KURASA

Wednesday, November 23, 2011

MAGONJWA MAKUU YA NDEGE

Magonjwa huainishwa kulingana na baiolojia yao,kama Virusi,Bakteria,Kupe,ukungu,na chanzo chao,kwa mfano magonjwa ya lishe yaliyoangaliwa hapo juu.Hata hivyo,magonjwa makuu katika ndege yamegawanywa katika makundi matatu kulingana na makali yao na umuhimu katika mfumo wa uzalishhaji mdogo katika vijiji.Vitu muhimu kama tabia zao wakati wa mlipuko(dalili),na matibabu yanayowezekana(kuzuia ama kudhibiti)vile vile wakati wa kutokea magonjwa hayo.Umuhimu wa ugonjwa huthaminiwa na idadi ya vifo na athari kwa uzalishaji,na itatofautiana kutoka eneo hadi eneo na msimu hadi msimu.

MCHANGANYIKO WA MAGONJWA

Magonjwa kadhaa yasiyo maku yanaweza kukutana na magonjwa mengine na kusababisha madhara makali kwa ndege.Hii ndio hali kwa mfano maambukizo ya E.coli, utapiamlo na kupe wa ndani.Magonjwa kama haya ni vigumu kuua ndege lakini huwa na madhara makubwa kwa kinga ya ndege dhidi ya magonjwa,na kujenga msingi wa maambukizo rahisi ya magonjwa mengine baada ya kuwafanya ndege kuwa dhaifu kiafya.

Umuhimu mkubwa huashiria ugonjwa wa kawaida wenye vifo vingi(zaidi ya asilimia 30 ya kundi),husambaa kwa urahisi na ni vigumu kutibu au hautibiki kabisa.Umuhimu wa wastaani kawaida ,vifo vya wastani(10-30%) kwa kundi na /ama vigumu kutibu.Ugonjwa usio mkuu huashiria wa kawaida, vifo vichache na /ama rahisi kutibu.

UGONJWA WA KUAMBUKIZANA WA KUKU UNAOSHAMBULIA MAPAFU NA MFUMO WA NEVA - NEWCASTLE DISEASE (NCD)
Ugonjwa huu huua, ni wa kawaida katika msimu wa mvua,na hutokea mara kwa mara katika vifaranga wachanga,lakini pia katika kuku waliokomaa.Vifo vya juu katika kundi,mara kwa mara baina ya aslimia 30 na asilimia 80 ya ndege hufa,ugonjwa unapowakumbaKuku hupoteza hamu ya kula na usagaji mbaya wa chakula tumboni.Unaweza kuonyesha upumuaji mzito,kinyesi cha kijani na wakati mwingine kuhara damu. Unaweza kuonyesha dalili za kuchanganyikiwa,kiharusi na hufa ghafla.Dalili zinaweza kutokea zote wakati mmoja.Ugonjwa huu ni wa virusi (virus)kwa hivyo hauna tiba,lakini unaweza kuzuiwa kwa kuwachanja ndege wote ukijumuisha vifaranga wa kutoka wiki mbili.

HOMA YA NDEGE - AVIAN INFLUENZA(AI)

Ugonjwa huu hubebwa na bata na bata maji,na unaweza kusambaa kwa urahisi na ni hatari sana kwa kuku.Vifo vya juu katika kundi,ndevu na panga za jogoo huvimba na kuwa na rangi ya kibuluu (samawati).Husambaa kupitia chakula na maji yaliyochafuliwa katika madimbwi na vyombo vya maji/chakula.Ugonjwa huu husababishwa na virusi (virus),kwa hivyo hauna tiba.

Ili kujikinga na ugonjwa huu zingatia usafi kwenye banda lako na vyombo vya kuku, ukiona dalili za ugonjwa huu waondoe kuku wagonjwa, wachinjwe na kuchomwa moto. Kabla ya kuingiza kundi lingine la kuku kwenye banda lenye ugonjwa hakikisha unapulizia dawa za kuua virusi ka a VIRU KILL. Mara uonapo dalili za ugonjwa huu muite afisa ugani wa mifugo (Veterinarian)

NDUI YA KUKU - FOWL POX

Huonekana mara kwa mara katika vifaranga wadogo,lakini pia kwenye kuku waliokomaa na huonekana uvimbe mdogo mdogo kwenye ndevu,panga na uso wa kuku.joto la kuku hupanda,uchovu unaoambatana na vifo vya ghafla.Ugonjwa huu ni wa kawaida wakati wa msimu wa kiangazi,lakini pia unaweza kutokea mwaka mzima.Ugonjwa huu ni virusi kwa hivyo hauna tiba.Chanjo inapatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.

UGONJWA WA MAREK - MAREK DISEASE

Huonekana tu katika ndege walio na zaidi ya wiki 16 kwa hiyo hauwapati kuku wa nyama labda kama umewafuga kwa ajili ya uzalishaji (parent stock).Mwanzoni ndege wanaweza kuonyesha bawa moja kushuka au yote mawili.Ama mguu mmoja ama yote inaweza kupooza.Ugonjwa huu ni virusi,kwa hivyo hauna tiba,lakini Chanjo inapatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo

MAAMBUKIZO YA BAKTERIA WA E.coli

Hutokea sana sana katika vifaranga walioanguliwa (Day old chicks),na husababisha maambukizo katika tumbo.Dalili katika ndege wakubwa:kupumua kwa tabu au maambukizo katika mayai na kupungua au kuacha kabisa kwa utagaji kwa kuku wa mayai, kinga bora ni usafi katika mayai kwa ajili ya .Tiba kwa vifaranga wagonjwa inawezekana ukiwa na kiua vijisumu (antibiotics) kama OTC 10%, 20%, 30%.

KIPINDUPINDU CHA KUKU - pasteurellosis

Unaweza kutokea wakati wowote na kwa rika zote.Dalili ni kuharisha sana kwa kuku,kupumua kwa tabu,kukosa hamu ya kula,ndevu na panga za jogoo huwa na rangi ya kibuluu(samawati).Unaweza kutokea kama ugonjwa sugu na kuku kufariki ghafla .Mambukizo kupitia chakula na maji yaliyochafuliwa.Hauna tiba.kinga ni usafi wa hali ya juu na chanjo.Ua na uchome moto kuku wote walioathirika.Chanjo inapatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.

UGONJWA WA KUHARA VIFARANGA

Ugonjwa huu unasababishwa na bacteria aina ya salmonella pullorum(Bacillary white bacteria)

Hutokea sana sana katika vifaranga wadogo.Vifaranga hutembea kwa tabu sana,tumbo huvimba na hukokota mbawa zao.Kinyesi chao huwa maji maji na hugeuka cheupe.Hauna tiba.Kuzuia ni kutilia usafi maanani.Ikiwa ugonjwa utatokea,tenga ama ua na uchome ndege.Ugonjwa huu husambazwa kwa kifaranga kutoka kwa mayai ya kuku aliyeathirika,ambaye haonyeshi daalili zozote za kuwa mgonjwa.

HOMA YA MATUMBO YA KUKU - TYPHOID

Huonekana zaidi kwenye kuku wakubwa.Dalili:joto huwa kali,uchovu,panga na ndevu za kuku huwa za kibuluu (samawati).Hauna tiba.Kinga ni kutilia usafi maanani na kuua kuku wagonjwa.Usinunue vifaranga kutoka kwenye vyanzo ambavyo hauvijui,na usitumie mayai kwa ajili ya kuanguliwa kutoka kwenye kuku wagonjwa.

GUMBORO - Infectious Bursal Disease(IBD)

Huonekana tu katika vifaranga walio chini ya wiki 6,na ni wa kawaida katika makundi makubwa ambayo yamefugwa katika sehemu zilizofungwa (indoor).Sio wa kawaida katika mfumo mdogo wa ufugaji vijijini.Dalili za kawaida: kuharisha.Ugonjwa huu ni virusi ,kwa hivyo hauna tiba.Chanjo inapatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.

UGONJWA WA KUPUMUA

Dalili:Pua inayotoka makamasi,uvimbe chini ya macho,macho yaliyojifunga,upungufu katika utagaji wa mayai.Tiba ni kuongeza kiua vijisumu (antibotics) katika maji ya kunywa.

UGONJWA SUGU WA KUPUMUA - Mycoplsmosis

Dalili:Pua inayotoka makamasi ama iliyoziba,uso uliovimba,macho yaliyojifunga,upungufu katika utagaji wa mayai,vifo visivyo vya kawaida.Tiba ni kuongeza kiua vijasumu (antibotics)katika maji ya kunywa.

COCCIDIOSIS

Ugonjwa huu unaweza kutokea wakati wowote na katika rika zote,lakini unaweza kuzuiwa kwa kusafisha kwa makini nyumba za ndege.Dalili:hali dhoofu ya kuku,kuchoka,kutembea kichwa chini ,manyoya yaliyotimka,kuhara damu.Vifo katika vifaranga wachanga.Ikiwa vifaranga wataendelea kuishi watabakia kuwa wembamba na watachelewa kutaga.Tiba:Weka dawa ya Coccidiostatics katika maji ya kunywa au chakula.Kuzuia:Usiweke ndege wengi pamoja.Epuka kuweka ndege wa rika mbalimbali katika nyumba moja kwani ugonjwa unaweza kusambaa kutoka kwenye kuku wakubwa hadi kwa vifaranga.

MINYOO

Minyoo ni vimelea vya ndani na ni vya kawaida katika umri wote katika mfumo wa uzalishaji vijijini na mjini.Vimelea hivi husababisha afya mbovu,kupoteza uzito,kupungua kwa uzalishaji wa mayai.Tiba bora ni kuongeza dawa ya minyoo kama piperazine katika maji ya kunywa mara moja ama mbili kwa mwaka,ikiwezekana wiki mbili kabla ya chanjo yoyote.

CHAWA, KUPE, VIROBOTO NA UTITIRI

Huvamia rika zote wakati wowote,lakini hutokea mara kwa mara katika nyumba za kuku zenye unyevunyevu na uchafu.Ndege waliokomaa husumbuliwa na hutumia wakati mwingi wakidonoa na kujikuna.Vifaranga wachanga wanaweza kufa kwa sababu ya upungufu wa damu (anaemia).Kama hautatibiwa utitiri,chawa,viroboto,kupe watasababisha kuku kupungua uzito na pia kuna uwezekano wa kupoteza manyoya kwa sababu ya kunyonywa damu na vimelea na kuwashwa na ngozi.Chawa wanaweza kuonekana karibu na macho na pua.Viroboto vinaweza kuonekana kwenye tumbo.Tiba:Nyunyiza dawa ya kuua vimelea kama Akheri powder,jivu na mafuta.Jivu na poda ya salfa inaweza kutumiwa mahali ambapo kuku huoga na mchanga.Viota vinaweza kulindwa kwa kuwekewa majani kadhaa ya tumbaku yaliyochanganywa na jivu katika viota.

MAGAMBA KWENYE MIGUU

Miguu yenye magamba husababishwa na vimelea vya nje vinavyowasha ngozi kwenye miguu ya ndege.Dalili:Miguu ina magamba yanayoonekana na majeraha na anaweza kulemazwa katika kutembea.Tiba:Weka miguu kila siku kwenye mafuta taa,ama katika dawa kuogeshea mifugo hadi magamba yatoweke.

LISHE DUNI

Ndege wanaoathirika zaidi ni wale wanaofugwa ndani kuliko wale wanaojtafutia chakulaDalili:mifupa kukua vibaya na kunyonyoka manyoya.Ndege hutembea kwa tabu;huchopea .Tiba,ukigundua mapema wape ndege wako vitamini na kalsiam ya ziada kwenye chakula, pia wape majani, mabaki ya mboga za majani au kinyesi cha ng'ombe

Thursday, November 10, 2011

KILIMO BORA CHA MINAZI




UPANDAJI
Uko wa ina mbili kuna wa vibox na wa pembetatu lakini kwa aina zote mbili umbali wa kupanda ni mita 7.6 kutoka shimo hadi shimo la mnazi, kiasi cha mashimo 175 kwa hecta huingia na kama utatumia mtindo wa pembetatu basi mashimo 13 zaidi yataingia kwa hecta.



Ukubwa wa shimo uwe futi tatu kwa kina, upana na urefu hi kwa maeneo yenye udongo mzuri na wakaida lakini maeneo yenye changarawe, mawe mawe na miamba ukubwa uongezeke hadi futi4 kwa mapana , urefu na kina, Shimo lijazwe majani kiasi cha kilo 15 – 20 unaweza kukisia kama theluthi moja ya shimo au futi moja baada ya kushindilia majani, weka juu yake kama, weka udongo wa juu (top soil) kiasi cha futi moja tena ongezea kiasi cha kilo 10 – 20 cha mbolea ya samadi.

Hakikisha haijai na kufunika shimo lote, pia kama utapata ule udongo mwekundu ambao wengi hupenda kuutumia kwenye bustani zao, pia weka humu kiasi kama utaukosa basi acha vivo hivyo, anza kumwagilia maji wiki moja kabla ya kupanda mbegu yako, kama shimo litatitia ongezea udongo wenye rutuba ya kutosha, kumbuka kuacha kisahani kwa ajili ya kukusanyia maji, ila kama ni sehemu ambazo hufurika kipindi cha mvua jaza udongo hadi kuweka tuta ili maji yasituame.

UPANDAJI
Ni vizuri kutumia mbegu ya nazi moja kwa moja kuliko kutumia miche, hii ni kwa sababu mbili kubwa, kwanza ukinunua mche unakuwa hujui imetoka mnazi gani, wenye ubora gani na hata uzaaji wake huujui, lakini inashauriwa kununua nazi kutoka kwenye mnazi moja kwa moja kwa kuchagua mnazi bora na unaozaa nazi nyingi na kubwa, chagua nazi kubwa zaidi kutoka katika kila mnzi bora.

Nazi ambayo haijafuliwa inakuwa na pembe tatu, moja ya pembe hizi huwa kubwa zaidi na mbili zilizobaki hufanan ukubwa, ule upande mkubwa ulazwe chini wakati wa kupandwa, na upande ule wenye kikonyo ambako nazi hujishika katika matawi ya mnazi (mahanda) ndipo ambapo huota, utatakiwa upatate au upapunguze kwa kisu ili kurahisisha kuota, wakati wa kupanda hakikisha nazi ina maji, ikiwa na maji kidogo sana usiipande, panda miezi miwili au mitatu kabla ya mvua kuanza, nazi inauwezo wa kuota yenyewe bila mvua kwa sababu ina maji ndani yake, ila baada ya kuanza kuota kama hakuna mvua ni muhimu kumwagilia ama sivyo mbegu yako itakufa.

Pia ni muhimu kutumia dawa za kuua mchwa au oil chafu wakati wa kupanda, pia kunadaadhi ya mimea ambayo mizizi yake hufukuza mchwa inaweza kupandwa pamoja na nazi yako. Kama utaamua kutumia miche basi hakikisha miche yako haipungui umri wa miezi sita tangu mbegu kupandwa ili kuzuia miche mingi kufa.

MAGONJWA YA MINAZI

- KUOZA VIKONYO
Huanza kwa majani machanga mawili ya mwanzo kubadilika rangi na kuwa njano na baadae huwa na vidoti vyeusi hutokea kwenye ukingo, majani hunyauka na kukauka na kisha sehemu ya chini linapoanzia jani huoza na kutoa harufu mbaya ambapo baadae mnazi wote hufa.

Ili kuzuia ugonjwa huu mara tu unapoona dalili za mwanzo tengeneza mchanganyiko ufuatao (gramu 100 za copper sulphate changanya na nusu lita ya maji) + (Gramu 100 za chokaa changanya na nusu lita ya maji) kila moja itengenezwe peke yake halafu kisha vichanganywe pamoja baadae kisha pulizia kwenye minazi iliyoanza kushambuliwa, kama mnazi umeshambuliwa sana ukatwe na kuchomwa moto kuzuia maambukizi zaidi. Pia pulizia mchanganyiko huu msimu wa baridi kuanzi mwezi wa 5 hadi wa 9 kwenye shamba lako kama kinga.

- KUOZA MAJANI
Majani huwa meusi kwenye ukingo na kuti likiliwa zaidi kati kati, majani machanga yakichomoza huwa dhaifu na kisha huchanguka, mnazi haufi ila mazao huwa duni kama ni mnazi unaozaa

ili kuzuia tumia dawa yoyote ya kuzuia fangasi za mimea kama Hexaconazol, Mancozeb au Dithane - M5, muhimu ukufika duka la pembejeo ulizia dawa ya kuua fangasi wa mimea utapata dawa na maelekezo ya kuchanganya usikariri haya majina ya dawa nilizotaja

Monday, November 7, 2011

MPWAPWA BREED - Mbegu bora ya ng'ombe iliyosahaulika

ASILI
Mbegu hii inatokana na mchanganyiko wa mbegu ya ng’ombe jike aina ya Zebu toka Tanzania na Red madume ya Sindhi na Sahiwal wenye asili ya india na Pakistan lakini waliotolewa nchini Kenya hii ilikuwa ni mwaka 1940 ambapo uzalishaji wa mbegu hii ulifanyika kwa mara ya kwanza katika kituo cha utafiti wa mifugo Mpwapwa Dodoma nchini Tanzania

Mwaka 1958 uboreshaji wa mbegu hii ulifanyika kwa kuongezea damu za ng’ombe wa ulaya (Bos Taurus) aina ya Ayshire na Jersey na mpaka kufikia mwaka 1960 mbegu ya Mpwapwa ikawa na na uwiano wa 20% Tanganyika Zebu 10% Boran 5% Ankole 55% Red Sindhi na Sahiwal na 10% Ayshire na Jersey. Mpaka mwaka 1971 mbegu hii ikawa na mchanganyiko wa 32% Red Sindhi, 30% Sahiwal, 19% Tanganyika Zebu 10% Boran na 10% Ayshire na Shorthorn, utagundua kwamba mbegu ya Jersey iliondolewa na kuingizwa short horn

MWONEKANO
Wanaonekana zaidi kama Sahiwal wakiwa na rangi nyekundu iliyofubaa mpaka kukooza sana au Nyekundu na nyeupe, Wana nundu kama ng’ombe wetu wa kienyeji, ngozi ya chini yashingo ijulikanayo kama DEWLAP ni ndogo zaidi ya Zebu lakini kubwa zaidi ya Ng’ombe wa kigeni, wana kiwele kikubwa zaidi ya ngombe wa kienyeji chenye kukamilika kirahisi ANGALIZO nundu na dewlap huwasaidia kupambana na mazingira ya Afrika hasa joto kali

MBEGU YA MPWAPWA


Madume yana uzito kati ya kilo 450 – 600 na majike kilo 275 – 300 wakati wa uzazi wa kwanza na huongezeka hadi kufikia kilo 450 hapo baadae, mbegu hii inauezo wa kuzalisha maziwa mengi kuliko ng’ombe wa kienyeji na pia uhimili mazingira ya joto na magonjwa kuliko Tanganyika Zebu

Serekali imeshindwa kusambaza mbegu hii kwa wafugaji na inasemekena karibia itapotea kwa sababu ng’ombe wa Mpwapwa waliobakia ni wachache sana na wanapatikana kwenye baadhi ya vituo vya utafiki kama Mpwapwa kwenyewe. Pia kuna tetesi kwamba kwa sasa hakuna MBEGU HALISI (pure breed) ya ng’ombe hawa kutokana na kuachwa wakapandana ndugu kwa ndugu (Inbreeding)