KURASA

Saturday, August 21, 2010

KILIMO BORA CHA MAHINDI

Mahindi ni chakula muhimu na ni aina ya nafaka katika mataifa ya Afrika yaliyomo kusini mwa jangwa la Sahara. Ni chakula cha matumizi ya nyumbani kwa idadi ya watu inayokadiriwa kuwa asilimia 50. Ni chanzo muhimu cha madini na kuongeza nguvu mwilini, protini, madini ya chuma (iron) vitamini na madini mengine asilia.Waafrika hutumia mahindi kwa njia mbalimbali – (uji, ugali na pombe). Na mahindi ya kuchoma. Kila sehemu ya mmea wa mahindi ina thamani kiuchumi : punje, majani, shina na magunzi huweza kutoa kiasi kikubwa cha bidhaa nyinginezo zilizo chakula na zisizokuwa chakula.

Vile vile mahindi ni chakula muhimu cha mifugo (ng’ombe) na huhifadiwa kama silage. Pia mabaki ya mimea na nafaka na pia hutumika viwandani kutengeneza wanga na mafuta.
Mahitaji ya mahindi katika hali ya hewa, udongo na Mahindi ni mimea ambayo hustahimili mabadiliko mengi ya hali ya hewa na humea katika maeneo mengi tofauti. Kuna aina nyingi za mahindi yanayotofautiana katika muda wa kukomaa, mahindi huwa na ustahimili mkubwa kwa mabadiliko katika kiwango cha joto. Mahindi haswa huwa mimea ya maeneo ya joto ambako unyevu ni wa kutosha. Mmea huu unahitaji kiwango cha joto cha kila siku cha nyuzi joto 20º ili umee vyema. Joto la juu sana kwa mazao mazuri ni kama nyuzi joto 30º. Hupandwa sana katika sehemu zilizo katika kimo cha mita 3000 kutoka bahari hadi kwenye ukanda wa pwani. mahindi yaweza kupandwa kama chakula cha mifugo.

SHAMBA LANGU NI SHAMBA DARASA


Mahindi huwa yanaathirika na ukosefu wa unyevu wakati wa kutoa maua na matunda. Pia yanahitaji maji ya kutosha wakati wa kupanda. Katika nchi za joto jingi (tropiki), mahindi hufanya vyema katika mvua ya kiwango cha milimita 600 hadi 900 wakati wa kukua. Mahindi yanaweza kukuzwa kwenye aina nyingi za udongo lakini hukua vyema zaidi katika mchanga, usiotuamisha maji mengi, ulio na hewa ya kutosha na ulio na rutuba na madini ya kutosha. Kuwepo kwa mazao mengi ya mahindi kunapelekea kunyonywa sana kwa madini kwenye udongo. Mahindi yaweza kukuzwa katika udongo ulio na hali ya mchanga na (PH) kutoka 5 hadi 8 ingawa 5.5 hadi 7 ndio mwafaka. Mahindi yako katika kikundi cha mimea kinachoaminika kuathirika na hali ya chumvi katika maji na udongo. Kwa vile mimea ambayo ni michanga huwacha sehemu kubwa bila kuzingirwa na ardhi, mmomonyko wa udongo na kupoteza maji hutokea sana sana hivyo basi ni bora umakini uzingatiwe katika uhifadhi wa udongo na maji kwa kuweka matandazo (mulching).

MATUMIZI YA MBOLEA
Mahindi hustawi zaidi yakiwekwa mbolea, iwapo mambo mengine yanayosaidia katika kukua pia yapo kwa kiwango kinachostahili. Mbolea inayotumiwa na wakulima wadogo mara yingi huwa haitoshi. Mahindi ya kiwango cha juu yaweza tu kufikia kiwango cha juu cha Uzalishaji iwapo yatapewa lishe na madini ya kutosha. Mahindi ya tani 2 kwa hekta na tani 5 kwa hekta hutumia karibu kilo 60 N, kilo 10 za P205 na kilo 70 K20 kutoka katika udongo. MAhindi hunyonya Nitrogen pole pole katika miezi ya kwanza baada ya kupanda, lakini huongezeka hadi kiwango cha juu kabisa wakati wa kutoa maua na kukuza tunda (gunzi). Mahindi huhitaji nitrogen kwa kiwango cha juu na ukosefu huwa ndio kizingiti. Kiwango cha juu cha nitrogen kinahitajika mara tatu; kwanza wakati wa kupanda, pili, wakati ambapo mmea umefikia sentimita 50 za urefu na tatu, wakati matunda ya mahindi yanaanza kutoa zile nyuzi nyuzi nyororo (silking).

Udongo mwingi huwa na madini ya phosphorous (P205) na potassium (K20) lakini sio kiwango kinachotosheleza mahitaji haswa ya mbegu za mahindi zinapochipua. Nyunyuzia P205 karibu na mbegu ili ziote kwa haraka. K20 hutumika kwa kiwango kikubwa lakini hitaji la mimea hubainika baada ya upimaji wa hali ya udongo kujua kiasi cha mahitaji (soil test).

DALILI ZA UPUNGUFU WA MBOLEA
Ukosefu wa K20 husababisha ncha za majani kuwa na rangi ya njano na kuunda gunzi (cob) lisilo na punje hadi juu. Ukosefu wa P205 hufanya matawi kuwa na rangi ya samawati na mbegu zisizo laini. Dalili za ukosefu wa nitrogen ni majani ya rangi ya manjano na mimea dhaifu mifupi. Phosphate haifyonzwi haraka na mahindi na pia udongo mwingi wa nchi za joto hukosa madini hayo ya phosphate. Inashauriwa unyunyuzie mbolea ya kiasili kama samadi kabla ya kulima ili uboreshe hali ya udongo na kuongezea madini.

Katika ukulima wa kiasili, (organic farming, Nitrogen (N) hutiwa kwenye udongo kupitia kwa upandaji wa mimea ya jamii ya mikunde (legumes) ambayo hutoa nitrogen katika hewa, Hata hivyo mapendekezo ya kimbolea yaliyo katika misingi ya uchunguzi wa udongo hutoa nafasi nzuri ya kupata kiasi kizuri cha mbolea bila kuweka kiwango cha chini au juu. Omba msaada kutoka kwa mafisa ugani wa kilimo waliyo katika eneo lako.
Katika maeneo yanayo tegemea mvua kukuza mahindi, panda mbegu wakati wa mvua ya kwanza. Hii itaruhusu mizizi kunyonya madini yaliyotengenzwa na bakteria katika udongo. Maji yaliyosimama huyeyusha na kuondoa madini ya nitrogen kutoka katika udongo na kusababisha ukosefu wa Nitrogen.


KUDHIBITI MAGUGU
Udhibiti wa magugu ni muhimu sana. Katika wiki 4 hadi 6 za mbele baada ya kumea, mahindi huathiriwa sana na magugu. Ni lazima mahindi yapandwe mara moja baada ya kutayarisha shamba. Unaweza kulima katikati ya laini za mahindi ili udhibiti magugu. Nchini Tanzania, kupalilia mara mbili kunahitajika kwa aina nyingi za mahindi, ingawa kupalilia kwa mara ya tatu kutahitajika kwa aina ambazo zinahitaji miezi 6 hadi 8 kukomaa. Kupalilia kwa mikono kunahitaji siku 15 kwa hekta la mikono (power tiller) ni masaa mawili mpaka matatu kwa ekari.

UHUSIANO WA NIPE NIKUPE
Desmodium (desmodium uncinatum) nyasi ya Molasses (melinis minutifolia) zikipandwa kati kati ya laini za mahindi huzuia wadudu kama stalk borers moths. Mimea hii hutoa kemikali ambazo huwafukuza wadudu aina stem borers’ moths. Zaidi ya hayo Desmodium huzui gugu haribifu,witchweed striga hermonthica. Napier grass (pennisetum purpureum) na Sudan grass (sorghum vulgare sodanese) ni mimea mizuri sana inayonasa wadudu aina ya stem borers. Napier grass ina njia yake madhubuti ya kujikinga dhidi ya wadudu wanaotoboa mmea kwa kutoa utomvu kutoka kwenye shina, ambayo huzuia wadudu kufyoza mmea na kusababisha uharibifu. Nyasi hizi pia huvutia adui wa stem borers kama mchwa, earwigs na buibui. Nyasi aina ya Sudan pia husaidia maadui asilia, kama nyigu (parasitic wasp)

MAHINDI TAYARI KWA KUVUNWA



Mahindi huweka kivuli kwenye mimea ya mboga mboga ikipandwa safu moja katikati ya mboga kwenye maeneo yaliyo na jua kali. Hii huongeza mazao ya mboga zilizopandwa hivi. na mimea jamii ya mikunde huongeza nitrogen kwenye udongo ambayo huitajika zaidi katika ukuaji wa mahindi pia hupunguza wadudu aina ya (leafhoppers, leafbeatles, stalk borers na fall army worm), upandaji wa mimea jamii ya mikunde ufanyike mara baada ya palizi ya kwanza


KUPUKUSUA MAHINDI KWA KUTUMIA MASHINE YA MKONO



UVUNAJI
Uvunaji hufanyika kwa kutumia mikono kwa mashamba madogo na mashine (combine harvester) hutumika kwa ajili ya mashamba makubwa, Zao la wastani la mahindi ulimwenguni mnamo mwaka 2000 lilikuwa kilogramu 4255 kwa kila hekta. Zao la wastani nchini Marekani ilikuwa kilo 8600 kila hekta, huku mataifa yaliyo chini ya jangwa la Sahara la Afrika yakivuna kilo 1316 kwa kila hekta ya shamba. Zao la wastani katika taifa la Tanzania kati ya mwaka 2001-2005 lilikuwa kati ya gunia 15-19 kwa hekta (sawa na kilo 1350-1750) Ukilima kwa kuzingatia ukulima wa kisasa na kanuni zake kwa Tanzania utavuna kilo 5000 kwa hecta (ukanda wa pwani) na kilo 7500 kwa nyanda za juu kama Iringa, Mbeya, Ruvuma, Arusha n.k

RUNDO LA MAHINDI BAADA YA KUPUKUSUA

26 comments:

Maisara Wastara said...

Kaka sikujua kama wewe ni mkulima hodari hivi...
Kuna mengi ninependa kujifunza kwani kule ukweni kwangu mikoa ya Kusini nimeona hakuna mwamko mkubwawa kilimo cha kisasa ingawa kuna vyanzo vingi vya maji.

nataka nimshauri mume wangu ajifunze kupitia kwako, kwani baba yake anayo mashamba mengi yaliyo karibu na vyanzo vya maji.

Nimejifunza jambo leo.

Yasinta Ngonyani said...

kweli hili ni darasa nzuri kabisa yaani kaka Bennet huna choyo. Safi sana.

Anonymous said...

Ben nakumbuka Yongolo alifikia mahali akawa anatumia Trekta kupukuchua mahindi pale nje(Unakumbuka?), hongera kwa hiyo mashine inapatikana wapi? JE HAIVUNJI MAHINDI(PUNJE)!
Mdau Bagamoyo

Bennet said...

Dada Maisara mimi sio hodari sana ila najitahidi kutumia ujuzi kidogo nilionao naamini kuna wajuzi zaidi yangu, ni vizuri ukimshauri mume wako maana sasa hivi kilimo kinalipa kwahiyo itasaidia kuongeza pato la familia
Dada Yasinta na wewe pia nakushukuru kwa kunitia moyo

Anonynakumbuka Yongolo alikuwa anatumia mashine aina ya Burch kupukuchulia mahindi, hii mashine niliinunua Mombasa na ilikuwa na njia mbili, moja imekufa ila nina mpango wa kuifufua na pia kuiwekea na mota ili kazi iwe rahisi zaidi, mashine ni nzuri na haivunji mbegu kabisa inatuma spring fulani kwa ajili ya auto adjust kutokana na ukubwa wa hindi lenyewe

emu-three said...

Hongera sana kwa ukulima , nyie ndio wajasiriamali halisi

Dada Elyc said...

Yaani kaka umenivutia ajabu! Mie nina heka 5 bagamoyo nimelima kilimo mseto (mananasi,mihogo,michungwa,ndimu,ndizi)kwa ufupi shamba lote limejaa na ninaamini baada ya miaka 3 litakuwa msitu wa matunda,mahindi yanaliwa na ngedere/nyani kwani bado watu hawajahamia sana. ningependa kupata hata heka 2 huko uliko ili nami nilime mahindi! Nitafutie heka 2-5 kaka.

Dada Elyc said...

Bennet niliahau kuandika hapo juu. ni kweli Kilimo kinalipa sana kama ukiweza kuyasoma majira,sema watu wanaogopa kujaribu. mimi ninavuna mihogo kipindi hiki,ninamshukuru Mungu kwa Mwezi huu wa ramadhani,nilipanda kama heka mbili na nusu now am a millionea.Jaribuni wapendwa ukipata hasara mwaka wa kwanza jaribu wa pili na watatu.....

Bennet said...

Aksante sana Emu -3 nami nitajitahidi zaidi

Dada Elyc hongera sana na wewe kwa kufanya kilimo mimi kilimo ndio ajira yangu dawa ya kilimo ni kufanya kilimo mseto ili kimoja kikikataa basi upande wa pili unapata, nitakuja siku moja Bagamoyo shambani kwako kukutembelea

Anonymous said...

Ben nitapata wapi mashine za kupukuchulia mahindi kwa Tanzania au Afrika Mashariki? iwe ya kutumia umeme, mkono au kuunganishwa kny pto ya trekta.

Mdau Bagamoyo

Bennet said...

Ngoja nikuulizie halafu nitakupigia kwenye namba yako
Aksante

Simon Kitururu said...

Bonge la shule hili!Asante Mkuu kuna bonge la kitu nimejifunza hapa.

Anonymous said...

Nimefurahiwa sana na article ya kilimo cha mahindi nami pia ni mshiriki na ningependa kulima kwa manufaa, ninalimia Ismani. Hivyo hebu nisaidie;
1. Maelekezo ya mbolea yamekuwa ya kitaalamu zaidi walau ungesema mifuko aina ipi kwa eka na kwa wakati gani,
2. Nahitaji elimu ya matumizi ya mbolea ya kuku na ya ng'ombe,
3. Mbegu za mahindi zimekuwa za aina nyingi kuchagua inakuwa ni kazi kweli kweli.
4. Je umwewahi kukutana na planter ya mkono kwa ajili ya kupandia mahindi?
Asante, na kama kuna vijarida vya kilimo cha mazao mbalimbali ningefurahi kuvipata.

Anonymous said...

kaka mimi ni mkulima wa mpunga mwaka jana ndio nimeaanza nililma heka 80 nilipatalakini ukawa umevunjika sana na soko likawa chini nilikuwa ifakara mwaka huu nikahamia madibira mbeya tatizo ni mvua imekuwa ndogo majaruba hakuwa na maji hadi mwakani nikatoa tractor hadi dakawa na dumira kilimo cha mahindi kikawa kimepita na mvua kidogo na sasa nalima alizeti

khalid83lab said...

KAKA HABARI!KIUKWELI NIMEAMIA IRINGA MWAKA HUU,NA LENGO LA KUTOKA KANDA YA KATI NI KUJA KUJARIBU MAISHA JAPO NIO MFANYAKAZI WA SERIKALI ILA NAAMINI KIWANGO NIKIPATACHO AKITAWEZA KUKWAMUA YALE YALIYO NDANI YA NDOTO ZANGU.
SIJAWAI KUPATA KUFANYA SHUGHULI YA KILIMO NA NINAAMINI NI ELIMU YA KILIMO BORA NDO ITAKOMBOA NIA YANGU.NIFANYEJE ILI NIIPATE KUJUA KWA KINA KUUDUMIA SHAMBA LA MAHINDI NATAKA KUANZA NA HEKARI KUMI NA TANO.
E-MAIL YANGU:khalid83lab@yahoo.co.uk

mafia kisiwani said...

mkuu babk kwa kutufungua macho sie wagema ulimbo,umenipa hasira lazima nilime

Anonymous said...

Nimefurahishwa sana na article yako, sasa kaka B mimi ni mwandishi wa hbr wa kujitegemea na kwa sasa nimeamua kujikita katika uandishi wa makala za kilimo naomba niambie ni wapi nitapata maelezo sahihi ya kilimo hasa cha mzao ya chakula? nisaidie mtu wangu

Anonymous said...

Asante sana kaka kwa elimu yako inatusaidia sana,mi nina mashamba eneo la kilwa Masoko ningependa kujua jinsi ya kufahamu mazao gani nilime pia ,katika heka moja kawaida unaweza kupata ton ngapi za mahindi asante sana

Anonymous said...

Bro, B
nimevutiwa sana na Elimu yako-Bravo!!!
Keep it up, ni watanzania wachache sana wenye moyo wa kukitoa wakijuacho kama ulivyo fanya wewe.mimi ndo kwanza naaza kuingia kwenye kilimo lakini kupitia watu kama wewe nadhani naweza pata mengi sana,ili niweze kufanikiwa.
naamini nina mengi sana ya kujifunza kutoka kwako.I'll keep in touch with you-definetly!!!!!

Paul said...

MPILUKA PAUL
Na mimi sipo mbali jamani kumbe nilikuwa nipo Porini leo nimeletwa barabani lazima tutoke hakuna kulala ni kazi kwenda mbele sizembei hata kidogo nakwenda shambani sasa hakuna masihara hapa

ALMASSTZ said...

kitu kikubwa ninachohitaji ni mafunzo kwa vitendo jee ntakuonaje mr bennet

Negative255 said...

Je kilimo hiki kinaweza kufanywa kwa umwagiliaji? Kibiashara

New Generation said...

Safi sana kaka....nimeipenda hiyo

New Generation said...

Safi sana kaka....nimeipenda hiyo

New Generation said...

Yap of coz...kilimo cha mitiki inaweza ukafanya cha umwagiliaji....na kumbuka kuwa mitiki haihitajii maji mengi sana...na watu wengi hufanya kilimo cha mitiki cha biashra...umwagiliaji hufanya zile sehemu ambazo hupata mvua chache kwa mwaka

New Generation said...

Yap of coz...kilimo cha mitiki inaweza ukafanya cha umwagiliaji....na kumbuka kuwa mitiki haihitajii maji mengi sana...na watu wengi hufanya kilimo cha mitiki cha biashra...umwagiliaji hufanya zile sehemu ambazo hupata mvua chache kwa mwaka

INJILILEO BLOG said...

NAOMBA NA MIMI TUWASILIANE NINAHITAJI MAHINDI HAPA