KURASA

Saturday, August 13, 2011

KILIMO CHA VITUNGUU TWAUMU - garlic





UDONGO
Vitunguu twaumu vinahimili aina nyingi za udongo, ila vinastawi zaidi katika udongo usiotuamisha maji kabisa na wenye mbolea asili, kama mbolea si ya kutosha kwenye udongo, tumia samadi iliyokwisha oza vizuri usitoe samadi bandani na kuipeleka shambani moja kwa moja kwenye shamba la vitunguu thwaumu, labda kama utaliacha shamba bila kulimwa kwa zaidi ya miezi 6, pia unaweza kutumia mbolea za viwandani kama ammonium nitrate, ammonium sulphate, urea n.k wakati wa kupanda na kila baada ya wiki 4 – 6 mara mbili zaidi

UPANDAJI
Kipindi kizuri kwa upandaji ni kipindi ambacho hakuna joto hasa miezi ya May mpaka August kwa Tanzania, Unachukua kitunguu twaumu na kutenganisha vitunguu kimoja kimoja (bulbs) na kuchagua vile vikubwa maana hivi ndivyo vitakavyo kupa mazao mengi na bora, nafasi kati ya kitunguu na kitunguu ni sentimeta 10 na kati ya mistari ni sentimeta 30. Baada ya kupanda pandishia udongo na uukandamize kuhakikisha kwamba kimekaa vizuri na hakiwezi kuathiriwa na mvua au maji wakati wa kumwagilia ili kisikae upande au kungolewa kabisa. Uotaji mzuri hutegemea pia namna vitunguu thwaumu vilivyo hifadhiwa kabla ya kupandwa, kama vilihifadhiwa sehemu zenye joto na hewa finyu uotaji wake utakuwa duni na dhaifu.


UMWAGILIAJI

Kama kuna upungufu wa mvua au ni kipindi cha kiangazi basi ni vizuri ukamwagilia shamba lako, wakati mzuri wa kumwagilia vitunguu twaumu ni asubuhi na sio jioni au mchana, hii inasaidia vitunguu twaumu kujijengea uwezo wa kupambana na magonjwa, baada ya mizi miwili unaweza kupunguza umwagiliajai huku ukiangalia kwa kuchimba kidogo kama vitunguu twaumu vimezaliana vya kutosha na kuanza kukomaa, ukiona vimekomaa acha kabisa kumwagilia ili visioze

UANGALIZI
Aina nyingi za vitunguu twaumu vitakuwa kama vinatoa mbegu kwenye mmea (angalia picha chini), ingawa kuna nadharia nyingi lakini inashauriwa kukata hizi mbegu chini kabisa kwa kisu kikali na kisafi, usikate mapema mara baada ya kutokeza bali subiri mpaka mmea unapoanza kama kujikunja ndipo ukate, kwa wale wanaoacha mbegu hizi ukiamua kuzipanda kwa msimu wa kwanza zitazaa kitunguu kimoja tu cha duara lakini chenyewe ukikipanda tena kwenye mzunguko wa pili kitazaa vitunguu vingi kama kawaida



Ungoleaji wa magugu na majani ni muhimu muda wote ili kuondoa kugombea rutuba, hewa na maji shambani, kwa wenye mashamba makubwa wanaweza kutumia dawa za kemikali kama ROUNDUP na nyinginezo ili kudhibiti magugu, ingawa mimi sishauri hivyo.

MAGONJWA
Magonjwa kama botrytis (kuoza shingo) blue mould na fusarium (kuoza kwa vitunguu) husababisha hasara kubwa kama hayatadhibitiwa kwa kutumia viuatilifu mara unapoona dalili, pia magonjwa kama white rot huchukua zaidi ya miaka 20 kuondoka kama yatavamia shamba lako, inashauriwa kufanya mabadiliko ya zao kila baada ya miaka mitano kwa kupanda mazao mengine yasiyo jamii moja kama vitunguu maji, unaweza kupanda maharage, mahindi, karoti na kabichi katika mzunguko huo. Pia magonjwa kama kutu ya majani husababisha na unyevu mwingi hasa kama mimea itakuwa kwenye udongo unaotuamisha maji au mimea kumwagiliwa jioni au usiku, kumbuka kumwagilia asubuhi tu Ili kudhibiti ugonjwa huu wa kutu mimea ingolewe na ichomwe au utumie viuatilifu vya kuulia fangasi wa mimea.

Monday, August 8, 2011

NANE NANE NA MELTON KALINGA

Leo ni siku ya wakulima yaani nane nane na maadhimisho kitaifa yanafanyika Dodoma, mimi niko na mtaalam wa Samaka Bw Melton Kalinga kwenye kituo cha Kingolwira nje kidogo ya Morogoro mjini kama km12. Kinachofanyika kwa leo ni upandishaji wa Samaki aina ya kambale

Unaanza kwa kutafuta majike makubwa yenye mayai tumboni, kisha unatafuta na Madume yaliyokomaa, ili kupandisha kwa njia ya kimaabara kambale dume inabidi umuue kisha unachukua pituitari gland na kumwingizia jike mwenye mayai aliye hai, baada ya masaa 24 mayai yanakuwa yame komaa, unayakamua toka kwa jike kisha unachanganya na mbegu za kiume toka kwa samaki uliyemuua jana yake, kwa kutumia mtambo wa maabara wenye maji ya vuguvugu unatotolesha mayai hayo kwa njia ya kitaalam.

Vifaranga wa samaki aina ya sato wanapatikana pia kwa shilingi 50 tu, kwa mawasiliano zaidi mpigie Bw Kalinga 0757891761 au 787596798

KAMBALE WAKIVULIWA KWENYE BWAWA






UKAGUZI NA UCHAMBUZI KUJUA MADUME NA MAJIKE WANAOFAA





SAMAKI JIKE MWENYE MAYAI

SAMAKI DUME



UTOAJI WA MBEGU TOKA KWA DUME

MTAMBO WA KUTOTOLESHEA MAYAI YA KAMBALE