KURASA

Tuesday, September 22, 2009

KILIMO KWANZA

AZIMIO LA KILIMO KWANZA


KWA KUWA Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lilifanya mkutano tarehe 2 na 3 mwezi Juni 2009 jijini Dar es Salaam, kujadili sera na mikakati ya kuleta mapinduzi ya kilimo cha Tanzania pamoja na utekelezaji wake chini ya kaulimbiu ya “KILIMO KWANZA”;


NA KWA KUWA asilimia themanini ya Watanzania hutegemea kilimo kwa ajili ya kuendeleza maisha yao;


KWA KUTAMBUA KUWA changamoto kubwa kwa Tanzania ni kupambana na umaskini na kwamba hili litawezekana hasa kwa kuongeza tija katika kilimo;


KWA KUZINGATIA KUWA Tanzania imejaaliwa kuwa na rasilimali za kutosha kwa ajili mazao, mifugo na uvuvi, ambazo kwa sasa matumizi yake yapo chini;


KWA KUFAHAMU KUWA Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kuwa na kiasi kikubwa cha maji kinachoweza kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji pamoja na ufugaji;


NA KWA KUTAMBUA KUWA jitihada za makusudi zimekuwa zikichukuliwa ili kuboresha kilimo bila mafanikio yakuridhisha;HIVYO IMEAZIMIWA KWAMBA:

1.KILIMO KWANZA iwe ndiyo dhana ya kuleta mapinduzi ya kijani kwa lengo la kukifanya kilimo cha Tanzania kuwa cha kisasa na cha kibiashara;

2.Dhana ya KILIMO KWANZA ijumuishwe kwenye mipango mbalimbali ya Serikali ili kuhakikisha mafanikio ya utekelezaji wake;

3.Jitihada zifanyike katika kuongeza rasilimali mbalimbali ili kufanikisha utekelezaji wa KILIMO KWANZA;

4.Sekta binafsi ihamasishwe ili iongeze uwekezaji kulingana na wajibu wake katika utekelezaji wa KILIMO KWANZA; na

5.Utekelezaji wa KILIMO KWANZA utaongozwa na nguzo kumi zifuatazo:

I. Utashi wa kisiasa kutoa msukumo wa mapinduzi ya Kilimo.
II. Kugharamia mapinduzi ya Kilimo
III. Uboreshaji wa mfumo wa utawala wa kilimo.
IV. Mabadiliko ya mfumo mkakati katika kilimo.
V. Upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya kilimo.
VI. Vivutio vya kuchochea uwekezaji katika kilimo.
VII. Uendelezaji wa viwanda katika kuleta mapinduzi ya kilimo.
VIII. Sayansi, Teknolojia na Rasilimali Watu katika kuwezesha mapinduzi ya kilimo.
IX. Uendelezaji wa Miundombinu ili kuwezesha mapinduzi ya kilimo.
X. Uhamasishaji na ushirikishwaji wa Watanzania kuunga mkono na kutekeleza KILIMO KWANZA.