KURASA

Monday, November 30, 2009

MABADILIKO YA TABIA YA NCHI KIKWAZO CHA KILIMO KWANZA

Katika miongo kadhaa ijayo kutakuwa na mabadiliko ya kitabia ya nchi katika hali ya hewa, hii inasababishwa na kuongezeka kwa kiwango cha joto katika dunia. Hali hii ina madhara ya moja kwa moja katika maji na uzalishaji wa chakula katika hali mbali mbali. Kuna dalil zilizo wazi zinazoonyesha kwamba nchi masiki zinazoendelea ikiwamo Tanzania ndizo zitakazo athirika zaidi kutokana na mabadiliko haya ya hali ya hewa kitabia.

Jamii zilizoko vijijini ambako ndio kuna watu wengi zaidi na wanategemea kilimo kama ajira yao au chanzo cha mapato ndiyo itakayo athirika zaidi na kusababisha wimbi la kuhamia mijini kuongezeka, Katika kilimo maji ndiyo hutumika sana na kutokana na mabadiliko haya kiasi cha mvua kitapungua kunyesha, kuna watakao amua kuhamia kulima kwenye vyanzo vya maji au maeneo tengefu ili kuweza kuhimili hali ya ukame, kwa kufanya hivyo basi hata upatikanaji wa maji kwenye mito na chemi chemi pia utaathiriwa kwa kiwango kikubwa



Kukoseka kwa maji ya uhakiwa kwa wakazi wa vijijni kutasababisha magonjwa ya milipuko kama kuhara, kichocho na hata kipindupindu kuibuka na hivyo wana vijiji kupoteza maisha, visima vichache ambavyo ni vyaasili na hata vile vya kuchimbwa ambavyo ni vifupi navyo vitakuwa havina maji kwa kipindi kirefu cha Mwaka.

Kuna haja kubwa kwa mamlaka husika za serekali kama Hali ya hewa, kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na nyinginezo kujiandaa mapema na kuwaanda wanavijiji na hali hiyo, kuna njia kama kubadili aina ya mazao na wanyama, namna ya ulimaji mfano kuanza kilimo cha umwagiliaji cha uhakika, pia kunahitajika aina mpya za mbegu kulingana na mahitaji ya hali ya hewa zaidi ikiwa ni za muda mfupi na zenye kuhitaji mvua pungufu lakini zenye kuzaa zaidi.

Aina za miti tuayopanda kwa ajili ya misitu yetu pia inabidi ibadilike, baadhi ya miti imelalamikiwa kwamba inaondoa maji mengi sana ardhini na hivyo kuwa chanzo cha ukame, ingawa bado utafiti unaendelea lakini miti kama mikaratusi na misoji ni dhahiri inatumia maji mengi katika ukuaji wake

Thursday, November 26, 2009

VITUNGUU

Ndugu Bunyanza kwa mara nyingine tena alitaka kujua kuhusu zao la vitunguu, na mimi bila hiyana naelezea yale machache ninayoyafahamu.



Zao la vitunguu hulimwa karibu kila mahali hapa nchini. Hata hivyo, mikoa inayolima kwa wingi ni Tanga, Arusha, Iringa, Kilimanjaro, Singida, Morogoro, Mara, Mbeya Dodoma na Manyara. Zao hili ni la biashara na chakula. Ekari moja inaweza kuzalisha gunia 80 – 100 za vitunguu zikitunzwa kitaalam, na mkulima anaweza kulima mara mbili kwa Mwaka kwa mbegu kubwa ambazo huchukua hadi miezi mitano (5) shambani. Bei ya wastani kwa gunia moja ni Tsh 60,000

MAMBO YA KUZINGATIA WA K ATI WA UZALISHAJI

Ili kupata vitunguu bora na vingi ni muhimu kuzingatia kanuni za kilimo bora cha vitunguu.Baadhi ya kanuni hizo ni kama zifuatazo: -



1 - Kuchagua aina ya mbegu

• Chagua aina bora kulingana na matakwa ya soko
• Pamoja na mahitaji ya soko ni muhimu pia kuchagua aina inayovumilia magonjwa, wadudu,kukomaa mapema na kutoa mazao mengi na bora.

2 - Kuweka mbolea
Vitunguu hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha.
• Tumia mbolea za asili ili kurutubisha udongo kwa lengo la kupata mazao mengi na bora.
• Iwapo ni lazima kutumia mbolea za viwandani muone mtaalam wa kilimo ili akuelekeze namna ya kutumia. Mbolea ikizidi huharibu ubora wa vitunguu.

3 - Kumwagilia maji
• Kagua shamba kuona kama udongo una unyevu wa kutosha. Iwapo unyevu ni mdogo mwagilia maji kufuata mahitaji ya mmea. Vitunguu vinapoanza kukomaa punguza kumwagilia ili kuepuka kuoza



4 - Kupalilia
• Palilia mara kwa mara ili kudhibiti magugu na kuwezesha vitunguu kutumia vizuri unyevu na virutubishi vilivyoko kwenye udongo. Pia magugu mengine huficha wadudu waharibifu kama vile utitiri mwekundu.
• Wakati wa kupalilia epuka kukata mizizi ya mimea.
• Pandishia udongo na kufunika shina la kitunguu wakati wa kupalilia ili kuzuia jua lisiunguze mizizi na kubabua vitunguu. Vitunguu vilivyoungua na kubabuliwa ubora wake hushuka napia huharibika upesi wakati wa kuhifadhi.

5 - Kudhibiti magonjwa na wadudu
Vitunguu hushambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali ambao huweza kusababisha upungufu na ubora wa mazao. Ili kudhibiti tatizo hilo kagua shamba mara kwa mara kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili za mashambulizi, chukua tahadhari ya kunyunyuzia dawa mapema kabla madhara hayajaleta upotevu mkubwa.

6 - Kupanda kwa nafasi:
Zingatia nafasi ya kupanda inayopendekezwa ili kupata vitunguu vyenye ukubwa uliokusudiwa. Wastani ni inchi 4 - 5 kutoka kitunguu kimoja hadi kingine, na inchi 12 - 18 kutoka mstari hadi mstari na kipandwe inchi 1 - 1.5 chini ya udongo

MAANDALIZI KABLA YA KUVUNA

1 - Kukagua shamba
• Kagua shamba ili kuhakikisha kuwa vitunguu vimekomaa. Vitunguu huwa tayari kuvunwa miezi mitatu hadi mitano tangu kusia mbegu kutegemea aina ya mbegu na hali ya hewa.Dalili za vitunguu vilivyokomaa:

• Majani hunyauka na kuanza kukauka
• Asilimia kumi hadi 20 ya mimea huanguka majani na shingo hulegea.
• Majani hubadilika rangi kuwa ya manjano na baadaye kaki

VITUNGUU VILIVYOKAUKA MAJANI TAYARI KWA KUVUNA



2 - Kuvuna
Vitunguu vinapaswa kuvunwa mapema mara tu vinapokomaa ili kupata mazao mengi na bora.Uvunaji hufanyika kwa mikono ambapo jembe uma hutumika kuchimbua au kulainisha udongo.Udongo ukishalainishwa vitunguu hung’olewa kwa mkono. Inashauriwa uvunaji uanze asubuhi ili vitunguu viweze kunyauka na kukomaza ngozi sehemu za michubuko. Vitunguu visiwekwe juani na inapobidi kukomaza ngozi shambani, majani ya vitunguu yatumike kufunika vitunguu ndani ya matuta yake wakati wa mchana ambapo kuna jua. Kusanya vitunguu kwenye vikapu kisha vipeleke sehemu ya kukaushia. Vitunguu vya kukaushia kwenye kichanja ni bora zaidi, mizizi na majani hupunguzwa na kuachwa urefu wa robo inchi . Vitunguu vya kukausha kwa kunining’iniza havikatwi majani bali hufungwa kwenye mafungu na kupelekwa sehemu ya kukaushia.

Saturday, November 21, 2009

MAHINDI NA MPUNGA KIPI KINA FAIDA ZAIDI

Kutokana na maombi ya Ndugu Buyanza ya kutaka kufahamu kati ya kilmo cha mahindi na Mpunda kipi kina faida zaidi, nami nimejaribu kuchambua kidogo kati ya mazao haya mawili

MPUNGA
Katika hecta moja ya mpunga unaweza kuzalisha mpaka kilo 3675 kwa mkupuo mmoja, kama shamba ni jipya itakuchukua miezi 6 mpaka kuanza uvunaji, hii ni kwa sababu ya kuliandaaa shamba lako, baada ya mvuno wa kwanza utaweza kuvuna mara 3 kwa Mwaka. Hii inamaanisha kwamba unaweza kuvuna kiasi cha tani 10 -11 kwa Mwaka kama utafanya kilimo cha umwagiliaji.



Kilo ya mpunga sasa hivi ni shilingi 700 – 800 ingawa bei hupanda baadae kama utahifadhi mpunga wako kwa maana hiyo kwa Mwaka unaweza kupata kati ya shilingi milioni 7 mpaka milioni 8, gharama za kulima mpunga ni wastani wa asilimia 20- 22 ya mauzo, kwa maana hiyo kwa Mwaka kilimo chako kitatumia si zaidi ya shilingi milioni 2 kwa mara zote 3 utakazolima, hii ikijumuisha vibarua na mbolea.



MAHINDI


Kama utalima mahindi, ambayo unaweza kulima mara 2 kwa Mwaka kwa ukanda wa pwani na mara moja kama nisehemu zenye baridi, MAvuno kwa hecta moja ni kilo 7500 kwa maeneo yenye baridi na kilo 5000 kwa ukanda wa pwani ambapo utavuna kilo 10,000 kwa Mwaka. Bei ya mahindi kwenye soko ni wastani wa shilingi 400 kwa maana hiyo unaweza kupata shilingi milioni 4 kwa Mwaka.



Matumizi ya mbolea za viwandani ni lazima ili kufikia mavuno haya, Mbolea kama UREA itawekwa mara mbili wakati wa kupandia na kukuzia ikichanganywa na DAP (diamonium phosphate) ghara jumla ya mbolea hizi kwa mpando mmoja hufikia kiasi cha shilingi laki 7 mara mbili ni shilingi 1,400,000 ukongeza na gharama za kuandaa shamba na kupalilia kama 200,000 unapata jumla ya 1,600,000 kwa hiyo utabakiwa na kama shilingi 2,400,000



HITIMISHO
Mpunga ukilimwa kitaalam unawezza kukupatia faida shilingi milioni 5 kwa Mwaka, wakati mahindi yatakupatia shilingi milioni 2.5, faida ya mpunga inakuwa kubwa kwa sababu utalima mara 3 kwa Mwaka lakini kama utategema mvua utalima mamra 2 tu kwa Mwaka na utapata faida ya shilingi 3,300,000 kwa Mwaka

Hizi data ni kwa uzoefu wangu tu wa haraka haraka, bei ya mazao inaweza kupanda au kushuka na kiasi cha uzalishaji kwa hecta kinaweza kupanda au kushuka kutokana na aina ya mbegu, hali ya hewa na uzoefu wa mkulima mwenyewe. Kwa sasa hivi kilo ya unga wa mahindi ni shilingi 700 na debe la mpunga wa kyela ni shilingi 20,000, unaweza kupata faida zaidi kama utaachana na madalali na kupeleka mazzao yako sokoni mwenyewe

Thursday, November 19, 2009

MIGRAVILLEA

Kutokana na maombi ya ndugu Leonard Kisenha mwenye shamba lake pale Goba, alitaka kujua kati ya Mitiki/misoji na migavilea (GRAVILLEA ROBUSTA), je ni miti gani itamfaa kupanda kwenye shamba lake? Jibu ni rahisi ukuaji mpaka kuvuna umri ni karibia sawa sawa ila wakati wa kuvuna mwenye mitiki atapa faida nyingi sana (maradufu) kutokana na bei ya mitiki kuwa juu sana, pia hali ya hewa ya pwani kwenye joto inafaa zaid kwa mitiki tofauti na migravilea ambayo hukua vizuri zaidi kwenye baridi



Asili ya miti hii ni nchini Australia lakini nchini Coasta rica na Guantemala (mita 1000 kutoka usawa wa bahari) Afika Mashariki (1200m – 1800m) Sri lanka (600m – 2000m) Israel, Cyprus na Afrika ya Kusini huota yenyewe ikichanganyika na miti ya mikaratusi. Miti hii hustawi zaidi kwenye maeneo yasiyo na joto na inahimili hali ya hewa hata kufikia kuganda ndio maana ukanda wetu hustawi zaidi mikoa ya Mbeya, iringa, Songea, Arusha, Kilimanjaro, Tanga (Lushoto)

Miti hii hukua hadi kufikia mita 30 – 35 ikiwa na kipenyo cha wastani 50cm – 60cm, inakuwa na majani kipindi chote cha Mwaka huwa na magamba ya kahawia huku mbao zake zikiwa na rangi nyekundu kuelekea hudhurungi iliyo kolea, huweza kuhimili kuota kwenye mchanga na udongo wenye asidi 5 – 7ph ingawa hukua vizuri zaidi kwenye udongo wenye rutuba na usiotuamisha maji.



Kiasi cha mvua kinachohitajika ni wastani wa 1200mm – 1800mm kwa mwaka, hutoa maua yenye rangi ya njano na kishubaka cha mbegu huwa na urefu wa senti meta 2 ambazo kwa Tanzania hukomaa kuanzia mwezi 5 mpaka 8, mbegu zake ni nyembamba kama karatasi (kilo moja huwa na mbegu 50,000 mpaka 150,000)

Umri mzuri wa kuvuna tangu kupandwa ni miaka 15 ambapo mbao nzuri hupatikana, lakini mti unaweza kuvunwa kabla ya hapo kama utahitajika kwa matumizi mengine kama kuni au nguzo za kujengea, mti huu unaweza kupandwa kwa ajili ya kivuli, mapambo au hata mipaka ya shamba na kuzuia upepo



Gamba la mbegu zake huwa gumu kiasi, njia nzuri ya kuhakikisha zinaota kwa wingi ni kwa kuzipitisha kwenye moto kidogo (heat seed scarification) mbegu zikiachwa wazi huweza kukaa bila kuharibika kwa miezi 2 – 3 lakini kama zitahifadhiwa kwenye mifuko ya plastic kwenye hali joto ya sentigredi 4 na unyevu kiasi cha asilimia 60 kisha mfuko ukazikwa kwenye mchangamkavu ulio ndani ya chombo maalum, basi mbegu huweza kuhifadhiwa mpaka miaka miwili

Thursday, November 12, 2009

KASUKU - DONDOO ZA KUMFUNDISHA KUONGEA



Watu wengi wamekuwa wakipenda kufuga kasuku lakini utakuta wanalalamika kwamba kasuku wake haongei, nimeamua kuweka vidokezo muhimu ili mfugaji aweze kuzingatia wakati wa kumfundisha
Kuna aina nyingi za kasuku duniani wengine wakiwa na rangi za kawaida na wengine wakivutia sana, kwa kawaida huwa hawaishi sehemu zenye baridi kali kwani hupendelea hali ya joto wastani

UCHAGUZI WA KASUKU
Mbegu kubwa ni waongeaji wazuri, mbegu ndogo ni wavivu kujifunza,
Akiwa mdogo anajifunza vizuri zaidi, ukiweza mpate yule anayetoka kulelewa kwenye kiota na ndio anajifunza kuruka/kupaa
Kasuku muoga hawezi kujifunza vizuri.
Kasuku mwenye tabia ya kung'ata anauwezo mkubwa wa kujifunza kungea.




MAZINGIRA
Kumbuka kasuku hujifunza maneno machache tu hawezi kuongea kama mtu.
Sehemu nzuri ya kumuweka nyumbani ni jikoni, kwa sababu kuna shughuli nyingi.
Huanza kuongea katika umri wa miezi 4-6.




UFUNDISHAJI
Wakati wa kumfundisha zima radio na TV (kusiwe na kelele)
Muda mzuri wa mafunzo ni asubuhi na jioni.
Mfundishe kupiga miluzi baada ya kuweza kuongea baadhi ya maneno na si kabla ya hapo.
Kumbuka kasuku hujifunza vizuri zaidi kwa vitendo mfano unamtoa nje ya kibanda chake huku unamwambia " toka nje mmmh" ukirudia rudia, jitahidi kutumia Mmmh kila baada ya neno, hii humsaidia kujifunza kwa urahisi.
Hakikisha anapata mlo kamili maji na matibabu

Saturday, November 7, 2009

SAANEN MBUZI BORA WA MAZIWA




ASILI Switzerland katika ukanda wa Saanen

RANGI nyeupe au maziwa

UZITO kilo 65-68

MAZINGIRA yasiyo na joto, wanapendelea baridi chini ya sentigredi 15c



UZAZI mtoto moja au mapacha (kila mwaka mara mbili)

UZALISHAJI lita 4 mpaka 7 kwa siku (mikamuo miwili)

MASIKIO yamesimama wima

MKIA umelala tofauti na mbuzi wengi ambao husimamisha mkia

NDEVU majike yana ndevu mara chache ingawa si nyingi kama madume

PEMBE ndefu zilizosimama wima

Monday, November 2, 2009

BORAN - MBEGU BORA YA NG'OMBE WENYE ASILI YA AFRIKA MASHARIKI

Asili yake ni maeneo ya borana kusini mwa Ethiopia ambako alipatikana baada ya mbegu tatu za ng’ombe zilichanganyika kwa bahati mbaya kutoka kwa wafugaji wa kienyeji waliotoa ngombe wao kutoka pande tofauti za afrika, hiyo ilikuwa zaidi ya miaka 1300 iliyopita lakini sasa hivi kuna taasisi inayoitwa Boran cattle breeder’s society iliyopo nchini Kenya.

DUME BORA LA BORAN


Taasisi hii iliamua sasa itafute mbegu bora ya Boran kwa kutumia njia za kitaalam tofauti na hapo mwanzo ambako Boran alitokea tu bila hata wafugaji kujua kwamba wanatengeneza mbegu bora ya ng’ombe.

JIKE BORA LA BORAN


Waalamu wa kupandisha (breeders) waliamua kuangalia vinasaba bora zaidi na kumfanya Boran awe wa kisasa zaidi na kuweza kuhimili hali ya Afrika mashariki huku uzalishaji wa maziwa na nyama ukiongezeka zaidi kuliko ule wa ng’ombe wetu wa kienyeji, Boran wa kisasa ana damu za aina tatu katika uwiano ufuatao N’gombe wa ulaya wasio na nundu (european bos taurus) 24% Ng’ombe wa Afrika mashariki wenye nundu wajulikanao kama Zebu (bos indicus)64% na ngombe wafrika wasio na nundu (african bos taurus ) 12%



SIFA
-Ni mkubwa kuliko ng’ombe wa kienyeji
-Ana kiwele cha wastani na chuchu ni kubwa kidogo
-Anazaa ndama wa wastani (kilo 25 – 28) kwa hiyo hakuna matatizo wakati wa kujifungua lakini watoto hukua haraka na ni mara chache sana ndama kufariki
-Anahimili hali ya mazingira ya Afrika kuliko ng’ombe wa kisasa (joto na magonjwa)
-Ngombe jike anaweza kuzaa bila matatizo mpaka akiwa na miaka 15, madume yanauwezo wa kuzalisha mpaka miaka 16
-Majike hubalehe baada ya siku 385 (mwaka na siku chache)
-Ni wapole na wenye nguvu kwa hiyo hufaa kwa shughuli za kulima na kukokota mikokoteni (maksai)
-Anaongezeka uzito haraka hata kama anakula majani makavu, majike yanayo nyonyesha hupungua uzito kidogo sana kipindi cha kunyonyesha
-Wanakula kwa mshikamano na hawatawanyiki wakiwa machungoni kiasi kwamba inakuwa vigumu kumuiba mmoja au kumtenganisha na wenzake

BORAN WAKICHUNGWA KATIKA KUNDI LENYE MSHIKAMANO



Wafugaji wengine wamejaribu kuchanganya mbegu hii na mbegu nyingine za kisasa kutoka bara la ulaya ili kuongeza uzalishaji wa maziwa au nyama kama wanavyoonekana hapo chini kwenye picha

BORAN NA FRIESIAN (maziwa)


BORAN NA BEEFMASTER (nyama)



BORAN NA JERSEY (maziwa)


BORAN NA DRANKENSBERGER (nyama na maziwa)

Friday, October 30, 2009

MABUA YA MAHINDI, NG'OMBE NA SAMADI-KUNA FAIDA HAPA

Unafahamu ni kiasi gani cha mabua kinabaki baada ya kuvuna shamba lako la mahindi? Jaribu kutazama vizuri shamba lako kwa macho na hutaamini !!!!!!!!!!! karbu nusu ya kile ulichovuna kimebaki shambani kama mabua yaani ile mbolea ya samadi uliyoweka bado iko shambani katika mfumo mwingine.

Mabua yanaweza kulishwa tena wakati wa ukame yakikatwa katwa na kuchamnganywa na molasses, ekari moja ya mabua intosha kumlisha ng’ombe mmoja mwenye kilo 500 kwa miezi miwili. Hili ni zoezi lenye lengo la kupunguza gharama na kuongeza faida lakini linahitaji umakini kidogo, ninashauri mara tu baada ya kumaliza kuvuna mabua haya nayo yavunwe na kuhifadhiwa sehemu yenye kivuli, na hao utaweza kumlisha mnyama wako mabua yakiwa na 65% chakula chakula mmeng’enyo (digestable food) huku kukiwa na protini kiasi cha 7%



Kama hunasehemu ya kuhifadhi mabua haya unaweza kuwachungia humo humo shambani ng’ombe wako ili wale wenyewe ila utahitajika kuwawekea mawe yenye madini ili walambe, kwa kuwachungia shambani ng’ombe wako utapata faida zifuatazo, kwanza hutahitaji kusafirisha mbolea ya samadi na kuirudisha shambani, pia nombe wanapo kanyaga shamba husaidia kupunguza mmong’onyoko wa udongo. Kama msimu uliopita ambao ndio mahindi yalilimwa kulikuwa na upungufu wa mvua inabidi uwe makini maana mabua yatakuwa na kiwango kikubwa cha madini ya nitrate ambayo yana madhara hasa kwa wanyama wanaokua wenye mimba au kunyonyesha, ili kuepuka hili unaweza kuwalisha wanyama wako chakula kingine kwanza na kumalizia na mabua au kama umeyakata basi changanya na majani mengine kasha ndio uwalishe. KUMBUKA ng’ombe mwenye kilo 500 anaweza kuzalisha molea hadi kilo 12 kwa siku je hii si faida kubwa?

Wednesday, October 14, 2009

TARATIBU NA MASHARTI YA MIKOPO YA KUNUNUA TREKTA JIPYA



1. Mwombaji atajaza fomu maalum ya maombi inayopatikana katika Ofisi za kilimo za Halmashauri za Wilaya na Makao makuu ya Mfuko wa Pembejeo, jijini Dar-es-salaam na katika tovuti ya wizara ya kilimo.

2. Fomu za maombi zilizojazwa na kuambatanishwa na vielelezo vinavyohitajika zitapitishwa/kuidhinishwa na Afisa Kilimo wa Maendeleo ya Mifugo wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya husika na baadaye kutumwa mapema kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Pembejeo.

3. Mikopo ya kununua matrekta inatolewa na Mfuko wa Pembejeo, baadhi ya benki na taasisi za fedha na SCCULT (T) Ltd. kwa niaba ya Mfuko, mwombaji sharti atimize yafuatayo:-

(A) Awe na dhamana yenye hati miliki isiyohamishika iliyoandikishwa kwa jina la mwombaji.
(B) Awe na shamba binafsi lisilopungua hekta 50 na awe tayari kutoa huduma ya kuwalimia wakulima wengine
(C)Awe tayari kutekeleza masharti yote ya Mfuko wa Pembejeo au taasisi ya fedha na SCCULT yanayohusu mkopo wa ununuzi wa trekta jipya.
(D)Awe tayari kulipa asilimia moja (1%) ya mkopo kama gharama za nyaraka za mkopo na kusajili trekta kwa pamoja kwa jina lake na Mfuko
(E) Riba inayotozwa ni asilimia nane (8%) na marejesho hufanyika kwa muda wa miaka mitatu kila baada ya miezi mitatu.

Saturday, October 10, 2009

KUKATA PEMBE NA KUZUIA PEMBE KUOTA

Mnyama asiye na pembe hasa ng’ombe hupunguza uwezekano wa wanyama kuumizana na hata kuwadhuru binadamu, wanyama wadogo kama miezi miwili hadi mitatu ni vizuri wakachomwa ili kuzuia pembe kuota (disbudding) lakini kama pembe zimetokeza hamna jinsi ila kuzikata kwa kutumia msumeno au waya maalum (phatetomy wire)

DISBUDDING IRONS


Zoezi la kuzuia pembe kuota hufanyika kwa kutumia vyuma maalum (disbudding iron) ambavyo hupashwa moto na kuwa vyekundu, ndama huandaliwa kwa kulazwa chini na kisha kupunguzwa manyoya sehemu itakayochomwa ambapo ni pale pembe zinakoota, unaweza kuitambua sehemu hii kwa kupapasa na utaona kama pembe ndogo ndani ya ngozi. Sehemu husika isafishwe kwa spirit au eusol kabla ya zoezi kuanza.



Mtaalamu wa mifugo ndiye atakaye fanya zoezi hili kwa kufuata kanuni za kitaalam, kabla ya kuanza zoezi ni muhimu mnyama kupigwa sindano ya ganzi, kisha sehemu husika huchomwa na chuma cha moto, na chuma kuzungushwa kila upande na mwisho kama anazibua ataondoa kile kipande kinachoota na kumalizia kwa kukausha sehemu iliyobaki kwa kutumia chuma kile kile, baada ya hapo dawa za kupulizia za vidonda, iodine tincture au dawa za kufukuza wadudu hupakwa sehemu husika na mnyama huachiwa huru.



Kuhusu ukataji wa pembe ambayo imeshaota, baada ya mnyama kufungwa na kulazwa chini huchomwa ganzi na ukataji huanza. Kama utatumia msumeno lazima damu nyingi itatoka, zuia damu hii kwa kuunguza sehemu ndogo ya pembe iliyobaki kwa kuichoma na disbudding iron au chuma chochote cha moto. Inashauriwa kutumia phatetomy wire kwa sababu wakati unakata pembe waya huu huunguza pembe na kufanya damu isitoke kabisa



Kuna baadhi ya aina za ngombe wa kisasa hazina pembe kabisa mfano Hereford na mbegu kama Friesian baadhi yao huwa hawana pembe, kwa mbegu za kienyeji kama zebu (SHZ)huwa na pembe fupi fupi

Saturday, October 3, 2009

KUKU WA KIENYEJI - UFUGAJI BORA




Kuku hutoka kwenye kizazi kinachojulikana kitaalam kama gallus gallus, Ufugaji huu nitaoelezea ni wa kienyeji kabisa ila huu umeboreshwa kidogo ili kuleta faida zaidi, kwanza itabidi uwe na eneo lakutosha kama ekari mbili (70m *140m) banda la kuku liwe linalohamishika na liwe limejengwa juu juu, hii husaidia kupunguza maambukizi ya magonjwa kwa sababu kinyesi cha kuku kikilundikana huweza kubeba vimelea vya magonjwa

BANDA BORA LINALOHAMISHIKA


Banda liwekewe viota vya kutagia na unaweza kuwafundisha kuku kuvitumia mapema kabla ya kuanza kutaga kwa kuchelewa kuwafungulia asubuhi. Kwa kawaida kuku hupenda kulala bandani wakiwa juu juu kwa hiyo uweke baadhi ya fito au mbao nyembamba zikining’inia pia kuwe na vyombo vya chakula nje ya banda

Hakikisha banda halivuji na wanyama wakali hawaingii lakini liwe na hewa ya kutosha na lisiwe na joto wala baridi kali, ni vizuri ukiliweka chini ya miti
Ili kuboresha ufugaji huu inashauriwa kutumia majogoo ya kisasa ambayo yana patika kwa mazalishaji wa kuku kote nchini, pia unaweza kutumia majogoo ya kuku aina ya KUCHI wanaopatikana zaidi miko ya Singida na Shinyanga. Majogoo ya kisasa huweza kuhudumia wastani wa majike 20-25 na kuchi huweza kuhudumia majike 10 -15 kwa sababu ni wavivu kidogo

MAJOGOO YA KISASA INA YA CORNISH


Andaa na banda la kukuziA watoto ambalo litawakinga na wanyama wakali na mwewe, banda linakuwa wazi juu hukulikizuiwa na waya kwa 75% na 25% iwe imezibwa kwa mbao ili kuwapatia kivuli wanapohitaji, banda hili lina hitaji kuhamishwa hamisha angalau mara 5 kwa siku kutika mahali pamoja hadi pengine, hakikisha banda la watoto lina maji na chakula muda wote, pia kumbuka kuwawekea mabaki ya mboga za majani kama mchicha, kunde, kisamvu n.k




FAIDA
(A) Mfumo hauhitaji chakula maalum kama kuku wa ndani
(B) Wadudu kama utitiri na virobot hushambulia kuku mara chache
(C) Kuku hupata muda wa mazoezi kwa kutembea tembea
(D) Gharama za uendeshaji ni kidogo
(E) Hautumii muda mwingi
(F) Kiasi cha uchafu ni kidogo

HASARA
(A)Vifaranga huweza kuliwa na mwewe au wanyama
(B) Mayai huweza kupotea yakitagwa nje ya banda
(C)Kuku huweza kula mbegu zilizopandwa mashambani
(D)Vifo vya kuku ni vingi

CHANJO
Kuku wapewe chanjo ya kideri/mdondo kila baada ya miezi mitatu chanjo hii hupatikana nchini kote ukifika dukani ulizia chanjo ya newcastle, utapata maelekezo ya jinsi ya kuwawekea kuku kwenye maji ya kunywa, chanjo hii wapewe kuku wazima tu na wagonjwa watengwe mbali

MINYOO
Kuku hunyweshwa dawa ya minyoo kila baada ya miezi mitatu, kuna dawa kama piperazine na nyinginezo ambazo huwekwa kwenye maji

CHAWA NA UTITIRI
Unaweza kutumia dawa za kuogeshea mifugo kama ecotix au dawa ya unga unga ya kunyunyuzia kama akheri powder, dawa ya akheri unaweza kuimwaga bandani na kisha kumnyunyuzia kuku mwilini ukiwa umemning’iniza kichwa chini miguu juu ili mayoya yaacha nafasi ya dawa kuingia

MAGONJWA YA MAPAFU
Kuna magonjwa mengi yanayoshambulia mfumo wa hewa, dawa ya tylosin inauwezo mkubwa wa kupambana na magonjwa karibu yote, wape dawa hii mara tu unapoanza kuona dalili za mafua

Tuesday, September 29, 2009

SEHEMU YA 4 - MATUNZO YA WATOTO WA NGURUWE




Kwa kawaida hunyonya kwa wiki 5 -8, na baada ya hapo hutengwa na mama yao na kuanza kupewa chakula chenye protini 25% kwa muda wa wiki 6 za mwanzo

KUKATA MENO
Mara baada ya kuzaliwa watoto wakatwe meno kwa kutumia mkasi mkubwa au kifaa cha kukatia waya (wire cutter) umuhimu wa zoezi hili ni kwa sababu nguruwe huzaliwa na meno na mara wanapoanza kunyonya huumiza chuchu za mama yao na kumsababishia ugonjwa wa chuchu (mastitis)

MADINI CHUMA
Wakizaliwa tu wanahitaji madini ya chuma kwa wingi, maziwa ya mama yanatoa kiasi cha 10% tu, huwa wanapigwa sindano (Iron Injection) kiasi cha 155mg kwa kitoto kimoja ili kuwaongezea madini ya chuma ya ziada, muone mtaalamu wa mifugo akusaidie kwa hili



KUHASI
Madume ambayo yatakuzwa kwa ajili ya nyama ni vizuri yakahasiwa, hii husaidia ukuaji wa haraka na pia huondoa harufu ya balehe, Zoezi hili lifanyike wakati wakiwa na wiki 2-3 inapofika wiki ya 5 zoezi huanza kuwa gumu kwa sababu watoto wanakuwa wakubwa na litahitaji sindano za ganzi, zoezi hili linahitaji mtaalamu wa mifugo.

MINYOO
Mzazi anapokaribia kujifungua wiki ya mwisho achomwe sindano ya kuondoa minyoo na magonjwa ya ngozi ijulikanayo kama IVOMEC SUPER au IVERMECTIN zinazopatikana kote nchini, dawa hii husaidia kuwalinda watoto na minyoo hadi wanapoacha kunyonya ndio na wao wapigwe sindano hii ambayo pia itasaidia kuua minyoo ya mapafu, minyoo ya macho, viroboto na kuondoa ukurutu.



CHAKULA
Baada ya wili chache vitoto vitaanza kula chakula kidogo kidogo kwa kuanzia na kile anachopewa mzazi, hakikisha mzazi anapewa chakula kingi na chakutosha kwa sababu atakuwa anakula yeye na watoto wake

KITIMOTO SEHEMU YA 3 - NGURUWE JIKE (MZAZI)

UCHAGUZI
Yawe na chuchu zisizopungua 18 na chuchu ziwe nene na ndefu, chuchu fupi na ndogo huleta matatizo wakati wa kunyonya , kumbuka mtoto wa nguruwe chuchu atakayo nyonya siku ya kwanza ndiyo hiyo hiyo atakayonyinya mpaka atakapoacha kunyonya
Awe na miguu ya wastani yenye nguvu na isiwe na kasoro kama matege au kukaa upande na kucheche mea, hii humsaidia kuhimili madume makubwa
Uke uwe na ukubwa wa kutosha na umbo la kawaida, pia upimwe na mtaalamu kwa kuingiza vidole na kuangalia kama wakati wa kuvitoa vina kwama kwama, hii huwa dalili ya majike dume (hermaphrodites)



CHAKULA
Maji yalishwe chakula cha kunenepesha mpaka yakifikisha uzito wa kilo 80, baada ya hapa yapewe chakula maalum cha wazazi ambacho kitasaidia wasinenepeane na kuwa na mafuta mengi kwenye njia ya uzazi

BANDA
Majike hukaa moja moja au mengi kwenye banda moja muda wote (kipimo ni 2.5m *1.5m ) kwa kila nguruwe kasoro tu yanapokaribia kuzaa ndio huhamishiwa kwenye banda la kuzalia

NGURUWE AKIWA KWENYE BANDA LA KUZALIA


UPANDISHAJI
Majike yapandishwe yakifikisha umri wa wiki 28 na uzito wa kati ya kilo 120 – 140, nguruwe aachwe mpaka aingie joto kwa mara ya 3 ndio apelekwe kwa dume ambapo kila baadda ya siku 21 nguruwe huingia kwenye joto

KUINGIA KWENYE JOTO
Dalili za joto ni guruwe kupiga kelele hovyona kuhangaika lakini ukimkandamiza kiunoni na mikono yako hutulia, uke huwa na rangi nyekundu na hutoa ute mweupe. Baada ya dalili za mwanzo nguruwe huwa tayari kupandwa baada ya masaa 38 – 42 na hudumu kwa masaa kama manne (4) inashauriwa ukiona tu dalili za mwanzo umpeleke jike kwenye banda la dume

MIMBA
Mimba huchukua siku 114 mpaka watoto kuzaliwa (miezi 3 wiki 3 siku 3) kipindi cha ujauzito nguruwe jike hula sana mpaka kiasi cha kilo 5 -7 kwa siku apewe mlo kamili lakini kuwe na umakini asinenepe sana na ikifika wiki ya mwisho ahamishiwe kwenye banda la kuzalia (furrowing pen)

BANDA LA KUZALIA


Liwe na ukubwa usiopungua 3m * 2m, liwe na sehemu ya watoto ambayo mama mtu hawezi kufika watoto waingie huko kwa kupenya, hii husaidia nguruwe asiweze kuwalalia watoto wake. Sehemu ya watoto iwe na chanzo cha joto kama vile jiko, hii husaidia kufundisha watoto wakimbilie kule muda wote

Friday, September 25, 2009

UFUGAJI WA NGURUWE - SEHEMU YA PILI

Sehemu ya pili ya maelezo kuhusu ufugaji wa nguruwe tuaangalia nguruwe dume ambaye ndiye atakuwa natumika kwa ajili ya kupandishia majike kwenye mradi wa nguruwe, wengine huwa wanatumia madume ya kukodi, lakini kama utakuwa na majike zaidi ya 10 utahitaji kuwa na dume kwenye mradi wako,

UCHAGUZI WA DUME
Dume litoke kwenye kizazi ambacho hakina historia ya magonjwa na wana historia ya kuzaa watoto wengi ,wenye afya bora, na ukuaji mzuri, angalia kizazi/ukoo wake uwe na chuchu nyingi zisizopungua 14 zikiwa 18 ni nzuri zaidi

BANDA LA DUME
Liwe na ukubwa usiopungua 3 m * 2.5m geti liwe lachuma na linafunguka kuelekea kwa ndani na nje pande zote mbili, siku zote majike ya pelekwe kwa dume na si kinyume chake.

CHAKULA
Dume alishwe kilo 2 – 3 za mlo kamili wenye kiasi cha wastani cha protini, epuka kumlisha mashudu mengi kwa sababu yana kuwa na kemikali inayojulikana kama omega 3 fatty acids ambayo hupunguza kiasi cha manii kwa nguruwe, tumia mimea kama lukina na desmodiam au dagaa kama chanzo cha protini

UPANDISHAJI
dume aina ya saddle back akimpanda jike aina ya landrace


Madume huanza kupanda yakifikisha umri wa miezi 12 – 14 hupanda jike moja mara 2 kwa siku na hupanda majike 6 kwa kila siku 8 na majike yasifululize kwa zaidi ya siku mbili zinazofuatana, majike yapelekwe asubuhi mapema kabla ya dume kula chakula
Dume linaweza kuendelea kutumika kwa upandishaji mpaka likifikisha miaka 3 – 4 ndipo unaweza kuanza kutumia dume lingine, uzoefu unaonyesha nguruwe chotara huwa na uwezo wa kupanda mara nyingi na kwa muda mrefu zaidi. Dume moja huweza kuhudumia majike 20 lakini kwa matokeo mazuri tumia dume moja kwa kila majike 15 – 18

UFUGAJI WA NGURUWE - SEHEMU YA KWANZA

Kutokana na maombi ya Bw John Mwaipopo kuhusu ufugaji wa Nguruwe na kuku, leo nimeamua kuanza kumuelezea njia bora na sahihi

AINA ZA NGURUWE (baadhi)
LARGE WHITE


-Hii ndiyo aina kubwa zaidi ya nguruwe wa kufugwa nyumbani
-Kama jina lake lilivyo ana rangi nyeupe mwili mzima
-masikio yake yamesimama wima
-Ana sura iliyobonyea kwa ndani (dish faced)

LANDRACE


-Weupe mwili mzima
-masikio yamelala kabisa
-Wana ukubwa wa wastani

SADDLEBACK


-Ni wakubwa
-Wana rangi nyeusi na mstari mweupe kuzunguka shingo na miguu ya mblele
-Masikio yamelala kiasi


DUROC

Asili yao inatoka tangu mwaka 1812 katika majimbo ya New York na New Jersey ambako ndio walizalishwa kwa mara ya kwanza ingawa pia kuna tetesi kwamba waliletwa toka Uingereza

Wana rangi ya kahawia iliyooza mpaka iliyopauka na kutaka kuwa kama njano, wana masikio yaliyolala kwa mbele na sura ndefu ilyonyooka, wana nyama tamu sana na isiyo na mafuta mengi, ni Mbegu inayotumika Zaidi kwenye kuchanganya na Mbegu nyingine ili kupata uzao wenye nyama tamu na yenye mafuta kidogo, Madume ndio hutumika kwenye kupanda majike ya Mbegu nyingine kama Large White na Lamd race sababu ni kwamba majike ya Duroc hayazai watoto wengi

CAMBOROUGH

Hii ni Mbegu mpya ambayo inatokana na Mbegu za Large white na Land race ambao walichanganywa kitaalam  ili kupata sifa za uzazi wa watoto wengi, ukuaji wa haraka, kutumia chakula vizuri, uzalishaji maziwa wengi kwa ajili ya watoto, sifa ya kipekee ni uwezo wa majike kuendelea kuzaa kwa miaka mingi zaidi ukilinganisha na wengine.


Wana rangi nyeupe tupu, masikio yamelala kidogo kwa mbele na wana uso mrefu ulioonyooka, wana uzazi wa wastani watoto 14 na majike huanza kupandwa wakiwa na miezi 8 tu