KURASA

Tuesday, September 29, 2009

SEHEMU YA 4 - MATUNZO YA WATOTO WA NGURUWE




Kwa kawaida hunyonya kwa wiki 5 -8, na baada ya hapo hutengwa na mama yao na kuanza kupewa chakula chenye protini 25% kwa muda wa wiki 6 za mwanzo

KUKATA MENO
Mara baada ya kuzaliwa watoto wakatwe meno kwa kutumia mkasi mkubwa au kifaa cha kukatia waya (wire cutter) umuhimu wa zoezi hili ni kwa sababu nguruwe huzaliwa na meno na mara wanapoanza kunyonya huumiza chuchu za mama yao na kumsababishia ugonjwa wa chuchu (mastitis)

MADINI CHUMA
Wakizaliwa tu wanahitaji madini ya chuma kwa wingi, maziwa ya mama yanatoa kiasi cha 10% tu, huwa wanapigwa sindano (Iron Injection) kiasi cha 155mg kwa kitoto kimoja ili kuwaongezea madini ya chuma ya ziada, muone mtaalamu wa mifugo akusaidie kwa hili



KUHASI
Madume ambayo yatakuzwa kwa ajili ya nyama ni vizuri yakahasiwa, hii husaidia ukuaji wa haraka na pia huondoa harufu ya balehe, Zoezi hili lifanyike wakati wakiwa na wiki 2-3 inapofika wiki ya 5 zoezi huanza kuwa gumu kwa sababu watoto wanakuwa wakubwa na litahitaji sindano za ganzi, zoezi hili linahitaji mtaalamu wa mifugo.

MINYOO
Mzazi anapokaribia kujifungua wiki ya mwisho achomwe sindano ya kuondoa minyoo na magonjwa ya ngozi ijulikanayo kama IVOMEC SUPER au IVERMECTIN zinazopatikana kote nchini, dawa hii husaidia kuwalinda watoto na minyoo hadi wanapoacha kunyonya ndio na wao wapigwe sindano hii ambayo pia itasaidia kuua minyoo ya mapafu, minyoo ya macho, viroboto na kuondoa ukurutu.



CHAKULA
Baada ya wili chache vitoto vitaanza kula chakula kidogo kidogo kwa kuanzia na kile anachopewa mzazi, hakikisha mzazi anapewa chakula kingi na chakutosha kwa sababu atakuwa anakula yeye na watoto wake

KITIMOTO SEHEMU YA 3 - NGURUWE JIKE (MZAZI)

UCHAGUZI
Yawe na chuchu zisizopungua 18 na chuchu ziwe nene na ndefu, chuchu fupi na ndogo huleta matatizo wakati wa kunyonya , kumbuka mtoto wa nguruwe chuchu atakayo nyonya siku ya kwanza ndiyo hiyo hiyo atakayonyinya mpaka atakapoacha kunyonya
Awe na miguu ya wastani yenye nguvu na isiwe na kasoro kama matege au kukaa upande na kucheche mea, hii humsaidia kuhimili madume makubwa
Uke uwe na ukubwa wa kutosha na umbo la kawaida, pia upimwe na mtaalamu kwa kuingiza vidole na kuangalia kama wakati wa kuvitoa vina kwama kwama, hii huwa dalili ya majike dume (hermaphrodites)



CHAKULA
Maji yalishwe chakula cha kunenepesha mpaka yakifikisha uzito wa kilo 80, baada ya hapa yapewe chakula maalum cha wazazi ambacho kitasaidia wasinenepeane na kuwa na mafuta mengi kwenye njia ya uzazi

BANDA
Majike hukaa moja moja au mengi kwenye banda moja muda wote (kipimo ni 2.5m *1.5m ) kwa kila nguruwe kasoro tu yanapokaribia kuzaa ndio huhamishiwa kwenye banda la kuzalia

NGURUWE AKIWA KWENYE BANDA LA KUZALIA


UPANDISHAJI
Majike yapandishwe yakifikisha umri wa wiki 28 na uzito wa kati ya kilo 120 – 140, nguruwe aachwe mpaka aingie joto kwa mara ya 3 ndio apelekwe kwa dume ambapo kila baadda ya siku 21 nguruwe huingia kwenye joto

KUINGIA KWENYE JOTO
Dalili za joto ni guruwe kupiga kelele hovyona kuhangaika lakini ukimkandamiza kiunoni na mikono yako hutulia, uke huwa na rangi nyekundu na hutoa ute mweupe. Baada ya dalili za mwanzo nguruwe huwa tayari kupandwa baada ya masaa 38 – 42 na hudumu kwa masaa kama manne (4) inashauriwa ukiona tu dalili za mwanzo umpeleke jike kwenye banda la dume

MIMBA
Mimba huchukua siku 114 mpaka watoto kuzaliwa (miezi 3 wiki 3 siku 3) kipindi cha ujauzito nguruwe jike hula sana mpaka kiasi cha kilo 5 -7 kwa siku apewe mlo kamili lakini kuwe na umakini asinenepe sana na ikifika wiki ya mwisho ahamishiwe kwenye banda la kuzalia (furrowing pen)

BANDA LA KUZALIA


Liwe na ukubwa usiopungua 3m * 2m, liwe na sehemu ya watoto ambayo mama mtu hawezi kufika watoto waingie huko kwa kupenya, hii husaidia nguruwe asiweze kuwalalia watoto wake. Sehemu ya watoto iwe na chanzo cha joto kama vile jiko, hii husaidia kufundisha watoto wakimbilie kule muda wote

Friday, September 25, 2009

UFUGAJI WA NGURUWE - SEHEMU YA PILI

Sehemu ya pili ya maelezo kuhusu ufugaji wa nguruwe tuaangalia nguruwe dume ambaye ndiye atakuwa natumika kwa ajili ya kupandishia majike kwenye mradi wa nguruwe, wengine huwa wanatumia madume ya kukodi, lakini kama utakuwa na majike zaidi ya 10 utahitaji kuwa na dume kwenye mradi wako,

UCHAGUZI WA DUME
Dume litoke kwenye kizazi ambacho hakina historia ya magonjwa na wana historia ya kuzaa watoto wengi ,wenye afya bora, na ukuaji mzuri, angalia kizazi/ukoo wake uwe na chuchu nyingi zisizopungua 14 zikiwa 18 ni nzuri zaidi

BANDA LA DUME
Liwe na ukubwa usiopungua 3 m * 2.5m geti liwe lachuma na linafunguka kuelekea kwa ndani na nje pande zote mbili, siku zote majike ya pelekwe kwa dume na si kinyume chake.

CHAKULA
Dume alishwe kilo 2 – 3 za mlo kamili wenye kiasi cha wastani cha protini, epuka kumlisha mashudu mengi kwa sababu yana kuwa na kemikali inayojulikana kama omega 3 fatty acids ambayo hupunguza kiasi cha manii kwa nguruwe, tumia mimea kama lukina na desmodiam au dagaa kama chanzo cha protini

UPANDISHAJI
dume aina ya saddle back akimpanda jike aina ya landrace


Madume huanza kupanda yakifikisha umri wa miezi 12 – 14 hupanda jike moja mara 2 kwa siku na hupanda majike 6 kwa kila siku 8 na majike yasifululize kwa zaidi ya siku mbili zinazofuatana, majike yapelekwe asubuhi mapema kabla ya dume kula chakula
Dume linaweza kuendelea kutumika kwa upandishaji mpaka likifikisha miaka 3 – 4 ndipo unaweza kuanza kutumia dume lingine, uzoefu unaonyesha nguruwe chotara huwa na uwezo wa kupanda mara nyingi na kwa muda mrefu zaidi. Dume moja huweza kuhudumia majike 20 lakini kwa matokeo mazuri tumia dume moja kwa kila majike 15 – 18

UFUGAJI WA NGURUWE - SEHEMU YA KWANZA

Kutokana na maombi ya Bw John Mwaipopo kuhusu ufugaji wa Nguruwe na kuku, leo nimeamua kuanza kumuelezea njia bora na sahihi

AINA ZA NGURUWE (baadhi)
LARGE WHITE


-Hii ndiyo aina kubwa zaidi ya nguruwe wa kufugwa nyumbani
-Kama jina lake lilivyo ana rangi nyeupe mwili mzima
-masikio yake yamesimama wima
-Ana sura iliyobonyea kwa ndani (dish faced)

LANDRACE


-Weupe mwili mzima
-masikio yamelala kabisa
-Wana ukubwa wa wastani

SADDLEBACK


-Ni wakubwa
-Wana rangi nyeusi na mstari mweupe kuzunguka shingo na miguu ya mblele
-Masikio yamelala kiasi


DUROC

Asili yao inatoka tangu mwaka 1812 katika majimbo ya New York na New Jersey ambako ndio walizalishwa kwa mara ya kwanza ingawa pia kuna tetesi kwamba waliletwa toka Uingereza

Wana rangi ya kahawia iliyooza mpaka iliyopauka na kutaka kuwa kama njano, wana masikio yaliyolala kwa mbele na sura ndefu ilyonyooka, wana nyama tamu sana na isiyo na mafuta mengi, ni Mbegu inayotumika Zaidi kwenye kuchanganya na Mbegu nyingine ili kupata uzao wenye nyama tamu na yenye mafuta kidogo, Madume ndio hutumika kwenye kupanda majike ya Mbegu nyingine kama Large White na Lamd race sababu ni kwamba majike ya Duroc hayazai watoto wengi

CAMBOROUGH

Hii ni Mbegu mpya ambayo inatokana na Mbegu za Large white na Land race ambao walichanganywa kitaalam  ili kupata sifa za uzazi wa watoto wengi, ukuaji wa haraka, kutumia chakula vizuri, uzalishaji maziwa wengi kwa ajili ya watoto, sifa ya kipekee ni uwezo wa majike kuendelea kuzaa kwa miaka mingi zaidi ukilinganisha na wengine.


Wana rangi nyeupe tupu, masikio yamelala kidogo kwa mbele na wana uso mrefu ulioonyooka, wana uzazi wa wastani watoto 14 na majike huanza kupandwa wakiwa na miezi 8 tu

Tuesday, September 22, 2009

KILIMO KWANZA

AZIMIO LA KILIMO KWANZA


KWA KUWA Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lilifanya mkutano tarehe 2 na 3 mwezi Juni 2009 jijini Dar es Salaam, kujadili sera na mikakati ya kuleta mapinduzi ya kilimo cha Tanzania pamoja na utekelezaji wake chini ya kaulimbiu ya “KILIMO KWANZA”;


NA KWA KUWA asilimia themanini ya Watanzania hutegemea kilimo kwa ajili ya kuendeleza maisha yao;


KWA KUTAMBUA KUWA changamoto kubwa kwa Tanzania ni kupambana na umaskini na kwamba hili litawezekana hasa kwa kuongeza tija katika kilimo;


KWA KUZINGATIA KUWA Tanzania imejaaliwa kuwa na rasilimali za kutosha kwa ajili mazao, mifugo na uvuvi, ambazo kwa sasa matumizi yake yapo chini;


KWA KUFAHAMU KUWA Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kuwa na kiasi kikubwa cha maji kinachoweza kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji pamoja na ufugaji;


NA KWA KUTAMBUA KUWA jitihada za makusudi zimekuwa zikichukuliwa ili kuboresha kilimo bila mafanikio yakuridhisha;



HIVYO IMEAZIMIWA KWAMBA:

1.KILIMO KWANZA iwe ndiyo dhana ya kuleta mapinduzi ya kijani kwa lengo la kukifanya kilimo cha Tanzania kuwa cha kisasa na cha kibiashara;

2.Dhana ya KILIMO KWANZA ijumuishwe kwenye mipango mbalimbali ya Serikali ili kuhakikisha mafanikio ya utekelezaji wake;

3.Jitihada zifanyike katika kuongeza rasilimali mbalimbali ili kufanikisha utekelezaji wa KILIMO KWANZA;

4.Sekta binafsi ihamasishwe ili iongeze uwekezaji kulingana na wajibu wake katika utekelezaji wa KILIMO KWANZA; na

5.Utekelezaji wa KILIMO KWANZA utaongozwa na nguzo kumi zifuatazo:

I. Utashi wa kisiasa kutoa msukumo wa mapinduzi ya Kilimo.
II. Kugharamia mapinduzi ya Kilimo
III. Uboreshaji wa mfumo wa utawala wa kilimo.
IV. Mabadiliko ya mfumo mkakati katika kilimo.
V. Upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya kilimo.
VI. Vivutio vya kuchochea uwekezaji katika kilimo.
VII. Uendelezaji wa viwanda katika kuleta mapinduzi ya kilimo.
VIII. Sayansi, Teknolojia na Rasilimali Watu katika kuwezesha mapinduzi ya kilimo.
IX. Uendelezaji wa Miundombinu ili kuwezesha mapinduzi ya kilimo.
X. Uhamasishaji na ushirikishwaji wa Watanzania kuunga mkono na kutekeleza KILIMO KWANZA.

Friday, September 18, 2009

NYUNGUNYUNGU JINSI YA KUWAKUZA KWA AJILI YA CHAKULA CHA SAMAKI

Kuna msomaji mmoja wa Zanzibar Bwana Ali Makame Juma (POLO) wa mahinda kaskazini B, ambaye alifurahishwa na maelezo ya ufugaji wa samaki na akaniomba nimwelekeze pia uzalishaji wa nyungunyungu



MAHITAJI
Nyungunyungu
Chombo cha kufugia
Udongo wa juu (top soil)
Mahindi (dona)
Majani makavu

JINSI YA KUFANYA

(A) Andaa chombo chako ambacho hakivuji mfano sinki la bafu, pipa la plastiki (likatwe nusu)
(B) Jaza udongo kiasi cha inchi 4 – 8 kwenye chombo
(C) Weka inchi moja ya majani makavu
(D) Weka mchanganyiko wa dona na vegetable shortenings
(E) Weka nyungunyungu
(F) Funika juu
(G) Ongeza mchanganyiko wa dona na vegetable shortenings baada ya mwezi mmoja na kila baada ya wiki mbili weka 1qt ya maji kila unapoongeza mchanganyiko huu
(H) Weka chombo chako pasipo na mwanga wa jua



KUKUZA NYUNGUNYUNGU KWA AJILI YA CHAKULA CHA SAMAKI NA MBOLEA
MAHITAJI

(a) nyungunyungu
(b) Mabaki ya jikoni/chakula
(c) Kinyesi cha mnyama ambaye hajatoka kupewa dawa za minyoo
(d) Ndoo 3 zenye matobo nusu sentimeta

JINSI YA KUFANYA
(a) Tafuta minyoo kutoka eneo ulilopo, chimba chini au kwenye vinyesi vya wanyama vilivyo lundikana, usi chukue minyoo wa sehemu nyingine kuzuia kuvamia mazingira mapya na kubadili mfumo wa maisha ya viumbe (biodiversity)
(b) Ndoo moja weka minyoo, ya pili weka mabaki ya jikoni nay a tatu iwe tupu
(c) Zipange kwa mpangilio huu ya chini iwe tupu, ya kati iwe na minyoo na ya juu iwe na mabaki ya chakula
(d) Ndoo ya juu ijazwe mabaki ya chakula mpaka juu, na inyunyuziwe maji kidogo kufanya mabaki yawe na unyevu, maji mengi yataua minyoo.
(e) Baada ya muda minyoo itapanda kwenye ndoo ya juu na kuanza kula chakula, chakula kikipungua na kubakia theluthi mbili, toa ndoo ya chini utakachokikuta ni mbolea uiweke bustanini/shambani na uiweke juu
(f) Ndoo yenye minyoo ambayo sasa iko chini itabaki na chakula kidogo na baadhi ya minyoo, minyoo irudishe ndoo ya kati ambayo mwanzo ilikuwa na chakula sababu minyoo mingi itakuwa huko
(g) Ndoo ya juu ijazwe na mabaki ya jikoni tena na endelea na mzunguko huu kwa muda wa miezi 3 minyoo itakuwa mingi tayari kwa ajili ya kulisha samaki
(h) Katikati ya zoezi hili unaweza kutumia baadhi ya minyoo kwa ajili ya kupandishia zamaki (breeding) kumbuka kuweka ndoo hizi kwenye kivuli wakati wote



NJIA NYINGINE RAHISI
Chukua kiroba cha katani na weka pumba za mahindi kama kilo 5 ziloweshe na maji kodogo, tafuta kwenye shina lamigomba mikubwa, chimba pembeni yake na uzike gunia lako, hakikisha mgomba wako haumwagiliwi na maji ya sabuni hata kidogo na wala hauwekewi kemikali yoyote. Acha gunia lako kwa muda wa mwezi mmoja nenda kachimbe ukiwa umevaa gloves za shamba pekua pekua na utakuta nyungunyungu kibao wamezaana, hamisha na ulishe samaki wako, endelea kuvuna kila baada ya mwezi mmoja na kuongeza pumba nyingine kiasi
Hii njia inafaa zaidi kwa ajili ya wale wanaohitaji nyungunyungu kidogo tu kwa ajili ya kulisha samaki wanaopandishwa (breeding stock)

Wednesday, September 16, 2009

HOLSTEIN FRIESIAN - kinara wa utoaji maziwa duniani



ASILI YAKE

Uholanzi katika jimbo la friesland

UZALISHAJI KWA MWAKA
10,158 kg za maziwa
3.64% mafuta
3.05% protini

RANGI
nyeupe na nyeusi, mkia huwa na rangi nyeupe na kwenye paji la uso huwa na rangi nyeupe yenye umbo kama la pembe tatu ,mara chache (1/1000) huzaliwa ndama mwenye rangi nyekundu na nyeupe

UZITO
kilo 1200 majike
kilo 1400 madume



Huyu ndiye aina ya ng'ombe anayeshikilia rekodi ya uzalishaji maziwa kwa kiwango cha juu, maziwa yake hayana mafuta mengi. Nimeshuhudia akitoa maziwa zaidi ya lita 70 kwa siku kwa mikamuo mitatu lita 30 / 20 / 25 Madume yanatumika kwa kulimia na kukokota mikokoteni, Ni mkubwa kushinda nyati ambaye ana uzito wa kilo 800-1000, kama wanavyoonekana kwenye picha urefu wao ni sawa na kimo cha mtu mwenye urefu wa wastani. Kwa Tanzania wanapatikana zaidi Kitulo mkoani Iringa na Uyole (kituo cha utafiti wa kilimo) Mkoani Mbeya, aina hii ya ng'ombe hustawi zaidi katika mazingira yenye baridi kali.

Kama unataka mbegu hii wasiliana na maafisa ugani wa mifugo ili waje kupandisha ng'ombe wako kwa njia ya chupa, mbegu zinazotumika kwa njia hii hutoka kwa madume PURE BREED CLASS A na matokeo yake ni kupata ndama bora

Saturday, September 12, 2009

MAZIWA - Jinsi ya kufahamu kama yameongezewa maji

Ubora wa maziwa hupimwa kwa njia nyingi, kwa mfano harufu ilikugundua kama ng’ombe alitumia dawa yoyote, pia kwa kuangalia unaweza kujua kama maziwa hayana rangi ya kawaida, na kwa vipimo maalum zikiwemo kemikali ili kujua kama maziwa yana ubora usio faa (maziwa hayapimwi kwa kuonja)



Mara kadhaa wafugaji wamekuwa wakiongeza maji kwenye maziwa ili kuweza kujipatia kipato zaidi na hii huwa ni hasara kwa mlaji. Kwa kawaida kuna kipimo kinachojulikana kama LACTOMETER, hiki ni kipimo ambacho kinaweza kutambua kama maziwa yameongezwa maji. Lactometer hutumiwa kwa kuweka maziwa kwenye chombo maalum cha maabara kama test tube na beaker , koroga ili kuyeyusha mafuta ya kwenye maziwa na kisha lactometer hutumbukizwa kwenye maziwa, maziwa mazuri lactometer itasoma kati ya 1.026 – 1.036 tofauti na hapo maziwa yatakuwa yameongezwa maji au kitu kingine, kwa kawaida kwenye maziwa huwa kuna protini, mafuta, maji , chumvi chumvi na sukari (lactose)

Kifaa hiki kinaweza kudanganywa kwa kuongeza sukari, ngano au maziwa ya kopo na kikasoma kwamba maziwa hayajatiwa maji, kwa sababu jinsi lactometer inavyoelea zaidi ndivyo maziwa yanaonekana bora zaidi (hayaongezewa maji)
Kama huna kipimo cha lactometer wala usiwe na wasiwasi wa kuyapima maziwa maana kuna njia za kienyeji ambazo zitakupa matokeo mazuri tu kama au zaidi ya lactometer

NJIA YA KWANZA


Chukua kibiriti toa njiti moja na uichovye kwenye maziwa (haraka) na kisha kuiwasha haraka haraka, kama maziwa hayajaongezwa maji njiti itawaka kama kawaida na kama kuna maji njiti haitawaka au itawaka kidogo na kuzimika hapo hapo kutegemeana na kiasi cha maji yaliyongezwa.


NJIA YA PILI



Mwaga tole la maziwa kwenye mkono wako kasha liache lile tone litirike na kumwagika chini, ukiangalia mule yalikotiririka maziwa utoana yameacha njia yenye rangi nyeupe, hii ni kwa maziwa halisi, na maziwa yaliyoongezwa maji yataacha njia nyeupe ambayo imepauka. Njia hii inahitaji uzoefu kidogo na unaweza kujizoesha kwa kununua maziwa ukayagawanya sehemu mbili na kisha sehem u moja kuyachanganya kiasi na maji, halafu mimina maziwa kutoka sehemu zote mbili na uangalie tofauti yake



TAHADHARI

Kwa wale wanaofuga ng'ombe aina ya Friesian (pure breed) wakati wa mvua nyingi kama ngombe wako utamlisha majani machanga tu bila ya majani makavu na pumba zenye virutubisho, basi maziwa atakayotoa yakipimwa kwa kutumia vipimo hivi yataonekana kama yameongezwa maji, ingawa ki ukweli ni kwamba hayaongezwa kitu chochote

Sunday, September 6, 2009

HOMA YA BONDE LA UFA- tishio kwa wanyama na binadamu

1.UTANGULIZI

Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever) kupitia vyombo vya habari na kupitia Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) umeripotiwa kulipuka mara kwa mara katika eneo letu la Afrika ya Mashariki hasa katika nchi jirani ya Kenya. Ugonjwa huu, kama jina lake linavyoonyesha hutokea kwenye nchi zenye bonde la ufa na Tanzania ni mojawapo ya nchi hizo. Ugonjwa hutokea baada ya mvua nyingi na mafuriko yanayofuatia kuwepo kwa ukame wa muda mrefu.

Uchunguzi wa “remote sensing” uliofanywa na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) unaonyesha kuwa maeneo yaliyo na hatari zaidi ya kuambukizwa na ugonjwa ni pamoja na Kenya, Kusini mwa Somalia, Kusini na Kusini Mashariki mwa Ethiopia, Kusini mwa Sudan na Kaskazini mwa Tanzania.



2.HISTORIA YA UGONJWA

Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever) katika nchi ya Kenya umefahamika kwa zaidi ya miaka 60 iliyopita. Ugonjwa unaofanana na Homa ya Bonde la Ufa ulionekana mara ya kwanza nchini Kenya mwaka 1913. Tangu wakati huo matukio makubwa ya ugonjwa yameonekana katika nchi nyingi za Bara la Afrika ikiwa ni pamoja na Misri, Sudan, Somalia, Kenya, Msumbiji, Nigeria, Senegal, Tanzania, Uganda, Zambia, Zimbabwe, Namibia na Afrika ya Kusini.
Nchi ya Misri ilikumbwa na ugonjwa huu mwaka 1977 na 1978 ambapo watu wapatao 18,000 waliugua na 598 walikufa. Nchi ambazo taarifa zilitolewa za matukio ya ugonjwa huu nje ya Bara la Afrika ni pamoja na Yemen na Saudi Arabia. Kwa hapa Tanzania ugonjwa huu ulionekana mwaka 1979 na 1998 katika mikoa ya Mara, Arusha na Kilimanjaro ambapo ng’ombe, Mbuzi, kondoo na ngamia waliathirika.

3.VISABABISHI VYA UGONJWA NA JINSI UNAVYOENEA


Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever) unasababishwa na virusi viitwavyo Phlebovirus na ambavyo kitaalam vimewekwa katika familia ya Bunyaviridae. Virusi hivi huweza kuishi kwenye mayai ya mbu aina ya aedes, ambayo yana tabia ya kuishi kwenye vumbi kwa muda mrefu na kuanguliwa wakati wa mafuriko. Baada ya kuanguliwa mbu hawa husambaza ugonjwa kwenye mifugo na kwa watu wakati wanapofyonza damu. Mbu aina nyingine kama vile Culex, Mansonia, Anopheles, na Eretmapodites wanaweza kusambaza virusi vya ugonjwa kati ya wanyama na wanyama na kati ya wanyama na binadamu.



Lakini zaidi ya kupata ugonjwa moja kwa moja toka kwenye mbu binadamu wanaweza kupata ugonjwa kupitia kugusa damu au majimaji ya aina nyingine ya wanyama wakati wa kuchinja, kuzalisha wanyama wagonjwa, kushika vitoto vya mbuzi au kondoo vilivyokufa.

Aidha binadamu wanaweza kupata ugonjwa kutokana na kula vyakula visivyopikwa vizuri vitokanavyo na wanyama wagonjwa au wenye virusi.


4.DALILI ZA UGONJWA

4.1.Dalili kwa mifugo
Ugonjwa huu huwapata ng’ombe, mbogo, kondoo, Mbuzi, ngamia na binadamu. Ugonjwa huonekana zaidi kwenye maeneo ya watu wenye mifugo mingi. Dalili za kwanza katika wanyama ni kutupa mimba kwa wingi hususan katika kondoo na ngamia na vifo vingi vya ghafla kwa karibu asilimia 90 ya mbuzi na kondoo wachanga. Kwenye mbuzi na kondoo wakubwa dalili za ugonjwa ni pamoja na kutapika, kutokwa makamasi yenye damu na kuharisha, rangi ya njano kwenye ngozi ya ndani inayofunika macho, midomo na sehemu za uzazi na vifo katika asilimia 10 hadi 20 ya wanyama hawa. Ng’ombe hawaugui sana kama ilivyo kwa mbuzi na kondoo.

4.2.Dalili kwa binadamu
Dalili za ugonjwa kwa binadamu ni pamoja na kuumwa kichwa, kuumia macho wakati yanapoangalia mwanga mkali, mafua, homa kali, tumbo kuuma, kutapika na wakati mwingine kutapika damu. Virusi huchukua muda wa siku mbili hadi sita tangu kuingia mwilini hadi kuanza kuonyesha dalili na ugonjwa unaweza kusumbua kwa muda wa siku tatu hadi saba au zaidi. Vifo kwa binadamu vinaweza kutokea baada ya virusi vya ugonjwa huu kushambulia ubongo na viungo vingine vya mwili ambapo husababisha kuvuja damu.




5.KINGA NA NAMNA YA KUUEPUKA

Kama ilivyokwishaelezwa Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa unasababishwa na virusi na unaenezwa na mbu. Kwa hiyo njia mojawapo ya kuzuia mifugo isipate ugonjwa ni kuiogesha au kuinyunyizia dawa aina ya pyrethroids ambazo ni pamoja na Flumethrin, Deltamethrin na Alphacypermethrin. Dawa hizi tayari ziko nchini na zinatumika kuogeshea mifugo ili kuikinga isishambuliwe na kupe au mbung’o na zinaweza kutumika pia ili mifugo isishambuliwe na mbu.

Njia ya kuzuia binadamu wasipate ugojwa huu ni kutumia vyandarua. Pia wananchi wanaweza kuepuka ugonjwa huu kwa kupika vizuri vyakula vitokanavyo na mifugo. Wizara inashauri wananchi wachukue tahadhari hizi hata kama ugonjwa haujaonekana popote nchini kwa sababu kinga ni bora kuliko tiba.