KURASA

Thursday, November 18, 2010

KILIMO BORA CHA MAEMBE




Maembe hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Tabora, Pwani, Mtwara, Tanga, Mwanza, Morogoro na Mbeya. Uzalishaji wake ni wastani wa tani 159,472 kwa mwaka. Maembe ni zao muhimu la biashara na chakula.

MAMBO YA KUZINGATIA WAKATI WA UZALISHAJI
Ili kupata mazao bora ni muhimu kuzingatia kanuni bora za kilimo cha maembe hasa kanuni
zifuatazo:
Kuchagua aina bora ya kupanda kulingana na mahitaji ya soko.
Panda umbali wa mita 10 kwa kumi kama utatumia miembe ya kuunga, hii ni kwa sababu haiwi mikubwa sana kwa sababu haiishi miaka mingi, kwa ile ambayo si ya kuunga panda umbali wa mita 15 kwa 15 kwa kila mti mmoja wa muembe

DHIBITI MAGONJWA, WADUDU, NA MAGUGU

• Fanya ukaguzi wa shamba mara kwa mara ili uweze kudhibiti wadudu na magonjwa ya matunda kabla madhara hayajawa makubwa

UGONJWA WA KUTU KWENYE MAJANI



• Ni muhimu kudhibiti wadudu, magonjwa na magugu ili kupata mazao bora ambayo yatapata soko zuri na kuweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu.
• Hakikisha shamba ni safi wakati wote ili kupata matunda bora na kurahisisha uvunaji.

MAANDALIZI KABLA YA KUVUNA

Kusafisha shamba pamoja na barabara za shamba
• Safisha shamba ili kurahisisha uvunaji na usafirishaji shambani.
Kukagua shamba kuona maembe kama yamekomaa Maembe hukomaa katika kipindi cha miezi 4 hadi-6 tangu kutoa maua kutegemea hali ya hewa na aina.

DALILI ZA MAEMBE YALIYOKOMAA

• Maembe hung’ara
• Kwa aina nyingine rangi ya kijani hufifia na kuanza kubadilika kuwa ya manjano.

ANDAA VIFAA VYA KUBEBEA, SEHEMU YA KUFUNGASHIA NA USAFIRI.


VIFAA VYA KUBEBEA
• Ngazi
• Vikapu
• Mifuko
• Ndoo
• Vichumio

VIFAA VYA KUFUNGASHIA
• Makasha ya mbao/plastiki na ya makaratasi magumu na matenga

VYOMBO VYA KUSAFIRISHIA
• Matoroli
• Magari
• Baiskeli
• Matela ya matrekta

KUVUNA
Njia bora ya kuvuna maembe ni Kuchuma kwa mkono
• Kwa miembe mifupi chuma maembe pamoja na kikonyo chake
• Kwa miembe mirefu chuma kwa kutumia kichumio maalumu

KICHUMIO MAALUM


• Acha kikonyo chenye urefu wa sentimita tatu hadi nne ili kuzuia madoa ya utomvu. Utomvu huchafua matunda na hushusha ubora. Pia embe lililovunwa bila kikonyo chake huingiliwa na vimelea vya ugonjwa kwa urahisi.
• Vuna wakati wa asubuhi au jioni ili kuepuka jua kali linaloweza kubabua matunda.
• Wakati wa kuvuna hakikisha maembe hayadondoshwi chini, ili kuepuka kuchubuka kwa matunda ama kupondeka hasa yale yaliyoiva barabara. Aidha beba matunda kwa vikapu au mifuko na kusanya kwenye kivuli.



KUCHAMBUA MAEMBE
Kuchambua ni kutenga matunda yaliyooza, kupasuka, yenye dalili za magonjwa au kubonyea, ili kupata matunda yenye ubora kwa ajili ya matumizi, kusindika au kuuza.
• Matunda yaliyooza na yenye wadudu ni vyema yafukiwe ili kuzuia kuenea kwa wadudu waharibifu na vimelea vya magonjwa.
• Matunda yaliyopasuka, kubonyea , kuchubuka kidogo wakati wa kuvuna au kuiva sana yatumike haraka kwa chakula.
• Matunda mazuri ambayo hayajapata madhara yoyote yatunzwe kwa ajili ya kusindikwa, kutumika au kuuzwa.

KUSAFISHA MAEMBE
• Baada ya kuchambua, safisha matunda kwa maji safi ili kuondoa uchafu na mabaki ya madawa.
• Maembe yanayokusudiwa kuuzwa nje ya nchi hunyunyiziwa nta ili kuzuia kunyauka na kudumisha ubora.
• Baada ya kusafisha tumbukiza maembe kwenye maji yenye nyuzi joto zipatazo 52 za Sentigredi kwa muda wa dakika tano. Maji haya pia yanaweza kuchanganywa na madawa ya klorini asilimia 1 ili kuzuia magonjwa ya ukungu.

KUPANGA MADARAJA
Madaraja hupangwa kwa lengo la kurahisisha ufungashaji, usafirishaji na uuzaji. Madaraja hupangwa kulingana na ubora, ukubwa , aina rangi na uivaji.


KUFUNGASHA MAEMBE

Ufungashaji hufanyika katika sehemu safi na yenye kivuli. Ufungashaji wa kujaza kupita kiasi husababisha upotevu wa maembe. Aidha ubora hushuka kutokana na kuminyana na kubonyea kwa matunda wakati wa kusafirisha

TENGA LA KUFUNGASHIA MAEMBE



Inashauriwa kufungasha kwenye makasha ya mbao/ plastiki , makaratasi magumu au tenga kwa sababu zifuatazo:
• Matunda yanaweza kupangwa na kusafirishwa bila kuchubuka, kubonyea au kupasuka.
• Huweza kupakiwa na kupakuliwa kwenye chombo cha usafiri kwa urahisi.

Wakati wa ufungashaji ni muhimu kuzingatia yafuatayo:
• Kasha moja lisizidi uzito wa kilo 20 ili kurahisisha ubebaji.
• Makasha yawe imara na yenye matundu ya kutosha ili kuruhusu mzunguko wa hewa.
• Ni muhimu kutanguliza vitu vilivyo safi ndani ya vifungashio ili kuzuia michubuko na mipasuko ya matunda wakati wa kusafirisha.
• Maembe yapangwe kwa kubananisha na kwa kuhakikisha kuwa vikonyo havitoboi matunda na kusababisha majeraha wakati wa kusafirisha. Kubananisha matunda husaidia kuzuia mgongano unaoweza kusababisha matunda kusambaratika na hivyo kubonyea au kupasuka wakati wa kusafirisha.

KUSAFIRISHA

Ili kuepuka upotevu na uharibifu wakati wa kusafirisha, ni muhimu maembe yapangwe kwenye vyombo vya kufungashia na kusafirisha kwa uangalifu, ndani ya matela, mikokoteni na magari. Epuka kutupa matunda wakati wa kupakia na kupakua. Wakati wa kupanga mazao katika vyombo vya usafiri yasirundikwe ovyo na yasijazwe kupita kiasi ili yasimwagike. Vilevile yafunikwe ili yasipigwe na jua. Jua huongeza kasi ya kuoza. Matunda yakipigwa na jua kwa muda wa saa mbili mfululizo husababisha kuoza kwa asilimia 100.

KUHIFADHI

• Maembe huweza kuhifadhiwa kwenye chumba chenye hali ya hewa yenye joto la nyuzi 8 hadi 10 za Sentigredi na unyevu wa asilimia 85 hadi 90. Katika hali hiyo, maembe yanaweza kuhifadhiwa bila kuharibika kwa mwezi mmoja.
• Kagua mara kwa mara ili kugundua uharibifu unaoweza kutokea

13 comments:

Nayma said...

Ahsante kaka bennet juzi nilikuwa navuna maembe yangu shambani lakini sikuwa na elimu hii nzuri nimepita hapa nimejifunza namna ya matayarisho na uvunaji mzuri naamini mwaka ujao nitaafuata taratibu zote ili niweze kupata maembe bora. Nina miembe dodo ambayo nashindwa kuiweka vizuri ili nipate maembe bora mengi yanakuwa na wadudu yaani mabovu yanapoiva hivyo wakanambia niwe nayachuma kabla hayajaiva ingawa yamekomaa. Kuna baadhi ya miembe imepata huo ugonjwa wa kutu na matokeo yake umepukutisha maua mengi na kusababisha mipate maembe machache kinyume na nilivyozoea. Nashukuru sana kwa elimu ya bure uliyonipa mungu atakulipa.

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Bennet ahsante sana kwa darasa hili halafu hicho kichumia nimekipenda kwani watu huwa wanaumia kweli kukwea mitini kutafuta maembe. Ahsante...

Anonymous said...

Kwa miembe ya kisasa ya miaka miwili na nusu au mitatu, kwa wastani inatoa kiasi gani cha maembe kwa msimu? Kwenye kupanda, umbali gani unashauriwa? Unaweza kupanda miti mingine kati ya mwembe na mwembe? Inadumu kwa miaka mingapi? Asante Bennet.

Bennet said...

Dada Nayma we ni mkulima kweli mpaka naanza kukuogopa maana kila zao wewe umepanda, hongera sana ngoja nikuandalie makala kuhusu magonjwa ya miembe hasa huu ugonjwa wa kutu

Dada yasinta karibu sana, hiki kichumio ni rahisi sana kutengeneza, unaweza jaribu

Anony upandaji wa meiembe ni wastani wa mita 20 kwa ishirini au unaweza kuongeza moja au mbili kwa ajili ya barabara miti itakapokuwa mikubwa sana kwa miembe ya miaka mitano uzao wa wastani ni kama kilo 50 kujua ni maembe mangapi inategemea na ukubwa wa maembe kutegemeana na aina mfano kama ni dodo au apple mango lazima maembe yawe machache

Anonymous said...

Kaka Bennet naomba namba yako ya simu niwasiliane na wewe kuna mengi ya kuzungumza ikibidi tuonane kabisa

Nayma said...

Najifunza kutoka kwako kaka Bennet, Nitashukuru sana ukiweka makala hiyo pia.

Unknown said...

Habari,
Nashukuru wakati umefika walau watanzania tunaweza kutumia teknologia kwa kujifunza,
Nimefurahishwa na maelezo kuhusiana na kilimo cha maembe na sababu kubwa iliyonisukuma kutafuta maelezo ni muamko ambao nataka kuwa nao katika kilimo ambacho tunasema ni uti wa mgongo.
Nimefurahishwa na maelezo na ningependa kujua zaidi kuhusiana na kilimo cha matunda kwa ujumla.
basi sitasita kuuliza maswali na kupata maelekezo.

joyce m, said...

asante sana kwa kutufikishia habari njema ya kilimo cha embe, nina shamba nataka kupanda embe 100 naomba masaada wa kitaalam, cmu ni 0756624989

joyce m

Nayma said...

Piga hii +255222126118 Amagro.
(About Amagro)Associate of Mango Grower.

mwanambunga said...

Asante kaka Bannet kwa uelimishaji uma juu ya kilimo cha miembe.

Naomba tufafanulie zaidi juu ya ukubwa wa shimo la kupanda muembe, Kiasi cha mbolea (kama kinahitajika) na msimu mzuri wa kupanda miembe ni upi!!!!

Thanks!!

Sylvester said...

Habari, Nini tiba ya ugonjwa wa kutu ya majani?



































Unknown said...

asante kwa elimu

Unknown said...

Asante kwa elimu maridhawa