PUNDAMILIA - MIKUMI
Nchi yetu Tanzania imebahatika kuwa na vivutio vingi vya utalii zikiwemo mbuga za wanyama, sehemu za kihistoria na sehemu za kijografia kama milima na mapango. Mara nyingi tumezoea kuona wageni wakija nchini mwetu kutalii na kutembelea vivutio vyetu wakati sisi wenyewe tukiwa wavivu kutembelea sehemu hizi adimu.
TWIGA - MBUGA YA ARUSHA
Kwa bahati nzuri mimi ni mtembezi/msafiri sana na ninapenda sana safari, hii imenisababishia kuweza kutembelea baadhi ya sehemu za utalii kama mbuga za Serengeti, Ngoro ngoro, Saadani, Mikumi, Manyara, Katavi, Arusha, Selous, sehemu nyingine za kitalii ni kama Kitulo, Amboni, Bagamoyo, msitu wa kazimzumbwi ulioko kisarawe, Kimondo cha Mbozi, daraja la Mungu Kiwira, Ziwa ngosi katika kreta iliyoko karibu na isangati katika safu za milima ya Rungwe na mara kadhaa nimeshiriki uwindaji katika mapori ya akiba.
TANDALA - KATAVI
Mara nyingi wizara ya utalii imekuwa ikihamasisha utalii wa ndani kwa kuweka ada ndogo kwa waTanzania kwenye mbuga zake, na mara nyingine huandaa safari za kitalii kwa gharama nafuu. Kwa Mfano mwaka jana wakati wa saba saba kulikuwa na safari za kutembelea mikumi kwa siku moja kutokea dsm kwa gharama za shilingi 10,000 kwa kila mtu, hii ilijumuisha usafiri na ada ya kuingia mbugani, Ukiangalia gharama halisi hiki kiasi kilikuwa kinatosha nauli ya kwenda tu mikumi nahisi watu walikuwa wanachangia mafuta tu lakini basi lilikuwa halijai watu kila siku ya safari.
FLAMINGO - ZIWA MANYARA
Kumekuwa na uhamasishaji wa wanafunzi kwenda mbugani wakati wa likizo, ambapo huchangishwa kiasi Fulani cha fedha na kisha kusafirishwa kwa pamoja kwa kutumia mabasi kwenda mbugani. Mara nyingi shule binafsi ndio zimekuwa zikijihusisha na safari hizi za utalii wa ndani, wakati kumekuwa na msukumo mdogo kutoka shule za serekali.
KIFARU - NGORONGORO
Utalii pia umekuwa na mwamko mdogo kutokana na gharama za usafiri na malazi, kwa sababu sehemu za kitalii zina malazi aghali hata kama utalala nje ya mbuga, kwa mfano mji wa mto wa mbu ulioko nje ya mbuga ya Manyara gharama ya malazi iko juu. Pia kuingia mbugani kunahitaji gari la 4WD ambalo itabidi ukodi toka kwenye makampuni ya kitalii na pia utajitaji mtu wa kukuongoza (guide) kwa wale walio karibu na mbuga hizi wanaweza kutumia usafiri binafsi ili kupunguza gharama.
SIMBA - SERENGETI
2 comments:
Kwa kweli ni kweli kabisa inasikitisha sana kuona sisi wenyewe hatutembelei sehemu hizi. Ngoja nikuambia mwaka juzi mimi na familia yangu tulikuwa tukipita pale Mkumi na baadaye tukasimama kuangalia wanyama na pia kupiga picha kidogo. Mara likaje gari na dada mmoja akatuambia kama ni wapita njia haturuhuwsiwi kupiga picha ni watalii tu. Niliumia sana.
Safi sana kwa kuitangaza Tanzania.
Mimi nimeshatembelea karibu mbuga zote za wanyama, mpaka Ngorongoro crater, nimeenda kama mara 7. Zile zilizoko Kigoma na Rukwa ndio sijawahi fika
Post a Comment