KURASA

Monday, August 26, 2013

FISH CENTRE & AQUARIUM


 Samaki wa aina mbali mbali kama Gold (aina zote), koi, Salasa, Sotas, Angels, Gupies, zebra nk


 Vyakula vya aina mbali mbali kwa ajili ya samaki wako. kwa ajili ya ukuaji mzuri, kinga ya magonjwa na utoaji wa rangi


Filter na pampu za aina na ukubwa mbalimbali

Urembo na mapambo ya kuweka ndani ya vyombo vya kufugia

Vyombo vya kufugia samaki (aquarium) aina na ukumbwa tofauti tofauti kulingana na matakwa yako












 Hii ni aquarium ya kusimama, ndefu kwenda juu zaidi ya upana
 Kwa mawasiliano zaidi piga simu namba 0753-151811, 0787151811, 0715151813

Sunday, August 18, 2013

KUPUNGUZIA MATAWI KWENYE MICHE YA NYANYA

Kuna baadhi ya wasomaji wangu walipenda kufahamu umuhimu wa kupunguzia matawi kwenye zao la nyanya na pia jinsi ya kupunguzia matawi hayo.
Umuhimu wa kupunguzia matawi kwenye zao la nyanya ni kupata nyanya bora, kubwa na zenye afya, ukiacha mti uwe na matawi utatoa maua mengi sana na utaishia kupata nyanya ndogo ndogo ambazo hazina soko zuri, lakini ukipunguzia matawi nyanya zako zitakuwa kubwa na mmea wako utazaa kwa mpangilio na kwa muda mrefu

Jinsi ya kupunguzia matawi ni kwa kutofautisha maua ni yapi na matawi ni yapi kisha unaondoa matawi kwa kutumia mkono tu, usitumie kisu maana itakuwa rahisi kusambaza magonjwa toka mme mmoja hadi mwingine, mara nyini matawi hutoke kati ya shina na jani kama inavyoonekana kwenye picha hapo chini




NYANYA KUBWA ZENYE AFYA


NYANYA DOGO TOKA KWENYE MMEA WENYE MATAWI MENGI


Tuesday, August 13, 2013

UMUHIMU WA MAJIVU KWENYE UDONGO WA BUSTANI

Watu wengi wamekuwa wakiulizia umuhimu wa madini kwenye udongo na namna ya asili ya kuongezea kosefu wa madini kama potasiam, fosforas, kalsiam na mengineyo, njia rahisi ya kuongeza baadhi ya madini kwenye udongo ni kwakutumia majivu

UMUHIMU
Majivu yanakiwango cha wastani wa madini kifuatacho potasiam 5% - 7%, kalsiam 25% - 50%, fosforas 1.5% - 2% na madini mengine kwa kiasi kidogo pia mabaki mabaki ya chenga za mkaa kwenye majivu pia yanasaidia kwenye kunyonya baadhi ya sumu kwenye ardhi, kumbuka mkaa ni kaboni halisi (pure carbon)

KIASI CHA KUTUMIA
Kiasi cha kilo 2.5 mpaka 5 kitumike kwenye eneo la mita za mraba 33 au futi 100 za mraba, na majivu yamwagwe wiki 3 - 4 kabla ya kupanda kitu chochote ardhini.

MADHARA
Kila kitu kikitumiwa zaidi ya kiasi kina madhara na majivu pia yana madhara kwenye udongo kwa sababu yana hali ya kuwa alkaline zaidi (10 - 12 pH)  kwa sababu baadhi ya mchanganyiko wake hauyayuki kwenye maji, kama utahitaji kuongezea kwenye mimea yenye upungufu wa madini kama fosforas na potasiam basi hakikisha majivu hayagusi mashina kwani yanaweza kuuungua haya kama mimea ni michanga.

Pia majivu yanan kiasi kidogo sana cha naitrojeni ambacho hakiwezi kukidhi mahitaji ya mmea wowote ule, kwa hiyo hakikisha pia unatumia vyanzo vingine kwa ajili ya naitrojeni, vyanzo kama mimea jamii ya mikunde, marejea, lukina, na alfalfa

NANE NANE 2013










BLOG AWARDS 2013



Wasomaji wa blog hii ya mitiki-kilimo kwanza, mwaka huu pia blog hii itashiriki kwenye kutafuta blog bora za mwaka 2013 kupitia  http://tanzanianblogawards.blogspot.com/ blog hii itaomba kushiriki kwenye vipengele viwili vya Best AgricultureBlog na Best Educational Blog. 


 



Mkumbuke blog hii kwa mwaka 2012 ndio ilikuwa blog bora kwenye kipengele cha Best Educational Blog, kwa mwaka huu upigajikura utaanza September 1 mpaka September 7 2013 kwa wale wanaoamini hii ni blog bora kwenye vipengele itakavyochaguliwa, nitawaomba watembelee linki hii hapa chini na kupiga kura zao. Aksante

http://tanzanianblogawards.blogspot.com
  

Tuesday, August 6, 2013

SEREKALI KUNUNUA MAZAO YOTE YA NAFAKA


 Serikali imetangaza kuanzia mwakani itaanza kununua mazao yote ya nafaka, ili wakulima nchini  wawe na soko la uhakika. Hatua hii inalenga kuweka ushindani wa biashara baada ya kuhodhiwa wa wanunuzi binafsi.

Mazao yatakayonunuliwa kupitia Bodi Mpya ya Mazao ya Nafaka ni mpunga, maharagwe, karanga, choroko, ulezi, ufuta na mahindi na kwamba yatanunuliwa kwa bei ya ushindani wa soko mwaka huu.
Mchumi wa bodi hiyo, Edwin Mkwenda, alisema hayo kwenye maonyesho ya wakulima yanayofanyika kitaifa  Viwanja vya Nzuguni, Dodoma.
Mkwenda alisema tayari Serikali imeikabidhi bodi hiyo maghala yote yaliyokuwa ya Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC), ambayo hayakubinafsishwa kwenye kanda saba za nchi ili kutunza mazao yatakayonunuliwa.
Naye Ofisa Ubora wa Mazao wa Bodi hiyo,  Dendego Abdallah, alisema kuundwa kwa bodi hiyo ni ukombozi kwa wakulima kwani watakuwa na uhakika wa kupata soko la mazao husika.
Abdallah alisema wafanyakazi wa bodi chini ya Mkurugenzi Mkuu, Eliampaa Kilanga, imejipanga kuanza biashara rasmi mwakani na kwamba, wakulima wajiandae kuzalisha mazao hayo kwa wingi kutokana na kuwapo uhakika wa soko.
Wakati huohuo, Shirika la kuendeleza Bonde la Mto Rufiji (Rubada), limetenga Sh300 milioni kujenga kituo cha pili cha kufundisha vijana kilimo cha biashara kwa vitendo eneo la Ngalimila, wilayani Kilombero.
Ofisa Kilimo wa Rubada, Joseph Lyafwila, alisema hayo kwenye maonyesho hayo kuelezea mkakati wa Serikali kubadili kilimo kwa vijana, ili walime kibiashara zaidi  kupitia mafunzo ya vitendo.

CHANZO http://www.mwananchi.co.tz/kitaifa/Serikali-kununua--nafaka-zote-nchini/-/1597568/1937656/-/13mbvgmz/-/index.html

Tuesday, July 30, 2013

KILIMO BORA CHA MANANASI

Zao la mananasi hulimwa sana hapa nchini maeneo ya Bagamoyo, Kibaha, Geita, Mwanza, Tanga, Mtwara, Lindi na maeneo mengine. Zao hili lina kiasi kikubwa cha vitamini A na B na kiasi kidogo cha vitamini C, pia kuna madini kama potasiam, kalsiam, chuma na magnesiam

HALI YA HEWA
Manansi hustawi sana ukanda wa pwani usawa usiozini mita 900 toka usawa wa bahari ambapo kuna mvua nyingi kiasi cha milimita 1500 na unyevu wa kutosha, pia unaweza kupanda kwenye maeneo yenye mvua chache lakini kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji, Hali ya joto ni kuanzia sentigredi 15 - 32, huwa haya stahimili baridi

UDONGO
Udongo wenye rutuba ya kutosha na usiotuamisha maji ndi unaofaa kwa ajili ya kilimo cha mananasi, unaweza kutumia samadi au mbole vunde ili kuongezea rutuba ya udongo wako.

MSIMU
Kwa ukanda wa pwani wenye mvua mbili kwa mwaka upandaji wa mananasi huanza mara baada ya mvua za kwanza kuanza, ni vizuri kupanda kwa muda mfupi ili uzaaji usipishane sana na pia kusaidia kupata mvua za kutosha kabla ya msimu kuisha.

UPANDAJI
Tumia miche ya aina moja na yenye umri sawa ili huduma zifanane na pia uzaaji uwe wa mpangilio, umbali toka mmea hadi mmea ni sentimeta 30 na mstari hadi mstari ni sentimeta 60, na umbali kila baada ya mistari miwili miwili ni sentimeta 90

Kwa ekari moja unaweza kupanda miche 25,200 na kwa hekta moja unaweza kupanda miche 44,000. ili mananasi yako yastawi vizuri basi tengeneza kama mtaro mdogo na kwenye mitaro ndio upande mananasi yako, hii husaidia kupata unyevu zaidi

MBOLEA
Kwa wale wanaotumia mbolea za viwandani, ni vizuri kutumia NPK na DAP ambazo utaweka miezi miwili baada ya kupanda na miezi 12 baada ya kupanda baada ya hapo hautahitaji mbolea tena, lakini ni vizuri zaidi kama utatumia mbolea za asili

WADUDU
Wadudu wanaoshambulia mananasi ni aina ya mealybug ambao huondolewa kwa kupulizia dawa kama dume na karate.

Ugonjwa wa kuoza moyo wa miche unaweza kuzuiwa kwa kupiga dawa za copper oxychloride au kwa kuzamisha miche kwenye dawa za fungasi (fungicides)kabla ya kupandwa shambani

UVUNAJI
Mananasi huwa tayari kuvunwa miezi 18  mpaka 24 baada ya kupandwa kutegemeana na mbegu na matunzo ikiwemo kiasi cha mvua, mbolea na unyevu shambani, Uvunaji  hufanyika kwa kutumia visu na vibebeo maalum kuhakikisha ubora wa zao hili


Thursday, July 25, 2013

ATHARI ZA MAFUTA YA UBUYU NA TFDA


 
Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) imesisitiza kwamba mafuta ya ubuyu yana athari kubwa za kiafya na ni hatari kwa sababu yana tindikali ya mafuta ijulikanayo kama Clycopropenoic, moya ya madhara ya mafuta ya ubuyu ni pamoja na kusababisha saratani. TDFA imesema pia kutumia unga wa ubuyu na majani yake hakuna athari zozote kiafya kwa hiyo watu wanaweza kuendelea kutumia bila matatizo yoyote.
Kitaalamu tindikali ya Clycopropenoic inaweza kuondolewa kwenye mafuta hayo iwapo tu yatachemshwa katika kiwango cha digrii 180 za sentigredi kwa masaa 8 au kwa teknolojia ya kuyagandisha (hydrogenation) ambapo katika njia hizo zote mbili hakuna hata moja ambayo inatumika hapa nchini.

Miaka ya karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya bidhaa za asili ikiwemo ya aloe vera, ubuyu na bidhaa zake, hii inatokana na matatizo ya kiafya kama kisukari, ugonjwa wa moyo, magonjwa ya ngozi, uzazi, nguvu za kiume na kuongeza kinga mwilini. kutokana na hili matumizi ya ubuyu, majani yake na mafuta yake yaliongezeka zana huku watu wakiamini kwamba ni dawa na kinga ya magonjwa mbali mbali.


Hili walilotuambia TDFA tusilipuuze ila taasisi nyingine za kiutafiti kama SUA na  NIMRI zifanye utafiti wa kutosha sio tu kwa mafuta ya ubuyu bali pia kwenye dawa nyingine na vitu vya asili ili kubaidi madhara yanayoweza kujitokeza kwa waTanzania iwapo watatumia.


Wednesday, July 24, 2013

KILIMO BORA CHA MATUFAA - APPLES

Tufaa ni tunda moja maarufu duniani ambalo hupendwa kuliwa na watu wa jamii zote, hii inatokana na utamu wake pamoja na faida za kiafya zinazopatikana kwa kula matufaa. Matunda haya hustawi zaidi kwenye nyanda za juu ambako joto sio kali, sehemu kama lushoto, Arusha, miteremko ya Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Njombe, Songea nk. Udongo ni wenye rutuba ya kutosha na usiotuamisha maji

Unaweza kupanda kwa kutumia mbegu au kwa kununua miche bora kutoka kwenye taasisiza kilimo mfano Uyole Mbeya. kama utatumia mbegu basi ni bora kununua mbegu bora au ukikosa mbegu basi jaribu kutumia zile utakazopata kutoka kwenye tunda lenyewe

Kama utachukua za kwenye tunda basi zikaushe kwenye jua kwanza mpaka zikauke kabisa, zile za kukununua huwa zimekauka kwa hiyo huna haja ya kuzikausha, Chukua karatasi laini (napkins/tissues) iloweshe maji kiasi kidogo kisha chukua mbegu zako na uzifunge na  karatasi hii vizuri kisha ziwekw kwenye jokofu kwa kiasi cha wiki 3-4 zitaanza kuota/kumea, kuziweka kwenye friji husaidia kuua vijidudu vya magonjwa ambavyo huenda vilikuwepo kwenye tunda au mbegu

Chukua mbegu yako na uipande kwenye mifuko au chombo kama ndoo, usipande kwenye vifuko vidogo maana mmea huu hukua mkubwa kiasi na wenye mizizi mikubwa kabla ya kupandwa. Mmea wako ukifikia ukubwa wa futi moja mpaka pili ni kipindi kizuri kuuhamishia shambani,

Umbali wa shimo hadi shimo ni kiasi cha futi 15 mpaka 18 kutoka mti hadi mti. Hakikisha unapanda miche yako wakati wa mvua za kwanza, Mashimo yawe na kina cha futi mbili na upana futi 3. Weka kasi cha debe 1 la samadi au mboji na changanya vizuri na udongo.

kumbuka kuacha kisahani kwa ajili ya kukusanya maji ya mvua au unapomwagilia na utandaze majani/nyasi kiasi cha futi 3 kuzunguka mti wako, hakikisha wanyama kama mbuzi na ng'ombe hawaingii shambani na kula miti yako. Baada ya mwaka hutakuwa tena na haja ya kumwagilia miti yako kwani itaweza kukua yenyewe kwa kutegemea mvua

WADUDU NA MAGONJWA
Wadudu wanaoshambulia zaidi mitufaa ni vidukari (moth) na pia ugonjwa wa madoa meusi (black spot) ndio unaoshambulia zaidi, ili kupambana na ugonjwa na wadudu hawa hakikisha unatuma kiutilifu chochote che nye pareto (pyrethrum) ndani yake
KUVUNA
Uvunaji ni baada ya miaka mitatu lakini miche ya kuunga huanza kuzaa mapema hata ndani ya mwaka, ila nashauri usiruhusu matunda mengi kwenye miti midogo ili kuzuia matawi kuvunjika kwa hiyo punguza matunda kabla hayajawa makubwa na kubakisha machache

Wednesday, July 17, 2013

BLACK QUARTER - CHAMBAVU

Huu ni ugonjwa wa mifugo unaoshambulia ng'ombe, kondoo na mara chache farasi. Unasababishwa na vijidudu  ina ya Clostridium chauvoei  ambavyo hushambulia bila uwepo wa oksijeni ya kutosha (anaerobic) na kuzalisha sumu kwenye mwili wa myama na kusababisha kifo.

KUSAMBAA
Vijidudu husambaa kwa kupitia kwenye udongo ambapo mnyama huvipata anapokula majani, pia huweza kusambazwa kwa njia ya vidonda na mate toka kwa mnyama mwenye ugonjwa huu.

DALILI
-homa kali
-Misuli ya miguu ya nyuma huvimba na kuwa na joto kali, inauma ikiguswa na rangi ya sehemu hiyo ya ngozi hubadilika
-Ukigusa sehemu iliyoshambuliwa inatoa sauti ya kama majani makavu
-Mnayama huchechemea mguu wa nyuma sababu ya maumivu

UCHUNGUZI
Uchunguzi ufanyike na maafisa ugani wa mifugo kwa kufuatilia dalili na historia ya sehemu husika
-Kipande cha msuli na majimaji toka sehemu iliyoathiriwa kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara
-Uchunguzi wa mwili wa myama aliyefariki (post Mortem)

MATIBABU
-Penicilin inasaidia kutibu ugonjwa kama matibabu yataanza katika hatua za mwazo, ukichelewa hutaweza kmtibu mnyama wako.
-Tumia b-complex, na dawa za kupunguza uvimbe  kama visaidizi vya tiba
-Kupachana sehemu iliyoathirika ilikutoa majimaji na kuingiza hewa ili kuharibu mazingira ya kuishi vijidudu

KINGA
-Chanjo ya mara moja kwa mwaka kwa wanyama wakubwa.
-Wanyama wadogo wachanjwe mara wafikishapo umri wa miezi mitatu
-kwa sehemu ambayo kuna mlipuko wa ugonjwa huu wanyama wote wachanjwe kisha wapigwe dozi kubwa ya penicilin (kama ugonjwa hautaibuka ndani ya siku 14 wanyama wako watakuwa salama)
-Miili ya wanyama walikufa ichomwe na kuzikwa kwenye shimo refu sana


Thursday, April 25, 2013

NAMNA YA KUPAMBANA NA HARUFU MBAYA YA MBWA NDANI YA NYUMBA YAKO

Je unafuga mbwa  wako ndani ya nyumba yako kwa usafi wa hali ya juu, lakini umegundua harufu mbaya ya mbwa wako bado ipo ndani ya nyumba yako?  inawezekana ni kwa kiasi kidogo sana lakini bado inakera maana harufu mbaya ni mbaya tuu. Ambacho hujagundua ni kwamba kuna sehemu kadhaa ambapo hii harufu imejificha, sasa hapa nitakupa siri ya kuondoa harufu hii

(a)Matandiko anayolalia mbwa wako hakikisha yanafuliwa kila wiki, na itapendeza kama utakuwa na seti mbili ili wakati moja imefuliwa na kusubiria ikauke na jua basi unamtandikia hii nyingine

(b)Kama tandiko la mbwa huwa lina kaa kwenye kreti maalum basi tumia brashi kulisafisha na sabuni kisha nalo lianikwe, hii iwe angalau mara 1 kwa wiki, pia katikati ya wiki unaweza kuwa unalisafisha mara kwa mara kwa kutumia masine ya vakyum ya kusafishia mazulia

(c)Kama mbwa wako huwa analalia mito ya makochi yako, basi hakikisha ni mito ambayo inaweza kufulika ili nayo iwe inafuliwa mara kwa mara

(d)Midoli ya kuchezea mbwa wako nayo pia iwe ni ile ambayo inaweza kufuliwa na ifuliwe mara kwa mara ili kuondoa harufu

(e)Angalia sehemu ambazo mbwa wako hupenda kujificha mara kwa mara maana wakati mwingine huwa wanasahau mabaki ya chakula  na kusababisha harufu mbaya

(F)Kabla ya kusafisha mazulia yako yanyunyuzie na baking soda (sina jina la kiswahili) kisha safisha kwa kutumia mashine ya vakyum