KURASA

Saturday, June 20, 2009

MMBONO- JATROPHA (bio diesel)

1.0 UTANGULIZI
Mmbono kwa kitaalam Jatropha curcas ni mti jamii ya nyonyo wenye mbegu zitoazo mafuta yenye sifa kama nyonyo. Huota kwenye maeneo ya nyanda kame na yenye upungufu wa rutuba. Mmea hauliwi na mifugo wala wanyama pori na kufanya mmea ufae kulimwa kwenye maeneo ya wafugaji huria. Mmea hutoa mbegu zenye mafuta ambayo hayaliwi bali hutengenezea sabuni, kuendesha mitambo, gesi kama nishati. Kutokana na faida nyingi kwa binadamu kiafya, kiuchumi na mazingira, mmea unaweza kuzalishwa kama zao. Mmea huu umetokea Marekani ya Kati na kusambazwa hadi Afrika Mashariki na Wareno.

2.0 AINA
• Mmea ni wa jinsia moja (monoecious) na maua yake huwa ya jinsia moja.
• Mmea unaweza kudumu hata zaidi ya miaka 50.
• Kuna aina tatu za mmea ambapo aina moja iliyopo Mexico huliwa baada ya kukaangwa.
• Kwa sasa aina inayopo hapa Tanzania; Jatropha curcas haifai kuliwa bali kwa matumizi mengine.
3.0 MAZINGIRA:
Mmea huweza kustawi katika mvua za kuanzia 250mm hadi 2380, lakini uzalishaji mzuri huwa kwenye 625mm – 750mm. Kwenye sehemu zenye unyevu wa kutosha, mkulima atapata matunda wakati wote wa mwaka.Mmea hustawi kwenye nchi za Kitropiki na una tabia ya kustahimili ukame. Mmea hustawi kwenye udongo usiotuamisha maji, wenye tindikali kuanzia Ph 4.5. Mmea hupatikana kwenye mwinuko kuanzia mita 0 hadi mita 1600 juu ya usawa wa bahari ila hustawi vizuri kati ya mita 450-750 juu ya usawa wa bahari.

4.0 UTAYARISHAJI SHAMBA
Shamba litayarishwe mapema kwa kuchimba mashimo kabla ya mvua.

5.0 UTAYARISHAJI MBEGU/VIPANDIKIZI

Tumia mbegu zilizokomaa na kujaa vizuri. Mbegu zioteshwe katika vitalu ili kupata miche bora. Miche ikae kitaluni miezi 2 hadi 3. Kama utapanda moja kwa moja shambani, tumia kilo 5-6 kwa hekta. Au pandikiza vipandikizi vyenye urefu wa sm 45–100 katika shimo la sm 30. Mbegu huota kuanzia siku 9 na kutoa matunda baada ya miaka 3–4. Vipandikizi hutoa matunda kuanzia miezi 9 kutegemea na sehemu.

6.0 KUPANDA KWA NAFASI.

Panda mbegu 2 kwa shimo kwa kina cha sm 2 hadi sm3. Nafasi kati ya mche ni 2.5m x 2.5m.Nafasi kama hiyo hukupatia miti 1600 kwa hekta moja.Aidha nafasi ya 3mx3m itumiwe katika kilimo mchanganyiko wa mibono na mazao mengine.

7.0 PALIZI NA KUPUNGUZA MICHE
Punguzia miche baada ya wiki 4 na kubakiza mmoja, kutegemea na utayarishaji shamba. Palizi sio lazima ifanyike isipokuwa kama umefanya kilimo mchanganyiko palizi inaweza kufanyika kwa kuzunguka mmea au kufyeka magugu mara moja kwa mwaka. Kukata matawi kufanyike baada ya mwaka mmoja au miwili.

8.0 KUZUIA MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU
Hakikisha mimea haisongani na shamba ni safi. Mmea haushambuliwi na magonjwa ila wadudu jamii ya beetle, golden flea beetle wanashambulia majani. Athari ya mavuno hutokea endapo uharibifu katika majani utafikia zaidi ya asilimia 40. Mkulima afanye ukaguzi wa shamba lake mara kwa mara na kuwasiliana na wataalam wa kilimo kabla ya kupiga madawa.
9.0 UVUNAJI
Matunda yaliyokomaa tayari kwa kuvunwa huwa na rangi ya kahawia. Uvunaji hufanywa wa mikono au kwa kupiga kwa fimbo au kifaa maalum kilichotengenezwa kwa kutumia waya, mfuko wa pamba na fimbo ndefu, mbegu huguswa na kipande cha waya na kudondoka kwenye mfuko au kitambaa kilichowekwa chini ya mmea.Kiasi cha kuanzia gramu 300 hadi kilo 9 za mbegu zinaweza kuvunwa kwa mmea au tani 2 – 6 kwa mwaka kwa hekta. Mti unaweza kutoa mbegu mfululizo kwa mwaka kwa sehemu zenye unyevu au kuzaa mara mbili kwa msimu sehemu zenye ukame.

10.0 HIFADHI YA MAZAO
Baada ya kubangua mbegu kwenye matunda zikaushwe vizuri kabla ya kuhifadhiwa kwenye mifuko ya plastiki/magunia. Hifadhi mavuno kwenye sehemu kavu na dhibiti viumbe waharibifu kama panya.


11.0 MANUFAA YA MMEA

(1)Mbegu hutoa mafuta mengi yanayotengeneza sabuni na nishati ya kuwashia taa, jiko na gas, nchi nyingi hutumia mafuta haya kama diesel. Nishati hiyo mbadala hupunguza kasi ya matumizi ya kuni/mkaa na hivyo kuhifadhi mazingira.
• Zao linafaa katika maeneo ya nyanda kame yenye migogoro ya wafugaji na wakulima kwa vile mmea hauliwi na mifugo.
• Baada ya kusindika mbegu, mashudu hutoa mbolea ya komposti yenye ubora kama mbolea ya kuku.
• Uzalishaji wake una gharama ndogo ukilinganisha na mazao mengine
• Kama zao, wakulima wataongeza pato na kupunguza kasi ya magonjwa ya ngozi.
• Kuzuia mmomonyoko wa udongo kwa njia ya upepo na maji.

12.0 MASOKO
Mmea hutoa bidhaa kama mafuta, sabuni, gesis na mbolea zenye manufaa mengi kwa jamii. Hivyo wakulima wazalishe kwa wingi, wafanye mikataba na wasindikaji, wasafirishaji na wanunuzi wa mazao, kutumia mbinu za masoko na kupata mafunzo ya kutosha ili kutosheleza mahitaji ndani na nje ya maeneo ya uzalishaji

Kuna baadhi ya wanamapinduzi ya kilimo wanaupinga mmea huu, wakiamini kwamba kwa sababu mkulima anapata hela nyingi na kwa muda mfupi, basi wakulima wengi wataacha kupanda mazao ya chakula na badala yake watapanda mmea huu. matokeo yake ni kuwa uzalishaji wa chakula utapungua sana duniani na kusababisha njaa