UTANGULIZI
Milibagi (Pseudococcus longispinus) ni wadudu waharibifu
katika zao la korosho, waliojitokeza kuwa maarufu sana katika miaka ya tisini.
Hawa ni wadudu wanaoonekana katika maeneo mengi ulimwenguni, lakini hushamiri
na kuleta athari kubwa katika mazingira ya Tropikali. Mnamo mwaka 1990,
milibagi walionekana kushambulia mikorosho katika maeneo ya mjini Masasi. Mwaka
1993, walionekana kuenea hadi wilaya za Nachingwea na Tunduru. Hivi leo, wadudu
hawa wameenea karibu sehemu nyingi za kanda ya kusini, ingawa mashambulizi
makubwa yapo wilayani Masasi, Tunduru, Nachingwea na Liwale. Milibagi ni moja ya wadudu waharibifu wanaoishi
na kuponea mimea. Wadudu hawa hutengeneza utando mweupe (scale) juu ya miili
yao kwa ajili ya kinga na kujihami dhidi ya adui zao.
Milibagi huonekana katika mazao ya aina nyingi ikiwa ni
pamoja na miembemafuta, mihogo, michungwa, minanasi nk. Pamoja na hivyo, kuna
tofauti kati ya milibagi wanaoshambulia hayo mazao mbalimbali. Kwa mfano,
milibagi wa mihogo (Phenacoccus manihoti), miembe (Rastrococcus invadens) ni tofauti
na wale wa mikoroshoni (P. longispinus). Dalili za Mashambulizi ya Milibagi. Maeneo
yaliyoshambuliwa na milibagi huonekana yamefunikwa na weupe weupe ambao ni
utando unaofunika miili ya wadudu hao. Mikorosho iliyoshambuliwa sana na
milibagi, huonekana kwa mbali kama vile imefukikwa na theluji. Mashambulizi ya
Milibagi Milibagi wanaweza kushambulia eneo lolote la mmea kwa njia ya
kufyonza. Kwa jinsi hiyo, milibagi huingiza matemate yao katika maeneo ya mashambulizi na hatimaye
huweza kueneza vimelea vya virusi. Milibagi hutoa utomvu mweupe mweupe kama asali
na kufunika maeneo ya mashambulizi, hata kufanya mmea usiweze kupata mwanga wa
jua vizuri hata kuzuia utengenezaji wa chakula cha mimea (photosynthesis). Majani yaliyoshambuliwa sana na milibagi, hupukutika
hivyo kuathiri uzalishaji. Maua yaliyoshambuliwa mapema na milibagi yanashindwa
kuzaa. Korosho zilizoshambuliwa zingali zinakomaa, zinachafuliwa kwa utando na
utomvu.
Korosho hizo yamkini zisafishwe kwa mchanga kabla ya kufikiria kuuzwa, vinginevyo
hutengwa katika daraja la pili. Mashambulizi ya milibagi, yanaweza kupunguza
uzalishaji kwa kiwango cha asilimia 50% Kustawi kwa Milibagi. Milibagi
huonekana kwa wingi wakati wa kiangazi, hasa mwezi Septemba hadi Novemba.
Milibagi hupungua sana wakati wa mvua. Inaelekea kwamba mabadiliko ya hali ya hewa
ni chanzo kikubwa cha mashambulizi ya milibagi kwenye mimea. Maisha ya
Milibagi. Milibagi wa kike hutaga kiasi cha mayai 50-500 kutegemeana na
mazingira. Mayai huanguliwa na kutokea Vitambaazi (crawler). Hatua hii ni muhimu
kwa usambaaji wa milibagi. Hawa hutambaa mpaka kwenye ncha au vilele vya miti
na kujitegeshea miguu yao ili wasambazwe kwa upepo, ndege au wadudu wengine.
Binadamu pia wanahusika sana kusambaza wadudu hawa katika hatua hii. Hatua za
lava zinazofuata ndizo za ulaji na uharibifu. Milibagi waliokomaa (adults) huwa
hawajishughulishi (inactive), huwa hawali chakula na huishi muda mfupi (wiki au
mwezi)
KUDHIBITI
Zipo njia mbili
ambazo zinaweza kutumika kudhibiti milibagi:
◊ NJIA YA KIBAIOLOJIA
Utafiti umeonesha kwamba
wapo wadudu wengine ambao
wanaweza kushambulia milibagi, kama vile:
a) Ladibedi bito (Chilocorus spp)
b) Manyigu (Chrysopa spp)
Utafiti umeonesha kwamba idadi ya wadudu hawa mashambani ni
ndogo kwa kuweza kudhibiti idadi kubwa ya milibagi. Utafiti wa kina zaidi
unafanyika kuona jinsi ya kuwafanya wadudu
hawa waongezeke idadi ili kuweza kuwadhibiti milibagi mikoroshoni.
◊ NJIA YA KUTUMIA MADAWA
Njia pekee inayotumika hivi sasa kuwadhibiti milibagi ni
kutumia madawa. Dawa aina ya Selecron 720 EC
ndiyoiliyothibitishwa na utafiti itumike dhidi ya milibagi.
Dawa ya Selecron 720 EC Dawa hii ni ya aina ya maji, inayosambazwa na kampuni ya Norvatis (Ciba Geigy).
Inapulizwa kwa kutumia mashine za
moto (motorized blowers) kama vile Maruyama 150DX au Solo
◊ Kiwango cha upuliziaji
ni mililita 7.1 ya dawa, ndani ya lita 1 ya maji kwa mti mkubwa.
◊ Upuliziaji unaanza mara tu
baada yakuona dalili
za mashambulizi yamilibagi.
◊ Marejeo ya
upuliziaji yafanyike kila baada ya siku 7 – 14 kutegemeana na hali ya
mashambulizi yalivyo.
No comments:
Post a Comment