KURASA

Monday, December 22, 2008

MILONGE (moringa oleifera)Hii ni miti ambayo haiwi mikubwa sana, inakuwa na maua meupe na kisha hutoa mbegu ndogo zinazokuwa kwenye magamba marefu kama kisu. miti hii hustawi zaidi ukanda wa pwani wenye mvua kiasi na joto, hustawi zaidi kwenye udongo usiotuamisha maji na inaweza kustawi kwenye udongo usio na rutuba nyingi na inahimili ukame kwa kiasi kikubwa.

MATUMIZI
Majani yake huweza kupikwa kama mboga na kuliwa, pia yanaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu bila ya kuathiri ubora wake wa virutubisho (nutritional value) majani yake yanavirutubisho vingi kuliko vyakula vingi tulivyozoea mfano


Ina vitamin A nyingi zaidi ya karoti
Ina Calcium nyingi zaidi ya Maziwa
Ina madini ya chuma zaidi ya spinach
Ina vitamin C nyingi zaidi ya Machungwa
Ina madini na pottasium zaidi ya Ndizi
ina protein nyingi zaidi ya nyama na mayaiMATUMIZI MENGINE
Maganda ya mbegu zake yanaweza kutumika kutibu maji(water treatment)unachukua maji yako ambayo unahisi si salama, unachanganya na maganda ya mbegu zilizopondwa pondwa kiasi, unayaacha kwa muda yatuame kisha unayachuja na yanakuwa salama kwa matumizi


Mbegu za milonge zinaweza kutumika kama dawa ya kupunguza sukari mwilini kwa wagonjwa wa kisukari, unachukua mbegu mbili au tatu unazipasua na kuchukua kokwa ya ndani na kutafuna mara 3 kwa siku, matumizi yanaweza kuongezeka au kuzidi kutegemeana na hali ya mgonjwa

Picha hapo chini inaonyesha mbegu za mlonge juu na kulia kwake ni baada ya kupasuliwa na kupata kokwa ya ndani (ambayo ni dawa ya kupunguza sukari mwilini), funguo imewekwa ili kujua ukubwa halisi wa mbegu


Sehemu yoyote ya mmea kama majani, magamba, mizizi, au maua yakipondwa pondwa na kupakwa kwenye sehemu yenye uvimbe ni dawa tosha ya kupunguza hali hiyo, pia dawa hii inauwezo mkubwa wa kupunguza sumu kama umeng'atwa na wadudu kama nyuki, manyigu/dondola, siafu, tandu, nge nk

Mbegu zake zinatoa mafuta (40%) yanayojulikana kama BEN OIL, ambayo hutumika kulainishia mitambo maalum kama saa za ukutani, pia mafuta haya ni dawa ya upele na harara

Monday, December 15, 2008

MAGONJWA YA SAMAKI NA TIBA

Kuna magonjwa mengi ya samaki yanayosababishwa na fangasi, bacteria, protozoa, parasites, virus na mazingira yenyewe. Hapa nitajaribu kuongelea magonjwa machache ambayo mimi ninauzoefu nayo yaani yameshanitokea na nikapambana nayo

Ichthyosporidium (WHITE SPOTS)
Huu ugonjwa kwa kifupi hujulikana kama ICHI, husababishwa na fungus ambao huingia kwa kupitia ngozi na kisha kushambulia maini na figo.
Dalili zake ni samaki kuogelea kwa kupindapinda au kivivu, tumbo kuonekana kama halina kitu (hollow) na alama nyeupe nyeupe kwenye mwili wa samaki

Tiba yake ni pottasium per manganate kwenye maji, Phenoxethol 1% kwenye chakula na Chloromycetin kwenye chakula, dawa zote zinapatikana kwenye maduka (pet shops). kwa kawaida ICHI wana miznguko miwili ya maisha, akizaliwa anaogelea na kujishikiza kwenye mwili wa samaki, kisha anashuka chini kwenda kuzaana (replitications)na kurudi kwenye mwili wa samaki tena. Kwenye hatua hii pottasium per manganate ndio inafanya kazi ya kuzuia ICHI kurudi tena kwenye mwili wa samaki


LEECHES
Ugonjwa huu husababishwa wadudu wa nje (external parasites)ambao hujishikiza kwenye mapezi na mikia ya samaki. Dalili yao ni kuwaona wakiwa wamejishikiza kwenye sehemu zilizotajwa na ndani ya ngozi, huwa na umbo la kama moyo na rangi ya kijivu/nyeupeKwa sababu dalili zinaonekana wazi kwa macho, mara nyingi ugonjwa huu huingia kwenye tank lako kwa njia ya konokono na majani

Matibabu ni kuwaweka samaki ndani ya maji yenye chumvi kiasi cha asilimia 2.5, baada ya dakika 15 leeches wengi watakuwa wamedondoka chini na wale watakaobaki unaweza kuwatoa kwa kutumia kibanio (forceps)
Tiba nyingine ni kwa kutumia Trichlorofon kiasi cha 0.25m/l (robo miligram kwa lita moja ya maji) majani yanaweza kuondolewa ugonjwa kwa kutumia potassium permanganate kiasi cha 5mg/l (miligram 5 kwa lita moja ya maji)

KUOZA MKIA NA MAPEZI
Huu ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria, dalili zake kubwa ni kuwa na rangi nyekundu au rangi ya udongo (hudhurungi) kama damu imevilia kwenye kona za mapezi na mkia na kisha baadae sehemu hizi hunyofoka na kubakia kibubutu.
Sababu kubwa ni kuumia kunakosababishwa na kujigonga au madume kupigana, TB pia inaweza kusababisha hali hii

Tiba yake ni kwa kutumia antibiotics kama tetracycline au chloramphenicol kiasi cha 20-30mg/l (miligramu 20-30 za dawa kwa lita moja ya maji)au mili gramu 250 (1 capsule) kwa chakula cha gramu 25

ingawa magonjwa mengi yanasababishwa na vimelea lakini mazingira nayo pia yanachangi katika kuongeza kasi ya magonjwa, ukizingatia yafuatayo unaweza kuwakinga samaki wako.
(a)Nunua samaki wako toka kwa mtu mwenye uzoefu wa kufuga na ambaye unauhakika samaki wake hawana magonjwa

(b)Samaki wapya watengwe kwa muda kwenye chombo kingine (hospital tank0 kwa siku kadhaa kabla ya kuchanganywa na wengine

(c)hakikisha samaki wako hawali zaidi ya kiwango chao na kuvimbiwa, lisha kwa kipimo sahihi

(d)Epuka kuwaweka samaki kwenye mazingira mabaya kama maji machafu, kuweka samaki wasiopatana pamoja, kuwasumbua kwa kuwashikashika na kugonga gonga tanki

(e)Samaki wagonjwa watengwe kwenye tank lingine (hospital tank)

(F)Nyavu zilizotumika kutolea samaki wagonjwa ziwekwe dawa (disinfection) zikaushwe juani na zioshwe vizuri hii ni pamoja na tank na vitu vyake

(g)hakikisha tank halina kitu chochote cha chuma (metal) na maji ya hospital tank yasiingie kwenye tank kuu

Sunday, December 7, 2008

UPANGAJI (AQUARIUM ARRANGEMENTS)

Upangaji wa tank lako ni muhimu ili kuwapa samaki mazingira mazuri kwa matokeo bora, wakati wa kupanga kuna vitu vya msingi na muhimu vya kuzingatia, na kabla ya kununua au kujenga tank lako lazima ujue ni samaki gani unataka kuweka na idadi yao. Baadhi ya samaki kama Goldfish,, Shaks, Koi n.k huwa wakubwa mpaka kufikia futi moja, kwa hiyo wanahitaji chombo kikubwa zaidi.


WATER PUMP
Hii hukaa nje na kusukuma hewa ndani kwa kupitia mawe ya hewa (air stones) ambazo lazima zikae katikati ya tank, pia kuna aina mbali mbali za urembo ambazo nazo zinaingiza hewa, hizi zinaweza kuwekwa kokote ila ni muhimu zisambae ndani ya tank.

WATER FILTER
Ni vizuri kama itawekwa upande mmoja wa tank na kusukuma maji kwa urefu kuelekea upande mwingine, hii husaidia kuweka mzunguko wa maji ambapo chini maji yanavutwa na na juu yanatolewa na pump.

SAKAFU
Sakafu ya tank lako lazima iwe na mchanganyiko wa mchanga na changarawe, ambao hutumika kwa ajili ya mimea kujishikiza. Mchanga na changarawe pia zinatumika kama filter kwa sababu zinachuja uchafu na mabaki ya chakula

MAPAMBO
Hii inajumuisha mimea, urembo na sehemu za kujificha samaki, mapambo yawe ya kutosha ili samaki wajisikie huru kwa sababu inawafanya waone kama wako kwenye mazingira yao halisiMAJI
Kama unatumia maji ya bomba ni vizuri yawe yamekaa angalau masaa 12 baada ya kukingwa toka bombani. Hii ni kwa sababu huwa yanatiwa chlorine ili kuuyafanya yawe salama kuyanywa, hii chlorine huua samaki. Ukiyaweka wazi kwa masaa zaidi ya 12 chlorine huondoka kwa njia ya mvuke (evaporation), maji wazuri zaidi kutumia ni ya visima vya kuchimba (drilled water wells)kwa sababu yana chumvi chumvi za asili zinazosaidia kuwakinga na magonjwa

baada ya kuweka maji ya bomba kwenye tank unaakiwa uweke chumvi ya mezani kijiko kidogo kwa lita kwa lita 25 za maji, ukianzia na kumuweka samaki mmoja na kumwacha kwa saa zima huku ukimchunguza, ukimwona yuko salama unaweza kuwaweka samaki wote waliobakia

MAJANI NA MIMEA (aquatic plants)

Majani ni kitu muhimu sana katika ufugaji wa samaki, kazi ya majani ni kusafisha maji na kuweka mazingira ya uhasilia kwa samaki, kuna majani ya bandia lakinioiyanabakia kama urembo tu kwa sababu hayawezi kusafisha maji. Ili majani yakue kwa kiwango kizuri ni lazima mahitaji yafuatayo yazingatiwe


MWANGAZA
Mwanga wa kutosha unahitajika kwa ajili ya ukuaji wa majani na mimea ya majini, hii husaidia katika tengenezaji wa chakula kwa kutumia majani yake, mwanga wa tube lights ni mzuri zaidi ila usiwe mwingi sana kwa sababu utachangia ukuaji wa algae kwenye maji. kiwango cha mwanga kinachoshauriwa ni 1.5 watts kwa kila galon ya maji (1.5wpg), mfano tank la galon 20 linahitaji taa ya watts 30
MIZIZI
Mizizi ya mimea na majani inahitaji kujishikiza kwenye sakafu yenye udongo, changarawe au mchanga ili iweze kufyonza virutubisho, inashauriwa usiweke changarawe tu bali uchanganye na mchanga


VIRUTUBISHO
Ili mimea iweze kukua vizuri inahitaji virutubisho kama nitrogen, potasium, phosphorus, chuma na kadhalika, nitogen ambacho ni kirutubisho kikuu kinapatikana kwenye vinyesi vya samaki amabvyo vinatoka kama ammonia. Pia maji yenyewe na chakula cha samakikina madini haya kwa kiasi kidogoCARBON-DIOXIDE
Hii ndio hewa inayotumiwa na mimea na inapatikana kutokana na samaki wanavyo pumua (respiration). Kwa kawaida samaki wanavuta oxygen na kutoa CO2 ambayo ndio inatumiwa na mimea, wingi wa upatikanaji wa hewa hii ya co2 inategemeana na wingi wa samaki.

Saturday, December 6, 2008

WATER FILTER AND PUMP

WATER PUMPHiki ni chombo muhimu sana katika ufugaji wa samaki, kazi yake kubwa ni kuingiza hewa ndani ya chombo cha samaki. Kwa kawaida aquarium huwa inafunikwa sehemu kubwa ya juu na hivyo kupunguza kiwango cha hewa inayoingia. Water pump inaongezea hewa katika style tofauti, hewa inaingia kupitia mawe ya hewa(air stones) na pia kwa kupitia urembo mbali mbali ambao unakuwa ukicheza, kuzunguka au kufunuka na kuruhusu hewa kuingia

mirija ya pump


Kwa kawaida water pump inakuwa nje na inaingiza hewa kwa kutmia mirija inayoingia ndani ya maji mpaka kwenye sakafu ya chombo, ambako huunganishwa na vitu husika kama mawe ya hewa na urembo mbalimbali, pump pia husaidia kuleta mzunguko wa maji na kujenga hali ya mazingira ya uhalisia kwa samaki kama wako mtoni au bwawani/ziwani.

WATER FILTER
Hii hfanya kazi zote kama pump ila tofauti ni kwamba yenyewe ina kazi ya ziada ya kusafisha na kuchuja uchafu kwenye maji

Kwa filter ndogo huwa zinazama ndani ya maji (submeged) kwa sababu huwa zinapoozwa joto na maji hayo hayo,Sehemu ya chini ya filter huvuta maji na hewa huvutwa kutokea juu kwa kutumia mrija mdogo unaokuwa nje ya maji na sehemu ya kati huwa inatoa mchanganyiko wa maji na hewa.

Filter kubwa hukaa nje na mipira ya kutoa maji na kuingiza maji na hewa ndio huingia kwenye maji, hizi mara nyingi huwa zinatumiaka kwa ajili ya aquarium kubwa na mabwawa au vyombo vingi kwa mara moja kwa sababu vinaweza kusafisha vyombo zaidi ya kimoja kwa wakati

Ndani ya filter kuna chujio ambalo husafishwa kwa urahisi mara linapochafuka kwa wastani wa mara moja kwa wiki na likichoka huwa lina badilishwa

Friday, December 5, 2008

GOLD FISH

Hawa wapo aina nyingi sana duniani, lakini hapa kwetu Tanzania kuna aina ambazo ni maarufu zaidi aina hizo ni Gold, Black Moor, Bubbles eye,Oranda, Telescope eye Shibunkins, Red cap n.k


RED CAP
Ni samaki wagumu kiasi wanaoweza kuhimili mazingira ya wastani, wanahitaji joto la wastani mpaka baridi kiasi, kwa mazingira ya tanzania hawahitaji heater na wala wasiwekwe sehemu amabayo watapata mwanaga wa jua moja kwa moja (direct sunlight) labda kama uko sehemu zenye baridi sana

SHUBUNKINS


Hakikisha chombo cha kufugia kina nafasi ya kutosha, gold fish mkubwa nahitaji kiasi cha lita 25 za maji peke yake ili aweze kuishi maisha mazuri. kwa kaida samaki hawa huwa wanachafua sana maji kwa sababu ya tabia yao ya kula sana wakati wote (piggy), na inamchukua muda mfupi kukitoa chakula kwa njia ya kinyesi

BLACK MOOR


Chombo cha kufugia kinatakiwa kiwe na sehemu za kujificha samaki kiasi cha 50% - 70% ili samaki wajione wako salama. Hakikisha unapunguza maji 25% kila baada ya wiki na kuweka maji mapya, na kila baada ya wiki 4 unatoa maji yote, unasafisha chombo chako, mawe, filter pamoja na urembo uliopo ndani na kuweka maji mapya 100%

TELESCOPE EYES

Gold fish huwa wanakula mara mbili kwa siku, tumia chakula maalum ambacho kinauzwa madukani, vyakula kama uduvi, dagaa na ubongo vinaweza kulishwa kama wako kwenye bwawa tu kwa sababu huchafua sana vioo na maji. Gold fish huwa wanakula chochote kile (omnivorous)ila inabidi uwe makini usije ukawalisha zaidi (overfeeding) kwa sababu wanaweza kufa

GOLDHakikisha chombo kina mfumo wa kusafisha maji (filter) na mfumo wa uingizaji hewa (pump)ili kujua kipimo halisi cha ukubwa wa filter na pump itabidi usome mwongozo wa mtumiaji na mtengenezaji (user manual)

BUBBLES

Sunday, November 30, 2008

SAMAKI WA UREMBO (AQUARIUM FISH)

Baada ya kuongelea kilimo cha mitiki, sasa naomba nigeukie upande mwingine wa ufugaji wa samaki wa urembo majumbani au popote.

Samaki wa urembo wako aina nyingi, wanamahitaji na tabia tofauti, tumezoea kuona wengi wakifugwa kwenye vyombo vya kioo (aquarium) na mara chache kwenye mabwawa. Mara nyingi majumbani wanakuwa kwenye aquarium na kwa wale wazalishaji (breeders) wnazalisha na kukuza kwenye mabwawa, mara chache sana wanatumika kwa ajili ya urembo kwenye mabwawa


Samaki wako aina nyingi lakini kwa hapa Tanzania waliozoeleka sana ni goldfish, koi, angels, cichlids, barbs, sharks, parots, catfish, gupies, sotas, zebra na kadhalika, na mimi nitajaribu kuwachambua ufugaji na mazingira wanayohitaji kwa baadhi ya samaki ingawa mahitaji yao hayatofautiani sana

Tuesday, October 7, 2008

UANDAAJI WA VIPANDIKIZI KABLA YA KUPANDA


Kabla ya kupanda mche wa mtiki inabidi uandaliwe kukabiliana na mazingira magumu hasa ukame, ili miche iweze kumea vizuri baada ya kupandwa inabdi ikatwe juu na kwenye mizizi na kubakia kama vipandikizi.


Mche unakatwa juu na chini na kubakia juu robo na robotatu kwenye mzizi, hii inasaidia kuanza kukua mara moja na hata kama mvua zitakuwa hafifu bado miche hii itahimili ukame kwa muda mrefu zaidi.


Vipandikizi pia vina sifa ya kuwa na uwezo wa kunyooka bila kupinda pinda wakati wa ukuaji, tofauti na miche ya kwenye vipakti.
Sehemu ya juu ya kipandikizi inaachwa na macho mawili tu kwa ajili ya kutoa matawi ambapo yatakapoanza kuchipua moja litakatwa na kubakia na moja ambalo litakuja kuwa mche na mti bora hapo baadae


Ukiangalia picha hapo juu, kulia kwako ni miche kabla haijakatwa kubakia vipandikizi na kushoto kwako ni fungu la vipandikizi kabla ya kukatwa. Na huyo jamaa hapo anaonekana akipanda kwenye shimo la wastani moja ya vipandikizi vyake

Tuesday, June 10, 2008

KUPUNGUZA MAJANI


Hii ni hatua muhimu sana kwa ukuaji wa miti ya mitiki, na mara nyingi hufanyika ili kupunguza upotevu wa maji toka kwenye mmea. Mara nyingi kipindi cha jua miche midogo huwa ipata tabu sana kupambana na hali ya ukame, na kama ilivyozoeleka ukanda wa pwani ambako ndio miti hii inastawi zaidi huwa na jua kali sana mpaka kufikia kiasi cha nyuzi joto za sentigredi 33 - 34.

Miti ya mitiki huwa inapoteza maji mengi sana kupitia majani yake kwa sababu ina majani mapana sana ambayo yanapoteza maji mengi sana kipindi cha jua (evaporation). Kipindi cha kupunguzia majani ni kipindi ambacho ardhi inakuwa wazi kwa sababu hatua hii hufanyika mara baada ya kupalilia miti yako

Wakati wa kupunguzia majani inabidi kuwe na umakini ili kuepuka kuvunja sehemu ya juu ya mti (kikonyo) na unapopunguzia majani ni lazima utoe jani moja kila upande. Unaweza kutumia mikono lakini ili kuepuka madhara nashauri visu vidogo vitumike kupunguza majani ya chini.Monday, June 9, 2008

UPANDAJI

Upandaji wa mitiki huafanyika mara baada ya mvua za kwanza kuanza kwa sababu ukuaji wa miche midogo huitaji mvua za kuendelea kwa kipindi kirefu, pia mvua za kwanza huwa na nitrogen ya kutosha kusaidia ukuaji wa mimea.

Vipimo vya upandaji kati ya mche na mche ni mita 2.5 mpaka 3, kama utatumia kipimo cha mita 3 kwa 3 ekari moja (mita 70 kwa 70) itaingia miche kama 530 kwa wastani. miche ya mitiki hubananishwa wakati wa upandaji ili kuisaidia ikue kwa kunyooka kwenda juu ingawa mingine ya katikati itapunguzwa baada ya miaka 5 - 6 kuipa nafasi ile iliyobaki kama 260 iweze kunenepa zaidi.

Mashimo ya mitiki hayahitaji kuchimbwa kabla kwa sababu yanaweza kufukiwa na mvua, kwa kawaida mashimo haya yana kuwa na urefu usiozidi futi moja (urefu wa rula ya mwanafunzi) kwa hiyo siku ya upandaji wachimbaji wa mashimo ndio wawe wapimaji wa nafasi kati ya mti na mti. Wale wapandaji wahakikishe kwamba sehemu ya mzizi inakuwa chini ya ardhi na imefunikwa na udongo yote na sehemu ya shina inakuwa juu.

Miti ikishapandwa iachiwe sehemu kidogo ya kisahani kwa ajili ya kuhifadhia maji kidogo, nyasi kidogo zinaweza kuwekwa kuzunguka shina ili kuzuia unyevu kunyonywa na jua (evaporation) ingawa hii wakati mwingine inaweza kuwavutia mchwa wakashambulia mche wako.

Miche ikianza kuchipua baada ya siku chache vichipukizi zaidi ya kimoja vitachipua, hapa inatakiwa uvikate vyote na kubakiza chenya afya (viwili vitakuwa sawa)

UANDAAJI WA MICHE KABLA YA KUPANDWA

Upandaji wa mitiki hufanyika katika namna mbili, wa kwanza ni ule wa kupanda miche ikiwa mizima kutoka katika vifuko na ya pili ni kutumia miche toka kwenye kitalu ambako inashauriwa kuing'oa na kisha kukata sehemu ya mzizi na shina, ambako utabakiwa na mzizi 70% na shina 30%.

Kitaalamu miche iliyokatwa na kubaki kama vipandikizi ina sifa mbili kubwa
(a) Miche itakayoota katika vipandikizi hivi ina uwezo mkuwa wa kuhimili ukame iwapo kutakuwa na upungufu wa mvua za msimu wakati wa upandaji. Mara nyingi miche ikipandwa kwenye mvua pungufu, huua sehemu ya juu ya shina/mche na sehemu ya chini ya mzizi kama vile miti inavyopukutisha majani, na hii husaidia kuhifadhi maji ndani ya mmea. Sasa kabla hili halijatokea sisi tunakata kabisa hizo sehemu zitakazo kufa iwapo kutakuwa na mvua pungufu.

(b) Miti inayoota katika vipandikizi inaasilimia kubwa zaidi ya kukua kwa kunyooka kwenda juu, wakati miti iliyokulia kwenye vifuko ina uwezo zaidi ya kupinda kwa sababu wakati wa uotaji ikiwa midogo, miche hushindana kukua na kukimbilia mwanga wa jua. Wakati huu ndio mche huanza kupinda kufuata mwanga ili kushindana na ile iliyokua haraka. Ili kuepuka hili, kata miche yako na ianze kuchipua upya ikiwa shambani kwenye nafasi.

Vipandikizi vilivyokatwa vinauwezo wa kukaa mpaka siku 7 bila kufa hadi siku ya kupandwa shambani, kwa maana hiyo unaweza kuvisafirisha toka mkoa mmoja hadi mkoa mwingine kwenda kuvipanda. Kama utakuwa umeandaa vipandikizi vyako na mvua zikawa bado kuanza, weka udongo kwenye chombo chochote mwagia maji kidogo (yasituame) halafu chomeka vipandikizi vyako na usubiri siku ya mvua kuanza ili ukavipande

UANDAAJI WA SHAMBA

Kabla ya kupanda miche ya mitiki shamba ni lazima liwe limeandaliwa, uandaaji wa shamba ni lazima ufanyike mapema kabla ya mvua kuanza kunyesha kwa sababu upandaju huanza mara baada ya mvua za kwanza kunyesha.

Uandaaji wa shmba la mitiki ni wakawaida kama ule wa mashamba mengine, visiki vyote ni lazima ving'olewe kisha majani yote yalimwe na ikiwezekana yatiwe moto kwa umakini wa hali ya juu kuepusha madhara ya moto.

Kama ulimaji utakuwa ni wa trekta au kutumia jembe la kukokotwa na wanyama (plau) hii ni nzuri zadi kwa sababu majani yatafukiwa ardhini na kuongeza rutuba kwenye udongo. uuaji wa magugu kwa kutumia madawa kama round up wanamazingira huwa hatushauri, ingwa ni njia moja ya haraka na nafuu zaidi kuliko kulima kwa jembe lolote lile.

Kwa ukanda wa pwani mvua za masika huanza kati ya mwezi wa 3 - 4 kwa hiyo ni vizuri sana kama utaanza kuandaa shamba kwenye mwezi wa 2 (february) na mvua za vuli huanza kwenye mwezi wa 11 (November) kwa hiyo shamba liwe tayari kwenye mwezi wa 10 (October)

Ni vizuri pia ukaangalia na mwenendo wa mvua na lini zinategemewa kuanza kwa kupitia kwa wakala wa hali ya hewa hapa nchini (Tanzania Meteological Agency) kupitia tovuti yao ambayo ni
http://www.meteo.go.tz/wfo/seasonal.php

Saturday, May 24, 2008

MICHE BORA KWENYE KITALU
SPECIE tectona grandis (teak)
SEEDS SOURCE Bombani Muheza Tanga
DATE PLANTED January 2008
AGE 3 moths from germination
GERMINATION RATE 70%
USED SEEDS TREATMENT METHOD deep soaking & changing water after 12hrs for 4 daysFriday, May 23, 2008

KITALU CHA MITIKI


Ninashauri kitalu kiwe karibu na shamba na pia chanzo cha maji kiwe karibu. Kitalu cha mitiki kinaweza kuwa katika tuta lolote lile la juu au la chini, udongo unaofaa ni ule wenye rutuba na usiotuamisha maji. Tuta liwe kwenye sehemu yenye mwanga wa kutosha na kusiwe na kitu kitakachokinga mwanga wa jua, hii ni kwa sababu mbegu na miche ya mitiki inahitaji mwanga wa jua wa kutosha.
UOTESHAJI


Mbegu za mitiki zioteshwe kwa mistari zifukiwe kiasi cha kama sentimeta moja chini ya udongo, hakikisha kwamba mbegu haziwi chini sana ya udongo hii itasaidia katika uchipuaji wa mbegu zako. Nafasi kati ya msitari na msitari ni sentimeta kumi (10).
Uotaji wa mbegu huchukua muda kiasi cha siku 30 - 45, wakati wote huu kabla na baada ya kuota kitalu inabidi kimwagiwe maji ya kutosha angalau mara moja kila siku, maji yamwagiwe taratibu kwa kutumia vyombo vya kuwagilia (watering can) ili kuzuia kuzifukua mbegu zilizopo ardhini. Mara baada ya mbegu kuota ziendelee kumwagiwa maji ya kutosha.
Maara baada ya miche kufikia uefu wa sentimea 8- 10, mbolea za kukuzia zinaweza kuwekwa ili kuhahkikisha miti inakuwa na nguvu, wkati huu unaweza kupunguza kiasi cha maji ya kumwagilia ili kuzuia mbolea kuchkuliwa na maji.
UTUNZAJI


Muda wote hakikisha magugu yanang'olewa ili yasinyang'a nyane chakula na miche yako, hakikisha pia kingo za tuna zinanyanyuliwa muda wote kuzuia upotevu wa maji. Huna haja ya kutandaza nyasi juu ya tutalako kwa ajili ya kuzuia upotevu wa maji, kumbuka mbegu za mitiki zinahitaji mwanga wa kutosha na hewa ili ziweze kuchipua.


Kama utagundua kuna wadudu wanaoshambulia kitalu chako, omba ushauri kwa mabwana shamba dawa gani utumie ingawa ni nadra sana mitiki kushambuliwa na wadudu.
Kwa wale watakaouza miche hii au wanategemea kuisafirisha umbali mrefu, basi itawalazimu kuiweka kwenye vifuko, hii iatahisisha usafirishaji mpaka shambani, ingawa kitaalamu miche ya kwenye vifuko huwa inakufa mingi zaidi na huwa inapindapinda wakati wa ukuaji. Uhamishaji wa miche kwenye vifuko hufanyka wakati miche ina urefu wa sentimeta za wastani 2

Thursday, May 22, 2008

MBEGU

Mbegu za mitiki lazima zikusanywe kutoka katika miti iliyokomaa, hii itasaidia katika uotaji kwa sababu mbegu za miti hii ni ngumu kidogo kuota. Unaweza kupata mbegu kutoka kwenye mashmba makubwa ya miti au ukanunua kutoka kwa wakala wa mbegu za miti wa taifa (TTSA) ambao wana matawi yao katika kanda tofauti nchini (Morogoro, Lushoto na Iringa) http://www.ttsa.co.tz/

Mbegu zilizo bora ni zile zilizohifadhiwa mahali pakavu, kabla ya kupanda mbegu inabidi ziloekwe kwenye maji yanayo tembea kama mto kwa siku 3 (masaa 72) au unaweza kuzitia kwenye gunia na kuloweka kwenye chomba chenye maji kwa masaa 72, huku ukibadilisha maji kila baada ya masaa 8 -12. Hakikisha unapoloweka mbegu, lile gunia unalifunga na kitu kizito kama jiwe ili ziweze kuzama kabasa ndani ya maji.

Kila unapobadilisha maji utagundua kwamba maji unayomwaga yanakuwa na rangi nyekundu, hii ni kawaida kwa miti hii huwa inaacha alama ya rangi nyekundu (red dye) kama utakata matawi yake kwa mkono.

Ukisha maliza kuloweka mbegu kwa masaa yasiyopungua 72, mbegu zianikwe kwenye jua ili ziweze kukauka kabisa. Unaweza kuzianika juu ya bati ili kuharakisha ukaukaji, hakikisha unazi tandaza ili zikauke vizuri, hii inaweza kuchukua hata siku mbili kama hamna jua la kutosha. Mara baada ya kukauka mbegu zikusanywe na kuhifadhiwa mahali pakavu na pasipo na joto tayari kwenda kupandwa kwwenye kitalu.

UTANGULIZI

Watu wengi siku hizi wamekuwa wakijihusisha na upandaji miti katika mashamba binafsi, miti hii ina matumizi mbali mbali ikitumika kama mipaka, chanzo cha kuni, mbao, chakula cha mifugo, urembo n.k.

Miti ya mitiki ni moja ya miti inayotoa mbao ngumu na aghali zaidi duniani, vitu kama boti na mashua, vitako vya bunduki, fimbo za askari, milango na samani mbalimbali za majumbani hutengenezwa kutokana na miti hii.

Mti hii inasifika kwa uimara wa kutoliwa na wadudu kama mchwa na kuoza kutokana na maji kwa sababu ina hali ya mafuta mafuta. Mbao zake zina rangi nyekundu iliyokolea na kama mti litunzwa vituri kwa kupunguziwa matawi mapema, mbao zinakuwa hazina vidoda vidonda.

Kwa hapa nchni mashamba makubwa yanapatikana Kilombero, mtibwa na longuza (Lushoto) pia kuna wakulima wadogo wadogo katika mikoa ya Tanga, Morogoro na Pwani.

Kwa kawaida miti hii hustawi zaidi katika ukanda wa pwani wenye joto na mvua nyingi, hustawi katika udongo wa kitifu tifu wenye mbolea ya kutosha na usio tuamisha maji kabisa. Miti inayopandwa mabondeni inakuwa haaraka sana kuliko iliyopandwa sehemu za miinuko, ingawa miti ilipondwa kwenye miinuko inatoa mbao bora zaidi kutokana na kukua taratibu kidogo.

Uvunaji unaanza baada ya miaka 6-7 kwa kutoa miti ya kujengea ambayo hupatikana kwa kupunguza miti ya kati ili ile inayobaki iweze kukua zaidi. Mbao huanza kuvunwa baada ya miaka 12 - 15, ikifuatiwa na miaka 18. 20, 25, kumbuka uvunaji huu unafanywa kwa kupunguza nusu ya miti (kati ya mti na mti) na kuacha inayobaki iendelee kukua zaidi
.