Kifa-uwongo (Mecocorynus loripes),. ni mdudu aina ya
“weevil” ambaye hushambulia mashina ya mikorosho hata kufikia hatua ya kuuwa mti
mzima. Mdudu huyu huitwa “kifa-uwongo” kwa sababu ya mbinu yake makini
anayotumia kujihami. Mara tu aonapo mtu anapita karibu yake, huanguka chini na
kujifanya kama amekufa kabisa. Kisha baada ya mtu yule kupita, yeye huamka tena
na kuendelea na shughuli zake kama kawaida. Wamakonde humwita mdudu huyu
“Nang’ang’ana”, ambapo Wayao nao humwita “Ng’ang’ani.
MAISHA YA KIFA UWONGO
“Kifa-uwongo” kama wadudu wengine, hupitia hatua za yai,
“lava” na “buu” kabla ya kuwa mdudu kamili. “Kifa uwongo” kamili aliyekomaa,
ana rangi ya kahawia na urefu wa kama sentimita 2. Ana mdomo mrefu uliochongoka
(snout) ambao daima anauficha kwa kuulaza kifuani pake. “Lava” wake ni aina ya
funza (grab) mweupe, mwenye ngozi ya kukunjamana na kichwa cha rangi ya kahawia
mzito (dark brown), yeye daima huonekana
amejikunja kama upinde.
“Kifa uwongo” wa kike hutoboa gamba la mkorosho kwa kutumia
mdomo wake mkali, na kutaga yai moja moja. Baada ya mayai kuanguliwa, mafunza
huanza kushambulia gamba la mti mara moja. Funza hawa wana midomo mikali kama
misumeno, nao wanakula kwa bidii sana gamba la mti. Kadri wanavyokula ndivyo
wanavyoongezeka ukubwa pia. Funza akaribiapo kuwa Buu (pupa), hupekecha ndani
ya mti (kiasi cha sentimita 2.5 chini ya gamba) na kutengeneza matundu kwa
ajili ya maficho ya buu (pupal chambers). Mabuu hujifungia ndani ya matundu
hayo na hatimaye hugeuka na kuwa “Kifa uwongo” kamili. Mzunguko wa kutokea yai
hadi “Kifa-uwongo” kamili, huchukuwa muda wa miezi sita, ambapo muda wa karibu
miezi 2 - 2.5 huwa katika hatua ya mafunza, ambayo ndiyo yenye uharibifu
mkubwa. “Kifa-uwongo” kamili ana mabawa na anaweza kuruka kwa nadra toka mti
hadi mwingine. Mara nyingi wadudu hawa, huonekana wakidumu katika maeneo ya mashambulizi. Mashambulizi yanaweza kuchukua muda wa mwaka
au miwili katika mti mmoja, ambapo mti wa jirani unaweza kuwa huru kabisa bila
mashambulizi!. Mara nyingi “Kifa-uwongo”
hupenda kuhamia mkorosho mwingine baada ya kuua kabisa mkorosho waliouanza
kushambulia.
DALILI ZA MASHAMBULIZI
Maeneo ya mashambulizi huonekana wazi wazi hata toka mbali,
kwa sababu ya uwepo wa Mchanganyiko wa utomvu na takataka kama za maranda ya
seremala ambayo hatimaye hugeuka rangi na kuwa nyeusi. Rangi ya majani ya mkorosho ulioshambuliwa
sana, hubadilika na kuwa njano, kisha hunyauka na hatimaye hukauka. “Kifa-uwongo”
hupendelea kushambulia miti mikubwa tu. Utafiti umeonyesha pia kwamba
hupendelea miti iliyojeruhiwa kutokana na kukatwa kwa ajili ya ubebeshaji (top-work) au hata ile ya kupunguzwa matawi.
Inasadikika kwamba aidha eneo la jeraha ni rahisi kwa kifa uwongo kutaga mayai
yake, au huenda kuna mvuto wa aina yake kutokana na harufu ya utomvu utokao eneo
lenye jeraha na kufanya mvuto wa pekee kwa kifa uwongo kushambulia!
MKOROSHO ULIOSHAMBULIWA NA KIFA-UWONGO
JINSI YA KUDHIBITI KIFA UWONGO
Hakuna dawa ambayo inashauriwa kutumika katika kuthibiti
wadudu hawa, badala yake, mkulima
mwenyewe anashauriwa kupambana nao ana kwa ana: Mwanzoni mwa mashambulizi. Ukaguzi
wa mara kwa mara ufanyike kwa kila mkorosho kukagua mashambulizi hayo. Mara tu
baada ya kuona dalili za mashambulizi ya wadudu hawa, bandua eneo la
mashambulizi kwa kutumia kisu au upanga
na kuwaondoa mafunza wote. Funza akidondoka chini hana uwezo tena wa kupanda kwenye mti au kufanya mashambulizi.
Mabuu waliojifungia kwenye matundu ya maficho yao, wanaweza kuuawa kwa kutumia ncha
kali, kama vile spoku yabaiskeli, ili kuwatoboa wakiwa ndani
yamashimo yao. Inashauriwa pia
kuwasaka na kuwaua kila “Kifa uwongo” kamili (adults) kwa kuwakata vichwa
vyao.
MASHAMBULIZI YALIYOKITHIRI
Inashauriwa
kukata na kuchoma moto mikorosho yote iliyoshambuliwa kwa kiwango cha
hali ya juu, ili kuuwa mabaki ya mayai na funza waliopo
No comments:
Post a Comment