KURASA

Monday, December 28, 2009

KUTU YA MAJANI - COFFEE LEAF RUST

Huu ni mwendelezo wa magonjwa makuu ya kahawa
Kutu ya Majani ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vya ukungu jamii ya Hemileia vastatrix; Ugonjwa huu ushambulia karibu aina zote za kahawa; hasa katika nyanda za chini ambako kuna joto zaidi. Ugonjwa wa kutu ya majani hujitokeza kabla ya mvua za masika kuanza.



MAZINGIRA MAZURI YA VIMELEA VYA KUTU YA MAJANI:
• Joto lililo ambatana na unyevu nyevu mwingi angani.
• Kivuli kinachosababishwa na miti mingi shambani au matawi
ya kahawa.
• Magugu jamii ya Oxalis.
• Kahawa zilizozeeka kupita kiasi nazo hushambuliwa kwa urahisi.

MASHAMBULIZI NA DALILI
• Kutu au rangi ya machungwa iliyochanganyika na manjano huonekana upande wa chini wa majani ya kahawa.
• Kudondoka kwa majani yangali bado machanga.
• Kudumaa kwa matawi.
• Kukauka kwa ncha za matawi.
• Hatimaye mavuno hupungua kwa kiasi kikubwa.

UGONJWA UNAVYOSAMBAZWA:
• Upepo huongeza kasi ya kusambaa kwa vimelea vya kutu ya majani.
• Wanyama (ndege) wadudu, husambaza vimelea vya kutu ya majani toka mmea mmoja hadi mwingine.
• Miezi michache kabla ya Vuli vimelea vya kutu ya majani huanza kukua;
- Vimelea hivi hujihifadhi kwenye magamba ya shina la kahawa na matawi makubwa (Primary branches) hasa kahawa zilizozeeka.
- Kipindi hiki huwa na joto.
• Vuli husaidia kuongeza kasi ya kukua kwa vimelea hivyo na kusambaza.
- Kutokana na unyevunyevu uliopo kwenye majani na kahawa kwa ujumla.
• Vimelea vya ukungu wa aina hii vinapoendelea kusambaa ndivyo na ashambulizi ya mmea yanavyoongezeka.
• Mashambulizi huendelea kipindi chote cha joto hadi masika, kipindi ambacho vimelea hukosa nguvu.
• Nguvu ya vimelea vya kutu ya majani huanza tena kidogo kidogo
baada ya masika kwisha.



KUPAMBANA NA KUTU YA MAJANI:
• Shamba liwe safi wakati wote.
- Punguza kivuli cha miti na migomba kwenye shamba la kahawa.
- Punguza matawi ya kahawa (pruning); wakati wa kukata matawi kata matawi yote yalivyozeeka; na yaliyo na ugonjwa.
- Lima ili kupunguza magugu hasa jamii ya oxalis.
• Hakikisha udongo una unyevunyevu wa kutosha, wakati wote: (weka matandazo, mbolea na kumwagilia maji)
• Ondoa magamba kwenye kahawa kwa kutumia brush / magunzi mbalimbali.
• Jaribu sumu za asili kama utupa (rejea makala zangu).
• Sumu za viwandani (mrututu) zitumike pale tu ambapo ni lazima kufanya hivyo kufuatana na hali ya hewa;
- mrututu (copper) utumike kama kinga mara baada ya mvua za masika kama joto liko juu likiambatana na unyevunyevu angani.
- Endapo kutu ya majani imeshamiri tumia Bayleton kama tiba (control) lakini si zaidi ya mara 2 kwa msimu.
NB: Wakati wa kunyunyuzia sumu elekeza bomba chini ya majani.