KURASA

Monday, December 28, 2009

KUTU YA MAJANI - COFFEE LEAF RUST

Huu ni mwendelezo wa magonjwa makuu ya kahawa
Kutu ya Majani ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vya ukungu jamii ya Hemileia vastatrix; Ugonjwa huu ushambulia karibu aina zote za kahawa; hasa katika nyanda za chini ambako kuna joto zaidi. Ugonjwa wa kutu ya majani hujitokeza kabla ya mvua za masika kuanza.



MAZINGIRA MAZURI YA VIMELEA VYA KUTU YA MAJANI:
• Joto lililo ambatana na unyevu nyevu mwingi angani.
• Kivuli kinachosababishwa na miti mingi shambani au matawi
ya kahawa.
• Magugu jamii ya Oxalis.
• Kahawa zilizozeeka kupita kiasi nazo hushambuliwa kwa urahisi.

MASHAMBULIZI NA DALILI
• Kutu au rangi ya machungwa iliyochanganyika na manjano huonekana upande wa chini wa majani ya kahawa.
• Kudondoka kwa majani yangali bado machanga.
• Kudumaa kwa matawi.
• Kukauka kwa ncha za matawi.
• Hatimaye mavuno hupungua kwa kiasi kikubwa.

UGONJWA UNAVYOSAMBAZWA:
• Upepo huongeza kasi ya kusambaa kwa vimelea vya kutu ya majani.
• Wanyama (ndege) wadudu, husambaza vimelea vya kutu ya majani toka mmea mmoja hadi mwingine.
• Miezi michache kabla ya Vuli vimelea vya kutu ya majani huanza kukua;
- Vimelea hivi hujihifadhi kwenye magamba ya shina la kahawa na matawi makubwa (Primary branches) hasa kahawa zilizozeeka.
- Kipindi hiki huwa na joto.
• Vuli husaidia kuongeza kasi ya kukua kwa vimelea hivyo na kusambaza.
- Kutokana na unyevunyevu uliopo kwenye majani na kahawa kwa ujumla.
• Vimelea vya ukungu wa aina hii vinapoendelea kusambaa ndivyo na ashambulizi ya mmea yanavyoongezeka.
• Mashambulizi huendelea kipindi chote cha joto hadi masika, kipindi ambacho vimelea hukosa nguvu.
• Nguvu ya vimelea vya kutu ya majani huanza tena kidogo kidogo
baada ya masika kwisha.



KUPAMBANA NA KUTU YA MAJANI:
• Shamba liwe safi wakati wote.
- Punguza kivuli cha miti na migomba kwenye shamba la kahawa.
- Punguza matawi ya kahawa (pruning); wakati wa kukata matawi kata matawi yote yalivyozeeka; na yaliyo na ugonjwa.
- Lima ili kupunguza magugu hasa jamii ya oxalis.
• Hakikisha udongo una unyevunyevu wa kutosha, wakati wote: (weka matandazo, mbolea na kumwagilia maji)
• Ondoa magamba kwenye kahawa kwa kutumia brush / magunzi mbalimbali.
• Jaribu sumu za asili kama utupa (rejea makala zangu).
• Sumu za viwandani (mrututu) zitumike pale tu ambapo ni lazima kufanya hivyo kufuatana na hali ya hewa;
- mrututu (copper) utumike kama kinga mara baada ya mvua za masika kama joto liko juu likiambatana na unyevunyevu angani.
- Endapo kutu ya majani imeshamiri tumia Bayleton kama tiba (control) lakini si zaidi ya mara 2 kwa msimu.
NB: Wakati wa kunyunyuzia sumu elekeza bomba chini ya majani.

4 comments:

Simon Kitururu said...

Asante kwa somo Mkuu! Natamani kweli uandikacho kingeweza kusambazwa mpaka haswa kwa Wakulima wahusika. Marehemu Babu yangu alilima Kahawa kwa bahati mbaya baada yake hakuna mwingine aliyejitokeza KATIKA FAMILIA kuendeleza kilimo hiki.

Navyokusoma kinamna nimejikuta nimerudi kimawazo shambani kwa babu:-(

Halil Mnzava said...

Somo hili kwangu ni hazina,kahawa imenilea ni basi tu kilimo hiki kimefifia sana.
nadhani una nafasi ya kuhamasisha jinsi ya kulifufua tena maeneo ambayo limefifia.
ahsante.
Nakutakia mwaka mpya wenye mafanikio na afya tele.

Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli ni somo nzuri na nakubalia na Mt. Simon ingekuwa safi kama wengi wangepata mafundisho haya na pengine kilimo cha kahawa kingekuwa bora.
Kaka Bennet nina swali natoka nje ya somo kidogo:- jana nilikuwa katika duka moja kutafuta mahitaji ya nyumbani, na mara nikaona majani ya migomba yaqliyosafirishwa toka Tailand yanauzwa na tena si kwa bei rahisi je majani ya migomba yana shughuli gani?

Unknown said...

Somo hili ni taa ya maishayangu katika kilimo hiki cha kahawa ,lakini nataka kuuliza,nidawa gani madhubuti yskumaliza tatizohili la kutu ya kahawa?