KURASA

Friday, April 12, 2013

FLAMINGO WA ZIWA MANYARA HATARINI KUTOWEKA

Ndege aina ya flamingo waliopo katika hifadhi ya taifa ya ziwa manyara wapo hatarini kutoweka, hii ni kwasababu ya matumizi ya mbolea za viwandani na viuatilifu kwenye kilimo katika mazingira yanayozunguka mbuga hii.

Siku hizi kumekuwa na matumizi makubwa sana ya mbolea na madawa ya kilimo katika kuongeza uzalishaji mashambani, baada ya kupuliziwa na kuwekwa ardhini mvua zinaponyesha kemikali hizi husombwa na maji hasa kutoka sehemu za miinuko. Maji haya ambayo mwisho wake huishia kwenye ziwa Manyara na kuchafua maji ya ziwa hili.

Ndege kadhaa hutumia maji ya ziwa hili ambalo lina magadi, wakinywa maji haya yenye kemikali hizo husababisha mapungufu kwenye mfumo wa umeng'enyaji chakula na madini aina ya kalsiam na fosforasi ndio huathirika. matokeo yake ni kwamba ndege hawa hutaga mayai ambayo maganda yake huwa dhaifu na kuathiri utotoaji wa vifaranga vya flamingo hawa.

Kutokana na athari hizi za mabadiliko katika ubora wa maji ya ziwa hili ni kwamba viumbe wote wanaotegemea ziwa hili kwa njia moja au nyingine nao wataathirika hasa baada ya kutokea athari za kiekolojia, kwa kawaida viumbe duniani huishi kwa kutegemeana na kwenye mfumo huu kiumbe kimoja tu kikiathirika maana yake ni kwamba viumbe wengine tegemezi wote wataathirika.
Ushauri muhimu ni kuendeleza kilimo cha asili kwa kutumia mbegu za asili, mbolea vunde au samadi za wanyama na pia kutumia dawa za asili kama utupa, muarobaini na pilipili kwa ajili ya kuulia wadudu waharibifu au kutumia njia za kibailojia kama sukuma vuta ili kukabiliana na wadudu waharibifu mashambani