Katika jitihada za kukabiliana na tatizo la wakulima kuuziwa mbegu za mahindi zisizofaa, kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) 842 KJ Mlale cha Songea mkoani Ruvuma, kimeanza uzalishaji wa mbegu za zao hilo ambazo zitakuwa mkombozi kwa wakulima wa Nyanda za Juu Kusini.
Mradi huo utawasaidia wakulima kulima mazao yao kwa uhakika na kwa utaalamu zaidi na kupata mavuno mengi na kuongeza kipato. Bwanashamba wa kikosi hicho Luteni Jackson Otaite, anasema kikosi kinajihusisha na kilimo cha mbegu za mahindi, mahindi ya chakula na kulima bustani za mbogamboga. “Mahindi yameuzwa kwa mkopo kwa Kampuni ya Highland Seed Growers ambayo ndiyo tuliingia mkataba kwa sababu kampuni hiyo haina fedha kwa sasa na bado thamani haijulikani kwa kuwa bado yanaendelea kuchambuliwa Kiwandani,” anasema. Anafafanua zaidi kuwa wanatarajia kuvuna tani 400 za mahindi ya chakula, tani 200 za mahindi ya mbegu na tani 25 za alizeti na mazao yote yanakadiriwa kuwa na thamani ya Sh330 milioni. Luteni Otaite anaeleza zaidi kuwa kikosi kimelima ekari 2.5 za mazao ya bustani na walivuna mbogamboga walizouza Sh7 milioni.
Anasema aina ya mahindi inayozalishwa na Mlale JKT ni Hybrid (H614) ambayo kukomaa baada ya miezi mitano na punje zake ni ngumu na haziliwi kirahisi na wadudu waharibifu, zinavumilia ukame na huzaa mahindi mawili kwa kila mmea na hutoa mavuno kati ya tani 1.5 hadi 2 kwa ekari. “Naiomba Serikali iongeze jitihada zaidi ya kuangalia uwezekano wa kupunguza bei za pembejeo za kilimo zikiwemo mbolea ambazo kwa sasa bei zake ziko juu sana,” anasema Luteni Otaite.
Kamanda wa kikosi hicho Meja Thomas Mpuku ameiomba Serikali kuanzisha utaratibu wa kutoa mbolea za ruzuku kwa vikosi vya JKT ili vizalishe mazao ya chakula na biashara kwa wingi pamoja na mahindi ya mbegu. Meja Mpuku, ameitaka Serikali kuwapa ruzuku za pembejeo ili waongeze uzalishaji badala ya utaratibu wa sasa wa kutoa ruzuku kwa wakulima pekee bila kuangalia wadau wanaowazalisha mbegu. Anasema baadhi ya matatizo ni upungufu wa wataalamu wa kilimo, kupanda kwa gharama za uzalishaji, uchakavu wa maghala, mchwa wanaoshambulia mahindi na kucheleweshwa kwa malipo.
JKT kuongeza uzalishaji
Anabainisha kwamba mipango ya baadaye ya kikosi hicho ni kuongeza ukubwa wa shamba kutoka ekari 650 hadi 800. Pia kupanua eneo la kulima bustani kutoka ekari 2 .5 hadi ekari 5 na kujenga bwawa litakalotumika kwa umwagiliaji. Mkuu wa Wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti amekipongeza kikosi hicho kwa jitihada hizo ambazo zinaonekana kuwa mkombozi wa kilimo. “Nimevutiwa na miradi yote ya maendeleo niliyoiona, nawatia moyo mkazane na jitihada hizo mtafika mbali, kwani miradi yenu ni madhubuti na hii iwe chachu kwa wanaohitimu, mkirudi majumbani kwenu mkawe mfano wa kuigwa kwa kilimo bora,” anasema Mkirikiti.
No comments:
Post a Comment