KURASA

Thursday, November 19, 2009

MIGRAVILLEA

Kutokana na maombi ya ndugu Leonard Kisenha mwenye shamba lake pale Goba, alitaka kujua kati ya Mitiki/misoji na migavilea (GRAVILLEA ROBUSTA), je ni miti gani itamfaa kupanda kwenye shamba lake? Jibu ni rahisi ukuaji mpaka kuvuna umri ni karibia sawa sawa ila wakati wa kuvuna mwenye mitiki atapa faida nyingi sana (maradufu) kutokana na bei ya mitiki kuwa juu sana, pia hali ya hewa ya pwani kwenye joto inafaa zaid kwa mitiki tofauti na migravilea ambayo hukua vizuri zaidi kwenye baridi



Asili ya miti hii ni nchini Australia lakini nchini Coasta rica na Guantemala (mita 1000 kutoka usawa wa bahari) Afika Mashariki (1200m – 1800m) Sri lanka (600m – 2000m) Israel, Cyprus na Afrika ya Kusini huota yenyewe ikichanganyika na miti ya mikaratusi. Miti hii hustawi zaidi kwenye maeneo yasiyo na joto na inahimili hali ya hewa hata kufikia kuganda ndio maana ukanda wetu hustawi zaidi mikoa ya Mbeya, iringa, Songea, Arusha, Kilimanjaro, Tanga (Lushoto)

Miti hii hukua hadi kufikia mita 30 – 35 ikiwa na kipenyo cha wastani 50cm – 60cm, inakuwa na majani kipindi chote cha Mwaka huwa na magamba ya kahawia huku mbao zake zikiwa na rangi nyekundu kuelekea hudhurungi iliyo kolea, huweza kuhimili kuota kwenye mchanga na udongo wenye asidi 5 – 7ph ingawa hukua vizuri zaidi kwenye udongo wenye rutuba na usiotuamisha maji.



Kiasi cha mvua kinachohitajika ni wastani wa 1200mm – 1800mm kwa mwaka, hutoa maua yenye rangi ya njano na kishubaka cha mbegu huwa na urefu wa senti meta 2 ambazo kwa Tanzania hukomaa kuanzia mwezi 5 mpaka 8, mbegu zake ni nyembamba kama karatasi (kilo moja huwa na mbegu 50,000 mpaka 150,000)

Umri mzuri wa kuvuna tangu kupandwa ni miaka 15 ambapo mbao nzuri hupatikana, lakini mti unaweza kuvunwa kabla ya hapo kama utahitajika kwa matumizi mengine kama kuni au nguzo za kujengea, mti huu unaweza kupandwa kwa ajili ya kivuli, mapambo au hata mipaka ya shamba na kuzuia upepo



Gamba la mbegu zake huwa gumu kiasi, njia nzuri ya kuhakikisha zinaota kwa wingi ni kwa kuzipitisha kwenye moto kidogo (heat seed scarification) mbegu zikiachwa wazi huweza kukaa bila kuharibika kwa miezi 2 – 3 lakini kama zitahifadhiwa kwenye mifuko ya plastic kwenye hali joto ya sentigredi 4 na unyevu kiasi cha asilimia 60 kisha mfuko ukazikwa kwenye mchangamkavu ulio ndani ya chombo maalum, basi mbegu huweza kuhifadhiwa mpaka miaka miwili