KURASA

Wednesday, December 30, 2009

MNYAUKO FUSARI - COFFEE FUSARIUM

Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vya fusari. Hushambulia mashina, machipukizi na hata punje. Ugonjwa wa mnyauko fusari unashamiri kwenye mashamba ambayo hayatunzwi vizuri inavyopasa. Viini vya ugonjwa huu vinauwezo mdogo sana wa kushambulia
mkahawa wenye afya nzuri, ukiona shamba limeshambuliwa na uonjwa huu jua moja kwa moja kwamba shamba hilo halitunzwi vizuri kwa kufuata kanuni za kilimo bora.

DALILI KUU:

Machipukizi yaliyoshambuliwa na ugonjwa huu hunyauka, na majani hubadilika na kuwa na rangi ya kahawia. Matawi na mashina yakishambuliwa hunyauka na kufa. Ukitaka kuthibitisha dalili za fusari kata shina utaona miviringo ya kahawia. (Brown ring)

JINSI YA KUZUIA
• Palizi ni muhimu kwenye shamba.
• Ukataji sahihi wa matawi.
• Matumizi ya mbolea kwa kiwango kinachoshauriwa.
• Ng’oa na choma moto mikahawa iliyokufa.
• Iwapo ni matawi yanayoonyesha dalili za ugonjwa matawi hayo yakatwe na kuchomwa moto.

NB: Miche mingine ya kahawa isipandikizwe sehemu ilikong’olewa
mikahawa yenye ugonjwa kabla ya miezi sita.

SALAMU ZA MWAKA MPYA

Jamani kwa mwaka huu hii ni makala yangu ya mwisho, mwenyezi Mungu akinijaalia nitaendelea mwakani kuwaletea makala nyingine, mwaka huu Mungu aliniwezesha kutuma jumla ya makala 77 ambazo naamini kuna watu zimewasaidia na kuwanufaisha, kuna wengine wamekuwa wakiniuliza maswali kwa faragha na hawakupenda nichapishe majina yao nawashukuru sana, kuna wale walioanzisha mashamba mapya au walikuwa na mashamba na walihitaji ushauri wa kitaalam nao nilishirikiana nao vizuri, kuna ambao walitaka msaada wangu walipata lakini walishindwa gharama za mradi nawaombea kwa Mungu awawezeshe kupata pesa za kuanzisha miradi hiyo, Kuna nilio wakwanza kwa kushindwa kuwasaidia, inawezekena nilibanwa na ratiba au ushauri wangu haukuwa na manufaa kwao na wale walioshindwa gharama za ushauri (ingawa ni sawa na bure) NAOMBA WANISAMEHE

Monday, December 28, 2009

KUTU YA MAJANI - COFFEE LEAF RUST

Huu ni mwendelezo wa magonjwa makuu ya kahawa
Kutu ya Majani ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vya ukungu jamii ya Hemileia vastatrix; Ugonjwa huu ushambulia karibu aina zote za kahawa; hasa katika nyanda za chini ambako kuna joto zaidi. Ugonjwa wa kutu ya majani hujitokeza kabla ya mvua za masika kuanza.



MAZINGIRA MAZURI YA VIMELEA VYA KUTU YA MAJANI:
• Joto lililo ambatana na unyevu nyevu mwingi angani.
• Kivuli kinachosababishwa na miti mingi shambani au matawi
ya kahawa.
• Magugu jamii ya Oxalis.
• Kahawa zilizozeeka kupita kiasi nazo hushambuliwa kwa urahisi.

MASHAMBULIZI NA DALILI
• Kutu au rangi ya machungwa iliyochanganyika na manjano huonekana upande wa chini wa majani ya kahawa.
• Kudondoka kwa majani yangali bado machanga.
• Kudumaa kwa matawi.
• Kukauka kwa ncha za matawi.
• Hatimaye mavuno hupungua kwa kiasi kikubwa.

UGONJWA UNAVYOSAMBAZWA:
• Upepo huongeza kasi ya kusambaa kwa vimelea vya kutu ya majani.
• Wanyama (ndege) wadudu, husambaza vimelea vya kutu ya majani toka mmea mmoja hadi mwingine.
• Miezi michache kabla ya Vuli vimelea vya kutu ya majani huanza kukua;
- Vimelea hivi hujihifadhi kwenye magamba ya shina la kahawa na matawi makubwa (Primary branches) hasa kahawa zilizozeeka.
- Kipindi hiki huwa na joto.
• Vuli husaidia kuongeza kasi ya kukua kwa vimelea hivyo na kusambaza.
- Kutokana na unyevunyevu uliopo kwenye majani na kahawa kwa ujumla.
• Vimelea vya ukungu wa aina hii vinapoendelea kusambaa ndivyo na ashambulizi ya mmea yanavyoongezeka.
• Mashambulizi huendelea kipindi chote cha joto hadi masika, kipindi ambacho vimelea hukosa nguvu.
• Nguvu ya vimelea vya kutu ya majani huanza tena kidogo kidogo
baada ya masika kwisha.



KUPAMBANA NA KUTU YA MAJANI:
• Shamba liwe safi wakati wote.
- Punguza kivuli cha miti na migomba kwenye shamba la kahawa.
- Punguza matawi ya kahawa (pruning); wakati wa kukata matawi kata matawi yote yalivyozeeka; na yaliyo na ugonjwa.
- Lima ili kupunguza magugu hasa jamii ya oxalis.
• Hakikisha udongo una unyevunyevu wa kutosha, wakati wote: (weka matandazo, mbolea na kumwagilia maji)
• Ondoa magamba kwenye kahawa kwa kutumia brush / magunzi mbalimbali.
• Jaribu sumu za asili kama utupa (rejea makala zangu).
• Sumu za viwandani (mrututu) zitumike pale tu ambapo ni lazima kufanya hivyo kufuatana na hali ya hewa;
- mrututu (copper) utumike kama kinga mara baada ya mvua za masika kama joto liko juu likiambatana na unyevunyevu angani.
- Endapo kutu ya majani imeshamiri tumia Bayleton kama tiba (control) lakini si zaidi ya mara 2 kwa msimu.
NB: Wakati wa kunyunyuzia sumu elekeza bomba chini ya majani.

Saturday, December 26, 2009

MAGONJWA MAKUU YA KAHAWA

Magonjwa makuu ya kahawa ni haya yafuatayo
- Chule buni (CBD)
- Kutu ya majani (Coffee leaf rust)
- Mnyauko fuzari (Fusarium)
Leo nitaongelea ugonjwa wa chule buni

CHULE BUNI (CBD- Coffee Berry Disease)
Chule Buni (CBD) ni ugonjwa wa matunda ya kahawa ambao umeenea sehemu nyingi nchini hasa zile za miinuko ya juu. Ugonjwa huu husababishwa na fangas wajulikanao kama colletotrichum kahawae. Ushambuliaji huwa ni mkubwa zaidi wakati wa mvua za masika kwani wakati huu hali ya unyevu unyevu kwenye hewa ni mkubwa na hali ya hewa ni ya baridi.

MFANO WA TUNDA LILISHAMBULIWA


MADHARA
Ugonjwa huu ni mbaya sana na huenea kwa kasi. Mbuni ulioshambuliwa haufi bali mkulima anaweza kupoteza mpaka asilimia 90 ya mavuno kwa mwaka kama hatazingatia namna bora ya kuuzuia.

Ugonjwa huu hushambulia mibuni katika hatua tatu muhimu nazo ni:
• Maua yanapochanua.
• Punje zikiwa changa na laini.
• Punje zinazoiva.

Madhara makubwa hutokea wakati punje zikiwa changa na laini.
Mara nyingi mibuni iliyoshambuliwa na Chule Buni matunda yake huwa na vidonda vyeusi na vilivyobonyea na hudondoka na mengine hubakia kwenye mibuni. Yale matunda yanayobakia yanakauka na kuwa chanzo cha uambukizaji kwenye mavuno ya msimu unaofuata. Picha ya mbuni ulioshambuliwa na Chule Buni

JINSI YA KUZUIA
Ili mkulima aweze kudhibiti vizuri ugonjwa huu anashauriwa:
• Kupunguza matawi yasiyotakiwa ili sumu iweze kupenya vizuri
na kufikia matunda yote.
• Kutumia sumu sahihi zilizopendekezwa kutumika kwenye kahawa.
• Kutumia kiasi na kipimo sahihi kilichopendekezwa.
• Kunyunyizia sumu wakati sahihi yaani:

1. Kabla ya ugonjwa haujatokeza.
2. Unyunyuziaji dawa uanze wiki tatu kabla ya mvua za vuli kuanza (Oktoba - Novemba) na kurudiwa tena mwezi mmoja baadae (Disemba).
3. Unyunyiziaji unaofuata ufanyike tena wiki tatu kabla ya mvua za masika (Machi) na kurudiwa kila mwezi hadi matunda yakomae (Julai)
• Aelekeze dawa kwenye matunda.



Mkulima anashauriwa kunyunyizia sumu mojawapo ya hizi zifuatazo:
1. Jamii ya mrututu - hasa zile nyekundu na za bluu zilizopendekezwa kudhibiti Chule buni. Mfano: Nordox, Cobox, Funguran-OH.
2. Jamii isiyo ya mrututu - hizi mara nyingi ni zile za maji maji zilizopendekezwa kutumika kwenye kahawa mfano: Bravo, Daconil na Dyrene.

FAIDA YA KUDHIBITI
Mkulima akidhibiti vizuri Chule Buni anapata faida zifuatazo:
1. Atakuwa amepunguza uwezekano wa kuendelea kuongeza kasi ya huu ugonjwa mwaka hadi mwaka.
2. Atakuwa ameongeza wingi na ubora wa kahawa.
3. Atakuwa amejiongezea kipato chake na kuwa na maisha bora zaidi.
4. Atakuwa ameongeza pato la taifa kwa ujumla.

MAMBO YA KUZINGATIA
• Mwisho wa msimu hakikisha unaondoa matunda yote haswa yale yaliyoshambuliwa na chule buni.
• Tambua wakati sahihi wa kuzuia huu ugonjwa.
• Nunua sumu sahihi zilizopendekezwa.
• Hakikisha matunda yote yanapata sumu vizuri.
• Epuka ununuzi holela wa sumu kwani unaweza kununua hata zile zilizokwisha muda wake.
• Mara upatapo tatizo onana na mtaalamu wa kilimo/afisa ugani aliyekaribu nawe.

Saturday, December 19, 2009

LEHEMU - CHOLESTEROL

Dada Mary Chuwa alipenda kujua kuhusu lehemu kwenye mafuta, kwa lugha ya kiingereza lehemu ni cholesterol, kwa kawaida kuna aina mbili za cholestrol low density lipoprotein na high density lipoprotein aina zote mbili zinatokana na balance ya kemikali mbili za mafuta zijulikanazo kama polyunsaturated fats na monounsaturated fats. kama hizi kemikali mbili zitabalance zitatengeneza low saturated fats ambazo ni high density lipoprotein, hii ni cholestrol nzuri kwa mwili wa binadamu kwa sababu haina madhara, ila kama polyunsaturated fats na monounsaturated fats hazita balance zitaengeneza low density lipoprotein ambayo ni cholestrol mbaya na inamadhara katika mwili wa binadamu.

Lehemu mbaya (low density lipoprotein) ikiingia mwilini huganda kwenye kuta za mishipa ya damu na kwenye moyo hivyo kufanya njia za damu kuwa nyembamba na kusababisha magonjwa ya moyo au kiharusi (stroke)

Mafuta yatokanayo na Alizeti, karanga na mahindi kwa asili huwa hayana lehemu mbaya an hivyo kuwa salama kwa matumizi ya binadamu. Mafuta ya mawese, nazi, na yale yatokanayo na wanyama pamoja na mazao ya maziwa huwa na lehemu mbaya

Mikoa ya Singida na Manyara imekuwa ikizalisha kwa wingi sana alizeti na kuna viwanda vya kukamua mafuta sehemu hizo, kwa hiyo nashauri kama unaweza agizia mafuta halisi ya alizeti toka sehemu hizo, mbegu za alizeti hukamuliwa ilikupata mafuta na baada ya hapo mafuta huchemshwa na kuchujwa kisha kuwekwa kwenye madumu tayari kwa kuuzwa.

Ili kupunguza lehemu mwilini mwako inashauriwa kutumia asali kijiko kimoja na mdalasini nusu kijiko kila asubuhi kabla hujala chochote, unaweza kutia kwenye chai au maji ya moto mchanganyiko huu.
nakaribisha maoni kwa wenye ufahamu zaidi

Monday, December 14, 2009

NDIGANA KALI - EAST COAST FEVER (ECF)

Huu ni ugonjwa wa ng’ombe, nyati na nyati wa India wakaao kwenye maji (water buffalo) ambao umeenea sana hapa nchini kwetu, msambazaji mkuu ni kupe (rephicephalus appendiculatus) na ng’ombe huanza kuugua siku 10 – 25 (wastani siku 14) toka kuambukizwa ugonjwa huu, protozoa aina ya theileria parva ndiye husababisha ugonjwa huu



DALILI KUU ZA NDIGANA KALI
-Joto kali hadi kufikia 42c kwa kawaida ng’ombe huwa na joto 38c
-Manyoya ya mgongoni husimama muda wote na huwa na rangi ya udongo (brown) kwa mbali
-Kuharisha
-Kutoa makamasi laini
-Matezi ya shingo kuvimba
-Kupe aina ya rephicephalus appendiculatus utawaona kwenye masikio ya mnyama (sio lazima)
-Mnyama hushindwa kula vizuri
-Pua (muzzle) huwa kavu bila unyevu unyevu



TIBA
Dawa aina ya BUTALEX ni maarufu sana hapa nchini kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huu, ni muhimu dalili za mwanzo zinapoonekana kumtaarifu mtaalam wa mifugo na ikithibitika ni Ndigana kali tiba ianze mara moja ikiambatana na OTC 20% ili kushusha homa.

KINGA
Kinga kubwa ni kuogesha mifugo yako mara kwa mara, dawa ya ruzuku ijulikana yo kama PARANEX hupatikana katika maduka yote ya kilimo na mifugo. Dawa nyingine nazo zinafaa kuogeshea kwa kufuata masharti ya mtengenezaji.

Friday, December 11, 2009

TANGAWIZI

1.0 UTANGULIZI:
Jina la kitaalamu ni Zingiber officinale
Tangawizi ni aina ya zao la kiungo ambalo sehemu inayotumika ni tunguu (rhizome) ambalo huonekana kama mizizi ya mmea. Asili ya zao hili ni maeneo ya kitropiki ya bara la Asia na hasa katika nchi za India na China. Zao hili linazalishwa kwa wingi kutoka katika nchi ya Jamaica. Hapa nchini zao hili hulimwa katika mikoa ya Kigoma, Tanga, Morogoro, Pwani, Mbeya na Kilimanjaro.



Tangawizi hutumika kama kiungo katika kuongeza ladha, harufu na kuchangamsha katika vinywaji (kama chai, soda, juisi, vilevi n.k) na vyakula mbalimbali kama mikate, biskuti, keki, nyama za kusaga, achari n.k. Hutumika pia katika viwanda vinavyotengeneza madawa ya tiba mbalimbali kama dawa za meno, kikohozi, tumbo na muwasho wa ngozi n.k. pia hutumika katika vipodozi kama poda n.k).

2.0 AINA ZA TANGAWIZI
Hakuna uthibitisho wa aina za tangawizi ambazo hulimwa hapa nchini ila kuna dalili ya kuwa na aina za White Africa (Jamaica) na Cochin (flint); hii huwa na tunguu ngumu zenye nyuzi.

3.0 TABIA YA MMEA
Tangawizi ni mmea unaotambaa chini ya ardhi, wakati wa masika hutoa majani juu ya ardhi. Jamaica ina rangi hafifu ya kahawia na tunguu fupi wakati Cochin ina tunguu fupi zaidi lenye ngozi ya rangi iliyo kati ya kijivu na nyekundu. Mmea una urefu wa futi mbili na majani yake ni membamba marefu ambayo hufa kila mwaka yakiacha tunguu ardhini likiwa hai. Maua ya mmea huu yana rangi nyeupe au manjano.

4.0 HALI YA HEWA NA UDONGO
Zao hili hustawi katika maeneo yenye hali ya kitropiki, kutoka usawa wa bahari hadi mwinuko wa mita 1,500 au zaidi. Huhitaji mvua kiasi cha mm.1,200-1,800 na joto la wastani wa nyuzi za sentigredi 20-25. Hustawi vema katika udongo tifutifu wenye rutuba na usiotuamisha maji.

MMEA WA TANGAWIZI


5.0 UPANDAJI
Zao la tangawizi hupandwa kwa kutumia vipande vya tunguu vyenye kichipukizi kizuri angalau kimoja na huweza kukatwa katika urefu wa sm.2.5-5. Wakati mwingine, vichipukizi vinavyopatikana katika kumenya tangawizi huweza kuhifadhiwa na kutumika kwa kupanda. Kiasi cha kilo 840-1700 cha vipande vya tunguu huweza kutumika kwa kupanda katika hekta moja. Nafasi inayotumika kupanda ni kati ya sentimita.23-30 kwa 15-23 na kina cha sentimita.5-10 na mara nyingi hupandwa katika matuta. Baadhi ya mazao huweza kupandwa katika shamba la tangawizi ili kuweka kivuli chepesi ingawa si lazima kivuli kiwepo. Inashauriwa kumwagilia maji endapo mvua inakosekana.

Wiki 1-2 kabla ya kupanda weka mbolea ya samadi au mboji kiasi cha tani 25-30 kwa hekta na kwa kukuzia weka kiasi cha NPK kwa uwiano wa kilo 36:36:80. Tandaza nyasi shambani kuhifadhi unyevunyevu hasa pale kivuli kinapokosekana. Palizi hufanywa mara magugu yanapoota, dawa ya kuua magugu, kama simazine au round up hutumika.

MKATE WA TANGAWIZI NA LIMAO


6.0 Magonjwa na wadudu:
• Madoa ya majani yanayosababishwa na viini vya magonjwa viitwavyo Colletotrichum zingiberis na Phyllosticta zingiberi.
• Kuoza kwa tunguu; kunasababishwa na viini viitwavyo Pithium spp
• Mizizi fundo; inasababishwa na Meloidegyne spp.

7.0 UVUNAJI
Tangawizi huweza kuwa tayari kwa kuvuna kati ya miezi 9-10 baada ya kupanda, wakati majani yake yanapogeuka rangi kuwa njano na mashina kusinyaa. Tangawizi inayohitajika kwa kuhifadhi kwenye kemikali (preserved ginger in brine) huvunwa kabla haijakomaa kabisa, wakati ile iliyokomaa kabisa huwa kali zaidi na huwa na nyuzi hivyo hufaa kwa kukausha na kusaga. Mavuno hutofautiana kulinganana na huduma ya zao, mavuno yanaweza kuwa kiasi cha tani 20-30 cha tangawizi mbichi huweza kupatikana.

8.0 USINDIKAJI
Tangawizi ikisindikwa utapata unga, mafuta maalum (essential oils) n.k. Tangawizi iliyovunwa huweza kumenywa, kukatwa na kukaushwa juani au mara nyingine huchovywa katika maji yaliyochemka kwanza na ndipo kukaushwa au hukamuliwa mafuta. Pia tangawizi husindikwa na kuhifadhiwa kwenye chupa zikiwa zimechanganywa na sukari na/au chumvi au bila kuweka kitu chochote. Hata hivyo tangawizi ina Kiasi cha mafuta cha 16.0-18.0%.



9.0 SOKO LA TANGAWIZI
Soko la tangawizi lipo ndani na nje ya nchi, kiasi kikubwa kinauzwa nchini. Bei yake ni kati sh. 300-1,500/- kutegemeana na msimu.

10.0 GHARAMA ZA UZALISHAJI NA MAPATO
GHARAMA YA HEKTA MOJA:
Mbegu Tshs. 240,000/-
Vibarua 250,000/-
Mbolea(mboji/samadi) 150,000/-
Jumla 640,000/-
MAPATO:
Kilo 20,000 X300 =6,000,000/-

Saturday, December 5, 2009

MIHOGO - NJIA BORA ZA UKAUSHAJI NA USINDIKAJI

1. Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Katika Utayarishaji Wa Mihogo
Mibichi Na Ukaushaji


1.1 UTAYARISHAJI
Mihogo mibichi iliyovunwa huoshwa mara mbili. Uoshaji wa kwanza ni ule wa kuondoa udongo baada ya kuvuna, na uoshaji wa pili ni baada ya kumenya mihogo kabla ya kukausha.Baada ya kuoshwa mihogo humenywa kwa kutumia kisu kikali, na kutumbukizwa ndani ya maji safi. Baada ya kumenya kiasi kinachotakiwa mihogo huoshwa na maji safi hadi kuwa myeupe.

1.2 UTENGENEZAJI WA CHIPSI

Mihogo iliyo safi huwekwa ndani ya mashine ya kuzungushwa kwa mikono au mashine ya kuzungushwa kwa mota ya umeme, kisha huparuliwa na kutoka vipande vidogo vidogo ambavyo huanikwa katika makaushio bora.



1.3 KWA MIHOGO MICHUNGU
Baada ya kuparuwa mihogo kuwa chipsi, huwekwa katika mifuko safi (viroba) na kuwekwa mahali penye kivuli kwa muda usiopungua saa sita ili kuacha sumu iliyoko kwenye mihogo kupotea kabla ya kukausha.

1.4 UKAUSHAJI

Mihogo safi ambayo imeparuliwa au kukatwa vipande vidogo vidogo hukaushwa katika makaushio bora kwenye jua kali. Makaushio bora huwa ni yale ambayo yamejengewa kichanja kilichoinuliwa mita mbili kutoka ardhini, na kutandazwa chekeche ya plastiki juu yake, yenye matundu madogo yasiyoweza kupitisha chembechembe za mihogo mikavu Kitambaa safi cha kaniki au mikeka safi huweza kutumika pia kama tandiko la juu ya kichanja ambapo chipsi za mihogo huweza kukaushwa kwa hali ya usafi.

VICHANJA BORA VYA KUKAUSHIA MIHOGO


Epuka kukaushia chipsi za mihogo katika majamvi mabovu juu ya ardhi kwani uchafu utakaoingia ndani ya mihogo hautakuwa rahisi kuondoa tena na husababishsa bidhaa ya unga kutokuwa na ubora.Ukaushaji duni wa mihogo Uharibifu au upotevu unaosababishwa na ukaushaji duni husababisha muhogo kubadilika rangi na kupata ukungu.

UKAUSHAJI DUNI WA MIHOGO


1.5 NJIA BORA ZA KUKAUSHA MIHOGO

Mihogo iliyoparuliwa (chipsi) hukaushwa na baadaye kusindikwa ilikupata unga.
VIFAA NA MALIGHAFI
• Mihogo safi
• Kisu kikali kisichoshika kutu.
• Mashine ya kuparua (grater)
• Kaushio bora
• Kitambaa cheusi kikubwa cha kutosha na kilicho safi au majamvi safi
• Vifungashio.

MASHINE YA KUPARUA MIHOGO(grater)



UTENGENEZAJI WA MAKOPA YA MIHOGO

• Menya mihogo safi kuondoa maganda
• Parua kwa kutumia mashine kupata chipsi.
• Anika kwenye kichanja au kaushio bora lilotandikwa kitambaa cheusi kilicho safi au jamvi safi ili kuzuia uchafu kuingia ndani ya chipsi.
• Sambaza na geuzageuza vipande hivyo ili kuharakisha ukaukaji.
• Muda wa kukausha hutegemea hali ya jua na ukubwa wa vipande. Vipande vidogo hukauka upesi na huwa bora kwa mlaji. Vipande vikubwa huchelewa kukauka na hupoteza ubora
• Fungasha vipande vilivyokaushwa kwenye magunia safi, kasha hifadhi kwenye maghala bora.

1.6 KUHIFADHI MIHOGO MIKAVU (Chipsi Au Makopa)
Njia pekee ya kuhifadhi mihogo kwa muda mrefu ni kwa kuhifadhi mihogo iliyokaushwa. Muhogo uliokaushwa huweza kuhifadhiwa kwa muda wa miezi 6 hadi 12 bila kuharibika. Makopa yanashambuliwa na dumuzi zaidi kuliko chipsi, hivyo inashauriwa kuhifadhi mihogo iliyoparuliwa na kukaushwa (chipsi) ambayo inakuwa katika hali ya unga unga na kufanya mashambulizi ya dumuzi yapungue kabisa.
Chipsi za mihogo zinaweza kuhifadhiwa katika magunia safi ya juti na kupangwa ndani ya ghala juu ya chaga. Pia chipsi zinaweza kuhifadhiwa katika hali ya kichele ndani ya sailo au kihenge bora. Mihogo haihifadhiwi kwa kutumia madawa ya viwandani. Hifadhi kwa hali ya ukavu, usafi na kagua ghala mara kwa mara kuona kama kuna mashambulizi ya panya na chukua tahadhari kuepuka upotevu wa chakula hicho. Aidha hifadhi kwa muda ulioshauriwa ili kudumisha ubora wa bidhaa.

2 KUSINDIKA MIHOGO ILIYOKAUSHWA

2.1 Kusindika muhogo uliokaushwa kupata unga
VIFAA
• Mashine ya kusaga
• Mifuko ya kufungasha
• Mashine ya kufungia mifuko
• Chekeche
• Mizani
• Muhogo safi uliokaushwa vizuri.

MASHINE YA KUSAGIA MIHOGO



JINSI YA KUSINDIKA
• Saga muhogo uliokaushwa kwenye mashine ili kupata unga.
• Chekecha kwa kutumia chekeche laini. Ukubwa wa matundu ya chekechekeche hutegemea kiwango cha ubora wa unga kinachotakiwa na soko.
• Weka unga kwenye mifuko kutegemea matakwa ya soko (kilo 1,2,5,10, au 50)
• Funga vyema kwenye mifuko ya kufungashia ili hewa isiingie
• Hifadhi kwenye chaga au fremu zilizowekwa mahali pakavu na pasipokuwa na mwanga mkali.

2.2 Viwango vya ubora wa unga wa muhogo uliokaushwa Unga laini
• Unga huu unapochekechwa kwa kutumia chekeche yenye matundu madogo
(milimita 0.60) hupenya karibu wote (asilimia 90)

Unga wenye ulaini kati
• Unga huu unapochekechwa kwa kutumia chekeche yenye matundu makubwa (milimita) 1.20) hupenya karibu wote (asilimia 90).

2.3 MATUMIZI YA UNGA WA MIHOGO
Hutumika kupika ugali, uji na katika kutengeneza maandazi, tambi, keki, biskuti,kababu, donati, mkate, chapati na chapati maji.


Virutubisho vinavyopatikana kwenye gramu 100 za unga wa muhogo ni kama ifuatavyo
Maji asilimia 13
Nguvu kilokalori 320
Protini gramu 1.7
Vitamini C miligramu 4
Kalsiamu miligramu 4
Fosiforasi miligramu 135
Potasiamu miligramu 885
W anga gramu 84
Madini ya chuma miligramu 2

Monday, November 30, 2009

MABADILIKO YA TABIA YA NCHI KIKWAZO CHA KILIMO KWANZA

Katika miongo kadhaa ijayo kutakuwa na mabadiliko ya kitabia ya nchi katika hali ya hewa, hii inasababishwa na kuongezeka kwa kiwango cha joto katika dunia. Hali hii ina madhara ya moja kwa moja katika maji na uzalishaji wa chakula katika hali mbali mbali. Kuna dalil zilizo wazi zinazoonyesha kwamba nchi masiki zinazoendelea ikiwamo Tanzania ndizo zitakazo athirika zaidi kutokana na mabadiliko haya ya hali ya hewa kitabia.

Jamii zilizoko vijijini ambako ndio kuna watu wengi zaidi na wanategemea kilimo kama ajira yao au chanzo cha mapato ndiyo itakayo athirika zaidi na kusababisha wimbi la kuhamia mijini kuongezeka, Katika kilimo maji ndiyo hutumika sana na kutokana na mabadiliko haya kiasi cha mvua kitapungua kunyesha, kuna watakao amua kuhamia kulima kwenye vyanzo vya maji au maeneo tengefu ili kuweza kuhimili hali ya ukame, kwa kufanya hivyo basi hata upatikanaji wa maji kwenye mito na chemi chemi pia utaathiriwa kwa kiwango kikubwa



Kukoseka kwa maji ya uhakiwa kwa wakazi wa vijijni kutasababisha magonjwa ya milipuko kama kuhara, kichocho na hata kipindupindu kuibuka na hivyo wana vijiji kupoteza maisha, visima vichache ambavyo ni vyaasili na hata vile vya kuchimbwa ambavyo ni vifupi navyo vitakuwa havina maji kwa kipindi kirefu cha Mwaka.

Kuna haja kubwa kwa mamlaka husika za serekali kama Hali ya hewa, kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na nyinginezo kujiandaa mapema na kuwaanda wanavijiji na hali hiyo, kuna njia kama kubadili aina ya mazao na wanyama, namna ya ulimaji mfano kuanza kilimo cha umwagiliaji cha uhakika, pia kunahitajika aina mpya za mbegu kulingana na mahitaji ya hali ya hewa zaidi ikiwa ni za muda mfupi na zenye kuhitaji mvua pungufu lakini zenye kuzaa zaidi.

Aina za miti tuayopanda kwa ajili ya misitu yetu pia inabidi ibadilike, baadhi ya miti imelalamikiwa kwamba inaondoa maji mengi sana ardhini na hivyo kuwa chanzo cha ukame, ingawa bado utafiti unaendelea lakini miti kama mikaratusi na misoji ni dhahiri inatumia maji mengi katika ukuaji wake

Thursday, November 26, 2009

VITUNGUU

Ndugu Bunyanza kwa mara nyingine tena alitaka kujua kuhusu zao la vitunguu, na mimi bila hiyana naelezea yale machache ninayoyafahamu.



Zao la vitunguu hulimwa karibu kila mahali hapa nchini. Hata hivyo, mikoa inayolima kwa wingi ni Tanga, Arusha, Iringa, Kilimanjaro, Singida, Morogoro, Mara, Mbeya Dodoma na Manyara. Zao hili ni la biashara na chakula. Ekari moja inaweza kuzalisha gunia 80 – 100 za vitunguu zikitunzwa kitaalam, na mkulima anaweza kulima mara mbili kwa Mwaka kwa mbegu kubwa ambazo huchukua hadi miezi mitano (5) shambani. Bei ya wastani kwa gunia moja ni Tsh 60,000

MAMBO YA KUZINGATIA WA K ATI WA UZALISHAJI

Ili kupata vitunguu bora na vingi ni muhimu kuzingatia kanuni za kilimo bora cha vitunguu.Baadhi ya kanuni hizo ni kama zifuatazo: -



1 - Kuchagua aina ya mbegu

• Chagua aina bora kulingana na matakwa ya soko
• Pamoja na mahitaji ya soko ni muhimu pia kuchagua aina inayovumilia magonjwa, wadudu,kukomaa mapema na kutoa mazao mengi na bora.

2 - Kuweka mbolea
Vitunguu hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha.
• Tumia mbolea za asili ili kurutubisha udongo kwa lengo la kupata mazao mengi na bora.
• Iwapo ni lazima kutumia mbolea za viwandani muone mtaalam wa kilimo ili akuelekeze namna ya kutumia. Mbolea ikizidi huharibu ubora wa vitunguu.

3 - Kumwagilia maji
• Kagua shamba kuona kama udongo una unyevu wa kutosha. Iwapo unyevu ni mdogo mwagilia maji kufuata mahitaji ya mmea. Vitunguu vinapoanza kukomaa punguza kumwagilia ili kuepuka kuoza



4 - Kupalilia
• Palilia mara kwa mara ili kudhibiti magugu na kuwezesha vitunguu kutumia vizuri unyevu na virutubishi vilivyoko kwenye udongo. Pia magugu mengine huficha wadudu waharibifu kama vile utitiri mwekundu.
• Wakati wa kupalilia epuka kukata mizizi ya mimea.
• Pandishia udongo na kufunika shina la kitunguu wakati wa kupalilia ili kuzuia jua lisiunguze mizizi na kubabua vitunguu. Vitunguu vilivyoungua na kubabuliwa ubora wake hushuka napia huharibika upesi wakati wa kuhifadhi.

5 - Kudhibiti magonjwa na wadudu
Vitunguu hushambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali ambao huweza kusababisha upungufu na ubora wa mazao. Ili kudhibiti tatizo hilo kagua shamba mara kwa mara kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili za mashambulizi, chukua tahadhari ya kunyunyuzia dawa mapema kabla madhara hayajaleta upotevu mkubwa.

6 - Kupanda kwa nafasi:
Zingatia nafasi ya kupanda inayopendekezwa ili kupata vitunguu vyenye ukubwa uliokusudiwa. Wastani ni inchi 4 - 5 kutoka kitunguu kimoja hadi kingine, na inchi 12 - 18 kutoka mstari hadi mstari na kipandwe inchi 1 - 1.5 chini ya udongo

MAANDALIZI KABLA YA KUVUNA

1 - Kukagua shamba
• Kagua shamba ili kuhakikisha kuwa vitunguu vimekomaa. Vitunguu huwa tayari kuvunwa miezi mitatu hadi mitano tangu kusia mbegu kutegemea aina ya mbegu na hali ya hewa.Dalili za vitunguu vilivyokomaa:

• Majani hunyauka na kuanza kukauka
• Asilimia kumi hadi 20 ya mimea huanguka majani na shingo hulegea.
• Majani hubadilika rangi kuwa ya manjano na baadaye kaki

VITUNGUU VILIVYOKAUKA MAJANI TAYARI KWA KUVUNA



2 - Kuvuna
Vitunguu vinapaswa kuvunwa mapema mara tu vinapokomaa ili kupata mazao mengi na bora.Uvunaji hufanyika kwa mikono ambapo jembe uma hutumika kuchimbua au kulainisha udongo.Udongo ukishalainishwa vitunguu hung’olewa kwa mkono. Inashauriwa uvunaji uanze asubuhi ili vitunguu viweze kunyauka na kukomaza ngozi sehemu za michubuko. Vitunguu visiwekwe juani na inapobidi kukomaza ngozi shambani, majani ya vitunguu yatumike kufunika vitunguu ndani ya matuta yake wakati wa mchana ambapo kuna jua. Kusanya vitunguu kwenye vikapu kisha vipeleke sehemu ya kukaushia. Vitunguu vya kukaushia kwenye kichanja ni bora zaidi, mizizi na majani hupunguzwa na kuachwa urefu wa robo inchi . Vitunguu vya kukausha kwa kunining’iniza havikatwi majani bali hufungwa kwenye mafungu na kupelekwa sehemu ya kukaushia.

Saturday, November 21, 2009

MAHINDI NA MPUNGA KIPI KINA FAIDA ZAIDI

Kutokana na maombi ya Ndugu Buyanza ya kutaka kufahamu kati ya kilmo cha mahindi na Mpunda kipi kina faida zaidi, nami nimejaribu kuchambua kidogo kati ya mazao haya mawili

MPUNGA
Katika hecta moja ya mpunga unaweza kuzalisha mpaka kilo 3675 kwa mkupuo mmoja, kama shamba ni jipya itakuchukua miezi 6 mpaka kuanza uvunaji, hii ni kwa sababu ya kuliandaaa shamba lako, baada ya mvuno wa kwanza utaweza kuvuna mara 3 kwa Mwaka. Hii inamaanisha kwamba unaweza kuvuna kiasi cha tani 10 -11 kwa Mwaka kama utafanya kilimo cha umwagiliaji.



Kilo ya mpunga sasa hivi ni shilingi 700 – 800 ingawa bei hupanda baadae kama utahifadhi mpunga wako kwa maana hiyo kwa Mwaka unaweza kupata kati ya shilingi milioni 7 mpaka milioni 8, gharama za kulima mpunga ni wastani wa asilimia 20- 22 ya mauzo, kwa maana hiyo kwa Mwaka kilimo chako kitatumia si zaidi ya shilingi milioni 2 kwa mara zote 3 utakazolima, hii ikijumuisha vibarua na mbolea.



MAHINDI


Kama utalima mahindi, ambayo unaweza kulima mara 2 kwa Mwaka kwa ukanda wa pwani na mara moja kama nisehemu zenye baridi, MAvuno kwa hecta moja ni kilo 7500 kwa maeneo yenye baridi na kilo 5000 kwa ukanda wa pwani ambapo utavuna kilo 10,000 kwa Mwaka. Bei ya mahindi kwenye soko ni wastani wa shilingi 400 kwa maana hiyo unaweza kupata shilingi milioni 4 kwa Mwaka.



Matumizi ya mbolea za viwandani ni lazima ili kufikia mavuno haya, Mbolea kama UREA itawekwa mara mbili wakati wa kupandia na kukuzia ikichanganywa na DAP (diamonium phosphate) ghara jumla ya mbolea hizi kwa mpando mmoja hufikia kiasi cha shilingi laki 7 mara mbili ni shilingi 1,400,000 ukongeza na gharama za kuandaa shamba na kupalilia kama 200,000 unapata jumla ya 1,600,000 kwa hiyo utabakiwa na kama shilingi 2,400,000



HITIMISHO
Mpunga ukilimwa kitaalam unawezza kukupatia faida shilingi milioni 5 kwa Mwaka, wakati mahindi yatakupatia shilingi milioni 2.5, faida ya mpunga inakuwa kubwa kwa sababu utalima mara 3 kwa Mwaka lakini kama utategema mvua utalima mamra 2 tu kwa Mwaka na utapata faida ya shilingi 3,300,000 kwa Mwaka

Hizi data ni kwa uzoefu wangu tu wa haraka haraka, bei ya mazao inaweza kupanda au kushuka na kiasi cha uzalishaji kwa hecta kinaweza kupanda au kushuka kutokana na aina ya mbegu, hali ya hewa na uzoefu wa mkulima mwenyewe. Kwa sasa hivi kilo ya unga wa mahindi ni shilingi 700 na debe la mpunga wa kyela ni shilingi 20,000, unaweza kupata faida zaidi kama utaachana na madalali na kupeleka mazzao yako sokoni mwenyewe

Thursday, November 19, 2009

MIGRAVILLEA

Kutokana na maombi ya ndugu Leonard Kisenha mwenye shamba lake pale Goba, alitaka kujua kati ya Mitiki/misoji na migavilea (GRAVILLEA ROBUSTA), je ni miti gani itamfaa kupanda kwenye shamba lake? Jibu ni rahisi ukuaji mpaka kuvuna umri ni karibia sawa sawa ila wakati wa kuvuna mwenye mitiki atapa faida nyingi sana (maradufu) kutokana na bei ya mitiki kuwa juu sana, pia hali ya hewa ya pwani kwenye joto inafaa zaid kwa mitiki tofauti na migravilea ambayo hukua vizuri zaidi kwenye baridi



Asili ya miti hii ni nchini Australia lakini nchini Coasta rica na Guantemala (mita 1000 kutoka usawa wa bahari) Afika Mashariki (1200m – 1800m) Sri lanka (600m – 2000m) Israel, Cyprus na Afrika ya Kusini huota yenyewe ikichanganyika na miti ya mikaratusi. Miti hii hustawi zaidi kwenye maeneo yasiyo na joto na inahimili hali ya hewa hata kufikia kuganda ndio maana ukanda wetu hustawi zaidi mikoa ya Mbeya, iringa, Songea, Arusha, Kilimanjaro, Tanga (Lushoto)

Miti hii hukua hadi kufikia mita 30 – 35 ikiwa na kipenyo cha wastani 50cm – 60cm, inakuwa na majani kipindi chote cha Mwaka huwa na magamba ya kahawia huku mbao zake zikiwa na rangi nyekundu kuelekea hudhurungi iliyo kolea, huweza kuhimili kuota kwenye mchanga na udongo wenye asidi 5 – 7ph ingawa hukua vizuri zaidi kwenye udongo wenye rutuba na usiotuamisha maji.



Kiasi cha mvua kinachohitajika ni wastani wa 1200mm – 1800mm kwa mwaka, hutoa maua yenye rangi ya njano na kishubaka cha mbegu huwa na urefu wa senti meta 2 ambazo kwa Tanzania hukomaa kuanzia mwezi 5 mpaka 8, mbegu zake ni nyembamba kama karatasi (kilo moja huwa na mbegu 50,000 mpaka 150,000)

Umri mzuri wa kuvuna tangu kupandwa ni miaka 15 ambapo mbao nzuri hupatikana, lakini mti unaweza kuvunwa kabla ya hapo kama utahitajika kwa matumizi mengine kama kuni au nguzo za kujengea, mti huu unaweza kupandwa kwa ajili ya kivuli, mapambo au hata mipaka ya shamba na kuzuia upepo



Gamba la mbegu zake huwa gumu kiasi, njia nzuri ya kuhakikisha zinaota kwa wingi ni kwa kuzipitisha kwenye moto kidogo (heat seed scarification) mbegu zikiachwa wazi huweza kukaa bila kuharibika kwa miezi 2 – 3 lakini kama zitahifadhiwa kwenye mifuko ya plastic kwenye hali joto ya sentigredi 4 na unyevu kiasi cha asilimia 60 kisha mfuko ukazikwa kwenye mchangamkavu ulio ndani ya chombo maalum, basi mbegu huweza kuhifadhiwa mpaka miaka miwili

Thursday, November 12, 2009

KASUKU - DONDOO ZA KUMFUNDISHA KUONGEA



Watu wengi wamekuwa wakipenda kufuga kasuku lakini utakuta wanalalamika kwamba kasuku wake haongei, nimeamua kuweka vidokezo muhimu ili mfugaji aweze kuzingatia wakati wa kumfundisha
Kuna aina nyingi za kasuku duniani wengine wakiwa na rangi za kawaida na wengine wakivutia sana, kwa kawaida huwa hawaishi sehemu zenye baridi kali kwani hupendelea hali ya joto wastani

UCHAGUZI WA KASUKU
Mbegu kubwa ni waongeaji wazuri, mbegu ndogo ni wavivu kujifunza,
Akiwa mdogo anajifunza vizuri zaidi, ukiweza mpate yule anayetoka kulelewa kwenye kiota na ndio anajifunza kuruka/kupaa
Kasuku muoga hawezi kujifunza vizuri.
Kasuku mwenye tabia ya kung'ata anauwezo mkubwa wa kujifunza kungea.




MAZINGIRA
Kumbuka kasuku hujifunza maneno machache tu hawezi kuongea kama mtu.
Sehemu nzuri ya kumuweka nyumbani ni jikoni, kwa sababu kuna shughuli nyingi.
Huanza kuongea katika umri wa miezi 4-6.




UFUNDISHAJI
Wakati wa kumfundisha zima radio na TV (kusiwe na kelele)
Muda mzuri wa mafunzo ni asubuhi na jioni.
Mfundishe kupiga miluzi baada ya kuweza kuongea baadhi ya maneno na si kabla ya hapo.
Kumbuka kasuku hujifunza vizuri zaidi kwa vitendo mfano unamtoa nje ya kibanda chake huku unamwambia " toka nje mmmh" ukirudia rudia, jitahidi kutumia Mmmh kila baada ya neno, hii humsaidia kujifunza kwa urahisi.
Hakikisha anapata mlo kamili maji na matibabu

Saturday, November 7, 2009

SAANEN MBUZI BORA WA MAZIWA




ASILI Switzerland katika ukanda wa Saanen

RANGI nyeupe au maziwa

UZITO kilo 65-68

MAZINGIRA yasiyo na joto, wanapendelea baridi chini ya sentigredi 15c



UZAZI mtoto moja au mapacha (kila mwaka mara mbili)

UZALISHAJI lita 4 mpaka 7 kwa siku (mikamuo miwili)

MASIKIO yamesimama wima

MKIA umelala tofauti na mbuzi wengi ambao husimamisha mkia

NDEVU majike yana ndevu mara chache ingawa si nyingi kama madume

PEMBE ndefu zilizosimama wima

Monday, November 2, 2009

BORAN - MBEGU BORA YA NG'OMBE WENYE ASILI YA AFRIKA MASHARIKI

Asili yake ni maeneo ya borana kusini mwa Ethiopia ambako alipatikana baada ya mbegu tatu za ng’ombe zilichanganyika kwa bahati mbaya kutoka kwa wafugaji wa kienyeji waliotoa ngombe wao kutoka pande tofauti za afrika, hiyo ilikuwa zaidi ya miaka 1300 iliyopita lakini sasa hivi kuna taasisi inayoitwa Boran cattle breeder’s society iliyopo nchini Kenya.

DUME BORA LA BORAN


Taasisi hii iliamua sasa itafute mbegu bora ya Boran kwa kutumia njia za kitaalam tofauti na hapo mwanzo ambako Boran alitokea tu bila hata wafugaji kujua kwamba wanatengeneza mbegu bora ya ng’ombe.

JIKE BORA LA BORAN


Waalamu wa kupandisha (breeders) waliamua kuangalia vinasaba bora zaidi na kumfanya Boran awe wa kisasa zaidi na kuweza kuhimili hali ya Afrika mashariki huku uzalishaji wa maziwa na nyama ukiongezeka zaidi kuliko ule wa ng’ombe wetu wa kienyeji, Boran wa kisasa ana damu za aina tatu katika uwiano ufuatao N’gombe wa ulaya wasio na nundu (european bos taurus) 24% Ng’ombe wa Afrika mashariki wenye nundu wajulikanao kama Zebu (bos indicus)64% na ngombe wafrika wasio na nundu (african bos taurus ) 12%



SIFA
-Ni mkubwa kuliko ng’ombe wa kienyeji
-Ana kiwele cha wastani na chuchu ni kubwa kidogo
-Anazaa ndama wa wastani (kilo 25 – 28) kwa hiyo hakuna matatizo wakati wa kujifungua lakini watoto hukua haraka na ni mara chache sana ndama kufariki
-Anahimili hali ya mazingira ya Afrika kuliko ng’ombe wa kisasa (joto na magonjwa)
-Ngombe jike anaweza kuzaa bila matatizo mpaka akiwa na miaka 15, madume yanauwezo wa kuzalisha mpaka miaka 16
-Majike hubalehe baada ya siku 385 (mwaka na siku chache)
-Ni wapole na wenye nguvu kwa hiyo hufaa kwa shughuli za kulima na kukokota mikokoteni (maksai)
-Anaongezeka uzito haraka hata kama anakula majani makavu, majike yanayo nyonyesha hupungua uzito kidogo sana kipindi cha kunyonyesha
-Wanakula kwa mshikamano na hawatawanyiki wakiwa machungoni kiasi kwamba inakuwa vigumu kumuiba mmoja au kumtenganisha na wenzake

BORAN WAKICHUNGWA KATIKA KUNDI LENYE MSHIKAMANO



Wafugaji wengine wamejaribu kuchanganya mbegu hii na mbegu nyingine za kisasa kutoka bara la ulaya ili kuongeza uzalishaji wa maziwa au nyama kama wanavyoonekana hapo chini kwenye picha

BORAN NA FRIESIAN (maziwa)


BORAN NA BEEFMASTER (nyama)



BORAN NA JERSEY (maziwa)


BORAN NA DRANKENSBERGER (nyama na maziwa)

Friday, October 30, 2009

MABUA YA MAHINDI, NG'OMBE NA SAMADI-KUNA FAIDA HAPA

Unafahamu ni kiasi gani cha mabua kinabaki baada ya kuvuna shamba lako la mahindi? Jaribu kutazama vizuri shamba lako kwa macho na hutaamini !!!!!!!!!!! karbu nusu ya kile ulichovuna kimebaki shambani kama mabua yaani ile mbolea ya samadi uliyoweka bado iko shambani katika mfumo mwingine.

Mabua yanaweza kulishwa tena wakati wa ukame yakikatwa katwa na kuchamnganywa na molasses, ekari moja ya mabua intosha kumlisha ng’ombe mmoja mwenye kilo 500 kwa miezi miwili. Hili ni zoezi lenye lengo la kupunguza gharama na kuongeza faida lakini linahitaji umakini kidogo, ninashauri mara tu baada ya kumaliza kuvuna mabua haya nayo yavunwe na kuhifadhiwa sehemu yenye kivuli, na hao utaweza kumlisha mnyama wako mabua yakiwa na 65% chakula chakula mmeng’enyo (digestable food) huku kukiwa na protini kiasi cha 7%



Kama hunasehemu ya kuhifadhi mabua haya unaweza kuwachungia humo humo shambani ng’ombe wako ili wale wenyewe ila utahitajika kuwawekea mawe yenye madini ili walambe, kwa kuwachungia shambani ng’ombe wako utapata faida zifuatazo, kwanza hutahitaji kusafirisha mbolea ya samadi na kuirudisha shambani, pia nombe wanapo kanyaga shamba husaidia kupunguza mmong’onyoko wa udongo. Kama msimu uliopita ambao ndio mahindi yalilimwa kulikuwa na upungufu wa mvua inabidi uwe makini maana mabua yatakuwa na kiwango kikubwa cha madini ya nitrate ambayo yana madhara hasa kwa wanyama wanaokua wenye mimba au kunyonyesha, ili kuepuka hili unaweza kuwalisha wanyama wako chakula kingine kwanza na kumalizia na mabua au kama umeyakata basi changanya na majani mengine kasha ndio uwalishe. KUMBUKA ng’ombe mwenye kilo 500 anaweza kuzalisha molea hadi kilo 12 kwa siku je hii si faida kubwa?

Wednesday, October 14, 2009

TARATIBU NA MASHARTI YA MIKOPO YA KUNUNUA TREKTA JIPYA



1. Mwombaji atajaza fomu maalum ya maombi inayopatikana katika Ofisi za kilimo za Halmashauri za Wilaya na Makao makuu ya Mfuko wa Pembejeo, jijini Dar-es-salaam na katika tovuti ya wizara ya kilimo.

2. Fomu za maombi zilizojazwa na kuambatanishwa na vielelezo vinavyohitajika zitapitishwa/kuidhinishwa na Afisa Kilimo wa Maendeleo ya Mifugo wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya husika na baadaye kutumwa mapema kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Pembejeo.

3. Mikopo ya kununua matrekta inatolewa na Mfuko wa Pembejeo, baadhi ya benki na taasisi za fedha na SCCULT (T) Ltd. kwa niaba ya Mfuko, mwombaji sharti atimize yafuatayo:-

(A) Awe na dhamana yenye hati miliki isiyohamishika iliyoandikishwa kwa jina la mwombaji.
(B) Awe na shamba binafsi lisilopungua hekta 50 na awe tayari kutoa huduma ya kuwalimia wakulima wengine
(C)Awe tayari kutekeleza masharti yote ya Mfuko wa Pembejeo au taasisi ya fedha na SCCULT yanayohusu mkopo wa ununuzi wa trekta jipya.
(D)Awe tayari kulipa asilimia moja (1%) ya mkopo kama gharama za nyaraka za mkopo na kusajili trekta kwa pamoja kwa jina lake na Mfuko
(E) Riba inayotozwa ni asilimia nane (8%) na marejesho hufanyika kwa muda wa miaka mitatu kila baada ya miezi mitatu.

Saturday, October 10, 2009

KUKATA PEMBE NA KUZUIA PEMBE KUOTA

Mnyama asiye na pembe hasa ng’ombe hupunguza uwezekano wa wanyama kuumizana na hata kuwadhuru binadamu, wanyama wadogo kama miezi miwili hadi mitatu ni vizuri wakachomwa ili kuzuia pembe kuota (disbudding) lakini kama pembe zimetokeza hamna jinsi ila kuzikata kwa kutumia msumeno au waya maalum (phatetomy wire)

DISBUDDING IRONS


Zoezi la kuzuia pembe kuota hufanyika kwa kutumia vyuma maalum (disbudding iron) ambavyo hupashwa moto na kuwa vyekundu, ndama huandaliwa kwa kulazwa chini na kisha kupunguzwa manyoya sehemu itakayochomwa ambapo ni pale pembe zinakoota, unaweza kuitambua sehemu hii kwa kupapasa na utaona kama pembe ndogo ndani ya ngozi. Sehemu husika isafishwe kwa spirit au eusol kabla ya zoezi kuanza.



Mtaalamu wa mifugo ndiye atakaye fanya zoezi hili kwa kufuata kanuni za kitaalam, kabla ya kuanza zoezi ni muhimu mnyama kupigwa sindano ya ganzi, kisha sehemu husika huchomwa na chuma cha moto, na chuma kuzungushwa kila upande na mwisho kama anazibua ataondoa kile kipande kinachoota na kumalizia kwa kukausha sehemu iliyobaki kwa kutumia chuma kile kile, baada ya hapo dawa za kupulizia za vidonda, iodine tincture au dawa za kufukuza wadudu hupakwa sehemu husika na mnyama huachiwa huru.



Kuhusu ukataji wa pembe ambayo imeshaota, baada ya mnyama kufungwa na kulazwa chini huchomwa ganzi na ukataji huanza. Kama utatumia msumeno lazima damu nyingi itatoka, zuia damu hii kwa kuunguza sehemu ndogo ya pembe iliyobaki kwa kuichoma na disbudding iron au chuma chochote cha moto. Inashauriwa kutumia phatetomy wire kwa sababu wakati unakata pembe waya huu huunguza pembe na kufanya damu isitoke kabisa



Kuna baadhi ya aina za ngombe wa kisasa hazina pembe kabisa mfano Hereford na mbegu kama Friesian baadhi yao huwa hawana pembe, kwa mbegu za kienyeji kama zebu (SHZ)huwa na pembe fupi fupi