KURASA

Tuesday, August 6, 2013

SEREKALI KUNUNUA MAZAO YOTE YA NAFAKA


 Serikali imetangaza kuanzia mwakani itaanza kununua mazao yote ya nafaka, ili wakulima nchini  wawe na soko la uhakika. Hatua hii inalenga kuweka ushindani wa biashara baada ya kuhodhiwa wa wanunuzi binafsi.

Mazao yatakayonunuliwa kupitia Bodi Mpya ya Mazao ya Nafaka ni mpunga, maharagwe, karanga, choroko, ulezi, ufuta na mahindi na kwamba yatanunuliwa kwa bei ya ushindani wa soko mwaka huu.
Mchumi wa bodi hiyo, Edwin Mkwenda, alisema hayo kwenye maonyesho ya wakulima yanayofanyika kitaifa  Viwanja vya Nzuguni, Dodoma.
Mkwenda alisema tayari Serikali imeikabidhi bodi hiyo maghala yote yaliyokuwa ya Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC), ambayo hayakubinafsishwa kwenye kanda saba za nchi ili kutunza mazao yatakayonunuliwa.
Naye Ofisa Ubora wa Mazao wa Bodi hiyo,  Dendego Abdallah, alisema kuundwa kwa bodi hiyo ni ukombozi kwa wakulima kwani watakuwa na uhakika wa kupata soko la mazao husika.
Abdallah alisema wafanyakazi wa bodi chini ya Mkurugenzi Mkuu, Eliampaa Kilanga, imejipanga kuanza biashara rasmi mwakani na kwamba, wakulima wajiandae kuzalisha mazao hayo kwa wingi kutokana na kuwapo uhakika wa soko.
Wakati huohuo, Shirika la kuendeleza Bonde la Mto Rufiji (Rubada), limetenga Sh300 milioni kujenga kituo cha pili cha kufundisha vijana kilimo cha biashara kwa vitendo eneo la Ngalimila, wilayani Kilombero.
Ofisa Kilimo wa Rubada, Joseph Lyafwila, alisema hayo kwenye maonyesho hayo kuelezea mkakati wa Serikali kubadili kilimo kwa vijana, ili walime kibiashara zaidi  kupitia mafunzo ya vitendo.

CHANZO http://www.mwananchi.co.tz/kitaifa/Serikali-kununua--nafaka-zote-nchini/-/1597568/1937656/-/13mbvgmz/-/index.html