Utitiri wa mikorosho
au kwa jina lingine thrips (Thrips rubrocinctus), ni wadudu wadogo sana wenye
mwili laini na rangi kati ya njano, kahawia au nyeusi. Utitiri wakubwa
(adults) hutambulika kwa kuwa na mabawa na mwili wa kahawia (dark brown)
au mweusi, pamoja
na upito (band) wa rangi nyekundu
kifuani. Wanaonekana vizuri kwa kutumia kikuzia umbo (lens).
Katika kipindi kirefu, utitiri ulikuwa ukionekana katika maeneo mengi yanayolimwa korosho, lakini
athari zake zilikuwa ndogo. Katika miaka ya hivi karibuni wameonekana kwa
uwingi na kuleta hasara kubwa hasa katika
tarafa za Lisekese na Chikundi
wilayani Masasi. Pia mashambulizi ya wadudu hawa yameonekana katika wilaya za
Nachingwea na Newala kwa kiwango kidogo.
Inakisiwa kuwa uongezekaji wa
wadudu hawa husababishwa na
mabadiliko ya hali ya hewa.
MZUNGUKO WA MAISHA
Utitiri wakubwa hutaga mayai katika sehemu yachini ya majani. Mayai yanaanguliwa baada ya siku 3
hadi 4 na kutoa vijititiri
vidogo sana (larva I) ambavyo
huwa ni vyepesi sana. Huingia
hatua ya pili (larva stage II)
baada ya siku 7 hadi 8. Hatua hizi
ndizo ziletazo uharibifu mkubwa maana
ndizo hatua za ulaji na ulafi wa hali ya juu. Baada ya wiki moja tena, ndipo
hutokeza hatua ya kwanza ya “ninfu” (Nymph stage I) na hatua yake ya pili baada
ya siku 3 hadi 4. Katika hatua hizi mbili (nymph stages), vijidudu hivi
havitembei wala kula chakula bali hukaa mahali pamoja, hasa
kwenye ardhi. Hatua hii ya “ninfu” hudumu kwa siku 11 hadi 12 kabla ya kupevuka
na kuwa utitiri wakubwa (adults). Hivyo Mzunguko wa maisha yao toka yai hadi
kupevuka ni mwezi mmoja. Utitiri hushamiri sana wakati wa kiangazi mara tu baada
ya mvua, hasa kati ya mwezi June
na Oktoba. Utitiri hupungua kabisa wakati wa mvua, hata hivyo huvuka msimu hadi
mwingine kama utitiri wakubwa.
MASHAMBULIZI
Utitili wachanga pamoja na
wakubwa, hushambulia upande wa chini wa majani hasa yaliyokomaa,
machipukizi na mashada ya maua. Utitili wachanga hubeba tone la majimaji mkiani
na kudondoshea juu ya majani, ambapo likikauka
huacha doa la kahawia au nyeusi, lakini hasa rangi ya kutu. Maeneo
yaliyoshambuliwa na utitili hubadilika rangi na kuwa na weupe weupe wenye
mng’aro wa rangi ya fedha (silvery).
Baadaye hubadilika na kuwa na rangi ya udongo (kahawia), hatimaye hukauka
na majani hupukutika Eneo
linaloshambuliwa hudumaa na uzalishaji
kuathirika. Maeneo mengi ambayo hushambuliwa na utitili huwa korosho
hazizai kabisa. Miti iliyopukutisha majani kwa sababu yamashambulizi ya utitiri, huweza kuchipuza tena kwenye
mwezi Novemba na Desemba.
MAZAO MENGINE YANAYOSHAMBULIWA NA UTITIRI
Wadudu hawa hushambulia majani na hata maua ya aina mbalimbali ya mazao na mimea, kama vile mazao ya bustani (vitunguu nk), michungwa,
pamba, aina ya nafaka. Kwa sababu ya wingi wa aina ya mimea inayoshambuliwa na utitiri, udhibiti
wa wadudu hao unaweza kuwa mgumu kwa kiasi fulani.
KUSHAMIRI KWA UTITIRI
Wadudu hawa hupendelea mikorosho iliyosongamana, isiyopitisha hewa vizuri, mikorosho isiyopogolewa na mashamba yasiyohudumiwa kwa
ujumla. Hupendelea hasa miti mikubwa.
Utitiri hupendelea hali ya ukame au kiangazi cha muda mrefu.
KUSAMBAA
Utitiri husambazwa hasa kwa njia ya upepo au kwa kupanda vipando (propagation
materials) ambavyo vimeshambuliwa.
KUDHIBITI KWENYE MIKOROSHO
Njia pekee inayotumika kudhibiti utitiri ni matumizi ya
madawa. Dawa ya BASUDIN au KARATE ndiyo iliyopendekezwa
na watafiti kudhibiti utitiri wa korosho. Mchanganyiko wa mililita 5 za KARATE
na lita moja ya maji unatosha kudhibiti wadudu hawa katika mti mkubwa usiozidi
kipenyo (diameter) cha mita 10. Ni jambo la muhimu kukagua mashambulizi kuanzia
mwezi Mei. Upuliziaji unaanza mara tu baada ya kuona dalili za mashambulizi
au kuwaona wadudu wenyewe na kurudia baada yawiki tatu (siku 21). Upuliziaji
unafanyika kutumia mashine ya moto (Mist blower) au yakawaida (Knapsack
sprayer) kutegemeana na ukubwa wa mti. Ni muhimu kuanza kupuliza
dawa mapema, ili kuweza kuwathibiti wadudu hawa wakiwa katika hatua zao za
mwanzo kabisa za ukuaji wao ( hatua za lava na ninfu). Hii ni muhimu kwa sababu ni vigumu kuudhibiti
utitiri wakubwa. Awamu 2 hadi 3
zinatosha kuthibiti wadudu hawa katika msimu mmoja. Ikibidi, matunda (mabibo) yaliyopuliziwa dawa
yasitumike mpaka baada ya siku 21
No comments:
Post a Comment