KURASA

Monday, May 31, 2010

KILIMO CHA PILIPILI MANGA


Utangulizi

Jina la kitalaam ni Piper nigram na kwa kiingereza ni black pepper. Zao hili asili yake ni Mashariki ya Mbali, na linalimwa zaidi katika mkoa wa Tanga na Zanzibar.

Matumizi
Pilipili nyeusi na nyeupe zote hutumika kwa mapishi ya nyama, samaki na kwa mapishi mengine mbalimbali. Nchi za magharibi zina matumizi makubwa ya viungo hivi. Aidha pilipili mtama nyeusi ndiyo huzalishwa zaidi hapa nchini.

Uzalishaji
Hali ya hewa na udongo
Viungo vingi humea katika maeneo yenye joto la wastani kati ya nyuzi joto 24-26 na huzalishwa maeneo ya mwambao. Udongo wenye rutuba na unaopitisha maji na wenye uchachu wa kiasi cha pH 6.5. Mahitaji ya mvua ni mililita 1500-2000 kwa mwaka.
• Uchaguzi wa mbegu
Uchaguzi huzingatia mambo yafuatayo:-
a) Urefu wa pingili na ukubwa wa majani
b) Ufupi wa pingili unaoambatana na majani madogo.
Tofauti iko hadi kwenye umbile la matunda. Majani ya mche mama sehemu kinapokatwa kipando huondolewa wiki mbili kabla ya kukata. Vipando vyenye macho (nodes) 3-4 humika. Macho mawili huzikwa kwenye udongo na kipando kiwekewe kivuli. Inashauriwa kuweka mbolea ya samadi wakati wa kupanda.

• Nafasi ya upandaji
Nafasi ya kupanda ni mita 2-3 kati ya mmea na mmea endapo miche imepandwa na miti inayotakiwa kupogolewa mara kwa mara.

Mahitaji ya mbolea
Matumizi ya mbolea hapa Tanzania si makubwa katika kilimo cha viungo. Ingawa kiasi cha kilo 0.4 cha Urea, kilo 0.3 cha Superphosphate na kilo 0.3 cha Potash ya Muriate kinaweza kutumika kwa miche mikubwa.

• Miti ya kusimikia miche

Miche hupandwa kwa kusimikiwa nguzo ili ikue kwa kujizungusha kwenye miti kama mijenga ua, n.k. Mti huo wa kusimikia nao pia hupaswa kupunguziwa majani ili kupunguza giza. Kila kabla ya msimu miti hiyo hupaswa kupunguziwa matawi (pruning).

Kupogolea miche ya pilipili mtama
Mche ukifikia miezi 18 inapaswa kupogolea kwa kukata sehemu ya juu ya mche ili kufanya matawi mengine yachipue chini ya mche. Inashauriwa mche kuwa na urefu wa mita 3-3.5.

Uvunaji
Maua ya kwanza hutoka baada ya miaka miwili. Matunda hukomaa miezi tisa (9) hadi kumi (10).
Uvunaji ni mizunguko 5 hadi 6 kwa mwaka. Pilipili mtama inaweza kuvunwa kwa misimu miwili. Mavuno ni kati ya tani 0.35-3.75 kwa hekta.

Kuhifadhi
Pilipili mtama inaweza ikawekwa kwenye chombo kisichopitisha hewa na kudumu kwa miaka 20 bila kuharibika.

Mashambulizi ya wadudu na magonjwa
Hapa nchini hakuna matatizo makubwa ya wadudu na magonjwa.

Masoko
Soko la pilipili matama linapatikana ndani ya nchi na nje pia. Bei ya ndani ni kati ya Sh1,000-1,500. Zao hili huuzwa katika nchi za Uganda, Kenya, Uingereza, Ujerumani, Mashariki ya Kati, n.k. Bei ya Nje ni wastani wa dola za kimarekani 1,985 kwa tani.

Thursday, May 27, 2010

BIO -GAS / HEWA VUNDE

Kuni na mkaa vimekuwa vikiongezeka bei kila siku pia vikiwa ni vyanzo vya uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji miti, njia mbadala inahitajika katika kutatua tatizo hili kwa wakulima, na kinyesi cha wanyama kinaweza kutumia kuzalisha nishati ijulikanayo kama BIO –GAS

Kinachofanyika ni kukusanya kinyesi cha wanyama hasa ng’ombe wanaofugwa ndani, kikichanganyika na mkojo pamoja na maji yanaelekezwa katika tanki maalum kwa ajili ya kuzalisha nishati hii. Baada ya bacteria kuozesha mchanganyiko huu kwa njia isiyohitaji hewa ya oksijeni (anaerobic fermentation) nishati ya bio gas huzalisha ikiwa na wastani wa hewa ya METHANE 65% na kasha gasi hii huelekezwa kwenye nyumba kwa kutumia mabomba hadi jikoni kwa ajili ya kupikia

Mchanganyiko uliokwisha tumika hutoka nje wenyewe kwa kusukumwa na mchanganyi ko mpya mara uingiapo, kinyeshi kinachotoka nacho pia hutumika kama mbolea kwa ajili ya kustawisha mazao ya mkulimaFAIDA ZA BIO-GAS
1-Huongeza kipato cha mkulima kwa kupunguza muda wa kutafuta kuni na mkaa

2-Husaidia katika utunzaji wa mazingira kwa sababu haichafui hewa na hupunguza ukataji miti hovyo

3-inaweza kutumika kuwashia taa kama itazalishwa ya kutosha

4-mbolea inayobaki hutumika kwa ajili ya kustawisha mazao

5-Afya ya mkulima hulindwa kwa sababu upikaji kwa kutumia bio gas hauna moshi, kina mama jikoni hawaathiriki na moshi kama wakitumia kuni, badala ya kinyesi cha wanyama kuwa kingi na kukosa matumizi na kugeuka uchafu sasa kitatumika kuzalisha nishati hii

Monday, May 17, 2010

ZANZIBAR HAKUNA MBUNG'O

Ni miaka zaidi ya sita (6) tokea mbung’o waache kuonekana katika visiwa vya Zanzibar na tokea kipindi hicho ng’ombe kadhaa wamekuwa wakipimwa damu ili kujua kama wana ugonjwa wa ndigana/nagana unaosambazwa na mbung’o lakini matokeo yamekuwa mazuri yakionyesha kwamba ng’ombe hawana vimelea vya ugonjwa huo hatari kwa mifugo

MBUNG'O WAKIPANDANA


Hii imesababisha uzalishaji wa maziwa kuongezeka mara tatu zaidi, uzalishaji wa nyama marambili zaidi, matumizi ya samadi ya mifugo nayo yameongezeka mara tano zaidi na hii inamaanisha kwamba wafugaji wa ng’ombe kipato chao kimeongezeka zaidi. Je sababu ya haya yote na mbung’o kupotea ni nini?

Kwa kawaida mbung’o jike akishapandwa mara moja hawezi kupandwa tena maisha yake yote, yaani inamaanisha kwamba huwa wana mzao mmoja tu katika maisha yao yote. Sasa kinachofanyika kitaalam ni kwamba mbung’o wanakamatwa wakiwa hai kisha wana tengwa majike na madume, majike yanauwawa na madume yanapelekwa kwenye maabara na kupigwa mionzi ya gamma kutoka katika cobalt 60, baada ya hapo yanakuwa yanapanda majike kama kawaida ila yanapoteza uwezo wa kuwazalisha kwa maana hiyo watapandana bila kuzalishana na pole pole kizazi kinapotea na kufutika kabisa

MTEGO WA KUKAMATIA MBUNG'OKwa Zanzibar zoezi lilifanikiwa asilimia 100 kwa sababu mbung’o hawawezi kutoka sehemu nyingine na kuhamia Zanzibar kwa kuwa ni kisiwa, pia wao walizalisha madume mengi kwenye maabara na kuyaachia baada ya kuyaua kizazi, njia hii inajulikana kama sterile male technique

Thursday, May 6, 2010

KUPUNGUZIA MATAWI MITI JAMII YA MICHUNGWA

Bw Elyc ameniambia kwamba nimwelekeze jinsi ya kupunguzia matawi ya miche yake jamii ya michungwa nami namwomba azingatie haya

1- Kipindi kizuri cha kupunguzia matawi miti yako ni kipindi cha jua na wakati huu mimea isiwe na matunda wala maua

2- Matawi yanakatwa sehemu zile zenye magonjwa , zilizokufa, matawi yaliyofungamana au katikati ya mti ili kuufanya utawanyike vizuri

3- Pia punguza matawi yaliyopo kwenye njia pamoja na matawi yanayoelekea kuelemewa kutokana na kuwa na matawi madogo mengi zaidi

4- Tumia zana maalum za kupunguzia matawi kama mikasi na misumeno maalum inayopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo, uwe mwanagalifu vifaa hivi visikuumize maana vina ncha kali na tumia vifaa vya kujikinga kama mabuti maalum ya mashambani na glovu za mikononi

5- Milimao inabidi ipunguziwe matawi kila Mwaka au kila baada ya miaka miwili, kila tawi lipunguze kiasi cha robo au theluthi ya juu, kwa kufanya hivi mlimao hautakuwa mkubwa sana na kusababisha usumbufu wakati wa kuvuna

MCHUNGWA AINA YA JAFFER6- ZINGATIA
(a)Panda miche yako kwa nafasi zinazokubalika kitaalam laa sivyo mime yako ikibanana itakuwa inakimbilia juu, kwa michungwa aina ya jaffer panda mita 8 kwa 8 (8m * 8m) na kwa aina ya Valencia panda (5m * 8m)

(b)kumbuka kupunguzia miche yako jamii ya michungwa kuna maanisha kupunguza mazao kwa sababu mti mkubwa ndio unazaa matunda mengi, usiupunguze matawi mti wako kama huna sababu ya kufanya hivyo

(c)Vifaa vinavyotumika kwa ajili ya kupunguzia matawi viwe na makali ya kutosha kuepusha kupasua na kuchana matawi, unaweza kuomba afisa ugani wa eneo lako ili akuonyeshe kwa vitendo

(d)Kama utachanganya michungwa ya jaffer na Valencia uipande kwa uwiano wa 2:5 yaani katika kila michungwa 7 miwili iwe jaffer na mitano iwe Valencia, hii ni kwa sababu michungwa aina ya jaffer ni mikubwa na inazaa sana na inawahi kuiva lakini haihimili sana ukame, michungwa ya Valencia ina uzazi wa wastani na inahimili ukame kwa hiyo ukiichanganya shambani utapata mavuno ya mwanzo kwenye jaffer na mavuno ya kati yatakuwa na mchanganyiko wa jaffer za mwisho na Valencia za mwanzo na kisha mwisho utapata mavuno ya Valencia tu. Kwa hiyo utakuwa na machungwa katika msimu wote wa mavuno na ii itazuia machungwa kuiva yote pamoja na kuharibikia shambani

Tuesday, May 4, 2010

JINSI YA KULIMA BUSTANI KWENYE ENEO LENYE MAJIMAJI

Kutokana na tatizo la bwana Chacha Wambura Ng'wanambiti katika post hii hapa http://mataranyirato.blogspot.com/2010/05/aisifuye-mvua-imemnyea.html nimeamua kutoa maelezo kwa ufupi jinsi ya kukabiliana na sehemu ambazo maji husimama wakati wa mvua1- Lima na tifua udongo kwa kutumia trekta la mkono (power tiller) kiasi cha inchi 12 chini, udongo mwingine unaweza kuujaza kama matuta na kuweka mifereji pande zote la eneo lako. Kama huna trekta hili pia unaweza kutumia jembe la kukokotwa na ng’ombe (plau)

2- Jaza majani makavu, vijiti, maranda ya mbao n.k kiasi cha inchi 5 -6 halafu mbolea vunde au samadi kiasi cha inchi 4 halafu rudishia udongo wako juu yake na hapo utakuwa umeinyajua ardhi yako kiasi cha inchi 8 juu (kumbuka maranda na mbolea vitadidia kidogo) kisha pitisha harrow au jembe la kukokotwa na ng’ombe ili kuweza kuchanganya vitu hivi3- Acha udongo wako ukauke kiasi cha siku 3 kisha pitisha harrow au jembe la kukokotwa na ng’ombe tena ili kuvunja vunja mabonge ya udongo yaliyotokea wakati wa udongo kukauka na pia kuchanganya mchanganyiko huu zaidi

4- Weka tena mbolea vunde au samadi kiasi cha nchi mbili juu ya mchanganyiko huu kisha panda mbegu au miche yako na uizungushie udongo kiasi

5- Mwagia maji kadri inavyo hitajika kama udongo utakuwa mkavu, na uendelee kufuata kanuni za kilimo bora kama inavyoshauriwa kitaalamu