KURASA

Friday, May 29, 2009

UTALII WA NDANI

PUNDAMILIA - MIKUMI



Nchi yetu Tanzania imebahatika kuwa na vivutio vingi vya utalii zikiwemo mbuga za wanyama, sehemu za kihistoria na sehemu za kijografia kama milima na mapango. Mara nyingi tumezoea kuona wageni wakija nchini mwetu kutalii na kutembelea vivutio vyetu wakati sisi wenyewe tukiwa wavivu kutembelea sehemu hizi adimu.

TWIGA - MBUGA YA ARUSHA


Kwa bahati nzuri mimi ni mtembezi/msafiri sana na ninapenda sana safari, hii imenisababishia kuweza kutembelea baadhi ya sehemu za utalii kama mbuga za Serengeti, Ngoro ngoro, Saadani, Mikumi, Manyara, Katavi, Arusha, Selous, sehemu nyingine za kitalii ni kama Kitulo, Amboni, Bagamoyo, msitu wa kazimzumbwi ulioko kisarawe, Kimondo cha Mbozi, daraja la Mungu Kiwira, Ziwa ngosi katika kreta iliyoko karibu na isangati katika safu za milima ya Rungwe na mara kadhaa nimeshiriki uwindaji katika mapori ya akiba.

TANDALA - KATAVI



Mara nyingi wizara ya utalii imekuwa ikihamasisha utalii wa ndani kwa kuweka ada ndogo kwa waTanzania kwenye mbuga zake, na mara nyingine huandaa safari za kitalii kwa gharama nafuu. Kwa Mfano mwaka jana wakati wa saba saba kulikuwa na safari za kutembelea mikumi kwa siku moja kutokea dsm kwa gharama za shilingi 10,000 kwa kila mtu, hii ilijumuisha usafiri na ada ya kuingia mbugani, Ukiangalia gharama halisi hiki kiasi kilikuwa kinatosha nauli ya kwenda tu mikumi nahisi watu walikuwa wanachangia mafuta tu lakini basi lilikuwa halijai watu kila siku ya safari.

FLAMINGO - ZIWA MANYARA


Kumekuwa na uhamasishaji wa wanafunzi kwenda mbugani wakati wa likizo, ambapo huchangishwa kiasi Fulani cha fedha na kisha kusafirishwa kwa pamoja kwa kutumia mabasi kwenda mbugani. Mara nyingi shule binafsi ndio zimekuwa zikijihusisha na safari hizi za utalii wa ndani, wakati kumekuwa na msukumo mdogo kutoka shule za serekali.

KIFARU - NGORONGORO


Utalii pia umekuwa na mwamko mdogo kutokana na gharama za usafiri na malazi, kwa sababu sehemu za kitalii zina malazi aghali hata kama utalala nje ya mbuga, kwa mfano mji wa mto wa mbu ulioko nje ya mbuga ya Manyara gharama ya malazi iko juu. Pia kuingia mbugani kunahitaji gari la 4WD ambalo itabidi ukodi toka kwenye makampuni ya kitalii na pia utajitaji mtu wa kukuongoza (guide) kwa wale walio karibu na mbuga hizi wanaweza kutumia usafiri binafsi ili kupunguza gharama.

SIMBA - SERENGETI

Wednesday, May 27, 2009

VUNJA - JUNGU




Huu ni msimu ambao huku kwetu wanakuwa wengi sana, hiki ni kipindi ambacho mvua zinaishia na kuelekea kwenye majira ya baridi (joto kupungua) hawa wadudu huzaana sana kipindi hiki na hujazana kwenye taa za majumbani na wakati mwingine huingia ndani

DUME



Kuna baadhi ya jamii huwakamata na kuwala kama vile kumbi kumbi na senene, lakini si wengi waliozoea kuona wakiliwa, ukimshika vibaya na anakapata nafasi anaweza kuku ng'ata ingawa hana sumu yoyote na kidonda chake ni kidogo kinachoweza kupona chenyewe.

JIKE



Kama una bustani ya maua na mboga mboga na unasumbuliwa na wadudu kuvamia mara kwa mara, basi unaweza kuwapandikiza wadudu hawa na wakakusaidia katika kuondoa wadudu waharibifu kwa njia ya kibaiolojia, kwa sababu wana tabia ya kula wadudu wengine kama chakula chao. ili kuweza kujua madume na majike angalia rangi zao, madume huwa na rangi zilizokooza na kijivu wakati majike huwa na rangi ya kijani kibichi


WAKIPANDANA

Thursday, May 21, 2009

MICHONGOMA

Sehemu nyingi za duniani ikiwemo nchi yetu Tanzania michongoma imekuwa ikitumika kwa miaka mingi kwa matumizi mbali mbali, matumizi ya michingoma yameanzia zaidi ya miaka 4000 – 6000 iliyopita na michongoma iliyopo ambayo ina umri mkubwa zaidi ni miaka 700 na inapatika nchini ujerumani kiwa na urefu zaidi ya nyumba ya kawaida
Michongoma hutokana na aina mbali mbali za mimea ambayo baadhi ni miti na mingine hukua kama vichaka, yote hii huwa na sifa ya kuwa na miiba na kuhimili ukame ingawa baadhi ya mimea na miti ambayo haina miba hutumika kama michongoma mfano mi krismas (cupresus lusitanica, thujia orientalis)

thujia orientalis


UPANDAJI
Upandaji hutegemeana na aina ya mmea wenyewe, baadhi hutumia vipandikizi, mingine hutumia mbegu na mingine kwa njia zote mbili, ile inayooteshwa kwa vipandikizi huweza kuoteshwa sehemu na ikimea huhamishiwa sehemu husika wakati ile inayooteshwa kwa mbegu mara nyingi huoteshwa sehemu husika moja kwa moja. Huwa haihitaji kumwagiliwa maji ila inapokuwa midogo, ikishakuwa nikubwa inauwezo wa kukua kwa kutegemea mvua tu labda kama kuna ukame

MATUMIZI

MIPAKA –

Mara nyingi hasa majumbani tumeina watu wakitumia michongoma kama mipaka, sehemu za pwani na sehemu zenye mvua chache hutumia zaidi ile yenye miiba, wakati sehemu za bara hasa zenye baridi hutumia ile isiyo na miiba kama mipaka.

UREMBO –
BOUGAINVILEA


MKRISMAS

Wakati mwingine michongoma hutumika kama urembo ikiwa kama mipaka au ikipandwa mmoja mmoja kama maua au miti ya urembo, miti kama mikrismas (cupresus lustanica) na (thujia orientalis) ambayo iko kama mikrismas ila majani yake yako bapa kama yamepigwa pasi. Inapatikana mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Lushoto, Mbeya, Iringa, Songea n.k pia kuna inayojuliakana kama boganivilia

KUKINGA UPEPO

–Mara chache sana ambapo michongoma huachwa na kuwa mikubwa kama miti na kutumika kukinga upepo kwenye nyumba na mashamba, sehemu nyingine huwa tu imesahaulika kukatwa na kuwa mikubwa na kufanya kazi ya kukinga upepo.

ULINZI

Hii ndio kazi hasa ya michongoma na haya matumizi yake yalianzia huku, na miti inayotumiaka hapa ni ile yenye miiba zaidi, unaweza kukuta imepandwa kama mpaka na ulinzi au ulinzi peke yake ikiwa ndani ya mipaka. Hutumika kulinda makazi, mazao na mifugo kwenye mazizi, kuna baadhi ya mimea ambayo huwekwa kwenye mazizi na jamii za wafugaji ambazo huaminika kufukuza wanyama wakali kama simba na fisi wasishambulie mifugo.

Monday, May 18, 2009

UPANDISHAJI/UZALISHAJI SAMAKI

Kama wewe ni mfugaji wa samaki kwenye mabwawa kwa ajili ya biashara, basi ni vizuri ukazalisha samaki wako, ndipo uwaweke kwenye bwawa wakiwa katika idadi inayojulikana nah ii itakusaidia kwenye ulishaji sahii na mavujo ya juu kulingana na ukubwa wa bwawa lako.

UTAMBUZI WA JINSIA
Hii ni kazi inayohitaji utaalamu na mazoea kidogo. Kwa kawaida samaki jike huwa na tumbo la mviringo kidogo wakati tumbo la samai dume huwa bapa, samaki dume huwa na vidoti vyeupe kwenye mapezi afikiapo umri wa kupanda, na huruka ruka zaidi ya jike mara watolewapo kwenye maji.



UPANDISHAJI
Kwa kawaida upandishaji hufanyika kwenye sehemu isiyo na kina kirefu kwenye vyombo maalumu, chombo kisiwe kwenye jua, na kiwekewe majani ya kutosha na mchanga chini. Kabla ya kuwapandisha samaki wawe kwenye vyombo tofauti kwa siku 3 – 4 na muda wote walishwe vyakula maalum nyenye protein nyingi, katika mazingira ya kawaida huwa tunawalisha nyungunyungu (earth worms) ambao hupatikana kwa kuchimba sehemu chepechepe, kama una samaki wazazi itakubidi uzalishe nyungunyungu (somo kuja baadae) walishe samaki wako kadri wanavyoweza kula
Baada ya kuridhika na maandalizi ya samaki wako, sasa unalichukua jike na kulipeleka kwa dume na si kinyume, dume huwalimechimba vishimo kwenye mchanga ambavyo baada ya muda jike likihamasishwa hutaga ndani yake na dume hurutubisha mayai, baada ya kurutubishwa jike huyachukua mayai na kuyaweka mdomoni kwake, baada ya hapo lazima jike arudishwe kwenye chombo chake kwa siku 6 – 10 na hapo watoto hutotolewa toke mdomoni mwake. Watoto wakitotolewa tu jike ataondolewa na kurudishwa kwenye bwawa la kawaida kwa sababu atawala watoto wake.

SAMAKI JIKE MWENYE MAYAI MDOMONI




Baada ya watoto kutotolewa utawalisha baada ya siku mbili na chakula chao kikuu ni viini vya yai na baada ya wiki wanaweza kula watoto wa dagaa uduvi ambao nao utawazalisha (somo kuja baadae)Samaki wako wakifikia ukubwa wa kutosha utawaingiza kwenye bwawa lako na kuendelea kuwalisha mpaka kufikia umri wa kuvuna.
Kama una mabwawa tayari na samaki wako wanapandana , ukienda ule upande wenye kina kifupi utakuta samaki dume amechimba vishimo vya kutagia, mara baada ya watoto kutolewa mdomoni na mama yao, unatakiwa kuwawahi na kuwahamishia kwenye sehemu salama ili wasiliwe na samaki wakubwa.

SAMAKI AKITOA WATOTO MDOMONI


Upandishaji wa samaki wa urembo ni kama huu sema wenyewe tofauti inakuja kwamba samaki kama gold fish hutaga popote pale hawachimbi vishimo na baada ya kutaga dume hurutubisha mayai, ili kujua mayai yamerutubishwa maji hubadilika rangi na kuwa kama ukungu, basi hapo utawatoa jike na dume na kuyaacha mayai, mayai yao huwa hayaatamiwi kwenye mdomo wa samaki jike.

SAMAKI BAADA YA KUVUNWA

Thursday, May 14, 2009

UFUGAJI WA SAMAKI WA CHAKULA - SEHEMU YA PILI

TILAPIA



Katika sehemu ya pili tutaongelea ufugaji katika bwawa la wastani kwa ajili ya samaki wa kitoweo na kuuza. Baada ya kuchagua sehemu ya kuchimba bwawa lako na kuzingatia vigezo vyote, kinafuatia ni uchimbaji wa bwawa lenyewe, kwa bwawa dogo uchimbaji unafanyikwa kwa kutumia mikono na vifaa kama jembe, sururu na chepe, kwa mabwawa makubwa inabidi kutumia mashine za kuhimbulia. udongo unaotolewa uwekwe kwenye kingo za bwawa na kutumika kuongeza kina, bwawa linatakiwa kuwa na kina kirefu upande mmoja na kina kinapungua kuelekea upande mwingine wenye kina kifupi, mfano mzuri angalia mabwawa ya kuogelea. Kwenye kina kirefu unaweka bomba lenye chekeche la nyavu za mbu kwa upande wa ndani ya bwawa kwa ajili ya kutolea maji, na bomba hili huzibwa lisitoe maji ila pale inapohitajika kupunguza maji.

MDAU AKICHIMBA BWAWA LA SAMAKI



Baada ya bwawa kukamilika kuchimbwa jaza maji mpaka juu ili kuangalia kama yanatuama na kama kuna kingo zinavuja, kisha weka chakula cha samaki ambacho ni mbolea ya samadi mchanganyiko ya kuku na ng’ombe kwa kipimo cha sehemu tatu za ng’ombe kwa moja ya kuku. Kwa bwawa lenye ukubwa wa ekari moja (70m*70m) kilo 80 za mchanganyiko huu huitajika kila siku, acha chakula kikae kwa siku 3 ndio uweze kuingiza samaki wako. Unaweza pia kuwalisha mabaki ya vyakula, pumba na mboga mboga, Lisha samaki wako kwa siku 6 na siku ya 7 usiwalishe , punguza maji robo na kujaza mengine. Bwawa lenye ukubwa wa ekari moja linaweza kuchukua samaki aina ya tilapia 2800-3000 ambao watakuwa tayari kuvunwa baada ya siku 90 – 120. Nivizuri kutumia samaki waliokwisha zalishwa sehemu /pembeni kwa sababu, ukiwaweka ili wazaliane wenyewe itachukua muda mrefu kuvuna kwa sababu samaki wakubwa wanatabia ya kula mayai na samaki wadogo. Kwa maelezo jinsi ya kutagisha samaki nitaanda makala inayojitegemea.

UJENZI WA MABWAWA YA KUDUMU



Uvunaji wa samaki hufanywa kwa kutoa maji yote katika bwawa na kuvuna samaki kwa ajili ya kuuza au kitoweo, baada ya kuvuna samaki wote bwawa limwagiwe chokaa, hii husaidia kuua vijidudu na kuzuia magonjwa kabla hujaingiza samaki wapya.
Adui mkubwa wa samaki wako ni vyura na baadhi ya ndege ambao hula samaki, pia kuna wanyama kama fisi maji ambao nao pia hula samaki, jinsi ya kujikinga na vyura ni kwa kuwaua kwa mkono na kuharibu mayai yao, ndege na wanyama unaweza kuwazui kwa kuweka uzio wa nyavu pande zote na juu.

BAADHI YA NDEGE WALAO SAMAKI

Wednesday, May 13, 2009

UFUGAJI WA SAMAKI WA CHAKULA KWENYE BWAWA-SEHEMU YA KWANZA

BWAWA LA KUCHIMBA KWA AJILI YA SAMAKI WA CHAKULA


Ufugaji wa samaki ni kama ufugaji mwingine wowote wa wanyama, kwa sababu wanahitaji uangalizi kama wanyama wengine mfano vitu kama kula, usafi, tiba na mengineyo yote yanahitajika kwa ajili ya ufugaji wa samaki

VITU MUHIMU
Baada ya kuamua kufuga samaki ili kuchagua sehemu ya kufugia ni lazima uzingatie mambo yafuatayo
(a)MAJI- Ufugaji wa samaki unahitaji maji mengi ya kutosha kwa hiyo sehemu ya kufugia lazima iwe na chanzo cha uhakika cha maji kwa mwak a mzima, vyanzo kama ziwa, bwawa, mto, kisima ni vyanzo vizuri sana lakini maji ya bomba hayawezi kutumika moja kwa moja kwa sababu huwa yanatiwa dawa ya chlorine ambayo huua samaki. Ukitaka kutumia maji ya bomba ni lazima uyakinge kwanza sehemu kama kwenye matanki yakikaa kwa masaa kama 12 chlorine huondoka. Tatizo la maji ya mto, ziwa na bwawa ni maambukizi ya magonjwa kwa samaki.

BWAWA LA ASILI


(b)UDONGO- Sehemu utakayochagua kwa ajili ya bwawa lako la samaki lazima iwe na udongo unaotuamisha maji ili kuzuia upotevu wa maji na kupunguza gharama za uendeshaji, unaweza pia kujenga kwa simenti

(c)MAFURIKO-Sehemu ya bwawa isiwe ambayo inaweza kupatwa na mafuriko kila msimu wa mvua sababu samaki wataondoka na mafuriko, pia magonjwa na kemikali zisizohitajika zitaingia bwawani na kuua samaki wako

BWAWA LILOJENGWA KWA AJILI YA SAMAKI WA UREMBO


(d)JOTORIDI-Ni muhumu kujua aina ya samaki unaotaka kufuga kama wataweza kuishi kulingana na kiasi cha joto cha sehemu husika.

(e) MIPANGO YA BAADAE- Seehemu husika lazima iendane na mipango ya baadae hasa kama unampango wa kutanua ufugaji wako, ni muhimu mradi uwe sehemu moja kupunguza gharama za usimamizi

MFANO WA BWAWA LILOJENGWA KWA AJILI YA UZALISHAJI WA SAMAKI WA CHAKULA

Monday, May 11, 2009

MGENI NO 2 - NA JIWE LINALOISHI

Leo asubuhi nilikuwa na mgeni mwingine ambaye ni mfugaji wa samaki anayeanza/mwanafunzi , alikuwa amekuja nyumbani kwangu kunitembelea na kujifunza. Kwangu pia ilikuwa ni bahati kwa sababu ilikuwa ni siku ya kufanyia usafi wa jumla chombo cha kufugia samaki (aquarium), nilimwomba anisaidie kwa sababu ki ukweli chombo ni kikubwa kiasi maana inachukua lita za maji 220 sawa na ndoo 11 za lita 20 zilizojaa.

JIWE LENYEWE



Kazi ilianza kwa kupunguza maji kwa kutumia kinyonyeo (syphone) na kwenda kuyamwaga maji kwenye maua, ikifuatiwa na kutoa urembo wote wa ndani pamoja na majani, sasa kuna mawe matatu ambayo nilipoyatoa sikuyaweka mahali pakavu na kuyasafisha kama urembo mwingine bali nilichota kiasi cha maji tuliyoyatoa na kuyaweka kwenye chombo kingine na kuweka mawe haya. Mgeni wangu akaniuliza kwanini hayo mawe siyasafishi, nikamjibu haya mawe yanaishi jamaa akashangaa na mimi ikanibidi nianze kumfafanulia maana yake.


MAWE YANAYOISHI YAKIHIFADHIWA KWENYE MAJI(PEMBENI) USAFI UKIENDELEA KWENYE CHOMBO KIKUU




Kwa chombo ambacho ndio kwa mara ya kwanza kinatumika kufugia samaki, inashauriwa yale maji uliyochukulia samaki toka kule uliko wanunua yawe ni kutoka katika chombo chenye samaki na yasiwe yametoka bombani moja kwa moja. Katika kanuni za usafishaji chombo cha samaki, unatakiwa usisafishe filter zaidi ya cheke cheke lake ambalo ndilo huchuja uchafu, nia na madhumuni kwa yote mawili ni kuhakikisha kwamba ule mfumo wa bakteria muhimu ndani ya chombo chako unakuwepo na haufi kabisa hata baada ya kufanya usafi wa jumla na kuweka maji mapya.


CHOMBO MARA BAADA YA USAFI KABLA YA KURUDISHIWA MAWE, UREMBO MWINGINE NA MFUNIKO WA JUU WENYE TAA NA WATER PUMP




Kwa kuzingatia hayo mimi niliamua kutumia mawe haya ambayo yanapatika kwenye mito hapa nchini, kila ninaposafisha na kuondoa maji yote kwenye chombo cha samaki. Mawe haya yana nafasi za matundu mengi yanayoruhusu maji kujaa ndani ya jiwe hili, kwa hiyo mfumo wa bakteria muhimu nao huwa ndani na ndio maana nikaliita jiwe linaloishi . Faida ya mawe haya ni kwamba yakuwa na mazingira ya kujificha na giza ndani yake kwa hiyo kufaa zaidi kama makazi ya bakteria hawa muhimu na huwa nayaweka ule upande wa pili ambao hauna filter. Ikumbukwe kwamba upande wenye filter ndio upande unaowekwa chakula kwa hiyo kuwa na vinyesi vingi na mabaki mengi ya chakula na kuwa na mazingira mazuri zaidi ya bakteria kuishi, sasa ili kufanya mazingira yawe sawa basi mimi niliamua kuweka mawe haya upande wa pili.


JIWE NDANI YA CHOMBO KAMA LINAONEKANA CHINI YA SAMAKI MWEKUNDU




Kama unafuga samaki aina ya CAT FISH ambao hula utando na ukungu ndani ya chombo chako mara zote hupenda kukaa upande wa filter na wakati mwingine kunata kwenye filter yenyewe kwa sababu ndipo kwenye ukungu mwingi uletwao na bakteria, sasa ukiweka mawe haya upande wa pili utaona kwamba cat fish wako wanatembea pande zote za chombo chako na hapo utaona umuhimu wa jiwe linaloishi.


CHOMBO CHA SAMAKI BAADA YA USAFI KUKAMILIKA FILTER IKO PEMBENI KUSHOTO NA MAWE YAPO CHINI KULIA

Friday, May 8, 2009

MGENI

Jana nilipata mgeni ambaye ameomba jina lake nilifiche, mgeni huyu aliomba tukatembelee shamba langu dogo la miti ya mitiki lililopo Kiluvya umbali wa kama km 30 kutoka jijini Dar es salaam. Shamba hili dogo (la mfano) lina ukubwa wa ekari mbili ambazo ziko bondeni, ni bonde lenye rutuba sana na sehemu ya bonde hili hutuamisha maji wakati wa mvua nyingi.

MGENI WANGU

CHINI YA MITIKI KUNA MPUNGA, HII NDIYO SEHEMU INAYOTUAMA MAJI NA HAINA MITI MINGI

Eneo la shamba hili kama likipandwa lote linauwezo wa kuchukua miti 1000 ila kwa sababu sehemu ya bonde hutuamisha maji basi kuna miti 800 tu, kwa sababu mitiki haiwezi kuota sehemu yenye kutuama maji (rejea makala zangu za mwanzo) Msimu huu wakati mvua zitakapokuwa zinaishia na bonde halituamishi maji, nitajaribu kurudishia hiyo miti 200 iliyobaki ili nione kama itashika, kwa sababu nina imani kama itashika mpaka mvua zijazo hata kama maji yatatuama haitakufa.

CHINI YA MITIKI KUMEPANDWA MIHOGO



Huyu mgeni wangu ni mkulima ambaye ana shamba lake kiasi cha ekari 50 sehemu za vigwaza unaingia ndani kulia kuufuata mto Ruvu. Hili shamba lake ni jipya na anategemea kuanza kupanda miti ya mitiki wakati wa mvua zamwezi wa 11, kwa sasa hivi anaanda shamba lake kwa kukata miti michache iliyopo pamoja na kulima vichaka na majani

CHINI YA MITIKI KUMEPANDWA MAHINDI


Ameniambia ataanza na ekari kumi kwa msimu wa kwanza kwa hiyo anahitaji kiasi cha miche 5000, kwa hiyo nina kibarua cha kuanza kuandaa kitalu cha kuoteshea mbegu hizo. Kitalu changu nitakiandaa kule kluvya kwa sababu ya urahisi wa kupitia miche wakati wa kupanda, yaani unangoa miche na kwenda kuipanda siku hiyo hiyo, nilimwomba tukatembelee shamba hilo ili niweze kujua vitu kama udongo unarutuba kiasi gani na je unatuamisha maji au la na kwa kaisi gani? Pili kujua kiasi cha mvua cha eneo husika kwa kuangalia uoto wa asili. Pia alikuwa anataka kujua kama anaweza kuchimba kisima cha asili na kukilinda kwa miti ya mikuyu.

Tuesday, May 5, 2009

LEUCAENA - VIBIRITI




Huu ni aina ya mti ambao unaweza kuukuta umeota mingi mingi pamoja kama kichaka au mmoja mmoja na kuwa mti mkubwa kabisa. Unastawi zaid sehemu za joto na kukua haraka, kwenye baridi ukuaji wake si wa haraka sana kama sehemu za joto, una mbegu nyingi sana zikiwa kwenye maganda mengi pia,
Upandaji wake ni kwa kukusanya mbegu zilizo komaa na kukauka na kisha kuzi mwaga sehemu unayotaka ziote kisha kuzifukia kwa udongo kiasi kidogo sana, upandaji ufanyike mara baada ya mvua za kwanza kuanza

MATUMIZI
(A)Mmea hu una protini nyingi sana kwenye majani yake kiasi cha asilimia 25%, kwa hiyo unafaa kwa ajili ya chakula cha mifugo kama ng’ombe, mbuzi, nguruwe na kuku. Unachanganya majani yake (makavu au mabichi) katika mlo wa wanyama. Kiasi cha lukina kisizidi asilimia 30% ya mlo kwa sababu kinaweza kusababisha wanyama kunyonyoka manyoya baada ya miezi 6 na pia kupata ugonjwa goita (goiter)



Kwa wafugaji wa nguruwe unaweza kutumia lukina 30% majani ya kawaida 70% na udongo mwekundu kama chanzo cha madini ya chuma kutengeneza mlo kamili kwa ajili ya nguruwe wako, inashauriwa pia kuwapa pig mix ili kuepukana na upungufu wa madini mengine.
Kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa changanya pumba 60% na lukina 40% na cattle mix kisha uwalishe kama chakula cha ziada chenye virutubisho(concentrates) wakati wa kukamua ng’ombe maziwa. Kwenye mlo kamili kumbuka lukina isizidi kiasi cha 30%
Pamoja na kuwa na madini mengine lakini mmea huu una kirutubisho kinachojulikana kama carotene ambacho husababisha wanyama wanaokula lukina kuwa na provitamin A nyingi sana kwenye nyama baada ya kuchinjwa. UVunaji wake ni kwakupunguza matawi na kama unahitaji kuhifadhi basi unakausha kwenye kivuli na majani yakipukutika unayakusanya na kuyatunza mahali pakavu.




(B) Lukina pia inaweza kutumika kwa ajili ya kuongeza kiasi cha nitrogen kwenye udongo kwa kupanda kati ya mimea au kwa wale wanaotumia kontua kwenye miteremko wakatumia kontua za lukina kwa kukinga mmong’onyoko wa udongo lakini isiache kukua na kuwa miti mikubwa labda kwa wale wanaohitaji kukinga upepo tu.



(C)Miti hii pia inaweza kutumika kwa ajili ya sehemu zilizokumbwa na balaa la kupoteza uoto juu ya ardhi, sababu kubwa ni ukuaji wake wa haraka na ikipandwa sehemu hata kama ni michache husambaa haraka kwa sababu inazalisha mbegu nyingi sana na zinasambaa kwa upepo ingawa haziendi mbali zaidi