KURASA

Monday, June 9, 2008

UPANDAJI

Upandaji wa mitiki huafanyika mara baada ya mvua za kwanza kuanza kwa sababu ukuaji wa miche midogo huitaji mvua za kuendelea kwa kipindi kirefu, pia mvua za kwanza huwa na nitrogen ya kutosha kusaidia ukuaji wa mimea.

Vipimo vya upandaji kati ya mche na mche ni mita 2.5 mpaka 3, kama utatumia kipimo cha mita 3 kwa 3 ekari moja (mita 70 kwa 70) itaingia miche kama 530 kwa wastani. miche ya mitiki hubananishwa wakati wa upandaji ili kuisaidia ikue kwa kunyooka kwenda juu ingawa mingine ya katikati itapunguzwa baada ya miaka 5 - 6 kuipa nafasi ile iliyobaki kama 260 iweze kunenepa zaidi.

Mashimo ya mitiki hayahitaji kuchimbwa kabla kwa sababu yanaweza kufukiwa na mvua, kwa kawaida mashimo haya yana kuwa na urefu usiozidi futi moja (urefu wa rula ya mwanafunzi) kwa hiyo siku ya upandaji wachimbaji wa mashimo ndio wawe wapimaji wa nafasi kati ya mti na mti. Wale wapandaji wahakikishe kwamba sehemu ya mzizi inakuwa chini ya ardhi na imefunikwa na udongo yote na sehemu ya shina inakuwa juu.

Miti ikishapandwa iachiwe sehemu kidogo ya kisahani kwa ajili ya kuhifadhia maji kidogo, nyasi kidogo zinaweza kuwekwa kuzunguka shina ili kuzuia unyevu kunyonywa na jua (evaporation) ingawa hii wakati mwingine inaweza kuwavutia mchwa wakashambulia mche wako.

Miche ikianza kuchipua baada ya siku chache vichipukizi zaidi ya kimoja vitachipua, hapa inatakiwa uvikate vyote na kubakiza chenya afya (viwili vitakuwa sawa)

UANDAAJI WA MICHE KABLA YA KUPANDWA

Upandaji wa mitiki hufanyika katika namna mbili, wa kwanza ni ule wa kupanda miche ikiwa mizima kutoka katika vifuko na ya pili ni kutumia miche toka kwenye kitalu ambako inashauriwa kuing'oa na kisha kukata sehemu ya mzizi na shina, ambako utabakiwa na mzizi 70% na shina 30%.

Kitaalamu miche iliyokatwa na kubaki kama vipandikizi ina sifa mbili kubwa
(a) Miche itakayoota katika vipandikizi hivi ina uwezo mkuwa wa kuhimili ukame iwapo kutakuwa na upungufu wa mvua za msimu wakati wa upandaji. Mara nyingi miche ikipandwa kwenye mvua pungufu, huua sehemu ya juu ya shina/mche na sehemu ya chini ya mzizi kama vile miti inavyopukutisha majani, na hii husaidia kuhifadhi maji ndani ya mmea. Sasa kabla hili halijatokea sisi tunakata kabisa hizo sehemu zitakazo kufa iwapo kutakuwa na mvua pungufu.

(b) Miti inayoota katika vipandikizi inaasilimia kubwa zaidi ya kukua kwa kunyooka kwenda juu, wakati miti iliyokulia kwenye vifuko ina uwezo zaidi ya kupinda kwa sababu wakati wa uotaji ikiwa midogo, miche hushindana kukua na kukimbilia mwanga wa jua. Wakati huu ndio mche huanza kupinda kufuata mwanga ili kushindana na ile iliyokua haraka. Ili kuepuka hili, kata miche yako na ianze kuchipua upya ikiwa shambani kwenye nafasi.

Vipandikizi vilivyokatwa vinauwezo wa kukaa mpaka siku 7 bila kufa hadi siku ya kupandwa shambani, kwa maana hiyo unaweza kuvisafirisha toka mkoa mmoja hadi mkoa mwingine kwenda kuvipanda. Kama utakuwa umeandaa vipandikizi vyako na mvua zikawa bado kuanza, weka udongo kwenye chombo chochote mwagia maji kidogo (yasituame) halafu chomeka vipandikizi vyako na usubiri siku ya mvua kuanza ili ukavipande

UANDAAJI WA SHAMBA

Kabla ya kupanda miche ya mitiki shamba ni lazima liwe limeandaliwa, uandaaji wa shamba ni lazima ufanyike mapema kabla ya mvua kuanza kunyesha kwa sababu upandaju huanza mara baada ya mvua za kwanza kunyesha.

Uandaaji wa shmba la mitiki ni wakawaida kama ule wa mashamba mengine, visiki vyote ni lazima ving'olewe kisha majani yote yalimwe na ikiwezekana yatiwe moto kwa umakini wa hali ya juu kuepusha madhara ya moto.

Kama ulimaji utakuwa ni wa trekta au kutumia jembe la kukokotwa na wanyama (plau) hii ni nzuri zadi kwa sababu majani yatafukiwa ardhini na kuongeza rutuba kwenye udongo. uuaji wa magugu kwa kutumia madawa kama round up wanamazingira huwa hatushauri, ingwa ni njia moja ya haraka na nafuu zaidi kuliko kulima kwa jembe lolote lile.

Kwa ukanda wa pwani mvua za masika huanza kati ya mwezi wa 3 - 4 kwa hiyo ni vizuri sana kama utaanza kuandaa shamba kwenye mwezi wa 2 (february) na mvua za vuli huanza kwenye mwezi wa 11 (November) kwa hiyo shamba liwe tayari kwenye mwezi wa 10 (October)

Ni vizuri pia ukaangalia na mwenendo wa mvua na lini zinategemewa kuanza kwa kupitia kwa wakala wa hali ya hewa hapa nchini (Tanzania Meteological Agency) kupitia tovuti yao ambayo ni
http://www.meteo.go.tz/wfo/seasonal.php