KURASA

Monday, December 19, 2011

MGOGORO WA KILIMO CHA MAHINDI MKOANI SINGIDA




Umeibuka mgogoro mkoani Singida mara baada ya mkuu wa mkoa Dr.Parseko Kone kupiga marufuku kilimo cha mahindi mkoani humo. Mmoja wa waliopinga mpango huo ni Mheshimiwa Salome Mwambu mbunge wa Iramba mashariki kwa tiketi ya CCM.

Akitetea kilimo cha mahindi MH Mwambu alisema kwamba hilo silo tamko la mkoa kwa sababu hakuna hata kiongozi mmoja wa mkoa au wilaya ambaye alijaribu kuwashirikisha wananchi kwenye mchakato huo

Pia alisema kwamba kilimo cha mahindi kilikuwepo kwa miaka mingi mkoani humo na zao hilo likiwa ni la biashara na chakula kwa wananchi wenyewe



MAONI YANGU

Viongozi wote wawili walikuwa na nia njema sana kwa wananchi wa Singida, mkuu wa mkoa alikuwa anajitahidi kukabiliana na njaa mkoani mwake na ndio maana akawa anasisitiza kilimo cha mazao ya kinga ya njaa,ambayo ni yale yanayohimili ukame na uhaba wa mvua kama mtama, ufuta na uwele n.k

Mh mbunge naye alikuwa akiwatetea wananchi wake kwa sababu ndio wapigakura wake na yeye ndiye mwakilishi wao, akiangalia anaona kwamba miaka mingi watu wamekuwa wakitegemea mahindi kama zao la chakula na biashara, ndio maana akashauri kwamba watu wasikatazwe kulima mahindi bali walazimishe kupanda na mazao ya kinga ya njaa

Kwa ujumla wote wamefanya maamuzi bila ya kuwashirikisha wataalamu wa kilimo na hali ya hewa, kila mtu alikuwa anatetea kibarua chake. kama wange washirikisha wataalamu basi nina imani kwamba mabo yangekuwa mazuri.

Mkoa wa Singida ni moja ya mikoa inayopata mvua moja kubwa kwa mwaka, na hali yake ni ya ukame kiasi ingawa mvua zinaweza kuwa kubwa zikiambatana na upepo ambao pia huleta madhara kama ya kuharibu mazao na makazi ya watu, mabadiliko tabia nchi yamesababisha kuwe na mvua zisizotabirika na tume shuhudia mara kadhaa zikiwa chini ya kiwango. mkoa huu pia umeathirika na ukataji miti kwa ajili ya kuni, mkaa na matumizi mengine, na pia ufugaji uliokithiri umesababisha uharibifu wa udongo na kusababisha mmong'onyoko wa udongo kwenye baadhi ya sehemu. kwa sababu hizi na nyinginezo zote kwa pamoja zimesababisha madhara kwenye mfumo wa kilimo uliozoeleka na wenyeji wa mkoa huu.



USHAURI
1 - Wakulima walime mahindi kwenye sehemu zilizo tambarare na kwenye mabonde ambako unyevu unachelewa kukauka na wasilime mahindi kwenye uwanda wa juu na milimani kwani sehemu hizo ndizo zinafaa kwa mazao ya kinga ya njaa

2 - Matumizi ya kanuni za kilimo kilimo bora yazingatiwe kama kutumia mbegu bora za mahindi zinazokomaa muda mfupi za zinazoendana na hali ya hewa ya Singida, matumizi ya mbolea za samadi, viuatilifu salama n.k

3 - Upandaji wa mbegu kwa wakati, na kwa kufuata majira ya hali ya hewa, hii ni baada ya kufuata ushauri wa watabiri wa hali ya hewa, hili la hali ya hewa lifanywe na Mbunge akishirikiana na Mkuu wa Mkoa, yaani wafuatilie na wawaeleze wakulima muda sahii wa kuandaa mashamba na kuanza kupanda (wasilete siasa hapa)

4 - Viongozi wa siasa wakae na wakulima/maafisa kilimo na kushauriana nao kuhusu kilimo kwa ujumla, ikiwezekana wasaidie kuanzia upatikanaji wa mbegu bora watakazozichagua kwa pamoja, madawa ya kuua wadudu na taarifa za wadudu au magonjwa ya mazao ili kuzuia kusambaa (wanasiasa wasikae maofisini sana ila watembee kwenye himaya zao kujua matatizo)

Saturday, December 17, 2011

SAMAKI WA MAPAMBO TOKA TANZANIA - (Ornamental Fish From Tanzania)

Tanzania imejaliwa kuwa na aina mbalimbali za samaki wa mapambo wanaopatikana katika maji baridi na maji chumvi. Samaki hawa hupatikana kwa wingi katika maji ya asili na baadhi yao hupatikana humu nchini tu. Kuna samaki wa mapambo ambao wapo katika hatari ya kutoweka. Kwa kiasi kikubwa samaki wa mapambo, wamekuwa wakivuliwa na kupelekwa nje ya nchi na wafanyabiashara.

HALI YA BIASHARA YA SAMAKI WA MAPAMBO
Samaki wengi wa mapambo kwenye maji baridi ni jamii ya Cichlids. Ziwa
Tanganyika lina spishi zaidi ya 200 lakini wanaosafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya mapambo ni wastani wa spishi 30 Ziwa Nyasa lina spishi zaidi ya 750 lakini wanaosafirishwa nje ya nchi kama samaki wa mapambo ni takriban spishi 5 ambazo ni Aulo mamelela, A. blue neon, A. hongi, Proto steven na Tropheus ndole. Ziwa Victoria lilikuwa na spishi zaidi ya 300 katika miaka ya 1970 kabla samaki aina ya Sangara aliyepandikizwa hajasambaa na kula jamii ya Cichlid. Hivi sasa baadhi ya spishi zimetoweka na biashara ya samaki wa mapambo haipo Ziwa Victoria.

CICHLIDS TOKA ZIWA TANGANYIKA


Kwa upande wa samaki wa maji chumvi wanaoishi kwenye matumbawe (coral fish species), spishi zilizopo Tanzania ni nyingi lakini idadi kamili haijulikani. Hata hivyo, kati ya spishi takriban 4,000 zilizopo duniani ni spishi 200 – 300 ndio wanaotumika kwa mapambo.
Samaki aina ya “Cichilid” hutumika sana kwa mapambo duniani kote kwa kuwa wana uwezo wa kuzoea mazingira mapya kwa haraka kuliko samaki wengine (Koning, 1995). Hii inatokana na tabia yao ya kuwa na uwezo mkubwa wa kuvumilia hali tofauti ya mazingira ya maji ikiwemo pH na uchumvi chumvi (salinity). Pia, wana tabia ya kula aina mbalimbali za vyakula kutokana na mpangilio wa midomo, meno na taya (Pharyngeal jaws). Kuna wanaokula mwani (algae), mimea (plants), samaki, konokono n.k. Pia, aina hizi za samaki wanaweza kuishi na kusafirishwa kwa muda wa siku tano (5) bila kula alimradi mazingira ya maji yanaruhusu na vifo vinaweza kuwa chini ya asilimia 2 tu wakati wa kuwasafirisha.




Takwimu za biashara ya samaki wa mapambo duniani sio sahihi sehemu nyingi. Hata hivyo takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa Uingereza mwaka 1987 waliuza samaki wa kiasi cha Paundi za Uingereza milioni 17 na Marekani waliuza samaki wa thamani ya Dola za Kimarekani milioni 739 mwaka 1988. Hata hivyo taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa tabia ya kupenda (hobby) kufuga samaki wa mapambo inaongezeka kwenye nchi mbalimbali zikijumuisha, Japan, China, Australia, Afrika ya Kusini, Korea, Ujerumani na Malaysia. Mara nyingi ufugaji hufanyika kwenye mabwawa na matanki (aquarium).

Kwa upande wa Tanzania, takwimu za biashara ya samaki wa mapambo kutoka kwenye maji baridi kuanzia mwaka 2006 mpaka mwaka 2009 ni kama ifuatavyo: Kwa ujumla biashara ya samaki hawa huingizia Serikali pesa kidogo sana. Samaki wengi waliosafirishwa nje ya nchi katika mwaka 2006 walitoka Ziwa Nyasa. Jumla ya samaki 12,661 ambao walikuwa na thamani ya shilingi 100 87,143,451.25 waliingizia Serikali ushuru wa shilingi 6,541,825.56 tu. Jumla ya samaki 9,080 kutoka Ziwa Tanganyika waliokuwa na thamani ya shilingi 58,770,742.7 waliingizia Serikali kiasi cha shilingi 4,292,456.39. Mwaka
2009 samaki wengi walitoka Ziwa Tanganyika jumla ya samaki 23,500 wenye thamani ya shilingi 131, 356,148.5 waliingizia Serikali jumla ya shilingi 13,018,338.19 kama ushuru. Samaki kutoka Ziwa Victoria walisafirishwa wachache tu mwaka 2007, walikuwa 12 tu. Samaki wa mapambo kutoka Ziwa Victoria wako hatarini kutoweka kutokana na kuliwa na Sangara kwa hiyo wameingizwa kwenye “Red list” chini ya CITES,
hawasafirishwi tena. Kinachohimizwa ni ufugaji wa hao samaki.




FURSA YA UWEKEZAJI KATIKA SAMAKI WA MAPAMBO

i) Kuna fursa kubwa ya uwekezaji katika samaki wa mapambo wa Ziwa Tanganyika kwa kuwa samaki hao wapo wengi (Watson, 2000) na baharini kwenye matumbawe (Coral reef fish species)

ii) Kuwepo kwa masoko ya uhakika na mazingira mazuri ya kuvutia biashara Ili uendeleza na kuimarisha uwekezaji katika eneo hili ni muhimu kuhamasisha wananchi na wawekezaji kutoka nje katika kuwekeza kwenye biashara ya samaki wa mapambo. Pia, ni lazima kufanya utafiti wa kufahamu spishi zilizopo na wingi wa samaki wa mapambo ili kuepuka kumaliza baadhi ya samaki hao.

UMUHIMU WA BIASHARA YA SAMAKI WA MAPAMBO KATIKA KUONDOA UMASIKINI

Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa mapato ya biashara ya samaki wa mapambo kwenye nchi mbalimbali duniani ina thamani ya takriban Dola za Marekani milioni 186 na samaki wengi wanatoka nchi zinazoendelea (Watson, 2000). Kati ya hizi fedha Zinazobaki kwa jamii wanaokusanya samaki hao ni kidogo sana. Hata hivyo, kama jamii itawezeshwa kupata mtaji na teknolojia sahihi itaweza kujiongezea kipato na kupunguza umaskini. Asilimia 90 ya samaki wa mapambo duniani huzalishwa kwenye mabwawa hasa kwenye nchi zilizoendelea na samaki hao wametolewa kutoka kwenye nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania. Ili mwananchi aweze kunufaika na biashara ya samaki wa mapambo kuna umuhimu wa kuwaelimishwa kuhusu njia bora za kuwavua, kuwahifadhi na kuwasafirisha kwa ajili ya kuongeza kipato chao na taifa kwa ujumla.

SAMAKI WA UREMBO TOKA ZIWA NYASA

ATHARI ZITOKANAZO NA BIASHARA YA SAMAKI WA MAPAMBO

Shirika la Kimataifa la Hifadhi ya Viumbe na Mazingira kupitia kitabu cha “Red List’’ (IUCN, 1988) kimeainisha aina za samaki wa mapambo ambao wapo hatarini Kutoweka. Samaki hao ni pamoja na aina ya furu (Haplochromine). Athari za biashara hiyo ni kama ifuatavyo:

i) Kupungua wingi na makazi ya samaki waliopo kwenye maeneo ya asili ikiwa ni pamoja na maziwa, mito na bahari kwa njia mbalimbali. Hali ya aina hii imekwishatokea kwenye nchi ambazo biashara ya samaki wa mapambo ni kubwa kama vile Sri Lanka na Malaysia (Banister, 1989). Kwa upande wa Tanzania tathmini ya athari za biashara ya mapambo bado haijafanyika.

ii) Kuharibika kwa mfumo mzima wa ikolojia na kuharibu makazi ya samaki asilia (indigenous species). Hali hii hutokana na samaki wa mapambo kupelekwa kwenye maeneo ambayo sio ya asili yao kama vile mabwawa. Wakati mwingine samaki hawa huingia kwenye mito iliyo karibu na mabwawa wanayofugiwa na kwenda kwenye maziwa ambako
huchanganyika na samaki ambao ni wa asili kwenye maeneo hayo. Pia, biashara hii inaweza kuhatarisha ikolojia ya maji ya nchi waliyopelekwa.

CHANGAMOTO
i) Kuimarisha na kuendeleza miundombinu kwenye maeneo yenye vivutio kwa ajili ya utalii ikolojia ikiwa ni pamoja na barabara, umeme na maji safi;

ii) Upatikanaji wa mitaji na uwekezaji katika utalii ikolojia na biashara ya samaki wa mapambo;

iii) Kuweka bayana umiliki wa fukwe za bahari ambazo ziko nje ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu ili kuharakisha uwekezaji wa maeneo haya kwa nia ya kukuza utalii ikolojia;

iv) Kufanya utafiti wa kufahamu ikolojia, aina, wingi wa samaki wa mapambo n.k.;

v) Kuboresha mazingira ya utalii ikolojia na biashara ya samaki wa mapambo.

MAPENDEKEZO YANGU
i) Kufanya utafiti wa kufahamu wingi wa spishi mbalimbali za samaki wa mapambo ili uvunaji uwe endelevu;

ii) Kuhamasisha wananchi na wadau wengine kuwekeza katika biashara ya samaki wa mapambo na utalii ikolojia;

iii) Kuhamasisha wananchi kutembelea Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu ili kukuza utalii wa ndani; na

iv) Kufanya jitihada za kuhifadhi spishi za viumbe wa kwenye maji zilizo hatarini kutoweka.