KURASA

Thursday, April 25, 2013

NAMNA YA KUPAMBANA NA HARUFU MBAYA YA MBWA NDANI YA NYUMBA YAKO

Je unafuga mbwa  wako ndani ya nyumba yako kwa usafi wa hali ya juu, lakini umegundua harufu mbaya ya mbwa wako bado ipo ndani ya nyumba yako?  inawezekana ni kwa kiasi kidogo sana lakini bado inakera maana harufu mbaya ni mbaya tuu. Ambacho hujagundua ni kwamba kuna sehemu kadhaa ambapo hii harufu imejificha, sasa hapa nitakupa siri ya kuondoa harufu hii

(a)Matandiko anayolalia mbwa wako hakikisha yanafuliwa kila wiki, na itapendeza kama utakuwa na seti mbili ili wakati moja imefuliwa na kusubiria ikauke na jua basi unamtandikia hii nyingine

(b)Kama tandiko la mbwa huwa lina kaa kwenye kreti maalum basi tumia brashi kulisafisha na sabuni kisha nalo lianikwe, hii iwe angalau mara 1 kwa wiki, pia katikati ya wiki unaweza kuwa unalisafisha mara kwa mara kwa kutumia masine ya vakyum ya kusafishia mazulia

(c)Kama mbwa wako huwa analalia mito ya makochi yako, basi hakikisha ni mito ambayo inaweza kufulika ili nayo iwe inafuliwa mara kwa mara

(d)Midoli ya kuchezea mbwa wako nayo pia iwe ni ile ambayo inaweza kufuliwa na ifuliwe mara kwa mara ili kuondoa harufu

(e)Angalia sehemu ambazo mbwa wako hupenda kujificha mara kwa mara maana wakati mwingine huwa wanasahau mabaki ya chakula  na kusababisha harufu mbaya

(F)Kabla ya kusafisha mazulia yako yanyunyuzie na baking soda (sina jina la kiswahili) kisha safisha kwa kutumia mashine ya vakyum

PAMBANA NA KUNGUNI KWA KUTUMIA MAJANI YA MAHARAGE

Majani ya maharage yameonesha uwezo mkubwa wa kuweza kuwanasa kunguni kama watapita juu yake, majani ya maharage yanaweza kufanikisha zoezi hilo kwa sababu yana vinyweleo ambayo huwanasa kunguni mara wapitapo juu yake. Pia yana uwezo wa kudhoofisha miguu yao na kuwafanya wasiweze kutembea.

Matumizi ya majani haya kwa kutegesha kwenya chago za vitanda na sehemu nyinginezo yana uwezo mkubwa wa kupunguza uwepo wa kunguni ingawa shaka bado ipo kama yana uwezo wa kuangamiza na kutokomeza kizazi chote.

Kama njia hii itafanikiwa kwa asilimia 100 inamaanisha kupunguza gharama za kutumia kemikali za viwandani ambazo ni aghali ukilinganisha na majani ya maharage ambayo yanapatikana shambani na kwenye bustani zetu

Tatizo pekee ninaloliona kwenye njia hii ni muda wa kutokomeza kunguni kama wamevamia nyumba yako, njia hii inahitaji muda kiasi tofauti na kemikali ambazo zingeweza kuwaua mara upuliziapo, tatizo la kemikali nalo ni gharama, uchafuzi wa mazingira na pia usugu wa wadudu kwenye kemikali hizi ambazo wakati mwingine hupoteza uwezo wa kuangamiza wadudu.

jambo lingine gumu kwenye njia hii ni namna ya kuwafanya kunguni wavutiwe na kupita kwenye majani haya, kwani wasipopita juu yake njia hii haitakuwa na faida yoyote