KURASA

Monday, September 27, 2010

SIKU YA KICHAA CHA MBWA DUNIANI

Kila mwaka tarehe 28 ya mwezi wa tisa (september) ni siku ya kichaa cha mbwa duniani, hapa nchini serekali katika kampeni ya siku hii maalum imetoa kiasi cha chanjo 100,000 bure kwa mafugaji mbwa katika mikoa ta Dar es salaam, Mtwara, Lindi na Pemba

kutokana na takwimu za wizara ya mifugo na uvuvi inaonyesha mwaka jana watu 21,000 walingatwa na mbwa nchini Tanzania. Kati ya hao watu 51 walifariki dunia kwa sababu ya kichaa cha mbwa.

Ingawa kwa kiswahili ugonjwa huu unaitwa kichaa cha mbwa, lakini ukweli hushambulia hata wanyama wengine kama paka, ng'ombe, mbuzi, kondoo na hata binadamu, Ugonjwa huu kwa wanyama hauna dawa ila kinga tu kwanjia ya chanjo

Kuuelewa zaidi ugonjwa huu soma hapa
http://mitiki.blogspot.com/2009/08/kichaa-cha-mbwa.html

Thursday, September 23, 2010

DADA NAYMA ANAOMBA USHAURI ZAIDI

Hello Bro Bennet. Angalia miche yangu hatua iliyofikia bado sijaipeleka shambani,
naomba ushauri zaidi niliiotesha mwezi wa tano mwezi wa saba nikaiweka kwenye mifuko miche 300 tu.
nayma





Dada Nayma leo naomba nikuweke hadharani, wadau huyu dada nimekuwa nikimshauri kuanzia kuandaa mbegu, kitalu, kusia mbegu, umwagiliaji, kuhamisha mbegu kutoka kwenye kitalu hadi kwenye vipakti

Dada Nayma miche yako bado ni michanga kiasi, na kama unafuatilia utabiri wa mvua za msimu wa September mpaka November ni kwamba hakutakuwa na mvua za kutosha ila kwa mikoa ya kanda ya ziwa na zaidi Bukoba, nakushauri endelea kumwagilia miche yako ikue zaidi huku ukisubiri mvua za mwezi wa December mwishoni na January 2011, hapo itakuwa mikubwa ya kuweza kuhimili kama mvua zitakuwa chache

NB Hongera sana na anza kuandaa mbegu nyingine ili mwezi wa January uwe na miche mingi zaidi

KILA KAZI NA HATARI ZAKE

Leo nilikuwa nimekwenda kutibu mbwa 9 katika kampuni ya usafirishaji ijulikanayo kama Ruvuvu transport huko kurasini, mbwa hao walikuwa wanasumbuliwa na ugonjwa wa minyoo ya kwenye ngozi ujulikanao kama MANGE, ugonjwa huu husambazwa na viroboto wa mbwa


HAPA MBWA ANAANDALIWA



KUCHOMA SINDANO MBWA

Friday, September 17, 2010

SHARK - MKEMIA WA MAJI

Leo nilikuwa nabadili maji kwenye chombo cha kufugia samaki wa urembo (aquarium)baada ya kuweka maji masafi na kuwarudisha samaki wangu kuna kitu nikakigundua. Pamoja ya kwamba samaki wote ni wa urembo lakini kila mmoja anatabia yake, ni samaki wawili aina ya shark ambao wanauwezo wa kutambua maji kama yana kitu chochote kibaya, kwa mfano kama kemikali yoyote, chumvi au madini yoyote yale zaidi ya kiwango cha kawaida. Mara tu utakapowaweka kwenye maji ambayo hayako sawa basi utawaona wanakaa chini tu na wala hawaogelei kama kawaida yao.

Wakati narudishia mawe kwenye chombo chao yalisuguana na chenga chenga zake zikabadili ubora wa maji, ingawa hayakuwa na tatizo lolote kiafya lakini samaki hawa aina ya shark waliweza kugundua hilo na walikaa kama wanavyoonekana hapa kwenye picha mmoja aligeuka juu chini kama vile kafa.







Baada ya kuona wako hivo nikawasha pampu ya kuongeza hewa kwenye maji pamoja na filter baada ya dakika kama 10 samaki hao wakaanza kuogelea kama kawaida, angalia video hii


Hawa hapa kwenye video ni goldfish aina ya shubunkin, redcap na goldspike


Angel fish ni aina nyingine ya samaki nilionao


Huyu anajulikana kama catfish, nayeye kazi yake kubwa ni kisafisha vioo na urembo wa ndani, anauwezo pia wa kumla samaki yoyote aliyekufa bila ya wewe kuanza kuhangaika kumtoa

Saturday, August 21, 2010

KILIMO BORA CHA MAHINDI

Mahindi ni chakula muhimu na ni aina ya nafaka katika mataifa ya Afrika yaliyomo kusini mwa jangwa la Sahara. Ni chakula cha matumizi ya nyumbani kwa idadi ya watu inayokadiriwa kuwa asilimia 50. Ni chanzo muhimu cha madini na kuongeza nguvu mwilini, protini, madini ya chuma (iron) vitamini na madini mengine asilia.Waafrika hutumia mahindi kwa njia mbalimbali – (uji, ugali na pombe). Na mahindi ya kuchoma. Kila sehemu ya mmea wa mahindi ina thamani kiuchumi : punje, majani, shina na magunzi huweza kutoa kiasi kikubwa cha bidhaa nyinginezo zilizo chakula na zisizokuwa chakula.

Vile vile mahindi ni chakula muhimu cha mifugo (ng’ombe) na huhifadiwa kama silage. Pia mabaki ya mimea na nafaka na pia hutumika viwandani kutengeneza wanga na mafuta.
Mahitaji ya mahindi katika hali ya hewa, udongo na Mahindi ni mimea ambayo hustahimili mabadiliko mengi ya hali ya hewa na humea katika maeneo mengi tofauti. Kuna aina nyingi za mahindi yanayotofautiana katika muda wa kukomaa, mahindi huwa na ustahimili mkubwa kwa mabadiliko katika kiwango cha joto. Mahindi haswa huwa mimea ya maeneo ya joto ambako unyevu ni wa kutosha. Mmea huu unahitaji kiwango cha joto cha kila siku cha nyuzi joto 20º ili umee vyema. Joto la juu sana kwa mazao mazuri ni kama nyuzi joto 30º. Hupandwa sana katika sehemu zilizo katika kimo cha mita 3000 kutoka bahari hadi kwenye ukanda wa pwani. mahindi yaweza kupandwa kama chakula cha mifugo.

SHAMBA LANGU NI SHAMBA DARASA


Mahindi huwa yanaathirika na ukosefu wa unyevu wakati wa kutoa maua na matunda. Pia yanahitaji maji ya kutosha wakati wa kupanda. Katika nchi za joto jingi (tropiki), mahindi hufanya vyema katika mvua ya kiwango cha milimita 600 hadi 900 wakati wa kukua. Mahindi yanaweza kukuzwa kwenye aina nyingi za udongo lakini hukua vyema zaidi katika mchanga, usiotuamisha maji mengi, ulio na hewa ya kutosha na ulio na rutuba na madini ya kutosha. Kuwepo kwa mazao mengi ya mahindi kunapelekea kunyonywa sana kwa madini kwenye udongo. Mahindi yaweza kukuzwa katika udongo ulio na hali ya mchanga na (PH) kutoka 5 hadi 8 ingawa 5.5 hadi 7 ndio mwafaka. Mahindi yako katika kikundi cha mimea kinachoaminika kuathirika na hali ya chumvi katika maji na udongo. Kwa vile mimea ambayo ni michanga huwacha sehemu kubwa bila kuzingirwa na ardhi, mmomonyko wa udongo na kupoteza maji hutokea sana sana hivyo basi ni bora umakini uzingatiwe katika uhifadhi wa udongo na maji kwa kuweka matandazo (mulching).

MATUMIZI YA MBOLEA
Mahindi hustawi zaidi yakiwekwa mbolea, iwapo mambo mengine yanayosaidia katika kukua pia yapo kwa kiwango kinachostahili. Mbolea inayotumiwa na wakulima wadogo mara yingi huwa haitoshi. Mahindi ya kiwango cha juu yaweza tu kufikia kiwango cha juu cha Uzalishaji iwapo yatapewa lishe na madini ya kutosha. Mahindi ya tani 2 kwa hekta na tani 5 kwa hekta hutumia karibu kilo 60 N, kilo 10 za P205 na kilo 70 K20 kutoka katika udongo. MAhindi hunyonya Nitrogen pole pole katika miezi ya kwanza baada ya kupanda, lakini huongezeka hadi kiwango cha juu kabisa wakati wa kutoa maua na kukuza tunda (gunzi). Mahindi huhitaji nitrogen kwa kiwango cha juu na ukosefu huwa ndio kizingiti. Kiwango cha juu cha nitrogen kinahitajika mara tatu; kwanza wakati wa kupanda, pili, wakati ambapo mmea umefikia sentimita 50 za urefu na tatu, wakati matunda ya mahindi yanaanza kutoa zile nyuzi nyuzi nyororo (silking).

Udongo mwingi huwa na madini ya phosphorous (P205) na potassium (K20) lakini sio kiwango kinachotosheleza mahitaji haswa ya mbegu za mahindi zinapochipua. Nyunyuzia P205 karibu na mbegu ili ziote kwa haraka. K20 hutumika kwa kiwango kikubwa lakini hitaji la mimea hubainika baada ya upimaji wa hali ya udongo kujua kiasi cha mahitaji (soil test).

DALILI ZA UPUNGUFU WA MBOLEA
Ukosefu wa K20 husababisha ncha za majani kuwa na rangi ya njano na kuunda gunzi (cob) lisilo na punje hadi juu. Ukosefu wa P205 hufanya matawi kuwa na rangi ya samawati na mbegu zisizo laini. Dalili za ukosefu wa nitrogen ni majani ya rangi ya manjano na mimea dhaifu mifupi. Phosphate haifyonzwi haraka na mahindi na pia udongo mwingi wa nchi za joto hukosa madini hayo ya phosphate. Inashauriwa unyunyuzie mbolea ya kiasili kama samadi kabla ya kulima ili uboreshe hali ya udongo na kuongezea madini.

Katika ukulima wa kiasili, (organic farming, Nitrogen (N) hutiwa kwenye udongo kupitia kwa upandaji wa mimea ya jamii ya mikunde (legumes) ambayo hutoa nitrogen katika hewa, Hata hivyo mapendekezo ya kimbolea yaliyo katika misingi ya uchunguzi wa udongo hutoa nafasi nzuri ya kupata kiasi kizuri cha mbolea bila kuweka kiwango cha chini au juu. Omba msaada kutoka kwa mafisa ugani wa kilimo waliyo katika eneo lako.
Katika maeneo yanayo tegemea mvua kukuza mahindi, panda mbegu wakati wa mvua ya kwanza. Hii itaruhusu mizizi kunyonya madini yaliyotengenzwa na bakteria katika udongo. Maji yaliyosimama huyeyusha na kuondoa madini ya nitrogen kutoka katika udongo na kusababisha ukosefu wa Nitrogen.


KUDHIBITI MAGUGU
Udhibiti wa magugu ni muhimu sana. Katika wiki 4 hadi 6 za mbele baada ya kumea, mahindi huathiriwa sana na magugu. Ni lazima mahindi yapandwe mara moja baada ya kutayarisha shamba. Unaweza kulima katikati ya laini za mahindi ili udhibiti magugu. Nchini Tanzania, kupalilia mara mbili kunahitajika kwa aina nyingi za mahindi, ingawa kupalilia kwa mara ya tatu kutahitajika kwa aina ambazo zinahitaji miezi 6 hadi 8 kukomaa. Kupalilia kwa mikono kunahitaji siku 15 kwa hekta la mikono (power tiller) ni masaa mawili mpaka matatu kwa ekari.

UHUSIANO WA NIPE NIKUPE
Desmodium (desmodium uncinatum) nyasi ya Molasses (melinis minutifolia) zikipandwa kati kati ya laini za mahindi huzuia wadudu kama stalk borers moths. Mimea hii hutoa kemikali ambazo huwafukuza wadudu aina stem borers’ moths. Zaidi ya hayo Desmodium huzui gugu haribifu,witchweed striga hermonthica. Napier grass (pennisetum purpureum) na Sudan grass (sorghum vulgare sodanese) ni mimea mizuri sana inayonasa wadudu aina ya stem borers. Napier grass ina njia yake madhubuti ya kujikinga dhidi ya wadudu wanaotoboa mmea kwa kutoa utomvu kutoka kwenye shina, ambayo huzuia wadudu kufyoza mmea na kusababisha uharibifu. Nyasi hizi pia huvutia adui wa stem borers kama mchwa, earwigs na buibui. Nyasi aina ya Sudan pia husaidia maadui asilia, kama nyigu (parasitic wasp)

MAHINDI TAYARI KWA KUVUNWA



Mahindi huweka kivuli kwenye mimea ya mboga mboga ikipandwa safu moja katikati ya mboga kwenye maeneo yaliyo na jua kali. Hii huongeza mazao ya mboga zilizopandwa hivi. na mimea jamii ya mikunde huongeza nitrogen kwenye udongo ambayo huitajika zaidi katika ukuaji wa mahindi pia hupunguza wadudu aina ya (leafhoppers, leafbeatles, stalk borers na fall army worm), upandaji wa mimea jamii ya mikunde ufanyike mara baada ya palizi ya kwanza


KUPUKUSUA MAHINDI KWA KUTUMIA MASHINE YA MKONO



UVUNAJI
Uvunaji hufanyika kwa kutumia mikono kwa mashamba madogo na mashine (combine harvester) hutumika kwa ajili ya mashamba makubwa, Zao la wastani la mahindi ulimwenguni mnamo mwaka 2000 lilikuwa kilogramu 4255 kwa kila hekta. Zao la wastani nchini Marekani ilikuwa kilo 8600 kila hekta, huku mataifa yaliyo chini ya jangwa la Sahara la Afrika yakivuna kilo 1316 kwa kila hekta ya shamba. Zao la wastani katika taifa la Tanzania kati ya mwaka 2001-2005 lilikuwa kati ya gunia 15-19 kwa hekta (sawa na kilo 1350-1750) Ukilima kwa kuzingatia ukulima wa kisasa na kanuni zake kwa Tanzania utavuna kilo 5000 kwa hecta (ukanda wa pwani) na kilo 7500 kwa nyanda za juu kama Iringa, Mbeya, Ruvuma, Arusha n.k

RUNDO LA MAHINDI BAADA YA KUPUKUSUA

Sunday, August 15, 2010

KILIMO CHA MICHUNGWA NA MACHENZA

Ndugu Ali Kalufya alitaka kujua kwa kina ukuliama wa michungwa na jamii yake, aliuliza swali hili katika mtandao wa Dada Subi nami najaribu kumweleza haya...

Michungwa na Jamii yake hustawi zaidi ukanda wa pwani wenye joto kiasi, mvua nyingi na udongo wenye rutuba, kwa Tanzania mikoa kama Pwani, Dar es salaam, Tanga, Mtwara, Lindi, na Morogoro ni maarufu kwa kilimo hiki

MBEGU
Kwa kuanzia unakusanya mbegu za mlimao kutoka katika malimao yaliyokomaa na ikiwezekana yawe yameiva yakiwa mtini, kausha mbegu zake na kisha unaweza kutolea ganda la nje ili ziweze kuota vizuri.

KITALU
Mwaga mbegu zako kwenye kitali na uzifukie kwa udongo kiasi cha nusu sentimeta, mwagia maji kilasiku na baada ya wiki 3 - 6 mbegu zitaanza kuchipua,

MICHE YA MILIMAO TAYARI KWA KUUNGWA


baada miche kufikia kiasi cha sentimeta 3 - 5, miche ihamishiwe kwenye pakiti zenye udongo wenye mbolea ya kutosha na viwekwe kwenye kivuli kiasi

MICHE YA JAFFER BAADA YA KUUNGWA


KUUNGA MICHE
Miche ikifikia urefu wastani sentimeta 30 - 45 inawezwa kuungwa ikiwa unataka iwe michungwa au michenza, kazi hii inahitaji utaalamu kiasi na unaweza kuomba msaada kutoka kwa maafisa ugani wa Kilimo. Kwa michungwa kuna iana mbili kuu hapa Tanzania ambazo ni Jaffer na Valencia. Jaffer ni rahisi kuunga kwa sababu vikonyo vyake ni vikuwa na viko wazi kwenye miti,miti yake huwa mikubwa na inazaa sana, lakini huathirika sana jua likiwa kali na matun da mengi huanguka, pia machungwa yake hukua na kuiva haraka, soko likiwa baya mengi huishia shambani kwa kuanguka

MTI WA JAFFER


JINSI YA KUUNGA MICHE YA MILIMAO KUWA MICHUNGWA AU MACHENZA


Valencia ni miti ya wastani, vikonyo havipo wazi kwa hiyo huwapa kazi waungaji (hawaipendi) ina uzao wa wastani na inakabili ukame na matunda yake hayaivi haraka, msimu wa machungwa ukiwa katikati wewe ndio unaanza kuvuna na ukisha bado unakuwa na machungwa wakati bei iko juu

MTI WA VALENCIA



UPANDAJI
Baada ya uungaji kukubali unaweza kuandaa shamba lako kwa kuchimba mashimo, kuweka mbolea na kusubiri msimu wa mvua, miche ipandwe mara baada tu ya mvua za kwanza kunyesha, umbali wa kupanda ni mita 8 * 8 kwa jaffer na mita 5 * 8 kwa valencia

KUPALILIA
Miche isafishiwe si chini ya mara 2 - 4 kwa mwaka na miche ikifikisha miaka mitatu unaweza ukasafishia visahani na kufyeka sehemu nyingine

UZAO
Kuanzia miaka mitatu miche itaanza kutoa maua na kuzaa na huchanganya kuzaa baada ya miaka mitano, miche huendelela kuzaa hadi kufikia miaka 25 - 30 tangu kupandwa

WADUDU/MAGONJWA
Magonjwa makuu ni fangasi, miti kunyauka na nzi wa michungwa, dawa kwa ajili ya magonjwa yote haya zinapatikana madukani

CHUNGWA LILILOSHAMBULIWA NA NZI WA MICHUNGWA

Tuesday, July 6, 2010

WAKALA WA MBEGU ZA MITI NA SABA SABA

Kwa wale wanaohitaji mbegu za miti au miche kutoka kwa wakala wa mbegu za miti wa Taifa, mnaweza kuzipata sabasaba kwenye banda la maliasili badala ya kuzifuta mbegu au miche kule morogoro, wana mbegu nyingi na miche ya aina mbali mbali















Friday, June 18, 2010

UFUGAJI BORA WA SUNGURA

UTANGULIZI
Kabla hujaamua kufuga sungura hakikisha ya kwamba umejitoa na una muda wa kuwahudumia wanyama waha, ufugaji wao si rahisi kama vile ukifuga paka au mbwa, sungura wanahitaji uangalizi na hassa kwenye usafi kwa sababu ni rahisi kwao kupata maradhi yatokanayo na mazingira mabaya na machafu

MABANDA
Kuna aina mbili za mabanda ya kufugia kwanza ni yale ya kuwafungia ndani muda wote bila kutoka nje na ya pili ni ile ya pili ni nusu nusu yaani wanakuwa na mabanda na wanaweza kutoka nje kwenye ua maalum, katika aina zote mbili ni muhimu kuhakikisha hakuna upenyo wa kuruhusu panya kupita kwa sababu huwa wanakula watoto wa sungura.



UFUGAJI WA NDANI
1 - Usitumie banda la kioo (aquarium) kwa sababu halina hewa ya kutosha na ni vigumu kusafisha

2 - Sakafu ya nyavu za waya ni nzuri zaidi ila hakikisha hakuna sehemu zenye ncha kali inayoweza kuwaumiza sungura, kwani wakumia ni mpaka wapone wenyewe au umchinje kwa sababu ukitumia dawa za antibiotic sungura hana uwezo wa kuzimeng'enya na kuisha mwilini mwake, siku ukimchinja atabakia na dawa na hata ukinusa nyama yake utahisi harufu ya dawa

3 - Ukubwa wa banda usipungue mita 4 * 2 kwa kila sungura mmoja, likiwa kubwa zaidi ni vizuri

4 - Chini kuwekewe matandazio kama nyasi kavu au maranda ya mbao, lakini maranda yatokanbayo na miti yenye mafuta kama mi-pine na mikaratusi hayafai, wawekee kipande cha blanket au taulo la zamani kwa ajili ya kulalia na kujifungulia hasa kwa wazazi

5 - Ni muhimu kuwawekea sehemu ya kujificha mara wanapohisi hatari, unaweza kutumia mbao, box gumu au plastiki



UFUGAJI WA NJE
1 - Sehemu yote izungushiwe wavu wa kuku kuzuia panya kuingia na wanyama wengine kama paka, mbwa, mwewe nk

2 - Upande mmoja uwe na mabanda, sehemu ya chakula na maji pamoja na kivuli kwa ajili ya sungura kupumzika

3 - Futi moja chini ya udongo kuwe na zege kuzuia sungura kuchimba na kwenda mbali

4 - Eneo la wazi liwe huru na hatari zote za sumu kama dawa za kuulia wadudu au mbolea, pia majani yaliyoota yasiwe ni yale yenye sumu (waone wataalamu wakushauri au ng'oa yote)

MAJI
Tumia mabakuli ya kigae, usiweke vya plastiki maana huvitafuna na kuwaathiri au jengea kwa saruji, maji yabadilishwe kila siku na vyombo visafishwe kila siku

CHAKULA
Wapewe majani makavu kwani muhimu sana kwa ajili ya mfumo wa kumeng'enya chakula, mabaki ya mboga za jikoni baada ya kuchambuliwa, pia unaweza kuwawekea pumba au chakula cha kuku (growers mash) kwenye vyombo maalum kama chakula chenye virutubisho (concentrates) Kiasi cha protini wanachohitaji ni 17%

USAFI

Kila siku jaribu kuondoa uchafu kama vyakula vilivyo mwagika, na kinyesi kilichoganda kwenya matandazio, fagia na kubadili matandazio angalau mara moja kwa wiki, manyoya ya sungura mzazi yasiondolewe hii huonyesha kwamba anakaribia kujifungua watoto



MENO
Wakati mwingine meno ya mbele hukua sana na kumsababishia usumbufu wakati wa kula, waone wataalam ukiona ni marefu zaidi na yanahitaji kupunguzwa, dalili kuu ni sungura kushindwa kula kwa zaidi ya masaa 12

MIGUU
Miguu ya sungura si kama ya wanyama wengine, nyayo zake zimefunikwa kwa manyoya, angalia ukiona yananyonyoka kuna tatizo chunguza, kucha zake zinahitaji kupunguzwa zikikua sana waone maofisa ugani wa mifugo wakusaidie kwa hili

UBEBAJI

Usimbebe kwa kutumia masiki yake huwa wanaumia sana, shika ngozi nyuma ya shingo kama paka ukitaka kumbeba na pia weka mkono mmoja kwa chini ili kusapoti uzito

DAWA
Wapewe dawa ya minyoo kama piperazine kila baada ya miezi mitatu, dawa za wadudu kama akheri powdeer zinyunyuziwe kwenya mabanda yao kuzuia viroboto, usiwape dawa nyingine bila ushauri wa kitaalamu, antibiotics ndio usijaribu kabisa kama nilivyosema mwanzo

Thursday, June 10, 2010

AINA 10 ZA MBWA WENYE AKILI ZAIDI DUNIANI

1 - BORDER COLLIE



2 - POODLE



3 - GERMAN SHEPHERD / ALSATION


4 - GOLDER RETRIEVER


5 - DOBERMAN PINSCHER


6 - SHETLAND SHEEPDOG


7 - LABRADOR RETRIEVER


8 - PAPILLON


9 - ROTTWEILER


10 - AUSTRALIAN CATTLE DOG

Thursday, June 3, 2010

URAFIKI WA MBWA NA KOBE

Huyu mbwa mdogo ajulikanaye kama HOPE huwa anapenda kupanda juu ya mgongo wa kobe huyu ajulikanaye kama CARL, CARL naye bila hiyana huamua kumtembeza tembeza rariki yake

Monday, May 31, 2010

KILIMO CHA PILIPILI MANGA


Utangulizi

Jina la kitalaam ni Piper nigram na kwa kiingereza ni black pepper. Zao hili asili yake ni Mashariki ya Mbali, na linalimwa zaidi katika mkoa wa Tanga na Zanzibar.

Matumizi
Pilipili nyeusi na nyeupe zote hutumika kwa mapishi ya nyama, samaki na kwa mapishi mengine mbalimbali. Nchi za magharibi zina matumizi makubwa ya viungo hivi. Aidha pilipili mtama nyeusi ndiyo huzalishwa zaidi hapa nchini.

Uzalishaji
Hali ya hewa na udongo
Viungo vingi humea katika maeneo yenye joto la wastani kati ya nyuzi joto 24-26 na huzalishwa maeneo ya mwambao. Udongo wenye rutuba na unaopitisha maji na wenye uchachu wa kiasi cha pH 6.5. Mahitaji ya mvua ni mililita 1500-2000 kwa mwaka.




• Uchaguzi wa mbegu
Uchaguzi huzingatia mambo yafuatayo:-
a) Urefu wa pingili na ukubwa wa majani
b) Ufupi wa pingili unaoambatana na majani madogo.
Tofauti iko hadi kwenye umbile la matunda. Majani ya mche mama sehemu kinapokatwa kipando huondolewa wiki mbili kabla ya kukata. Vipando vyenye macho (nodes) 3-4 humika. Macho mawili huzikwa kwenye udongo na kipando kiwekewe kivuli. Inashauriwa kuweka mbolea ya samadi wakati wa kupanda.

• Nafasi ya upandaji
Nafasi ya kupanda ni mita 2-3 kati ya mmea na mmea endapo miche imepandwa na miti inayotakiwa kupogolewa mara kwa mara.

Mahitaji ya mbolea
Matumizi ya mbolea hapa Tanzania si makubwa katika kilimo cha viungo. Ingawa kiasi cha kilo 0.4 cha Urea, kilo 0.3 cha Superphosphate na kilo 0.3 cha Potash ya Muriate kinaweza kutumika kwa miche mikubwa.

• Miti ya kusimikia miche

Miche hupandwa kwa kusimikiwa nguzo ili ikue kwa kujizungusha kwenye miti kama mijenga ua, n.k. Mti huo wa kusimikia nao pia hupaswa kupunguziwa majani ili kupunguza giza. Kila kabla ya msimu miti hiyo hupaswa kupunguziwa matawi (pruning).

Kupogolea miche ya pilipili mtama
Mche ukifikia miezi 18 inapaswa kupogolea kwa kukata sehemu ya juu ya mche ili kufanya matawi mengine yachipue chini ya mche. Inashauriwa mche kuwa na urefu wa mita 3-3.5.

Uvunaji
Maua ya kwanza hutoka baada ya miaka miwili. Matunda hukomaa miezi tisa (9) hadi kumi (10).
Uvunaji ni mizunguko 5 hadi 6 kwa mwaka. Pilipili mtama inaweza kuvunwa kwa misimu miwili. Mavuno ni kati ya tani 0.35-3.75 kwa hekta.

Kuhifadhi
Pilipili mtama inaweza ikawekwa kwenye chombo kisichopitisha hewa na kudumu kwa miaka 20 bila kuharibika.

Mashambulizi ya wadudu na magonjwa
Hapa nchini hakuna matatizo makubwa ya wadudu na magonjwa.

Masoko
Soko la pilipili matama linapatikana ndani ya nchi na nje pia. Bei ya ndani ni kati ya Sh1,000-1,500. Zao hili huuzwa katika nchi za Uganda, Kenya, Uingereza, Ujerumani, Mashariki ya Kati, n.k. Bei ya Nje ni wastani wa dola za kimarekani 1,985 kwa tani.

Thursday, May 27, 2010

BIO -GAS / HEWA VUNDE

Kuni na mkaa vimekuwa vikiongezeka bei kila siku pia vikiwa ni vyanzo vya uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji miti, njia mbadala inahitajika katika kutatua tatizo hili kwa wakulima, na kinyesi cha wanyama kinaweza kutumia kuzalisha nishati ijulikanayo kama BIO –GAS

Kinachofanyika ni kukusanya kinyesi cha wanyama hasa ng’ombe wanaofugwa ndani, kikichanganyika na mkojo pamoja na maji yanaelekezwa katika tanki maalum kwa ajili ya kuzalisha nishati hii. Baada ya bacteria kuozesha mchanganyiko huu kwa njia isiyohitaji hewa ya oksijeni (anaerobic fermentation) nishati ya bio gas huzalisha ikiwa na wastani wa hewa ya METHANE 65% na kasha gasi hii huelekezwa kwenye nyumba kwa kutumia mabomba hadi jikoni kwa ajili ya kupikia

Mchanganyiko uliokwisha tumika hutoka nje wenyewe kwa kusukumwa na mchanganyi ko mpya mara uingiapo, kinyeshi kinachotoka nacho pia hutumika kama mbolea kwa ajili ya kustawisha mazao ya mkulima



FAIDA ZA BIO-GAS
1-Huongeza kipato cha mkulima kwa kupunguza muda wa kutafuta kuni na mkaa

2-Husaidia katika utunzaji wa mazingira kwa sababu haichafui hewa na hupunguza ukataji miti hovyo

3-inaweza kutumika kuwashia taa kama itazalishwa ya kutosha

4-mbolea inayobaki hutumika kwa ajili ya kustawisha mazao

5-Afya ya mkulima hulindwa kwa sababu upikaji kwa kutumia bio gas hauna moshi, kina mama jikoni hawaathiriki na moshi kama wakitumia kuni, badala ya kinyesi cha wanyama kuwa kingi na kukosa matumizi na kugeuka uchafu sasa kitatumika kuzalisha nishati hii

Monday, May 17, 2010

ZANZIBAR HAKUNA MBUNG'O

Ni miaka zaidi ya sita (6) tokea mbung’o waache kuonekana katika visiwa vya Zanzibar na tokea kipindi hicho ng’ombe kadhaa wamekuwa wakipimwa damu ili kujua kama wana ugonjwa wa ndigana/nagana unaosambazwa na mbung’o lakini matokeo yamekuwa mazuri yakionyesha kwamba ng’ombe hawana vimelea vya ugonjwa huo hatari kwa mifugo

MBUNG'O WAKIPANDANA


Hii imesababisha uzalishaji wa maziwa kuongezeka mara tatu zaidi, uzalishaji wa nyama marambili zaidi, matumizi ya samadi ya mifugo nayo yameongezeka mara tano zaidi na hii inamaanisha kwamba wafugaji wa ng’ombe kipato chao kimeongezeka zaidi. Je sababu ya haya yote na mbung’o kupotea ni nini?

Kwa kawaida mbung’o jike akishapandwa mara moja hawezi kupandwa tena maisha yake yote, yaani inamaanisha kwamba huwa wana mzao mmoja tu katika maisha yao yote. Sasa kinachofanyika kitaalam ni kwamba mbung’o wanakamatwa wakiwa hai kisha wana tengwa majike na madume, majike yanauwawa na madume yanapelekwa kwenye maabara na kupigwa mionzi ya gamma kutoka katika cobalt 60, baada ya hapo yanakuwa yanapanda majike kama kawaida ila yanapoteza uwezo wa kuwazalisha kwa maana hiyo watapandana bila kuzalishana na pole pole kizazi kinapotea na kufutika kabisa

MTEGO WA KUKAMATIA MBUNG'O



Kwa Zanzibar zoezi lilifanikiwa asilimia 100 kwa sababu mbung’o hawawezi kutoka sehemu nyingine na kuhamia Zanzibar kwa kuwa ni kisiwa, pia wao walizalisha madume mengi kwenye maabara na kuyaachia baada ya kuyaua kizazi, njia hii inajulikana kama sterile male technique

Thursday, May 6, 2010

KUPUNGUZIA MATAWI MITI JAMII YA MICHUNGWA

Bw Elyc ameniambia kwamba nimwelekeze jinsi ya kupunguzia matawi ya miche yake jamii ya michungwa nami namwomba azingatie haya

1- Kipindi kizuri cha kupunguzia matawi miti yako ni kipindi cha jua na wakati huu mimea isiwe na matunda wala maua

2- Matawi yanakatwa sehemu zile zenye magonjwa , zilizokufa, matawi yaliyofungamana au katikati ya mti ili kuufanya utawanyike vizuri

3- Pia punguza matawi yaliyopo kwenye njia pamoja na matawi yanayoelekea kuelemewa kutokana na kuwa na matawi madogo mengi zaidi

4- Tumia zana maalum za kupunguzia matawi kama mikasi na misumeno maalum inayopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo, uwe mwanagalifu vifaa hivi visikuumize maana vina ncha kali na tumia vifaa vya kujikinga kama mabuti maalum ya mashambani na glovu za mikononi

5- Milimao inabidi ipunguziwe matawi kila Mwaka au kila baada ya miaka miwili, kila tawi lipunguze kiasi cha robo au theluthi ya juu, kwa kufanya hivi mlimao hautakuwa mkubwa sana na kusababisha usumbufu wakati wa kuvuna

MCHUNGWA AINA YA JAFFER



6- ZINGATIA
(a)Panda miche yako kwa nafasi zinazokubalika kitaalam laa sivyo mime yako ikibanana itakuwa inakimbilia juu, kwa michungwa aina ya jaffer panda mita 8 kwa 8 (8m * 8m) na kwa aina ya Valencia panda (5m * 8m)

(b)kumbuka kupunguzia miche yako jamii ya michungwa kuna maanisha kupunguza mazao kwa sababu mti mkubwa ndio unazaa matunda mengi, usiupunguze matawi mti wako kama huna sababu ya kufanya hivyo

(c)Vifaa vinavyotumika kwa ajili ya kupunguzia matawi viwe na makali ya kutosha kuepusha kupasua na kuchana matawi, unaweza kuomba afisa ugani wa eneo lako ili akuonyeshe kwa vitendo

(d)Kama utachanganya michungwa ya jaffer na Valencia uipande kwa uwiano wa 2:5 yaani katika kila michungwa 7 miwili iwe jaffer na mitano iwe Valencia, hii ni kwa sababu michungwa aina ya jaffer ni mikubwa na inazaa sana na inawahi kuiva lakini haihimili sana ukame, michungwa ya Valencia ina uzazi wa wastani na inahimili ukame kwa hiyo ukiichanganya shambani utapata mavuno ya mwanzo kwenye jaffer na mavuno ya kati yatakuwa na mchanganyiko wa jaffer za mwisho na Valencia za mwanzo na kisha mwisho utapata mavuno ya Valencia tu. Kwa hiyo utakuwa na machungwa katika msimu wote wa mavuno na ii itazuia machungwa kuiva yote pamoja na kuharibikia shambani

Tuesday, May 4, 2010

JINSI YA KULIMA BUSTANI KWENYE ENEO LENYE MAJIMAJI

Kutokana na tatizo la bwana Chacha Wambura Ng'wanambiti katika post hii hapa http://mataranyirato.blogspot.com/2010/05/aisifuye-mvua-imemnyea.html nimeamua kutoa maelezo kwa ufupi jinsi ya kukabiliana na sehemu ambazo maji husimama wakati wa mvua



1- Lima na tifua udongo kwa kutumia trekta la mkono (power tiller) kiasi cha inchi 12 chini, udongo mwingine unaweza kuujaza kama matuta na kuweka mifereji pande zote la eneo lako. Kama huna trekta hili pia unaweza kutumia jembe la kukokotwa na ng’ombe (plau)

2- Jaza majani makavu, vijiti, maranda ya mbao n.k kiasi cha inchi 5 -6 halafu mbolea vunde au samadi kiasi cha inchi 4 halafu rudishia udongo wako juu yake na hapo utakuwa umeinyajua ardhi yako kiasi cha inchi 8 juu (kumbuka maranda na mbolea vitadidia kidogo) kisha pitisha harrow au jembe la kukokotwa na ng’ombe ili kuweza kuchanganya vitu hivi



3- Acha udongo wako ukauke kiasi cha siku 3 kisha pitisha harrow au jembe la kukokotwa na ng’ombe tena ili kuvunja vunja mabonge ya udongo yaliyotokea wakati wa udongo kukauka na pia kuchanganya mchanganyiko huu zaidi

4- Weka tena mbolea vunde au samadi kiasi cha nchi mbili juu ya mchanganyiko huu kisha panda mbegu au miche yako na uizungushie udongo kiasi

5- Mwagia maji kadri inavyo hitajika kama udongo utakuwa mkavu, na uendelee kufuata kanuni za kilimo bora kama inavyoshauriwa kitaalamu

Friday, April 30, 2010

MSEELE - delonix elata

Kutokana na maombi ya ndugu Godleader A Shoo alitaka kujua matumizi ya mti wa mdodoma, mti huu hujulikana kitaalam kama delonix elata na jina la kiswahili ni mseele lakini watu wengi wanauita mdodoma kwa sababu imepandwa sana Dodoma na hii inatokana na kuhimili kwake hali ya ukame



Miti hii inauwezo wa kuhimili joto kali na baridi ya wastani kwa hiyo inaweza kuota ukanda wa pwani hadi ukanda wa akti mikoa ya Dodoma, Singida, Shinyanga n.k

MATUMIZI
1- Wengi huipanda kwa ajili ya mapambo na hii hutokana na mwonekano wake mzuri na pia maua yake yanapochanua hupendeza pia
2- Kwenye miti hii tunapata pia kuni kwa ajili ya kupikia na ndio maana hupandwa sana maeneo makame kwa sababu pia inakuwa haraka kiasi
3-Nguzo za kujengea pia zinapatikana kama mti utaacha ukue, nguzo si kubwa sana lakini kwa nyumba za vijijini zinatosha kabisa, pia nguzo hizi huweza kutoa mbao
4- Dawa za magonjwa mbali mbali kama vile majani yakipondwa husaidia kupunguza uvimbe na pia kupunguza sumu ya wadudu kama nyuki, manyigu, na nge. Pia mizizi yake ikichemshwa na kunywewa husaidia matatizo ya tumbo
5- Majani yake huweza kutumika kama chakula cha mifugo, ukipanda miche hii hakikisha hamna wanyama kama mbuzi na Ng'ombe maana wataila ikiwa midogo

MAUA YA MSEELE

Friday, April 23, 2010

FUNGATE LA MKULIMA

Tukiwa na babu na bibi yangu mzee Msumari nyumbani kwake Makorora Tanga, huyu ni mdogo wa mwisho wa Bibi mzaa Baba na ndiye aliyebakia pekee



Tunapata msosi na my wife wangu tukiwa kijijini kwetu, hapa ni Ugali, kuku wa kienyeji na Mchunga bila kusahau ngogwe na chachandu la mbilimbi halafu tunashushia na mnazi au boha



Kaburi la Marehemu Baba yangu mzee Reginald Bennet huko Muhinduro Tarafa ya Maramba Wilaya ya Mkinga Mkoa wa Tanga




Hili ni kaburi la marehemu Bibi mzaa Baba aitwaye Perpetua Mohamed kijijini kwetu Muhinduro Tarafa ya Maramba Wilaya ya Mkinga Mkoa wa Tanga


Wife akishangaa machungwa, yakiwa madogo hivi tunaita mawashata taa



NB Picha za tukiwa Lushoto na Pangani sitaziweka humu kutokana na maombi ya mke wangu (privacy)