Vipandikizi pia vina sifa ya kuwa na uwezo wa kunyooka bila kupinda pinda wakati wa ukuaji, tofauti na miche ya kwenye vipakti.
Sehemu ya juu ya kipandikizi inaachwa na macho mawili tu kwa ajili ya kutoa matawi ambapo yatakapoanza kuchipua moja litakatwa na kubakia na moja ambalo litakuja kuwa mche na mti bora hapo baadae


Ukiangalia picha hapo juu, kulia kwako ni miche kabla haijakatwa kubakia vipandikizi na kushoto kwako ni fungu la vipandikizi kabla ya kukatwa. Na huyo jamaa hapo anaonekana akipanda kwenye shimo la wastani moja ya vipandikizi vyake

Tuesday, June 10, 2008

KUPUNGUZA MAJANI


Hii ni hatua muhimu sana kwa ukuaji wa miti ya mitiki, na mara nyingi hufanyika ili kupunguza upotevu wa maji toka kwenye mmea. Mara nyingi kipindi cha jua miche midogo huwa ipata tabu sana kupambana na hali ya ukame, na kama ilivyozoeleka ukanda wa pwani ambako ndio miti hii inastawi zaidi huwa na jua kali sana mpaka kufikia kiasi cha nyuzi joto za sentigredi 33 - 34.

Miti ya mitiki huwa inapoteza maji mengi sana kupitia majani yake kwa sababu ina majani mapana sana ambayo yanapoteza maji mengi sana kipindi cha jua (evaporation). Kipindi cha kupunguzia majani ni kipindi ambacho ardhi inakuwa wazi kwa sababu hatua hii hufanyika mara baada ya kupalilia miti yako

Wakati wa kupunguzia majani inabidi kuwe na umakini ili kuepuka kuvunja sehemu ya juu ya mti (kikonyo) na unapopunguzia majani ni lazima utoe jani moja kila upande. Unaweza kutumia mikono lakini ili kuepuka madhara nashauri visu vidogo vitumike kupunguza majani ya chini.



Monday, June 9, 2008

UPANDAJI

Upandaji wa mitiki huafanyika mara baada ya mvua za kwanza kuanza kwa sababu ukuaji wa miche midogo huitaji mvua za kuendelea kwa kipindi kirefu, pia mvua za kwanza huwa na nitrogen ya kutosha kusaidia ukuaji wa mimea.

Vipimo vya upandaji kati ya mche na mche ni mita 2.5 mpaka 3, kama utatumia kipimo cha mita 3 kwa 3 ekari moja (mita 70 kwa 70) itaingia miche kama 530 kwa wastani. miche ya mitiki hubananishwa wakati wa upandaji ili kuisaidia ikue kwa kunyooka kwenda juu ingawa mingine ya katikati itapunguzwa baada ya miaka 5 - 6 kuipa nafasi ile iliyobaki kama 260 iweze kunenepa zaidi.

Mashimo ya mitiki hayahitaji kuchimbwa kabla kwa sababu yanaweza kufukiwa na mvua, kwa kawaida mashimo haya yana kuwa na urefu usiozidi futi moja (urefu wa rula ya mwanafunzi) kwa hiyo siku ya upandaji wachimbaji wa mashimo ndio wawe wapimaji wa nafasi kati ya mti na mti. Wale wapandaji wahakikishe kwamba sehemu ya mzizi inakuwa chini ya ardhi na imefunikwa na udongo yote na sehemu ya shina inakuwa juu.

Miti ikishapandwa iachiwe sehemu kidogo ya kisahani kwa ajili ya kuhifadhia maji kidogo, nyasi kidogo zinaweza kuwekwa kuzunguka shina ili kuzuia unyevu kunyonywa na jua (evaporation) ingawa hii wakati mwingine inaweza kuwavutia mchwa wakashambulia mche wako.

Miche ikianza kuchipua baada ya siku chache vichipukizi zaidi ya kimoja vitachipua, hapa inatakiwa uvikate vyote na kubakiza chenya afya (viwili vitakuwa sawa)

UANDAAJI WA MICHE KABLA YA KUPANDWA

Upandaji wa mitiki hufanyika katika namna mbili, wa kwanza ni ule wa kupanda miche ikiwa mizima kutoka katika vifuko na ya pili ni kutumia miche toka kwenye kitalu ambako inashauriwa kuing'oa na kisha kukata sehemu ya mzizi na shina, ambako utabakiwa na mzizi 70% na shina 30%.

Kitaalamu miche iliyokatwa na kubaki kama vipandikizi ina sifa mbili kubwa
(a) Miche itakayoota katika vipandikizi hivi ina uwezo mkuwa wa kuhimili ukame iwapo kutakuwa na upungufu wa mvua za msimu wakati wa upandaji. Mara nyingi miche ikipandwa kwenye mvua pungufu, huua sehemu ya juu ya shina/mche na sehemu ya chini ya mzizi kama vile miti inavyopukutisha majani, na hii husaidia kuhifadhi maji ndani ya mmea. Sasa kabla hili halijatokea sisi tunakata kabisa hizo sehemu zitakazo kufa iwapo kutakuwa na mvua pungufu.

(b) Miti inayoota katika vipandikizi inaasilimia kubwa zaidi ya kukua kwa kunyooka kwenda juu, wakati miti iliyokulia kwenye vifuko ina uwezo zaidi ya kupinda kwa sababu wakati wa uotaji ikiwa midogo, miche hushindana kukua na kukimbilia mwanga wa jua. Wakati huu ndio mche huanza kupinda kufuata mwanga ili kushindana na ile iliyokua haraka. Ili kuepuka hili, kata miche yako na ianze kuchipua upya ikiwa shambani kwenye nafasi.

Vipandikizi vilivyokatwa vinauwezo wa kukaa mpaka siku 7 bila kufa hadi siku ya kupandwa shambani, kwa maana hiyo unaweza kuvisafirisha toka mkoa mmoja hadi mkoa mwingine kwenda kuvipanda. Kama utakuwa umeandaa vipandikizi vyako na mvua zikawa bado kuanza, weka udongo kwenye chombo chochote mwagia maji kidogo (yasituame) halafu chomeka vipandikizi vyako na usubiri siku ya mvua kuanza ili ukavipande

UANDAAJI WA SHAMBA

Kabla ya kupanda miche ya mitiki shamba ni lazima liwe limeandaliwa, uandaaji wa shamba ni lazima ufanyike mapema kabla ya mvua kuanza kunyesha kwa sababu upandaju huanza mara baada ya mvua za kwanza kunyesha.

Uandaaji wa shmba la mitiki ni wakawaida kama ule wa mashamba mengine, visiki vyote ni lazima ving'olewe kisha majani yote yalimwe na ikiwezekana yatiwe moto kwa umakini wa hali ya juu kuepusha madhara ya moto.

Kama ulimaji utakuwa ni wa trekta au kutumia jembe la kukokotwa na wanyama (plau) hii ni nzuri zadi kwa sababu majani yatafukiwa ardhini na kuongeza rutuba kwenye udongo. uuaji wa magugu kwa kutumia madawa kama round up wanamazingira huwa hatushauri, ingwa ni njia moja ya haraka na nafuu zaidi kuliko kulima kwa jembe lolote lile.

Kwa ukanda wa pwani mvua za masika huanza kati ya mwezi wa 3 - 4 kwa hiyo ni vizuri sana kama utaanza kuandaa shamba kwenye mwezi wa 2 (february) na mvua za vuli huanza kwenye mwezi wa 11 (November) kwa hiyo shamba liwe tayari kwenye mwezi wa 10 (October)

Ni vizuri pia ukaangalia na mwenendo wa mvua na lini zinategemewa kuanza kwa kupitia kwa wakala wa hali ya hewa hapa nchini (Tanzania Meteological Agency) kupitia tovuti yao ambayo ni
http://www.meteo.go.tz/wfo/seasonal.php

Saturday, May 24, 2008

MICHE BORA KWENYE KITALU




SPECIE tectona grandis (teak)
SEEDS SOURCE Bombani Muheza Tanga
DATE PLANTED January 2008
AGE 3 moths from germination
GERMINATION RATE 70%
USED SEEDS TREATMENT METHOD deep soaking & changing water after 12hrs for 4 days