KURASA

Wednesday, June 27, 2012

KILIMO BORA CHA MIPAPAI


MAHITAJI
Hali ya  hewa inayofaa kwa mipapai ni ya kitropik ambayo haina baridi kali na joto kiasi . Udongo usiotuamisha maji maji yakisimama kwa masaa 48 tu mpapai unaweza kufa, wenye ruruba ya kutosha kwa sababu mipapai haina mzizi mkuu haihiyaji udongo wenye kina kirefu, kipindi cha jua kali mpapai usiachwe zaidi ya wiki 8 bila kumwagiliwa maji kama hakuna mvua ingawa wakati wa mapapai kuiva kama kuna ukame basi hii huongeza ubora wa papai ikiwamo kutooza mapema sokoni

Mipapai ipandwe sehemu ambazo hazina upepo mwingi kwani huvunjika kirahisi, kama unashamba la mipapai itakubidi kupanda miti ya kukinga upepo kuzunguka shamba lako, miti kama miparachichi, migravilea, vibiriti (leucaena Spp) na miembe pia inafaa. Hakikisha miti ya kukinga upepo inakuwa mirefu kuzidi mipapai kwa mita 10 mpaka 20 juu zaidi

Kuendelea kupanda mipapai kwenye shamba moja kunaweza kusababisha usugu wa magonjwa, nashauri baada ya miaka 3 – 5 ubadilishe zao hili angalau kwa msimu mmoja ili kuua mzunguko wa magonjwa
Mipapai inaweza kuchanganganywa na miembe na mimea jamii ya michungwa, pia mazao ya msimu kama mahindi, mtama, ufuta , alizeti  na  mboga mboga yanaweza kulimwa

Kwa kaida kwenye mipapai kuna mipapai dume, majike  na yenye jinsia zote (multiplesex/hermaphrodite) ambayo huwa na mapapai marefu zaidi, na pia kuna isiyoeleweka ambayo huwa na mapapai mafupi sana

MBEGU
Kusanya mbegu toka kwenye mapai makubwa na yaliyo komaa na kuiva, kausha mbegu vizuri kbla ya kupanda, kama utapata mbegu za  kununua ni vizuri zaidi, baada ya kukausha hakikisha unazipanda ndani ya wiki moja

KUOTESHA MBEGU
Kuna wanaopendelea kuotesha mbegu kwanza na kisha kuhamishia miche shambani, sehemu ya kuoteshea iandaliwe miezi miwili kabla, mbegu zioteshwe kwenye kina kati ya sentimeta 1 – 2 chini ya udongo wenye rutuba au pakiti za plastiki, kiwango bora cha joto ni sentigredi 21 – 27 na itachukua kati ya wiki 1 – 4 kwa mbegu kuota, kwenye kila pakiti weka mbegu 2 – 3. Panda mbegu zako kwenye kitalu kwa umbali wa sentimeta 3 toka shimo hadi shimo na sentimeta 15 kati ya mistari, hakikisha maji hayatuami kabisa, pia unaweza kupiga dawa ya copper oxychloride gramu moja katika lita moja ya maji ilikukinga miche yako na fangasi

UOTESHAJI WA MOJA KWA MOJA
Kabla ya kupanda mbegu weka mchanganyiko wa majivu na mbolea ya kuku sehemu ya kupandia, mbolea husaidia ukuaji haraka na jivu husaidia kukinga mipapai na magonjwa. Panda mbegu 3 – 5 kila shimo maana miche mingine inaweza kufa kwa magonjwa, kuliwa na wadudu au ikaota dume

KUHAMISHA MICHE TOKA KWENYE KITALU
Miche ihamishiwe shambani ikiwa na urefu wa sentimeta 20 – 40, kama udongo unatuamisha maji panda kwenye matuta yenye urefu wa sentimeta 40 – 60 mashimo yawe na ukubwa wa sentimeta 45 upana na sentimeta 30 kina na shimo lichanganywe na udongo na samadi bila kuacha kisahani cha maji, umbali ni mita 3 kwa 3 kwani mipapai inahitaji jua la kutosha

KUPUNGUZA MIPAPAI
Baada ya miezi 3 – 5 baada ya kupanda mipapai itatoa maua na hapo jinsia ya mipapai itajulikana na mingine itabidi ipunguzwe na hasa midume, mipapai yenye jinsi zote inatakiwa isizidi asilimia 10 – 20 na midume ibaki mmoja katika kila mijike 25, mimea yenye magonjwa pia inabidi ing’olewe

RUTUBA YA UDONGO
Weka kiasi chakilo 2 – 5 za samadi kwenye kila mpapai kwa mwaka ili kuongeza ukuaji na uzazi, mabaki ya mimea yanaweza pia kuwekwa kama matandazo na h ii ni muhimu zaidi kipindi cha kiangazi ili kuzuia unyevu usipotee.

MAGUGU
Mipapai inapopandwa tu inaweza kuwekewa matandazo kuizunguka ili kuzuia uoataji wa magugu, magugu yang’olewe yakiwa machanga na epuka kuchimbua chini sana maana mizizi ya mipapai huwa juu juu, njia nzuri ni kuweka matandazo kwenye shamba lote ili kuzuia outaji wa magugu

UANGALIZI
  • Mipapai iangaliwe dhidi ya magonjwa, ing’olewe na kuchomwa au kufukiwa chini ikiwa itabainika kuwa na maonjwa, piga dawa dhidi ya magonjwa ya fangasi na virusi mara yanapoibuka ili kuongeza uzaaji nakipato chako
  • Ondoa matawi yote yatakayojitokeza pembeni ya mpapai wako, na hii ifanyike mapema kabla ya tawi kuwa kubwa.
  • Ondoa mapapi yote ambayo yatakuwa hayakuchavuliwa vizuri na acha yale yenye afya tu
  • Weka miti ya kuegemea kama mpapai utazaa matunda mengi na hasa wakati wa upepo mwingi ili kuzuia mipapai isivunjike
  • Mipapai ikitunzwa inaweza kuishi mika mingi, ila kwa ajili ya mazao bora ondoa mipapai na upande mingine baada ya kila miaka mitatu (3) kwani mpapai unapo kuwa mkubwa basi rutuba yote huishia kwenye mti wenyewe

Tuesday, June 19, 2012

UTITIRI - WADUDU WASUMBUFU WA MIKOROSHO


Utitiri wa mikorosho  au kwa jina lingine thrips (Thrips rubrocinctus), ni wadudu wadogo sana wenye mwili laini na rangi  kati  ya njano, kahawia au nyeusi. Utitiri  wakubwa  (adults) hutambulika kwa kuwa na mabawa na mwili wa kahawia (dark brown) au  mweusi,  pamoja  na upito  (band) wa rangi nyekundu kifuani. Wanaonekana vizuri kwa kutumia kikuzia umbo (lens).
Katika kipindi kirefu, utitiri ulikuwa ukionekana katika  maeneo mengi yanayolimwa korosho, lakini athari zake zilikuwa ndogo. Katika miaka ya hivi karibuni wameonekana kwa uwingi na kuleta hasara kubwa hasa katika  tarafa  za Lisekese na Chikundi wilayani Masasi.  Pia mashambulizi  ya wadudu hawa yameonekana katika wilaya za Nachingwea na Newala  kwa kiwango kidogo. Inakisiwa kuwa uongezekaji wa  wadudu  hawa husababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

MZUNGUKO WA MAISHA
Utitiri wakubwa hutaga mayai katika sehemu yachini  ya majani. Mayai yanaanguliwa baada ya siku 3 hadi 4 na  kutoa  vijititiri  vidogo  sana (larva I) ambavyo huwa ni  vyepesi  sana. Huingia  hatua  ya pili (larva stage II) baada ya siku 7 hadi 8.  Hatua hizi ndizo  ziletazo uharibifu mkubwa maana ndizo hatua za ulaji na ulafi  wa  hali ya juu. Baada ya wiki moja tena, ndipo hutokeza hatua ya kwanza ya “ninfu” (Nymph stage I) na hatua yake ya pili baada ya siku 3 hadi 4. Katika hatua hizi mbili (nymph stages), vijidudu hivi havitembei  wala  kula chakula bali hukaa mahali pamoja, hasa kwenye ardhi. Hatua hii ya “ninfu” hudumu kwa siku 11 hadi 12 kabla ya kupevuka na kuwa utitiri wakubwa (adults). Hivyo Mzunguko wa maisha yao toka yai hadi kupevuka ni mwezi mmoja. Utitiri hushamiri sana wakati wa  kiangazi mara tu  baada  ya mvua,  hasa kati ya mwezi June na Oktoba. Utitiri hupungua kabisa wakati wa mvua, hata hivyo huvuka msimu hadi mwingine kama utitiri wakubwa.

MASHAMBULIZI
Utitili wachanga pamoja na  wakubwa, hushambulia upande wa chini wa majani hasa yaliyokomaa, machipukizi na mashada ya maua. Utitili wachanga hubeba tone la majimaji mkiani na kudondoshea juu ya majani,  ambapo likikauka huacha doa la kahawia  au  nyeusi, lakini hasa rangi ya kutu. Maeneo yaliyoshambuliwa na  utitili  hubadilika rangi na kuwa na weupe weupe wenye mng’aro wa rangi ya fedha (silvery).  Baadaye hubadilika na kuwa na rangi ya udongo (kahawia), hatimaye hukauka na majani hupukutika Eneo  linaloshambuliwa hudumaa na uzalishaji  kuathirika. Maeneo mengi ambayo hushambuliwa na utitili huwa  korosho  hazizai kabisa. Miti iliyopukutisha majani kwa sababu yamashambulizi  ya utitiri, huweza kuchipuza tena kwenye mwezi Novemba na Desemba.

MAZAO MENGINE YANAYOSHAMBULIWA NA UTITIRI
Wadudu hawa hushambulia majani na hata maua ya aina  mbalimbali ya mazao na mimea, kama vile  mazao ya bustani (vitunguu nk), michungwa, pamba, aina ya nafaka. Kwa sababu ya wingi wa aina ya mimea inayoshambuliwa na utitiri,  udhibiti  wa wadudu hao unaweza kuwa mgumu kwa kiasi fulani.

KUSHAMIRI KWA UTITIRI
Wadudu hawa hupendelea mikorosho iliyosongamana,  isiyopitisha hewa vizuri, mikorosho  isiyopogolewa na mashamba yasiyohudumiwa kwa ujumla.  Hupendelea hasa miti mikubwa. Utitiri hupendelea hali ya ukame au kiangazi cha muda mrefu.

KUSAMBAA
Utitiri husambazwa hasa kwa njia ya upepo  au kwa kupanda vipando  (propagation  materials) ambavyo vimeshambuliwa.

KUDHIBITI KWENYE MIKOROSHO

Njia  pekee  inayotumika kudhibiti utitiri ni matumizi ya madawa. Dawa ya BASUDIN au KARATE ndiyo iliyopendekezwa  na watafiti kudhibiti utitiri wa korosho. Mchanganyiko wa mililita  5  za KARATE na lita moja ya maji  unatosha kudhibiti  wadudu hawa katika mti mkubwa usiozidi kipenyo (diameter) cha mita 10. Ni jambo la muhimu kukagua mashambulizi kuanzia mwezi Mei. Upuliziaji unaanza mara tu baada ya kuona dalili za  mashambulizi  au kuwaona wadudu wenyewe na kurudia baada yawiki tatu (siku 21).  Upuliziaji  unafanyika kutumia mashine ya moto (Mist blower) au yakawaida (Knapsack sprayer)  kutegemeana  na ukubwa wa mti. Ni muhimu kuanza kupuliza dawa mapema, ili kuweza kuwathibiti wadudu hawa wakiwa katika hatua zao za mwanzo kabisa za ukuaji wao ( hatua za lava na ninfu). Hii ni  muhimu kwa sababu ni vigumu kuudhibiti utitiri  wakubwa. Awamu 2 hadi 3 zinatosha kuthibiti wadudu hawa katika msimu mmoja. Ikibidi,  matunda (mabibo) yaliyopuliziwa dawa yasitumike mpaka baada ya siku 21

UBWIRI UNGA - UGONJWA MKUU WA MIKOROSHO


Moja ya matatizo makubwa ya uzalishaji wa  zao  la korosho ni ugonjwa wa Ubwiri unga.Ugonjwa huu unasababishwa  na vimelea aina ya uyoga (fungus) viitwavyo Oidium anacardii. Ugonjwa huu ni muhimu sana, kiasi kwamba kama haukuthibitiwa,  unaweza kupunguza mavuno kwa zaidi ya asilimia 70.       Ugonjwa huu umeenea katika  mikoa  yote inayolima zao hili Tanzania.  Hapo awali ugonjwa huu ulikuwa unaitwa kwa jina la“ukungu” kutokana na uhusiano wake mkubwa na haliya hewa ya ukungu  (litabwe  kwa  Kimakonde) unaoonekana  alfajiri/asubuhi katika miezi ya Juni - Septemba.  Hivyo  basi,  jina la Ubwiri unga linatumika sasa ili kuwawezesha wakulima wasichanganye vitu hivyo viwili.

MASHAMBULIZI
Ugonjwa huu unashambulia maeneo yote machanga na teketeke  katika  mti wa mkorosho, hasa machipukizi, majani, maua, mabibo na korosho changa (tegu). Athari kubwa  ya ugonjwa  huu inatokana na mashambulizi ya maua, ambayo hushindwa kufunguka  na  kuwezesha chavua kufanya kazi yake,  hatimaye  hunyauka  na kukauka.

DALILI
Maeneo yaliyoshambuliwa na ugonjwa huu, hufunikwa na unga unga mweupe au wakijivujivu  ambao huonekana kama vumbi vumbi. Vimelea au chembe chembe zinazoshambulia ni ndogo ndogo sana na hazionekani dhahiri kwa macho, ila kwa darubini. Chembe chembe hizi zinapozaliana kwa wingi katika maeneo ya mshambulizi, ndipo huonekana kama unga unga mweupe/kijivu. 

KWENYE MAJANI
Pamoja na kufunikwa na unga unga,  majani yaliyoshambuliwa husinyaa, hubadilika rangi, wakati mwingine hukunjamana. Majani machanga zaidi yanaweza kupukutika, ambapo yale yaliyokomaa hayashambuliwi. Masalia ya mashambulizi  kwenye majani yaliyokomaa, huonekana kama mabaka ya kahawia, hata hivyo hayapukutiki.

KWENYE MAUA
Maua yanaweza kushambuliwa hata kabla ya kuchanua. Pamoja  na  kufunikwa na unga unga weupe/kijivu, maua yaliyoshambuliwa sana hushindwa  kuchanua  na hatimaye hukauka kabisa na kuwa kama “majani yachai”. Hili ndilo sababisho kubwa la upungufu wa zao la korosho.

KWENYE MABIBO

Mabibo yaliyoshambuliwa huonyesha  unyafuzi,hupasuka pasuka na ngozi yake huonekana kuwa chafu. Hatimaye,  mabibo  hayo huwa madogo kwa umbo, yenye  maji kidogo  sana, hivyo kuyafanya maji yake kuwa matamu sana.
KWENYE TEGU NA KOROSHO
Tegu  zilizoshambuliwa  huweza kubadilika rangi yake ya kijani/nyekundu na kuwa ya hudhurungi au bluu iliyo mzito. Tegu zikishambuliwa zingali changa sana, huweza kupukutika. Tegu zilizoshambuliwa zikifikia kukomaa, zinaonyesha uharibifu mkubwa wa ngozi yake na huonekana chafu, hatimaye, wakati wa mauzo hutengwa katika  daraja  lachini (grade II).

KUSTAWI KWA UBWIRI UNGA
Vimelea vya Ubwiri unga vinaishi kwenye mimea iliyo hai tu, haijawahi kuoteshwa katika  maabara.  Ugonjwa huu hushamiri na kustawi vizuri katika  majira  yenye ukungu, hasa  kuanzia mwezi Mei/Juni hadi Septemba karibu kila mwaka. Mazingira mwafaka kwa ugonjwa huu ni:
• Joto: 26 - 28 0C (bora 25 C)
• Unyevu (RH): 80-100% (bora 95%)

Ubwiri unga pia hupendelea  zaidi mikorosho iliyosongamana na isiyopitisha hewa vizuri. Ugonjwa huu hupendelea mazingira ya kiangazi, hasa  kuanzia mwezi Juni hadi Septemba, haupendelei hali ya mvua na  joto jingi.  Hivyo basi, katika miezi mingine (hasa wakati wa masika), vimelea hujificha na kuishi Kwenye maotea  au machipukizi uvunguni  mwa mikorosho au kwenye maua yasiyo ya msimu. Hivi ndivyo  vyanzo vya Ubwiri unga, vyenye uwezo wa kuhifadhi ugonjwa msimu hadi mwingine. Ugonjwa huu husambazwa kwa upepo ambao nao  pia hushamiri sana katika miezi ya Mei/Juni hadi Septemba.

KUDHIBITI
Zipo njia aina tatu zinazotumika kuthibiti Ubwiri unga, nazo ni mbinu za asili, mbegu bora na madawa.

MBINU ZA ASILI (Cultural control)

Kuondoa vyanzo vya Ubwiri unga (sanitation).
Hii ni kazi ya mikono ya kuondoa machipukizi na maotea yanayojificha kwenye uvungu  wa  mikorosho, kutumia vifaa kama vile upanga, mundu, shoka nk. Msingi wa kazi hii ni kupunguza kasi ya ugonjwa huu katika shamba kwa kuchelewesha mlipuko na  kasi ya mashambulizi. 

Kubadili mazingira ya ugonjwa katika miti.
Kupunguzia  matawi  (prunning) ya mikorosho ili kufanya  umbile  la  mwamvuli katika miti, ili kuruhusu joto na upepo kupenya kirahisi, inasaidia sana kuthibiti Ubwiri unga.
Kupunguza  miti (thinning) iliyosongamana na kuacha nafasi ya kutosha kati  ya miti, itasaidia kupunguza kuenea kwa ugonjwa.  Miti ikiwa  katikanafasi  ya kutosha, itawezesha hewa  kupenya  vizuri na kubadili mazingira ili yasiwe mazuri kwa kustawi kwa ugonjwa.

Kupanda mikorosho inayovumilia/kuhimili ugonjwa.
Ipo baadhi ya mikorosho  ambayo  inaweza  kuhimili mashambulizi ya ugonjwa hata kuweza  kutoa  Mazao bila ya kutumia kinga yoyote.  Aina zingine zinaweza kutoa maua na kuzaa kabla  ya  athari za ugonjwa hata kuweza kukwepa mashambulizi.  Hii  ni  baadhi  ya mikorosho  bora  ambayo hatimaye imepandwa katika eneo moja katika vituo  vyetu vyote vya kuendeleza korosho (Cashewnut Development Centre )kama NALIENDELE. Mbegu zinazopatikana toka mashamba hayo ni mbegu bora (polyclonal seed) ambazo zinaweza kuzaa bila madawa, lakini huzaa vizuri zaidi kama mtu atatumia dawa pia.


MATUMIZI YA MADAWA

Dawa ya Salfa (Sulphur)
Salfa ndiyo dawa inayotumika kwa wingi zaidi kukinga ugonjwa wa Ubwiri unga. Dawa hii ambayo ni ya unga, inapulizwa kwa kutumia mashine maalumu (motorised blower)  ya kupulizia dawa k.m. Maruyamana Solo. Kiwango cha  gramu  250 kwa mti, kwa mzunguko, ndicho kinapendekezwa.  Hivyo basi kwa mizunguko mitano kiasi cha kilo 1.25  cha  salfa kwa mti kwa mwaka kinahitajika.  Pia kuna salfa za maji kama Thiovit ambazo unaweza kupulizia kwa kutumia vinyunyuzia dawa vya kawaida (knapsack sprayer)

Wakati wa kuanza kupulizia sailfa
Mpulizo wa kwanza unaanza ambapo karibu asilimia 20za maua yamejitokeza na wakati sawa, zaidi ya asilimia 5 ya maua hayo tayari yawe  yanaonyesha dalili  za ugonjwa. Upimaji wa maua ili kujua  lini  upuliziaji  uanze, inasaidia kufanya matumizi sahihi  ya  dawa,  hatimaye faida/pato litakuwa kubwa kwa mkulima.
Inashauriwa kwamba upuliziaji ufanyike asubuhi na mapema, wakati ambapo kuna umande. Asubuhi, upepo nao  huwa  hauna nguvu sana na inashauriwa upuliziajiusizidi ya saa 3 asubuhi. Umande unasaidia salfa ya unga iweze kunata kwenye majani na maua. Ila kwa salfa ya maji kama thiovit unaweza kupulizia wakati wowote.vipindi vifuatavyo, vimependekezwa katika upuliziaji:Siku 14      14      14       21     21 

Dawa zingine badala ya salfa.
Madawa kadha wa kadha yamefanyiwa  utafiti sambamba na salfa. Aina tatu za dawa hizo   (waterbased  organics), zimependekezwa kwa matumizi ya wakulima, nazo ni Bayfidan, Anvil na Topas.  Kiwango cha upuliziaji ni ml 10 - 15 za dawa ndani ya0.75  -  1.25  za  maji kutegemeana na ukubwa wa mti. Vipindi kati ya mipulizo ni wiki tatu (siku  21)  na awamu (raundi) 3 zinatosha kwa msimu. Inashauriwa kwamba kutokana na gharama za dawa yamaji, zinafaa zitumike kwenye mikorosho ambayomkulima ana uhakika wa kutoa zaidi ya kilo 4 baada ya kupulizia.  Miti inayotoa chini ya kiasi hicho heri isipuliziwe, vinginevyo italeta hasara

KIFA UWONGO - MDUDU HATARI KWA MIKOROSHO


Kifa-uwongo (Mecocorynus loripes),. ni mdudu aina ya “weevil” ambaye hushambulia mashina ya mikorosho hata kufikia hatua ya kuuwa mti mzima. Mdudu huyu huitwa “kifa-uwongo” kwa sababu ya mbinu yake makini anayotumia kujihami. Mara tu aonapo mtu anapita karibu yake, huanguka chini na kujifanya kama amekufa kabisa. Kisha baada ya mtu yule kupita, yeye huamka tena na kuendelea na shughuli zake kama kawaida. Wamakonde humwita mdudu huyu “Nang’ang’ana”, ambapo Wayao nao humwita “Ng’ang’ani.

MAISHA YA KIFA UWONGO
“Kifa-uwongo” kama wadudu wengine, hupitia hatua za yai, “lava” na “buu” kabla ya kuwa mdudu kamili. “Kifa uwongo” kamili aliyekomaa, ana rangi ya kahawia na urefu wa kama sentimita 2. Ana mdomo mrefu uliochongoka (snout) ambao daima anauficha kwa kuulaza kifuani pake. “Lava” wake ni aina ya funza (grab) mweupe, mwenye ngozi ya kukunjamana na kichwa cha rangi ya kahawia mzito (dark brown), yeye  daima huonekana amejikunja kama upinde.

“Kifa uwongo” wa kike hutoboa gamba la mkorosho kwa kutumia mdomo wake mkali, na kutaga yai moja moja. Baada ya mayai kuanguliwa, mafunza huanza kushambulia gamba la mti mara moja. Funza hawa wana midomo mikali kama misumeno, nao wanakula kwa bidii sana gamba la mti. Kadri wanavyokula ndivyo wanavyoongezeka ukubwa pia. Funza akaribiapo kuwa Buu (pupa), hupekecha ndani ya mti (kiasi cha sentimita 2.5 chini ya gamba) na kutengeneza matundu kwa ajili ya maficho ya buu (pupal chambers). Mabuu hujifungia ndani ya matundu hayo na hatimaye hugeuka na kuwa “Kifa uwongo” kamili. Mzunguko wa kutokea yai hadi “Kifa-uwongo” kamili, huchukuwa muda wa miezi sita, ambapo muda wa karibu miezi 2 - 2.5 huwa katika hatua ya mafunza, ambayo ndiyo yenye uharibifu mkubwa. “Kifa-uwongo” kamili ana mabawa na anaweza kuruka kwa nadra toka mti hadi mwingine. Mara nyingi wadudu hawa, huonekana wakidumu katika maeneo ya mashambulizi.  Mashambulizi yanaweza kuchukua muda wa mwaka au miwili katika mti mmoja, ambapo mti wa jirani unaweza kuwa huru kabisa bila mashambulizi!.  Mara nyingi “Kifa-uwongo” hupenda kuhamia mkorosho mwingine baada ya kuua kabisa mkorosho waliouanza kushambulia.

DALILI ZA MASHAMBULIZI
Maeneo ya mashambulizi huonekana wazi wazi hata toka mbali, kwa sababu ya uwepo wa Mchanganyiko wa utomvu na takataka kama za maranda ya seremala ambayo hatimaye hugeuka rangi na kuwa nyeusi.   Rangi ya majani ya mkorosho ulioshambuliwa sana, hubadilika na kuwa njano, kisha hunyauka na hatimaye hukauka. “Kifa-uwongo” hupendelea kushambulia miti mikubwa tu. Utafiti umeonyesha pia kwamba hupendelea miti iliyojeruhiwa kutokana na kukatwa kwa ajili ya ubebeshaji  (top-work) au hata ile ya kupunguzwa matawi. Inasadikika kwamba aidha eneo la jeraha ni rahisi kwa kifa uwongo kutaga mayai yake, au huenda kuna mvuto wa aina yake kutokana na harufu ya utomvu utokao eneo lenye jeraha na kufanya mvuto wa pekee kwa kifa uwongo kushambulia!

MKOROSHO ULIOSHAMBULIWA NA KIFA-UWONGO

JINSI YA KUDHIBITI KIFA UWONGO
Hakuna dawa ambayo inashauriwa kutumika katika kuthibiti wadudu hawa, badala  yake, mkulima mwenyewe anashauriwa kupambana nao ana kwa ana: Mwanzoni mwa mashambulizi. Ukaguzi wa mara kwa mara ufanyike kwa kila mkorosho kukagua mashambulizi hayo. Mara tu baada ya kuona  dalili  za mashambulizi ya wadudu hawa, bandua eneo la mashambulizi kwa kutumia kisu  au upanga na kuwaondoa mafunza wote. Funza akidondoka chini hana uwezo tena  wa kupanda kwenye mti au kufanya mashambulizi. Mabuu waliojifungia kwenye matundu  ya maficho  yao, wanaweza kuuawa kwa kutumia  ncha  kali, kama vile spoku yabaiskeli, ili kuwatoboa wakiwa  ndani  yamashimo yao.  Inashauriwa pia kuwasaka na kuwaua  kila “Kifa  uwongo” kamili (adults) kwa kuwakata vichwa vyao.

MASHAMBULIZI YALIYOKITHIRI
Inashauriwa  kukata na kuchoma moto mikorosho yote iliyoshambuliwa kwa kiwango  cha  hali ya juu, ili kuuwa mabaki ya mayai na funza waliopo

MILIBAGI - MDUDU MHARIBIFU WA MIKOROSHO


UTANGULIZI
Milibagi (Pseudococcus longispinus) ni wadudu waharibifu katika zao la korosho, waliojitokeza kuwa maarufu sana katika miaka ya tisini. Hawa ni wadudu wanaoonekana katika maeneo mengi ulimwenguni, lakini hushamiri na kuleta athari kubwa katika mazingira ya Tropikali. Mnamo mwaka 1990, milibagi walionekana kushambulia mikorosho katika maeneo ya mjini Masasi. Mwaka 1993, walionekana kuenea hadi wilaya za Nachingwea na Tunduru. Hivi leo, wadudu hawa wameenea karibu sehemu nyingi za kanda ya kusini, ingawa mashambulizi makubwa yapo wilayani Masasi, Tunduru, Nachingwea na Liwale.   Milibagi ni moja ya wadudu waharibifu wanaoishi na kuponea mimea. Wadudu hawa hutengeneza utando mweupe (scale) juu ya miili yao kwa ajili ya kinga na kujihami dhidi ya adui zao.

Milibagi huonekana katika mazao ya aina nyingi ikiwa ni pamoja na miembemafuta, mihogo, michungwa, minanasi nk. Pamoja na hivyo, kuna tofauti kati ya milibagi wanaoshambulia hayo mazao mbalimbali. Kwa mfano, milibagi wa mihogo (Phenacoccus manihoti), miembe (Rastrococcus invadens) ni tofauti na wale wa mikoroshoni (P. longispinus). Dalili za Mashambulizi ya Milibagi. Maeneo yaliyoshambuliwa na milibagi huonekana yamefunikwa na weupe weupe ambao ni utando unaofunika miili ya wadudu hao. Mikorosho iliyoshambuliwa sana na milibagi, huonekana kwa mbali kama vile imefukikwa na theluji. Mashambulizi ya Milibagi Milibagi wanaweza kushambulia eneo lolote la mmea kwa njia ya kufyonza. Kwa jinsi hiyo, milibagi huingiza matemate yao  katika maeneo ya mashambulizi na hatimaye huweza kueneza vimelea vya virusi. Milibagi hutoa utomvu mweupe mweupe kama asali na kufunika maeneo ya mashambulizi, hata kufanya mmea usiweze kupata mwanga wa jua vizuri hata kuzuia utengenezaji wa chakula cha mimea (photosynthesis).  Majani yaliyoshambuliwa sana na milibagi, hupukutika hivyo kuathiri uzalishaji. Maua yaliyoshambuliwa mapema na milibagi yanashindwa kuzaa. Korosho zilizoshambuliwa zingali zinakomaa, zinachafuliwa kwa utando na utomvu. 

Korosho hizo yamkini zisafishwe kwa mchanga kabla ya kufikiria kuuzwa, vinginevyo hutengwa katika daraja la pili. Mashambulizi ya milibagi, yanaweza kupunguza uzalishaji kwa kiwango cha asilimia 50% Kustawi kwa Milibagi. Milibagi huonekana kwa wingi wakati wa kiangazi, hasa mwezi Septemba hadi Novemba. Milibagi hupungua sana wakati wa mvua. Inaelekea kwamba mabadiliko ya hali ya hewa ni chanzo kikubwa cha mashambulizi ya milibagi kwenye mimea. Maisha ya Milibagi. Milibagi wa kike hutaga kiasi cha mayai 50-500 kutegemeana na mazingira. Mayai huanguliwa na kutokea Vitambaazi (crawler). Hatua hii ni muhimu kwa usambaaji wa milibagi. Hawa hutambaa mpaka kwenye ncha au vilele vya miti na kujitegeshea miguu yao ili wasambazwe kwa upepo, ndege au wadudu wengine. Binadamu pia wanahusika sana kusambaza wadudu hawa katika hatua hii. Hatua za lava zinazofuata ndizo za ulaji na uharibifu. Milibagi waliokomaa (adults) huwa hawajishughulishi (inactive), huwa hawali chakula na huishi muda mfupi (wiki au mwezi)

KUDHIBITI
Zipo  njia mbili ambazo zinaweza kutumika kudhibiti milibagi:
‰ 
NJIA YA KIBAIOLOJIA
Utafiti umeonesha kwamba  wapo wadudu  wengine ambao wanaweza kushambulia milibagi, kama vile:
 a) Ladibedi bito (Chilocorus spp)
b) Manyigu (Chrysopa spp)

Utafiti umeonesha kwamba idadi ya wadudu hawa mashambani ni ndogo kwa kuweza kudhibiti idadi kubwa ya milibagi. Utafiti wa kina zaidi unafanyika kuona jinsi ya kuwafanya wadudu  hawa waongezeke idadi ili kuweza kuwadhibiti milibagi mikoroshoni.

◊ NJIA YA KUTUMIA MADAWA
Njia pekee inayotumika hivi sasa kuwadhibiti milibagi ni kutumia madawa. Dawa aina ya Selecron 720 EC  ndiyoiliyothibitishwa na utafiti itumike dhidi ya milibagi.

Dawa ya Selecron 720 EC Dawa hii ni ya aina ya maji, inayosambazwa  na kampuni ya Norvatis (Ciba Geigy). Inapulizwa kwa  kutumia mashine za moto  (motorized  blowers) kama vile Maruyama 150DX au Solo
◊ Kiwango cha upuliziaji  ni  mililita  7.1 ya dawa, ndani ya lita 1 ya maji kwa mti mkubwa.
◊ Upuliziaji unaanza mara tu  baada  yakuona  dalili  za mashambulizi yamilibagi. 
◊ Marejeo  ya upuliziaji yafanyike kila baada ya siku 7 – 14 kutegemeana na hali ya mashambulizi yalivyo.