KURASA

Thursday, November 26, 2009

VITUNGUU

Ndugu Bunyanza kwa mara nyingine tena alitaka kujua kuhusu zao la vitunguu, na mimi bila hiyana naelezea yale machache ninayoyafahamu.



Zao la vitunguu hulimwa karibu kila mahali hapa nchini. Hata hivyo, mikoa inayolima kwa wingi ni Tanga, Arusha, Iringa, Kilimanjaro, Singida, Morogoro, Mara, Mbeya Dodoma na Manyara. Zao hili ni la biashara na chakula. Ekari moja inaweza kuzalisha gunia 80 – 100 za vitunguu zikitunzwa kitaalam, na mkulima anaweza kulima mara mbili kwa Mwaka kwa mbegu kubwa ambazo huchukua hadi miezi mitano (5) shambani. Bei ya wastani kwa gunia moja ni Tsh 60,000

MAMBO YA KUZINGATIA WA K ATI WA UZALISHAJI

Ili kupata vitunguu bora na vingi ni muhimu kuzingatia kanuni za kilimo bora cha vitunguu.Baadhi ya kanuni hizo ni kama zifuatazo: -



1 - Kuchagua aina ya mbegu

• Chagua aina bora kulingana na matakwa ya soko
• Pamoja na mahitaji ya soko ni muhimu pia kuchagua aina inayovumilia magonjwa, wadudu,kukomaa mapema na kutoa mazao mengi na bora.

2 - Kuweka mbolea
Vitunguu hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha.
• Tumia mbolea za asili ili kurutubisha udongo kwa lengo la kupata mazao mengi na bora.
• Iwapo ni lazima kutumia mbolea za viwandani muone mtaalam wa kilimo ili akuelekeze namna ya kutumia. Mbolea ikizidi huharibu ubora wa vitunguu.

3 - Kumwagilia maji
• Kagua shamba kuona kama udongo una unyevu wa kutosha. Iwapo unyevu ni mdogo mwagilia maji kufuata mahitaji ya mmea. Vitunguu vinapoanza kukomaa punguza kumwagilia ili kuepuka kuoza



4 - Kupalilia
• Palilia mara kwa mara ili kudhibiti magugu na kuwezesha vitunguu kutumia vizuri unyevu na virutubishi vilivyoko kwenye udongo. Pia magugu mengine huficha wadudu waharibifu kama vile utitiri mwekundu.
• Wakati wa kupalilia epuka kukata mizizi ya mimea.
• Pandishia udongo na kufunika shina la kitunguu wakati wa kupalilia ili kuzuia jua lisiunguze mizizi na kubabua vitunguu. Vitunguu vilivyoungua na kubabuliwa ubora wake hushuka napia huharibika upesi wakati wa kuhifadhi.

5 - Kudhibiti magonjwa na wadudu
Vitunguu hushambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali ambao huweza kusababisha upungufu na ubora wa mazao. Ili kudhibiti tatizo hilo kagua shamba mara kwa mara kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili za mashambulizi, chukua tahadhari ya kunyunyuzia dawa mapema kabla madhara hayajaleta upotevu mkubwa.

6 - Kupanda kwa nafasi:
Zingatia nafasi ya kupanda inayopendekezwa ili kupata vitunguu vyenye ukubwa uliokusudiwa. Wastani ni inchi 4 - 5 kutoka kitunguu kimoja hadi kingine, na inchi 12 - 18 kutoka mstari hadi mstari na kipandwe inchi 1 - 1.5 chini ya udongo

MAANDALIZI KABLA YA KUVUNA

1 - Kukagua shamba
• Kagua shamba ili kuhakikisha kuwa vitunguu vimekomaa. Vitunguu huwa tayari kuvunwa miezi mitatu hadi mitano tangu kusia mbegu kutegemea aina ya mbegu na hali ya hewa.Dalili za vitunguu vilivyokomaa:

• Majani hunyauka na kuanza kukauka
• Asilimia kumi hadi 20 ya mimea huanguka majani na shingo hulegea.
• Majani hubadilika rangi kuwa ya manjano na baadaye kaki

VITUNGUU VILIVYOKAUKA MAJANI TAYARI KWA KUVUNA



2 - Kuvuna
Vitunguu vinapaswa kuvunwa mapema mara tu vinapokomaa ili kupata mazao mengi na bora.Uvunaji hufanyika kwa mikono ambapo jembe uma hutumika kuchimbua au kulainisha udongo.Udongo ukishalainishwa vitunguu hung’olewa kwa mkono. Inashauriwa uvunaji uanze asubuhi ili vitunguu viweze kunyauka na kukomaza ngozi sehemu za michubuko. Vitunguu visiwekwe juani na inapobidi kukomaza ngozi shambani, majani ya vitunguu yatumike kufunika vitunguu ndani ya matuta yake wakati wa mchana ambapo kuna jua. Kusanya vitunguu kwenye vikapu kisha vipeleke sehemu ya kukaushia. Vitunguu vya kukaushia kwenye kichanja ni bora zaidi, mizizi na majani hupunguzwa na kuachwa urefu wa robo inchi . Vitunguu vya kukausha kwa kunining’iniza havikatwi majani bali hufungwa kwenye mafungu na kupelekwa sehemu ya kukaushia.